Israel inaamini imeidhoofisha Hezbollah lakini mzozo unazidi kukuwa

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Jumatatu ilikuwa ni siku ya umwagaji damu mkubwa zaidi nchini Lebanon tangu vita vya Hezbollah na Israel vya mwaka 2006.
Israel ilianzisha mashambulizi makubwa ya anga asubuhi, ambayo hadi sasa yameua watu 492 kulingana na serikali ya Lebanon na Israel inaonya mashambulizi zaidi yanakuja.
Vita hivyo vinaongezeka kwa kasi, kutokana na ukubwa wa mashambulizi ya anga ya Israel.
Israel inataka raia waondoke katika maeneo inayo yashambulia. Inasema, eneo lifuatalo, ni Bonde la Bekaa la kaskazini-mashariki mwa Lebanoni ambalo ni ngome ya Hezbollah.
Hata kabla ya kuongezeka kwa mashambulizi ya sasa, zaidi ya Walebanon 100,000 walilazimika kuondoka katika makazi yao kwa sababu ya mashambulizi ya Israel, na hawana matarajio ya kurudi haraka hivi karibuni.
Israel imeongeza mashambulizi. Labda wanaamini Hizbullah iko katika hali dhaifu hivi sasa na hii ni fursa yao ya kuletea uharibifu, na kubadilisha hali ya mambo katika vilima na miji ya pande zote za mpaka kati ya Israel na Lebanon.
Mzozo wa Israel na Hezbollah umekuwa ukiendelea kwa miongo kadhaa, lakini vita vya sasa vilianza siku moja baada ya mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba mwaka jana.
Hezbollah ilianzisha mashambulizi madogo madogo lakini endelevu ya kurusha roketi kwenda Israel. Takribani Waisrael 60,000 wamelazimika kuondoka katika makazi yao na kuhamia katikati mwa nchi hiyo.
Na sasa kuwarejesha makwao kumeongezwa kwenye orodha ya malengo ya Israel ya vita hivyo.
Marekani na Uingereza, na washirika wengine - na wakosoaji wa Israel wanaamini njia pekee ya kutuliza mzozo huu hatari ni kupata usitishaji vita huko Gaza.

Chanzo cha picha, EPA
Hassan Nasrallah, kiongozi wa Hezbollah, amesema mashambulizi dhidi ya Israel yataendelea hadi kupatikane usitishwaji wa mapigano huko Gaza.
Lakini inaonekana wazi kwa wakati huu, si kiongozi wa Hamas wala kiongozi wa Israel ambaye yuko tayari kukubali makubaliano ya usitishaji vita ambayo yamependekezwa na Marekani.
Vita vyenyewe vina ungwa mkono pakubwa na Waisraeli, ingawa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu bado haungwi mkono na sehemu kubwa ya wapiga kura wa Israel.
Waisraeli wengi wanaamini Netanyahu ni kiongozi mbaya ambaye anasema uwongo na amewasahau mateka huko Gaza. Kwa hivyo ni kiongozi mwenye utata sana. Lakini anaungwa mkono na vyama vya mrengo wa kulia bungeni, na hilo linamfanya awe salama kisiasa.
Uamuzi wake wa kuendelea na mashambulizi ni wa hatari.
Wakati Hezbollah imejeruhiwa, bado ina uwezo mkubwa wa kurudisha mapigo. Na ndio maana marafiki na maadui wa Israeli bado wanajitayarisha kwa hali mabaya zaidi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












