Pavel Durov: Bilionea mwanzilishi wa Telegram aliyekamatwa Ufaransa ni nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa sababu ya wasifu wake katika teknolojia, utajiri wake na umri wake, wengi wamembatiza Pavel Valeryevich Durov jina la "Mark Zuckerberg wa Urusi."
Durov aliunda mitandao miwili ya kijamii, wa kwanza ni VKontakte - mtandao mkubwa zaidi wa kijamii nchini Urusi ambao aliuanzisha akiwa na umri wa miaka 22 - na mwingine ni ule unaotumika ulimwenguni kote wa Telegramu.
Ni mfanyabiashara mashuhuri mwenye umri wa miaka 39. Kwa mujibu wa Forbes, utajiri wake unafikia dola za Marekani bilioni 15.5.
Lakini mwisho wa wiki, mamlaka za Ufaransa zilimshikilia bilionea huyo muda mfupi baada ya ndege yake ya binafsi kutua katika uwanja wa ndege wa Le Bourget mjini Paris. Durov anashutumiwa kwa kushindwa kuchukua hatua za kuzuia matumizi ya kihalifu ya Telegram.
Wachunguzi wa Ufaransa walitoa hati ya kukamatwa kwa Durov kama sehemu ya uchunguzi wa madai ya ulaghai, ulanguzi wa dawa za kulevya, uhalifu uliopangwa, utakatishaji fedha, kuendeleza ugaidi na unyanyasaji wa kingono kwa watoto.
Vyombo vya sheria nchini Ufaransa vinasema Durov anahusika katika uhalifu huu kwa sababu amekataa kudhibiti maudhui ya jukwaa lake. Bilionea huyo anaweza kukabiliwa na mashtaka ya uhalifu nchini Ufaransa.
Telegram inasema nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili jioni, Telegram ilisema "inatii sheria za Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Huduma za Kidijitali na udhibiti wa maudhui yake umo ndani ya viwango na unaendelea kuboreshwa."
"Mkurugenzi Mtendaji wa Telegram, Pavel Durov hana chochote cha kuficha na mara nyingi husafiri kuzunguka Ulaya. Ni upuuzi kudai kwamba jukwaa au mmiliki wake wanawajibika kwa matumizi mabaya yanayofanywa kwenye jukwaa hilo. Tunasubiri suluhu la haraka la hali hii," iliongeza taarifa hiyo.
Janis Sarts, mkurugenzi wa Kituo cha Mawasiliano ya Kimkakati cha NATO, ameliambia shirika la habari la LETA, ingawa katika hatua hii ni vigumu kujua kwa nini Ufaransa imeamua kumshikilia Durov, lakini ni jambo lisilopingika kwamba Telegram imekuwa ikitumika kwa kila aina ya uvunjaji wa sheria.
Kwa upande wake, wakili wa Durov, Dmitry Agranovsky, anasema kukamatwa huko ni "ujinga kabisa na shambulio la uhuru wa kujieleza.”
Durvo ni nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Durov alizaliwa mwaka 1984 huko Leningrad (sasa ni Saint Petersburg) na anaishi Dubai, ambako ndiko kwenye makao makuu ya Telegram. Mbali na uraia wa Urusi na UAE, pia ana pasipoti ya Ufaransa.
Akiwa mtoto alisoma shule ya St. Petersburg Academic Gymnasium. Shule yenye heshima kwa masomo ya sayansi na hisabati. Kisha akasoma kompyuta na hesabu katika chuo kikuu cha Saint Petersburg State University.
Katika mahojiano ya mapema mwaka huu, Durov alisema, Telegram inapaswa kubakia bila kuwa na upande na kutojihusisha na siasa za kikanda.
Profesa wa zamani wa MIT, Douglas C Youvan katika kitabu kuhusu mwanzilishi wa Telegram kiitwacho The Russian Jesus: A Beacon of Digital Freedom in an Age of Surveillance, anasema:
“Anajulikana kwa mtindo wake wa maisha ya kutopenda anasa, kujiepusha na pombe, kafeini na vyakula vilivyochakatwa, na kufuata sheria kali za binafsi zinazozingatia afya ya akili na afya ya mwili."
Kulingana na Forbes, Durov, mwenye watoto watano kutoka kwa wapenzi wake wawili wa zamani, hivi karibuni alidai kuwa alitoa mbegu za kiume ambazo zilimruhusu kuzaa watoto 100.
Mvutano na Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Telegram ina watumiaji milioni 900 walio hai kila mwezi na imeorodheshwa kama moja ya majukwaa ya kijamii yanayoongoza baada ya Facebook, YouTube, WhatsApp, Instagram, TikTok na Wechat.
Mtandao huo ndio mwasisi wa kutuma ujumbe kwa njia fiche. Kipengele ambacho mitandao mengine ya kijamii imeamua kukitumia pia.
Durov alikuja la kipengele cha jumbe fiche alipokuwa akikabiliwa na shinikizo kutoka kwa mamlaka ya Urusi kukabidhi data binafsi za watumiaji wa Ukraine wa mtandao wa kijamii wa Vkontakte - toleo la Kirusi la Facebook - na kutakiwa kuyaondoa makundi yanayokosoa Moscow.
Ujumbe fiche unamaanisha kuwa ujumbe unaweza kusomwa tu kwenye kifaa unachotumia kutuma na kifaa kinachopokea hiyo taarifa.
Na kukataa kutoa data kwa serikali ya Urusi, kulimfanya aondoke nchini mwake mwaka 2014 na kuacha kusimamia mtandao wa VK. Kuanzia wakati huo, jitihada zake zikaigeukia Telegram, ambayo aliianzisha na ndugu yake Nikolai mwaka 2013.
Kwenye mtandao huu, pamoja na kuwasiliana moja kwa moja, watumiaji wanaweza kujiunga na vikundi vyenye watu hadi 200,000.
Nchini Uingereza, kwa mfano, programu hiyo ilichunguza chaneli za mrengo wa kulia ambazo zilisaidia kuandaa ghasia katika miji ya Uingereza mapema mwezi huu.
Telegram iliondoa baadhi ya vikundi, lakini kwa ujumla mfumo wake wa kudhibiti maudhui yenye misimamo mikali na haramu ni dhaifu sana kuliko ule wa makampuni mengine ya mitandao ya kijamii, wataalamu wa usalama wa mtandao wanasema.
Baada ya kukamatwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Kukamatwa huko kulizua utata. Wengi wanasema Durov ni mtetezi wa uhuru wa kujieleza na faragha, wengine walizungumzia uhusiano wake wa karibu na Kremlin.
Mtaalamu wa mtandao Dmytro Zolotukhin alibainisha katika taarifa zilizoripotiwa na BBC Monitoring kwamba, tofauti na watu wengine mashuhuri ambao walikana uraia wa Urusi na baadaye kuandamwa na Kremlin, Durov anafurahia ulinzi wa serikali ya Urusi.
"Wizara ya Mambo ya Nje, Bunge na manaibu wanamtetea Durov, pamoja na Mfuko wa Uwekezaji wa Urusi, ambao ni mmiliki mwenza wa Telegram," anasema.
Maafisa kadhaa wa Urusi walilaani kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo, wakisema ilionyesha kuwa nchi za Magharibi zina undumilakuwili linapokuja suala la uhuru wa kujieleza na demokrasia.
Mwingine aliyemtetea ni afisa wa zamani wa ujasusi wa Marekani, Edward Snowden, ambaye alifichua nyaraka za siri zilizofichua kuwepo kwa programu za uchunguzi wa kimataifa, ambaye anaishi uhamishoni nchini Urusi tangu 2013.
Katika akaunti yake ya X, Snowden alibainisha kuwa kukamatwa kwa Durov "ni shambulio la haki za msingi za binadamu za kujieleza na kujumuika."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












