Tanzania: Tathmini ya hotuba ya Rais Samia: “Kwenye msiba, huwezi kumpangia mtu alieje”

.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Tanzania

Maelezo ya picha, Rais Samia Suluhu Hassan
    • Author, Sammy Awami
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Tanzania
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Wachambuzi wa siasa wameonesha kushangazwa kwa kiasi fulani na ukosoaji wa Rais Samia Suluhu Hassan juu ya hisia za umma kuhusiana na tukio la kutekwa na kisha kuuawa kwa kiongozi mwandamizi wa chama cha upinzani Chadema Ali Mohamed Kibao.

Katika kufunga mkutano mkuu wa maafisa waandamizi wa jeshi la polisi na maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi hilo mkoani Kilimanjaro Rais Samia alikosoa ukubwa wa hisia zilizotolewa juu ya tukio hilo na kusema uhai wa kila mtu ni wa thamani.

“Kifo cha ndugu yetu Kibao kimeibua wimbi kubwa, kulaani, kusikitika, kulaumu, kuita serikali ya wauaji, kufanyaje, hii sio sawa,” alisema Rais Samia.

Mtazamo huo wa Rais Samia haukutarajiwa na wengi, hasa baada ya tamko lake kupitia mtandao wa ‘X’ ambapo pamoja na kukemea tukio hilo, alitaka mamlaka zifanye uchunguzi.

“Kwenye msiba, huwezi kumpangia mtu analiaje. Kila mtu anavyosikia maamivu anajua namna ya kuomboleza. Katika hali ya kawaida, wale wanaopaza sauti ndiyo wanasababisha kujulikana kwamba tatizo lipo” anasema Fulgence Massawe, Mkurugenzi wa uchechemuzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Massawe ameongeza kwamba tukio la Kibao limekuwa kama sura tu ya matukio mengine yaliyotokea pasipo majibu, na kuwaonesha watu wengi kwamba inawezekana hicho ndicho kilichowapata watu wengine wasiojulikana waliko.

Mwandishi wa habari mwandamizi, Jesse Kwayu amekumbusha kuwa umma umekuwa ukikemea matukio mengi ya utekaji na kupotezwa kwa watu zaidi ya tukio la Kibao.

“Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) walipata kutoa taarifa yao wakionesha orodha ya watu takribani themanini na nne hivi. Lakini watu wa Chadema pia walipata kuleta hadi mashuhuda wa ndugu zao waliofanyiwa matendo yale. Kwa hiyo si jambo moja tu hili. Hili la mzee Kibao ni kama limeongeza tu chumvi kwenye kidonda ambacho tayari kilikuwepo,” amesema Kwayu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo, wafuatiliaji hawa wa masuala ya kisiasa na kijamii wanasema inawezekana mtazamo wa Rais Samia unatokana na taarifa alizonazo ambazo umma kwa ujumla hauna.

“Yawezekana alivyokuja kwenye jukwaa tayari alikuwa ana taarifa nyingi ambazo si nzuri, si za kufurahisha zinazogusa pengine ulinzi na usalama na amani ya nchi. Inawezekana sasa kama binadamu, taarifa hizo zilimfanya kughafirika na hata kushindwa kutimiza majukumu yake kama mfariji mkuu (wa taifa),” amesema Dkt. Richard Mbunda, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mhadhiri mwingine wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Muhidin Shangwe, ambaye kwa udadisi wake anasema uchaguzi wa maneno, aina ya sauti na lugha ya mwili vinamuaminisha kwamba Rais Samia alikemea zaidi hisia za umma na wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa kuliko jeshi la polisi linaloshutumiwa kuhusika na kutokuchukua hatua za kutosha kukawapa wahalifu na kudhibiti matukio ya utekaji.

Je, watekaji wameingia hofu?

“Kama wewe ni mtekaji, baada ya kuiskiliza hotuba ya jana, umeingiwa hofu kwamba unatafutwa? Kwamba siku zako zinahesabika? Kwamba utakiona cha mtema kuni kwa uovu unaoufanya?” amehoji Shangwe.

Ufafanuzi wa Rais Samia juu ya uwepo wa sheria za zamani kando na 4R pia umeelezwa kubeba wasiwasi wa kurudi enzi iliyopita iliyosababisha kutambulishwa kwa 4R zenyewe.

“Mimi nilidhani dhamira ya 4R kwanza ingelenga kurekebisha sheria ambazo zilitufikisha hapo tulipokuwa. Sasa inaonekana 4R zimekuwa kama hisani tu bila kulenga kukata mzizi wa fitna. Ni kama Rais anasema ‘haya niliyoyafanya nimefannya kwa uungwana wangu tu, lakini mkijifanya kuota mikia tutarudi, sheria zipo pale pale’. Sasa hiyo inatia hofu,” amesema Dkt. Shangwe.

Hata hivyo, Dkt. Mbunda anaiona falsafa ya 4R ikiwa imejikita kwenye dhana ya utawala bora ambayo anaamini haiwezi kutolewa kama hisani tu na kuondolewa kirahisi.

“Watu wana haki ya kulalamika na kuelezea hisia zao, kufanya maandamano ya amani, kwa mfano juu ya haya matukio ya hivi karibuni ya utekaji kwa sababu ni kinyume cha Katiba. Kwa hiyo utagundua kwamba hakuna hisani wanayofanyiwa, wapo katika misingi ya sheria’” anasema Mbunda.

Kwayu anasema ni vyema Rais Samia akakumbuka sababu za yeye kuja na 4R zilizochangiwa na mazingira ya kisiasa yaliyokuwepo wakati ule.

“Hizo 4R alikuja nazo yeye kwa sababu alijua mazingira anayotaka kutujengea. Watu walishangilia kwa sababu walijua ametambua nchi alivyoikuta alipochukua madaraka. Sasa leo akituambia kwamba 4R zisichukuliwe kama kisingizio, hatusemi kwamba ni kisingizio, tunasema tu kwamba mfumo na utawala wa sheria utamalaki. Kwa sababu 4R ziwepo au zisiwepo, utawala wa sheria lazima uwepo” amefafanua Kwayu.

Mitazamo hii ya wachambuzizo wa siasa ni ishara tosha kuwa mjadala juu ya utekaji na mauaji ya watu hauwezi kuhitimishwa haraka bila hatua madhubuti kuchukuliwa kukomesha hali hii inayoleta hofu katika jamii.