Uchaguzi wa Marekani 2024: Je, muhula wa pili wa Donald Trump utakuwaje?

Chanzo cha picha, EPA
Kwa baadhi ya wachambuzi, wanaamini Rais Donald Trump ataendelea pale alipomalizia mwaka 2020 - mwishoni mwa muhula wake wa kwanza wa urais.
Mradi mmoja ambao haujakamilika ni kufunga mpaka wa kusini mwa Marekani kwa ujenzi wa ukuta - sera hii ya muhula wake wa kwanza; haikuweza kupata idhini ya Congress ya ufadhili, ambao aliuhitaji ili kujenga ukuta.
Anatarajiwa kutimiza ahadi yake ya kukamilisha ujenzi wa ukuta.
Kuwafukuza wahamiaji

Chanzo cha picha, Reuters
Rais Trump pia ana uwezekano wa kutafuta uungwaji mkono wa bunge kuhusu mpango wake wa kuwatimua watu wengi ambao hawana vibali vya kisheria vya kuwa nchini humo.
Makadirio ya Kituo cha Utafiti cha Pew, yanasema kuna wahamiaji wasio na vibali wapatao milioni 11 nchini Marekani hadi 2022, ingawa Trump na timu yake ya kampeni anadai kuna mamilioni.
Wataalamu wanaonya kuwa uhamisho wowote wa watu wingi kutoka kundi la wahamiaji utakuwa wa gharama kubwa na vigumu kuutekeleza, na unaweza kuwa na athari mbaya katika maeneo ya uchumi ambayo watu hao wanafanya kazi.
Donald Trump alipokubali uteuzi wa Chama cha Republican kama mgombea urais mwezi Julai, aliahidi "kumaliza mfumuko wa bei mara moja, kupunguza viwango vya riba na kupunguza gharama ya nishati."
Ni marekebisho makubwa zaidi ya kodi katika miongo kadhaa, yenye lengo la kurahisisha kanuni za kodi na kukuza uwekezaji. Lakini punguzo hilo liliwanufaisha zaidi wafanya biashara na matajiri.
Vita vya biashara
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Pia anataka kuchimba mafuta zaidi kwani anaamini gharama ya juu ya mafuta imechangia mfumuko wa bei, na kufanya hivyo kutapunguza gharama za nishati.
Pia anasema ana mpango wa kutoza ushuru wa 10% -20% kwa bidhaa nyingi za kigeni huku bidhaa kutoka China zikibeba ushuru mkubwa wa 60%. Wanauchumi wengi wanaonya, hatua kama hizo zitaishia kulipwa na watumiaji wa bidhaa wa Marekani kwa kununua bidhaa hizo kwa bei ya juu.
Katika muhula wake wa kwanza, Rais Trump alianzisha vita vya kibiashara na Beijing, akiishutumu China kwa mifumo isiyo sawa ya biashara na wizi wa mawazo.
Hata hivyo, muundo wa Bunge la Marekani bila shaka utaamua iwapo ataweza kutimiza sera zake kwa njia anayotaka.
Inafaa kukumbuka kuwa katika miaka ya 2017-2019, Warepublican walikuwa na udhibiti wa Seneti na Baraza la Wawakilishi.
Lakini wakati huo, Trump alionekana kutofahamu kazi za Congress na hiyo ilizuia uwezo wake wa kuongeza faida kwa Republican katika Ikulu ya White House.
Kwa vile Warepublican wameweza kupata udhibiti wa Seneti mara hii, utawala wa Trump unatarajiwa kufanya kazi katika njia zote ikiwa unataka kupata ufadhili wa usalama wa mpaka, kukamilisha ukuta na kupunguza ushuru.
Marufuku ya kutoa mimba
Wakati wa muhula wake wa kwanza, Trump alisimamia uteuzi wa majaji watatu wa Mahakama ya Juu ambao walikuwa muhimu katika kutengua haki ya kikatiba ya utoaji mimba. Kwa hivyo wengi wanajiuliza kipi - rais mpya anaweza kukifanya wakati wa muhula wake wa pili.
Alisema wakati wa mjadala wake wa televisheni wa Septemba na Kamala Harris kwamba hatatia saini marufuku ya utoaji mimba kwa nchi nzima kwani "hakuna sababu ya kutia saini marufuku hiyo, kwa kuwa tumepata kile ambacho kila mtu anakitaka.”
Mambo ya Nje
Kuhusu sera ya mambo ya nje, muhula wa pili wa Rais Trump huenda ukafanana na ule wake wa kwanza – kuiweka kando Marekani na mizozo ya duniani.
Anasema atavimaliza vita nchini Ukraine "ndani ya saa 24" kupitia maafikiano na Urusi.
Trump amejiweka kama muungaji mkono mkuu wa Israel, lakini hajasema mengi kuhusu jinsi atakavyomaliza vita huko Gaza.
Jamie Shea, afisa wa zamani wa Nato na sasa profesa wa mikakati na usalama katika Chuo Kikuu cha Exeter, anasema mtindo wa Rais Trump wa muhula wa kwanza ulikuwa wa kutatanisha.
"Hakujiondoa katika Nato, hakuwaondoa wanajeshi wa Marekani kutoka Ulaya na alikuwa rais wa kwanza wa Marekani kutoa silaha kwa Ukraine."
Donald Trump ndiye rais wa pili tu katika historia ya nchi hiyo kuhudumu mihula miwili isiyokuwa mfululizo.
Aliyetangulia alikuwa Grover Cleveland, ambaye alikuwa ofisini kati ya 1885 na 1889, alishindwa kuchaguliwa tena na miaka minne baadaye akaingia tena Ikulu kati ya 1893 na 1897.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












