Je, ni uwezo gani wa kijeshi uliofichuliwa na Hezbollah wakati wa mashambulizi dhidi ya Israel?

Chanzo cha picha, Getty Images
Huku hali ya wasiwasi ikiongezeka kati ya Hezbollah na Israel kwenye mpaka wa kusini mwa Lebanon, wachunguzi wa mambo wanaamini kuwa mahasimu wote wawili wanafanya siri kuhusu aina ya silaha wanazotumia, hasa Hezbollah, ambayo mara kwa mara hufichua silaha mpya inazotumia kulenga maeneo ya Israel.
Chama cha Hezbollah cha Lebanon kilirusha makombora "mazito" ya masafa marefu, yaliyotumika kwa mara ya kwanza, kwenye maeneo makubwa ya Galilaya na mashariki mwa mji wa Haifa, na kutangaza kulenga kambi ya anga ya Israel ya "Ramat David" na majengo ya viwanda vya kijeshi.
Hezbollah ilitangaza Jumapili, katika taarifa rasmi, kwamba "ilirusha makumi ya makombora ya Fadi 1 na Fadi 2."
Chama hicho hakikutoa taarifa zaidi kuhusu uwezo wa makombora ya Fadi 1 na Fadi 2, kwa kuzingatia masafa na kiasi cha vilipuzi vilivyobebwa na aina hii ya kombora, au kuhusu mahali vilipotengenezwa, au kama viliongozwa au la.
Kwa mujibu wa vyanzo vya idhaa ya Al-Mayadeen inayoungwa mkono na Iran, makombora hayo yanatumiwa kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mashambulizi hayo. Kombora la Fadi 1 lina masafa ya kilomita 80 na ni nakala ya kombora la milimita 220 la Khaibar M220, lililotengenezwa Syria, ambalo linatumika kuongeza uwezo wa kushambulia wa Hezbollah.
Kuhusu kombora la Fadi 2, ni kombora la M302 lenye caliber ya 303 na safu ya kilomita 105, kwa mujibu wa Al-Mayadeen.
Televisheni ya Al-Manar, yenye uhusiano na Hezbollah, inasema, "Kombora hilo lilipewa jina la shahidi Fadi Hassan Tawil, kaka wa kiongozi aliyeuawa shahidi Wissam Tawil, ambaye aliuawa barabarani kuelekea Jerusalem mapema 2024."
Kinyume chake, Hezbollah hapo awali ilitangaza silaha nyingi inazomiliki. Ifuatayo ni uwezo mashuhuri zaidi wa kijeshi ambao Hezbollah inao.
Ndege zisizo na rubani zenye silaha

Chanzo cha picha, Hezbollah website
Matumizi ya Hezbollah ya makombora ya S5 yameibua wasiwasi wa Israel kuhusu utengenezaji wa silaha za kivita; gazeti la Israel la Yedioth Ahronoth liliripoti kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Hezbollah kutumia ndege isiyo na rubani yenye makombora, badala ya vilipuzi ambavyo kundi hilo la Lebanon limekuwa likitumia mara nyingi kwa miezi kadhaa.
Mtaalamu wa kijeshi wa Lebanon Brigedia Jenerali Hisham Jaber, mkuu wa Kituo cha Mashariki ya Kati cha Mafunzo na Mahusiano ya Umma, alieleza BBC kwamba "makombora hayo yanapiga kwa usahihi zaidi kuliko mabomu ambayo yanaweza kurushwa kutoka kwenye ndege isiyo na rubani."
Tovuti ya Hezbollah kwenye Telegram ilichapisha picha ya maelezo ya kombora la Urusi S5 lisiloongozwa na anga hadi ardhini, ikieleza kuwa lina urefu wa mita 1.4,
"Silaha mpya"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uwezo wa kijeshi wa Hezbollah nchini Lebanon umeshuhudia maendeleo ya ajabu katika miaka michache iliyopita. Chama hicho kimetumia silaha nyingi mpya tangu Oktoba 7.
Brigedia Jenerali Hisham Jaber alieleza kuwa Hezbollah huweka asili ya silaha zake kuwa siri na huzifichua tu taratibu, kulingana na maendeleo ya uwanja wa mapigano.
Aliongeza kwa BBC kwamba Hezbollah ilitumia makombora yake ya ulinzi wa anga mara mbili: "Mara ya kwanza ilipotungua ndege isiyo na rubani ya Hermes 450, na mara ya pili ilipoiangusha ndege iliyotengenezwa na Israel ya Hermes 900, Aprili mwaka jana."
Mnamo Mei 13, mtandao wa televisheni wa Al-Mayadeen wa Lebanon uliripoti kwamba Hezbollah ilifichua kwa mara ya kwanza matumizi ya kombora jipya zito liitwalo "Jihad Mughniyeh." Pia ilionesha kuwa ilitumia ndege mpya isiyo na rubani iitwayo "Shehab" kulenga mfumo wa Iron Dome wa Israeli.
Ripoti ya Taasisi ya Washington ya Sera ya Mashariki ya Karibu siku ya Alhamisi ilieleza kwamba Hezbollah ilitumia ndege zake zisizo na rubani za kizazi cha tatu kwa mara ya kwanza, na kuongeza kuwa kundi hilo lilitumia "aina ya hali ya juu zaidi ya ndege zisizo na rubani za Ababil zenye uwezo wa kutambua shabaha maalum."
Afisa wa Hezbullah aliifichulia idhaa ya Al-Mayadeen ya Lebanon kwamba kundi hilo hivi karibuni limeongeza kiwango cha uhifadhi wa silaha.
Nawaf al-Moussawi, mkuu wa Hezbollah wa faili ya "rasilimali na mipaka", alisema kuwa kundi hilo sasa linaweza kupokea idadi ya silaha ndani ya mwezi mmoja, baada ya kuzipokea kwa muda wa miezi sita.
Al-Moussawi alidokeza kwamba Hezbollah ina "silaha mpya" ambayo inaitumia dhidi ya Israel, ikiwa ni pamoja na makombora sahihi zaidi ambayo yanaweza kutumika katika eneo la bahari au nchi kavu, pamoja na ndege zisizo na rubani.
Gazeti la Israel, Jerusalem Post, liliripoti kuwa Hezbollah ina mfumo wa makombora wa kutoka ardhini hadi angani wenye urefu wa chini, wa masafa mafupi, SA8, na mifumo ya makombora ya ulinzi wa anga, SA17 na SA22, katika safu yake ya ushambuliaji, ili kurudisha Israeli. mgomo wa hewa.
Gazeti hilo lilimnukuu kamanda mstaafu wa kijeshi Tal Perry, ambaye anafanya kazi kama mkuu wa idara ya utafiti katika Kituo cha Alma cha Israel, akisema kuwa Hezbollah pia imetuma betri za SA8 kusini mwa Lebanon, ambayo anasema inaweza kuwa tishio kwa ndege za Israel zinazofanya kazi nchini Lebanon.
Uwezo wa kijeshi wa Hezbollah

Chanzo cha picha, Getty Images
Kituo cha Utafiti cha Alma cha Israel kimefuatilia mashambulizi ya Hezbollah dhidi ya Israel katika kipindi cha nyuma, kwa kutumia moto wa mwendo wa kasi, yakiwemo makombora ya Grad, makombora ya kukinga vifaru na ndege zisizo na rubani.
Mtaalamu wa masuala ya kijeshi Hisham Jaber aliieleza BBC kwamba inajulikana kuwa Hezbollah ina boti za majini katika jeshi lake la majini, lakini bado haijaonyesha makombora ya bahari hadi bahari iliyonayo.
Aliongeza kuwa Hezbollah ina makombora yenye nguvu ya Yakhont ya kuzuia meli ya Urusi, ambayo yanajulikana kwa usahihi wake, ambayo mtaalam wa kijeshi alielezea kuwa "inaweza kuharibu sio tu malengo ya majini, lakini pia majukwaa ya mafuta na gesi."
"Inajulikana kuwa Hezbollah inamiliki makombora 10,000," Jaber alisema, akiongeza kuwa Waisraeli wanakadiria kuwa kundi la Lebanon lina silaha ambazo bado hazijaoneshwa.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












