Jeshi la Israel lasema kamanda wa Hezbollah ameuawa katika shambulizi lake Beirut
Huku mzozo mapigano ukiendelea kati ya Israel na Hezbollah, msemaji wa jeshi la Israel (IDF) Avichay Adraee anasema wanajeshi wa Israel wamemuua Ibrahim Muhammad al-Qubasi leo.
Muhtasari
- Jeshi la Israel lasema kamanda wa Hezbollah aliuawa katika shambulizi
- Urusi yafanya makubaliano ya satelaiti na serikali za kijeshi za Afrika Magharibi
- Jeshi la Israel lafanya mashambulizi ya anga katika eneo 'lililolengwa' Beirut
- Israel na Hezbollah: Uwezo wa Israel kupigana na Hezbollah hauko wazi
- Zelensky: Vita vinakaribia kumalizika kuliko wengi wanavyofikiria
- Wizara ya afya ya Lebanon inasema watu 558 wameuawa tangu mashambulizi ya Jumatatu
- Makumi ya makombora ya Hezbollah yarushwa kaskazini mwa Israel
- British Airways yafuta safari za ndege za Tel Aviv
- Mwanaume raia wa Korea Kusini akiri kumzika mpenzi wake kwenye saruji
- Israel yasema ilishambulia maeneo kadhaa ya Hezbollah usiku kucha
- Telegram sasa itatoa baadhi ya data za watumiaji kwa mamlaka
- Marekani kupiga marufuku teknolojia ya Kichina kwenye magari
- Meli ya Misri yapeleka silaha Somalia
- Tanzania: Viongozi wakuu wa Chadema waachiwa na polisi
- Mshukiwa aliandika maelezo ya 'kumuua Trump' kitambo kabla ya jaribio lake
- Mashambulizi ya Israel yaua watu 492 Lebanon
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Dinah Gahamanyi
Jeshi la Israel lasema kamanda wa Hezbollah ameuawa katika shambulizi lake Beirut

Chanzo cha picha, Reuters
Huku mzozo mapigano ukiendelea kati ya Israel na Hezbollah, msemaji wa jeshi la Israel (IDF) Avichay Adraee anasema wanajeshi wa Israel wamemuua Ibrahim Muhammad al-Qubasi leo.
Al-Qubaisi alikuwa kamanda wa mfumo wa makombora na roketi wa Hezbollah, Adraee amesema kwenye chapisho kwenye X.
Taarifa yake inaongeza kuwa mwanachama huyo wa Hezbollah alikuwa pamoja na maafisa wengine wakuu kutoka kundi hilo wakati wa shambulio hilo.
Hapo awali tuliripoti kuwa IDF ilithibitisha kuwa walikuwa wameanzisha mashambulizi kwenye maeneo"yanayolengwa" katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Kabla ya hapo walisema walikuwa wamepiga "makumi" ya maeneo yaliyolengwa ya Hezbollah katika mashamulizi ya usiku mmoja.
Unaweza pia kusoma:
Urusi yafanya makubaliano ya satelaiti na serikali za kijeshi za Afrika Magharibi

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Satelaiti hizo zinasemekana kuwa za TV na redio, upelelezi na kufuatilia majanga ya asili Mali, Niger na Burkina Faso zimetangaza makubaliano na Urusi ambayo yataziwezesha kupata mawasiliano ya simu na satelaiti za upepezi.
Nchi hizo tatu za Afrika Magharibi, zinazoendeshwa na wanaharakati wa kijeshi, zimekuwa zikijitahidi kuwadhibiti waasi wa Kiislamu kwa miaka mingi na zimeigeukia Urusi kwa msaada wa kijeshi.
Urusi inakanusha kuwa mamluki wake wamefanyaukatili dhidi ya raia na kwamba kueneza propaganda na habari potofu katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi.
Mawaziri kutoka nchi hizo tatu walikutana na maafisa wa shirika la anga la Urusi Roscosmos katika mji mkuu wa Mali, Bamako, siku ya Jumatatu, kujadili makubaliano hayo.
Teknolojia hiyo itaongeza ufuatiliaji wa mpaka na usalama wa taifa katika nchi zote tatu, anasema waziri wa fedha wa Mali, Alousséni Sanou, akiongeza kuwa itawezesha mawasiliano salama.
Wapiganaji wa Kiislamu hukuvuka mipaka mirefu ya nchi hizo tatu katika eneo kubwa la jangwa la Sahel kusini mwa Jangwa la Sahara.
Sanou pia alisema satelaiti hizo zitawasaidia kufuatilia na kukabiliana na mafuriko, ukame, mikasa ya moto na dharura nyinginezo.
Jeshi la Israel lafanya mashambulizi ya anga katika eneo 'lililolengwa' Beirut

Chanzo cha picha, Reuters
Jeshi la Israel limesema limefanya mashambulizi ya anga katika eneo "lililolengwa" katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Timu za dharura zimepelekwa mara moja kutoka kwenye shule tulipo wakati Israel ilipofanya mashambulizi ya anga katika katika eneo Ghobairi lililopo kwenye kitongoji cha Dahieh, kusini mwa mji mkuu wa Lebanon Beirut.
Mashambulizi haya yamefanyika huku mazishi ya watu wanne yakipangwa kufanyika katika eneo hilo, wakiwemo wanawake watano, wote wa familia moja ambao waliuawa katika shambulio la Israel wiki iliyopita huko Dahieh.
Vyanzo vilisema kuwa ilibidi rafiki wa familia hii kutambuliwa kwa uchunguzi wa vinasaba (DNA).
Unaweza pia kusoma:
Israel na Hezbollah: Uwezo wa Israel kupigana na Hezbollah hauko wazi,
Hezbollah ina nguvu zaidi, kwa namna nyingi, kuliko Hamas: silaha bora zaidi; mafunzo bora zaidi; walipigana kwa miaka nchini Syria kwa ajili ya Rais Assad hivyo wana uzoefu wa kutosha.
Na katika ardhi laini ya Gaza, Hamas wana mahandaki ambayo kimsingi yamechimbwa kwenye mchanga kusini mwa Lebanon ambako kuna miamba na milima, bila shaka kuna mitandao ya Hezbollah ya mahandaki, lakini yalitengenezwa kwenye miamba.
Israeli wanajipongeza kuhusu shambulio hili la kushtukiza kama wanavyolichukulia, lakini wanafikiria jinsi watakavyoweza kuilazimisha Hezbollah kuwa katika hali ambayo haitalazimika kuendelea na vita zaidi.
Je, hii itamaanisha kuwa Israeli inaweza kufikia malengo yao yaliyotajwa kuruhusu Waisraeli zaidi ya 60,000 ambao wamehamishwa kutoka kwa makazi yao kurudi kaskazini; kuisukuma Hezbollah nyuma kutoka mpakani na kuharibu miundombinu yao ya kijeshi katika eneo hilo?
Kwa hivyo nadhani kuna maswali makubwa juu ya uwezo wa Israeli kufikia haya yote, ikiwa Hezbollah itaendelea kuvuka mpaka kati yake na Israel.
Unaweza pia kusoma:
Zelensky: Vita vinakaribia kumalizika kuliko wengi wanavyofikiria

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anaamini vita vya Urusi dhidi ya Ukraine vinakaribia kumalizika kuliko wengi wanavyofikiria na ametoa wito kwa washirika kuimarisha jeshi la Ukraine.
"Mpango wa ushindi ni kuimarisha Ukraine. Ndiyo sababu tunawaomba marafiki zetu, washirika wetu, kutuimarisha. Hii ni muhimu sana." "Nafikiri tuko karibu na amani kuliko tunavyofikiria. Tunakaribia kufikia mwisho wa vita," Zelensky aliliambia shirika la habari la ABC.
Urusi imejibu kauli ya Rais Zelensky kuwa vita vinakaribia kuisha kupitia Msemaji wa Rais Vradimir Putin: “Unajua kwamba vita vyovyote, kwa njia moja au nyingine, huisha kwa amani. Lakini kwetu sisi hakuna njia mbadala kabisa ya kufikia malengo yetu. Punde tu malengo haya yakifikiwa kwa njia moja au nyingine, operesheni maalum ya kijeshi itakamilika,” alisema Dmitry Peskov, msemaji wa rais wa Urusi.
Rais wa Ukraine amekuwa katika ziara rasmi nchini Marekani tangu Jumapili. Anapanga kuwasilisha "mpango wa ushindi" wa Ukraine kwa Rais wa Marekani Joe Biden, wajumbe wa Congress, na wagombea wa urais Kamala Harris na Donald Trump.
Siku ya Jumanne, Zelensky atashiriki katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini Ukraine, na Jumatano atahutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Vita vya Ukraine: Soma zaidi:
KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
Habari za hivi punde, Wizara ya afya ya Lebanon inasema watu 558 wameuawa tangu mashambulizi ya Jumatatu
Katika taarifa zao za hivi punde, wizara ya afya ya Lebanon inasema watu 558 wameuawa tangu Jumatatu baada ya mashambulio ya Israel nchini humo.
Waziri wa afya wa Lebanon Firass Abiad anasema kati ya waliouawa, 50 walikuwa watoto.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari, amesema wanahabari "sekta ya afya inahitaji msaada wetu".
"Tunatumai kinachokuja sio kibaya zaidi. Tutaendelea kutekeleza jukumu letu.
"Wahudumu wa matibabu wanne walifariki jana wakati magari ya kubebea wagonjwa na gari la kubebea wagonjwa vilipopigwa na kombora la Israel. Asubuhi ya leo waliiga kombora hospitali ya Bint Jbail," Abiad anasema.
Itakumbukwa kuwa Jumatatu ilikuwa siku mbaya zaidi ya mashambulizi nchini Lebanon tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo 1990.
Makumi kadhaa ya makombora yarushwa kaskazini mwa Israel

Chanzo cha picha, Reuters
Jeshi la Israel linasema kuwa makumi ya roketi yamerushwa kaskazini mwa Israeli kati ya 03:30 na 03:45 asubuhi kwa saa za eneo. Watu huko wamekuwa wakipokea tahadhari za kufyatuliwa kwa roketi.
Kwanza, roketi tano zilidunguliwa na "baadhi yake zilizuiwa angani katika maeneo wazi," Jeshi la Ulinzi la Israeli linasema.
Kisha, takriban roketi 50 zilidunguliwa katika eneo la Upper Galilaya jeshi la Israel (IDF) linasema.
Mengi ya makombora yalizuiwa lakini kumekuwa na uharibifu wa majengo na wazima moto wanafanya kazi ya kuzima moto, IDF imeongeza.
Katika taarifa yake Hezbollah inasema ilishambulia kwa mabomu makazi ya Qiryat Shmona "kwa msururu wa makombora".
Qiryat Shmona ni eneo lililoko katika eneo la Galilaya ya Juu (Upper Galilaya) kaskazini mwa Israel.
Unaweza pia kusoma:
British Airways yafuta safari za ndege za Tel Aviv

Chanzo cha picha, EPA
British Airways inasema kuwa imefuta safari zake za kwenda na kutoka Tel Aviv hadi Jumatano.
"Usalama daima ni kipaumbele chetu cha juu, na tunawasiliana na wateja ili kuwashauri kuhusu chaguo zao za usafiri," Shirika hilo la ndege la Uingereza limesema katika taarifa.
Vile vile, safari za ndege zingine kwenda Israel na Beirut zimefutwa kwa sababu ya hofu juu ya usalama wa abiria.
Shirika la ndege la Qatar Airways limesema kuwa limesimamisha kwa muda safari za ndege za kwenda na kutoka Beirut hadi kesho.
"Usalama wa abiria wetu unasalia kuwa kipaumbele chetu cha juu," inasema, kulingana na shirika la habari la AFP.
Leo asubuhi, ratiba ya wanaowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beirut-Rafic Hariri inaonyesha kufutwa kwa safari kadhaa ikiwa ni pamoja na Shirika la Ndege la Uturuki kutoka Istanbul, Air France kutoka Paris na Royal Jordanian kutoka Amman.
Mashirika ya ndege ya Lufthansa na Delta Air Lines ya Ujerumani pia yamesitisha safari za ndege kuelekea Beirut katika siku za hivi karibuni huku huduma za baadhi ya wasafirishaji kwenda Israel na Iran zikiathiriwa pia, AFP iliripoti.

Chanzo cha picha, Reuters
Shule zafungwa kaskazini mwa Israel na Lebanon
Wakati huo huo, shule zaidi kaskazini mwa Israel zimefungwa hii leo, gazeti la Times of Israel linaripoti.
Mapema wiki hii, shule katika eneo la Haifa na kaskazini zilifungwa, lakini nyingi zaidi sasa zinafungwa katika miji mingine ambapo milio ya roketi imeripotiwa katika mpaka wa kaskazini, ilisema.
Wakati huo huo, wizara ya elimu ya Lebanon imesema shule zote zitasalia kufungwa.
Kama tulivyoripoti hapo jana, shule za umma bado hazijaanza kwa mwaka wa shule, huku zile za kibinafsi katika maeneo mengi nchini humo zimetakiwa kusitisha masomo kuanzia leo.
Baadhi ya shule huko Beirut na kwingineko sasa badala yake zinatumika kama makazi ya watu waliokimbia makao yao kutokavita vya kusini mwa Lebanon.
Soma zaidi:
Mwanaume raia wa Korea Kusini akiri kumzika mpenzi wake kwenye saruji

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanaume mmoja nchini Korea Kusini amekiri kumuua mpenzi wake na kuficha mwili wake kwenye saruji - miaka 16 baada ya kuripotiwa kutoweka.
Mwanamume huyo, ambaye ana umri wa miaka ya 50, aliwaambia polisi wa eneo hilo kwamba alimpiga mwanamke huyo kwa kifaa butu wakati wakibishana katika nyumba yake kusini mwa mji wa Geoje.
Kisha akaweka maiti yake ndani ya sanduku, ambayo aliizika chini ya sakafu iliyojengwa kwa matofali na saruji barazani kwake.
Ilibakia hapo bila kutambuliwa hadi mwezi uliopita, wakati mtu mmoja aliyekuwa akifanya matengenezo alipogundua wakati akichimba kisima, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Mwili huo - ambao ulikuwa umehifadhiwa kwenye sanduku - ulitambuliwa kama mwanamke aliyepotea kupitia uchunguzi wa vidole.
Uchunguzi wa maiti ulionyesha kuwa alifariki dunia kutokana na maumivu ya kuumizwa kichwani na kifaa butu.
Mwanamume huyo, ambaye polisi wanamwita Bw A, hakuwa akiishi katika nyumba hiyo wakati mwili huo ulipogunduliwa lakini alipatikana mara moja na kukamatwa.
Aliwaambia polisi kwamba alikuwa akiishi na mwanamke huyo kwa takriban miaka mitano katika nyumba hiyo huko Geoje, kabla ya kutokea kwa mabishano mnamo Oktoba 2008 na kusababisha ampige kwa kutumia kifaa butu.
Kisha akazika sanduku lililokuwa na mwili wake chini ya sakafu yenye matofali na saruji kwenye kibaraza kidogo ghorofa ya tatu, ambayo inaweza kufikiwa tu kutoka kwenye moja ya vyumba vya kulala.
Israel yasema ilishambulia maeneo kadhaa ya Hezbollah usiku kucha

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Watu waliokimbia kutoka kusini mwa Lebanon wanakaa kwenye magari yao huko Beirut Wanajeshi wa Ulinzi wa Israel wametuma ujumbe mtandaoni, wakisema kwamba wakati wa usiku roketi zilirushwa kutoka Lebanon kuelekea eneo la Afula na eneo la mabonde kaskazini mwa Israel.
IDF inasema walishambulia vifaa vya kurushia roketi na kuongeza kuwa ndege zao za kivita pia zilishambulia "makumi" ya maeneo lengwa ya Hezbollah katika maeneo kadhaa kusini mwa Lebanon.
Israel inasema wanaamini kuwa walishambulia majengo ya kuhifadhi silaha, kwa sababu kuna "milipuko ya pili iliyoshuhudiwa".
Roketi za Hezbollah zasababisha ving'ora kaskazini mwa Israel
Wakati huo huo, ving'ora vya kuonya kuhusu moto wa roketi za Hezbollah vilisikika kaskazini mwa Israel.
Kundi hilo lenye makao yake makuu nchini Lebanon linasema kuwa lilirusha makombora katika maeneo ya jeshi la Israel, karibu na mji wa bandari wa Haifa na kambi mbili kulipiza kisasi mashambulizi ya jana.
Mashambulizi hayo, ambayo ni siku mbaya zaidi katika mzozo kati ya Hezbollah na Israel tangu 2006, yalilenga maeneo 1,300 kote Lebanon na kuua karibu watu 500.
Soma zaidi:
Telegramu sasa itatoa baadhi ya data za watumiaji kwa mamlaka

Chanzo cha picha, Reuters
Programu ya kutuma ujumbe ya Telegram imesema itakabidhi nambari ya kipekee ya utambulisho inayotolewa kwa kila kifaa kilichounganishwa kwenye mtandao kwa mamlaka zilizo na vibali vya kufanya upekuzi au maombi mengine halali ya kisheria.
Mabadiliko ya masharti yake ya huduma na sera ya faragha "yanapaswa kuwakatisha tamaa wahalifu", Mkurugenzi Mtendaji Mkuu Pavel Durov alisema katika ujumbe wake wa Telegraph siku ya Jumatatu.
"Ingawa 99.999% ya watumiaji wa Telegraph hawana uhusiano wowote na uhalifu, 0.001% wanaohusika katika shughuli za uhalifu wanatengeneza taswira mbaya kwa jukwaa zima, na kuweka masilahi ya karibu watumiaji wetu bilioni hatarini," aliendelea.
Tangazo hilo linaashiria mabadiliko makubwa kwa Bw Durov, mwanzilishi mwenza wa jukwaa hilo mzaliwa wa Urusi ambaye alizuiliwa na mamlaka ya Ufaransa mwezi uliopita katika uwanja wa ndege kaskazini mwa Paris.
Siku kadhaa baadaye, waendesha mashtaka huko walimshtaki kwa kuwezesha shughuli za uhalifu kwenye jukwaa.
Madai dhidi yake ni pamoja na kushiriki katika kueneza picha za unyanyasaji wa watoto na biashara ya dawa za kulevya.
Pia alishtakiwa kwa kushindwa kufuata sheria.
Bw Durov, ambaye amekanusha mashtaka hayo, alikashifu mamlaka muda mfupi baada ya kukamatwa, akisema kuwa kumshikilia ili kuwajibika kwa uhalifu uliofanywa na wahusika wa tatu kwenye jukwaa la Telegram ni jambo la "kushangaza" na "kupotosha."
Wakosoaji wanasema Telegramu imekuwa kitovu cha habari potofu, ponografia ya watoto, na maudhui yanayohusiana na ugaidi kwa sababu ya kipengele kinachoruhusu vikundi kuwa na hadi wanachama 200,000.
Ukilinganisha na jukwaa la WhatsApp inayomilikiwa na Meta, inaweka mipaka ya ukubwa wa vikundi hadi watu 1,000.
Soma zaidi:
Marekani kupiga marufuku teknolojia ya Uchina kwenye magari

Chanzo cha picha, Getty
Marekani inapanga kupiga marufuku programu fulani zinazotengenezwa nchini China na Urusi za magari, malori na mabasi kwasababu ya hatari za kiusalama.
Maafisa walisema walikuwa na wasiwasi kwamba teknolojia inayozungumziwa, inayotumika kwa magari yanayojiendesha yenyewe na kuunganisha magari kwenye mitandao mingine, inaweza kuruhusu maadui "kuongoza magari kwenye barabara za Marekani" wakiwa mbali.
Kwa sasa kuna matumizi madogo sana ya programu ya Kichina au Urusi katika magari ya Marekani.
Lakini Waziri wa Biashara Gina Raimondo alisema mipango hiyo "ililenga, hatua za haraka" za kulinda Marekani.
"Magari leo yana kamera, maikrofoni, ufuatiliaji wa GPS, na teknolojia zingine zilizounganishwa kwenye mtandao," alisema katika taarifa.
"Haichukui muda mrefu kuelewa jinsi adui ambaye yuko nje ya nchi anayepata habari hii ni kwa kiasi gani anaweza kusabaisha hatari kubwa kwa usalama wetu wa kitaifa na faragha ya raia wa Marekani."
Maafisa wa China walisema Marekani inaongeza zaidi "dhana ya usalama wa taifa" ili kulenga isivyo haki ya makampuni ya China.
Soma zaidi:
Meli ya Misri yapeleka silaha Somalia

Chanzo cha picha, Waziri wa Ulinzi wa Somalia
Meli ya Misri imewasilisha shehena kubwa ya vifaa vya kijeshi nchini Somalia, maafisa wa usalama katika mji mkuu, Mogadishu, wamenukuliwa wakisema.
Waziri wa Ulinzi wa Somalia Abdulkadir Mohamed Nur aliishukuru Misri katika chapisho la mtandao wa kijamii bila kutaja haswa silaha hizo.
Hii ni mara ya pili kwa silaha kutolewa kwa namna hiyo kutoka Misri katika kipindi cha mwezi mmoja huku mahusiano yakizorota kati ya Somalia na jirani yake na mshirika wake wa karibu wa wakati mmoja Ethiopia.
Misri, mpinzani wa muda mrefu wa Ethiopia, imechukua fursa hiyo kusogea karibu na Somalia, na kuzua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mvutano katika Upembe ya Afrika.
Shehena hiyo ya kijeshi, iliyobebwa kwenye meli ya kivita iliyowasili Jumapili, ilijumuisha bunduki za kupambana na ndege na mizinga, shirika la habari la Reuters linaripoti likinukuu maafisa wa usalama na bandari.
Mwandishi wa BBC mjini Mogadishu mwenyewe aliona silaha zikisafirishwa katika mitaa ya jiji hilo.
Katika chapisho lake kwenye X, Bw Nur anapigwa picha inayomuonesha mgongoni kwenye kamera akitazama chombo cha majini kilichotia nanga.
"Somalia imepita hatua ambapo itaamrishwa na kusubiri ruhusa ya wengine juu ya nani itashirikiana naye," aliandika.
"Tunajua maslahi yetu wenyewe, na tutachagua kati ya washirika wetu na adui zetu. Asante Misri."
Ethiopia kwa miaka mingi imekuwa muungaji mkono mkubwa wa serikali mjini Mogadishu katika mapambano yake dhidi ya kundi la wanamgambo wenye mafungamano na al-Qaeda al-Shabab.
Lakini Somalia ina hasira kwamba Ethiopia isiyokuwa na bandari ilitia saini makubaliano ya awali mwanzoni mwa mwaka huu na jimbo la Somaliland lililojitangazia uhuru kukodisha sehemu ya ufuo wake. Somalia inaiona Somaliland kama sehemu ya ardhi yake.
Ethiopia yajibu
Ethiopia imeelezea wasiwasi wake kwamba shehena ya silaha na vikosi vya kigeni inaweza kuzidisha hali ya usalama katika nchi jirani ya Somalia.
Pembezoni mwa mkutano wa Umoja wa Mataifa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Taye Atske-Selasie alielezea wasiwasi wake kwamba risasi na silaha zinazopelekwa Somalia zinaweza kuyafikia makundi ya kigaidi kutokana na hali ya usalama isiyo imara ya Somalia.
Siku ya Jumatatu, mawaziri wa mambo ya nje wa Somalia, Misri, na Eritrea pia walikutana pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na kuahidi "kufikia malengo na maslahi ya pamoja."
Unaweza pia kusoma
Tanzania: Viongozi wakuu wa Chadema waachiwa na polisi

Chanzo cha picha, AFP
Viongozi wakuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA wameachiwa huru na polisi baada ya kukamatwa jana wakijaribu kuandamana kupinga matukio ya watu kukamatwa,kutekwa,kupotezwa na kuuawawa.
Polisi walizima maandamano hayo yaliyokuwa yameitishwa na mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe mjini Dar es Salam.
Unaweza pia kusoma
Mshukiwa aliandika maelezo ya 'kumuua Trump' kitambo kabla ya jaribio lake

Chanzo cha picha, Reuters/Getty Images
Mtu anayeshukiwa kuwa na bunduki aliyekamatwa karibu na uwanja wa gofu wa Donald Trump aliandika barua miezi kadhaa nyuma akisema alikusudia kumuua rais huyo wa zamani, ripoti ya mahakama inaonyesha.
"Hili lilikuwa jaribio la kumuua Donald Trump," barua hiyo inasema.
Waendesha mashtaka walijumuisha barua hiyo katika jalada la mahakama siku ya Jumatatu, na walisema watajaribu kumfungulia mashtaka Ryan Routh mwenye umri wa miaka 58 kwa jaribio la kumuua mgombeaji mkuu wa kisiasa.
Routh amekuwa kizuizini tangu kukamatwa kwake tarehe 15 Septemba huko Florida.
Routh hadi sasa anakabiliwa na mashtaka mawili ya uhalifu ikiwa ni pamoja na kumiliki bunduki kama mhalifu aliyepatikana na hatia.
Waendesha mashtaka, hata hivyo, walisema mahakamani kwamba wangeomba baraza kuu la mahakama katika siku zijazo pia kumshtaki Routh kwa uhalifu mkubwa zaidi wa kupanga kumuua mgombeaji wa kisiasa, wakisema kwamba ushahidi unaonyesha kwamba alikuwa akipanga njama ya kumshambulia Trump.
Soma zaidi:
Mashambulizi ya Israel yaua watu 492 Lebanon

Chanzo cha picha, Reuters
Israel inasema ilifikia maeneo lengwa 1,300 ya Hezbollah na kuwataka raia kutoroka maeneo ya karibu na kwenye silaha za kundi hilo.
Mashambulizi ya anga ya Israel yauwa watu 492 nchini Lebanon
Takriban watu 492 wameuawa katika mashambulizi makali ya anga ya Israel yakulenga Hezbollah nchini Lebanon, wizara ya afya ya nchi hiyo inasema, siku mbaya zaidi ya vita katika kipindi cha takriban miaka 20.
Maelfu ya familia pia zimekimbia makwao huku jeshi la Israel likisema maeneo lengwa yalikuwa 1,300 ya Hezbollah katika operesheni ya kuharibu miundombinu ambayo kundi hilo lenye silaha lilijenga tangu vita vya 2006.
Wakati huo huo, Hezbollah, ilirusha zaidi ya roketi 200 kaskazini mwa Israel, kulingana na jeshi.
Wahudumu wa afya walisema watu wawili walijeruhiwa na vipande vya makombora.
Mataifa yenye nguvu duniani yamekuwa yakisisitiza kujizuia huku pande zote mbili zikionekana kukaribia kuelekea kwenye vita kamili.
Wizara ya afya ya Lebanon imesema watoto 35 na wanawake 58 ni miongoni mwa waliofariki, huku wengine 1,645 wakiwa wamejeruhiwa.
Haikuripoti ni wangapi kati ya waliouawa walikuwa raia au wapiganaji.
Waziri wa Afya Firass Abiad alisema maelfu ya familia pia wametoroka makwao kwasababu ya mashambulizi hayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea kusikitishwa kwake na hali inayozidi kuwa mbaya na kusema hataki Lebanon "igeuke Gaza nyingine".
Mkuu wa maswala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema "kuongezeka kwa mashambilizi hayo ni hatari sana na kunatia wasiwasi" kabla ya mkutano wa viongozi wa dunia katika Umoja wa Mataifa mjini New York, akiongeza kuwa "tunakaribia kutumbukia kwenye vita kamili".
Rais Joe Biden alisema Marekani ilikuwa "inashughulikia kupunguza kasi kwa njia ambayo inaruhusu watu kurejea nyumbani salama", wakati Pentagon ikitangaza kuwa inatuma "idadi ndogo" ya wanajeshi wa ziada Mashariki ya Kati "kutokana na tahadhari" kubwa.
Soma zaidi:
Ni wakati mwingine tena nakukaribisha katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 24/09/2024
