Vita vya Lebanon: Je, Israel inacheza bahati nasibu na Hezbollah?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Viongozi wa Israel wanafuraha kuhusu maendeleo ya mashambulizi dhidi ya Hezbollah, ambayo yalianza kwa milipuko ya vifaa vya mawasiliano na kuendelea na mashambulizi makali na mabaya ya anga.
Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant hakuzuia furaha yake baada ya mashambulizi ya anga ya Jumatatu.
"Hii ilikuwa wiki mbaya zaidi kwa Hezbollah tangu kuanzishwa kwake, na matokeo yanajieleza yenyewe."
Gallant alisema mashambulizi ya anga yaliharibu maelfu ya roketi ambazo zingeweza kuwaua raia wa Israel. Katika mashambulizi hayo Lebanon inasema Israel imeuwa zaidi ya raia 550 wakiwemo watoto 50. Ni karibu nusu ya waliofariki Lebanon katika mwezi mmoja wa vita kati ya Israel na Hezbollah mwaka 2006.
Israel inaamini mashambulizi makali yatailazimisha Hezbollah kufanya inachotaka. Wanasiasa na majenerali wa Israel wanahitaji ushindi.
Jeshi la Israel (IDF) na shirika la kijasusi la Mossad wamekuwa wakipanga vita vijavyo dhidi ya Hezbollah tangu vita vya mwisho vilipomalizika mwaka 2006.
Kiongozi wa Israel, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, anaamini mashambulizi ya sasa yanapiga hatua kubwa kuelekea lengo lake.
Anataka kuizuia Hezbollah kurusha maroketi mpakani mwa Israel. Wakati huo huo, jeshi la Israel linasema mpango huo ni kuilazimisha Hezbollah kurejea nyuma kutoka mpakani na kuharibu vituo vyao vya kijeshi vinavyoitishia Israel.
Vita vya sasa
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Israel ilitoa onyo kwa raia, kama ilivyofanya huko Gaza, kuondoka katika maeneo ambayo yangeshambuliwa huko Lebanon. Inailaumu Hezbollah, kama inavyoilaumu Hamas, kwa kutumia raia kama ngao.
Baadhi ya wakosoaji wa Israel walisema maonyo hayo hayakutoa muda wa kutosha kwa familia kuhama. Sheria za vita zinataka raia walindwe, na kukataza matumizi ya nguvu yasiyo na uwiano.
Baadhi ya mashambulizi ya Hezbollah dhidi ya Israel yamepiga maeneo ya raia, na kuvunja sheria za kuwalinda raia. Pia wameshambulia kambi za jeshi la Israel. Israel na washirika wake wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza, wanaitaja Hezbollah kama shirika la kigaidi.
Israel inasisitiza kuwa ina jeshi linaloheshimu sheria. Lakini sehemu kubwa ya dunia imelaani matendo ya jeshi lake hilo huko Gaza.
Israel inasema ililenga wapiganaji wa Hezbollah ambao walikuwa na vifaa vya mawasiliano. Lakini haikuweza kujua wangekuwa wapi wakati vifaa hivyo vinalipuka, ndiyo maana raia na watoto katika nyumba, madukani na maeneo mengine ya umma walijeruhiwa na kuuawa.
Baadhi ya wanasheria wanasema, hilo linathibitisha kwamba Israel ilitumia nguvu za kuua bila kutofautisha kati ya wapiganaji na raia; ukiukaji wa kanuni za vita.
Mapigano kati ya Israel na Hezbollah yalianza miaka ya 1980. Lakini vita hivi vya sasa vilianza siku moja baada ya Hamas kushambulia Israel tarehe 7 Oktoba, wakati Hassan Nasrallah alipowaamuru wapiganaji wake waanzishe mashambulizi madogo, ili kuunga mkono Hamas. Mashambulizi hayo yaliwalazimisha takribani watu 60,000 katika miji ya mpakani kuondoka makwao.
Vita vilivyopita

Chanzo cha picha, Getty Images
Sauti chache katika vyombo vya habari vya Israel zimelinganisha athari za mashambulizi ya anga kwa Hezbollah na Operesheni Focus, shambulio la kushtukiza la Israel dhidi ya Misri mwezi Juni 1967.
Ulikuwa ni uvamizi ambao uliharibu jeshi la anga la Misri wakati ndege zake zikiwa zimepangwa juu ya ardhi. Katika siku sita zilizofuata Israel iliishinda Misri, Syria na Jordan. Ushindi huo uliunda sura ya mzozo wa sasa baada ya Israel kuuteka Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Jerusalem mashariki, Ukanda wa Gaza na Miinuko ya Golan.
Sio ulinganisho mzuri, kwani vita na Hezbollah, ni tofauti. Israel imetoa mapigo mazito. Lakini hadi sasa haijazuia uwezo wa Hezbollah kufyatua makombora kwenda ndani ya Israel.
Vita vya hapo awali vya Israel na Hezbollah havikutoa ushindi kwa upande wowote. Na vita hivi vinaweza kuwa na matokeo kama hayo.
Mashambulio ya Israel yanategemea dhana – yaani kucheza kamari - kwamba wakati utafika Hezbollah itakapo haribiwa, kurudi nyuma kutoka mpakani na kuacha kufyatua makombora ndani ya Israel.
Waangalizi wanaamini kuwa Hezbollah haitoacha kufyatua makombora, kwani kupigana na Israel ndio sababu kuu ya uwepo wa Hezbollah.
Ikiwa Hezbollah itaendelea kuifanya kaskazini mwa Israeli kuwa hatari kwa raia wa Israel kurudi nyumbani, Israel italazimika kuamua ikiwa itafanya operesheni ya ardhini, na kushikilia kipande cha ardhi na kukifanya kuwa eneo la amani.
Israel iliwahi kuivamia Lebanon hapo awali. Mwaka1982 vikosi vyake vilifika hadi Beirut kujaribu kuzuia uvamizi wa Wapalestina ndani ya Israel. Walilazimika kurudi nyuma kutokana na hasira ndani ya Israel na nje, baada ya wanajeshi wake kuzunguka eneo hilo huku washirika wao wa Kikristo wa Lebanon wakiwaua raia wa Palestina katika kambi za wakimbizi za Sabra na Shatila huko Beirut.
Kufikia miaka ya 1990 Israeli bado ilikuwa inakalia eneo kubwa la ardhi ya Lebanon kwenye mpaka. Majenerali wa leo wa Israel walikuwa maafisa vijana, ambao walipigana dhidi ya Hezbollah.
Ehud Barak, waziri mkuu wa Israel wakati huo na mkuu wa zamani wa jeshi la IDF, alijiondoa katika kile kilichoitwa "eneo la amani" mwaka 2000. Alisema halikuifanya Israel kuwa salama na ilikuwa ikigharimu maisha ya wanajeshi wengi sana.
Mwaka 2006, uvamizi wa Hezbollah ndani ya Israel uliua na kuwakamata wanajeshi wa Israel. Baada ya vita kumalizika Hassan Nasrallah alisema hangeruhusu uvamizi huo utokee, kama angetambua kile ambacho Israel ingefanya. Ehud Olmert, aliyekuwa waziri mkuu wa Israeli wakati huo, aliingia vitani.
Israel ilitarajia nguvu za anga zingezuia mashambulio ya roketi ndani ya Israel. Hilo halikutokea, na askari wa ardhini na vifaru kwa mara nyingine tena walirudi nyuma. Vita hivyo vilikuwa janga kwa raia wa Lebanon. Lakini katika siku ya mwisho ya vita, Hezbollah ilikuwa bado inarusha makombora mengi ndani ya Israel.
Vita vilivyopo na vijavyo
Makamanda wa Israel wanajua kwamba kuingia Lebanon itakuwa changamoto kubwa zaidi kuliko kupambana na Hamas huko Gaza. Hezbollah imekuwa ikifanya maandalizi tangu mwisho wa vita vya 2006, na itakuwa ikipigana katika ardhi ya nyumbani, kusini mwa Lebanon, kwenye maeneo mengi ya milima yenye miinuko ambayo yanafaa kwa mbinu za waasi.
Israel haijaweza kuharibu mahandaki yote ya Hamas huko Gaza. Katika mipaka ya kusini mwa Lebanon, Hezbollah imetumia miaka 18 iliyopita kuandaa mahandaki katika miamba imara. Ina silaha za kutisha, zinazotolewa na Iran. Tofauti na Hamas, Hezbollah inaweza kupokea silaha kupitia Syria.
Inakadiriwa kuwa Hezbollah ina wapiganaji karibu 30,000 na wakujitolea 20,000, wengi wao wakiwa wamefunzwa kama wapiganaji wa ardhini. Wengi wana uzoefu wa mapigano katika kuunga mkono utawala wa Assad nchini Syria.
Makadirio yanasema Hezbollah ina kati ya makombora 120,000 na 200,000, kuanzia makombora ya masafa mafupi na masafa marefu ambayo yanaweza kushambulia miji ya Israel.
Israel inaweza kuwa inacheza bahati nasibu kwa kuamini Hezbollah haitazitumia silaha zote, ikihofia jeshi la anga la Israel litaifanya Lebanon kama kile ilichokifanya Gaza, kugeuza miji yote kuwa vifusi na kuua maelfu ya raia.
Iran huenda ikaitaka Hezbollah kutotumia silaha ambazo ingependa zibaki turufu dhidi ya shambulio la Israel kwenye vituo vya nyuklia vya Iran. Hiyo ni bahati nasibu nyingine. Hezbollah inaweza kuamua kutumia silaha zake kabla ya Israel kuziangamiza.
Huku vita vikiendelea Gaza, na kuongezeka kwa viwango vya ghasia kwenye Ukingo wa Magharibi, Israel pia inalazimika kujitafakari. Wanajeshi wake wamefunzwa vyema na wana vifaa, lakini vitengo vya akiba ambavyo vinatoa nguvu kubwa ya mapigano ya Israel tayari vinakabiliwa na uchovu baada ya mwaka wa vita.
Hatua zao kidiplomasia

Chanzo cha picha, Getty Images
Washirika wa Israel wakiongozwa na Marekani hawataki Israel ianzishe vita kamili na Hezbollah na wala hawataki iivamie Lebanon. Wanasisitiza, diplomasia pekee ndio inayoweza kuufanya mpaka kuwa salama kiasi cha raia kurejea makwao kila upande.
Wanadiplomasia wanajua kuwa bila ya kusitishwa mapigano huko Gaza bado hakutokuwa na amani. Hasan Nasrallah amesema Hezbollah itaacha tu kuishambulia Israel vita vya Gaza vitakapo koma.
Huku mashambulizi ya anga ya Israel yakiendelea kushambulia Lebanon, raia ambao tayari walikuwa wakihangaika kuhudumia familia zao katika hali mbaya ya uchumi wanakabiliwa na maumivu makali na kutokuwa na uhakika.
Na Waisraeli wanajua kuwa Hezbollah inaweza kuwaletea uharibifu mbaya zaidi kuliko mwaka uliopita.
Israel inaamini wakati umefika wa kuilipua Hezbollah. Lakini inakabiliwa na adui mwenye nguvu, mwenye silaha na hasira. Huu ni mgogoro hatari zaidi tangu Hamas ilipoishambulia Israel na kwa sasa hakuna kinachoizuia kuendelea na jambo baya zaidi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












