Kwa nini Pakistan na Iran zinashambuliana, na kwa nini hili linatokea sasa?

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Roohan Ahmed

BBC News, Islamabad

Watu tisa wamethibitishwa kufariki kutokana na mashambulizi ya anga ya Pakistan yaliyolenga maficho ya wanamgambo katika mkoa wa Sistan na Baluchistan nchini Iran Alhamisi asubuhi.

Ofisi ya masuala ya kigeni ya Pakistan imeyaelezea mashambulizi hayo asubuhi ya Alhamisi (Januari 18) kama "shambulio la kijeshi lililoratibiwa sana dhidi ya kambi maalum nchini Iran" na jeshi la Pakistan limesema katika taarifa yake kwamba "mashambulizi ya makundi ya kigaidi yalifanikiwa katika operesheni ya kijasusi".

Mashambulizi hayo yanafuatia mashambulizi ya makombora ya Iran dhidi kundi la kigaidi la Jaish al-Adl linalodaiwa kujificha katika jimbo la Balochistan nchini Pakistan. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, watoto wawili waliuawa na wasichana watatu kujeruhiwa katika shambulio la Iran, ambalo lilisababisha Pakistan kumrejesha nyumbani balozi wake kutoka Tehran.

Licha ya mashambulizi hayo, kila nchi inasisitiza kuwa nyingine sio lengo lililokusudiwa; Iran na Pakistan zote zinadai kuwa zinashambulia makundi ya wanamgambo wa kizalendo wa Baloch wenye makao yake katika eneo la nchi nyingine.

Tunafahamu nini kuhusu mashambulizi ya Pakistan?

f

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Watu wakiwa wamesanyika karibu na vifusi baada ya shambulizi la kijeshi la Pakistan katika kijiji cha Iran katika majimbo ya Sistan na Baluchestan

Jeshi la Pakistan limesema kuwa, wakati lilipokuwa likishughulikia taarifa za kijasusi, limelenga kambi za Jeshi la Ukombozi la Balochistan (BLA) na lile la Balochistan Liberation Front (BLF) nchini Iran, makundi ambayo yanatuhumiwa kwa vitendo vya kigaidi ndani ya Pakistan.

Jeshi linasema ndege zisizo na rubani, roketi, makombora na silaha nyingine zilitumika katika operesheni hii, na tahadhari kali ilichukuliwa ili kuepuka 'uharibifu wa jumla'.

Taarifa hiyo imewataja baadhi ya "magaidi" ambao walidhibiti kambi hizo na kusema kuwa jeshi la Pakistan daima liko tayari kuhakikisha usalama wa nchi hiyo.

Naibu Gavana wa masuala ya usalama wa jimbo la Sistan-Baluchestan nchini Iran, Ali Raza Marhmati, amekiambia kituo cha televisheni cha Iran kuwa shambulio hilo lilitekelezwa saa kumi na dakika 5 za asubuhi na kulenga kijiji kimoja karibu na mji wa Iran wa Saravan, ambao uko karibu na mpaka wa Pakistan na takriban kilomita 1800 kusini mashariki mwa mji mkuu wa Iran Tehran.

Jeshi la Ukombozi wa Baloch, (Baloch Liberation Front) na Jaish al-Adl ni akina nani?

f
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mashirika kadhaa ya Baloch yanayotaka kujitenga yamekuwa yakishiriki katika jimbo la Balochistan nchini Pakistan kwa miongo kadhaa, na mashirika haya yamedai kuhusika na mashambulizi kadhaa ya kigaidi dhidi ya vikosi vya usalama vya Pakistan, polisi na maeneo muhimu.

Makundi mawili makubwa ni BLF, linayoongozwa na Dk Allah Nazar Baloch, na BLA, ambalo kiongozi wake ni Bashir Zeb.

Maafisa wa Pakistan wamekuwa wakidai kwa miaka michache iliyopita kwamba wanamgambo wanaohusishwa na makundi haya yanayotaka kujitenga wamekimbilia nchini Iran.

Baada ya mashambulizi ya anga ya Pakistan, BLF ilitoa taarifa ikikanusha kwamba kundi hilo lilikuwa na kambi yoyote nchini Iran au kwamba wapiganaji wake wote wamejeruhiwa.

BLF linajulikana kuwa hai ndani na karibu na eneo la Makran la Balochistan na limedai kuhusika na mashambulizi kadhaa dhidi ya vikosi vya usalama vya Pakistan katika siku za hivi karibuni.

Mnamo Januari 2022, shirika hili lililopigwa marufuku lilishambulia kituo cha ukaguzi cha jeshi cha Pakistan katika mji wa Gwadar, Balochistan, ambapo wanajeshi 10 wa Pakistan waliuawa.

Aidha, BLF pia limeshutumiwa kwa mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wahamiaji na wakazi katika jimbo hilo.

g

Chanzo cha picha, BLA/BLF

Maelezo ya picha, Dk Allah Nazar Baloch (kushoto) na Bashir Zeb (kulia)

Kundi linapigania kujitenga la BLA ilianza kutumika katika miaka ya 1970 wakati uasi wa silaha dhidi ya jimbo la Pakistan ulipozuka huko Balochistan wakati wa muhula wa kwanza wa serikali ya Waziri Mkuu wa zamani Zulfikar Ali Bhutto.

Baada ya mapinduzi yaliyoongozwa na dikteta wa kijeshi Zia ul-Haq, mazungumzo na viongozi wa kizalendo wa Baloch yalisababisha kumalizika kwa muda kwa uasi wa silaha na shughuli za BLA zilipungua.

Hata hivyo, mgogoro huo ulitawala chini ya rais wa zamani Pervez Musharraf, baada ya kiongozi wa kizalendo wa Baloch, Nawab Khair Bakhsh Murri, kukamatwa kwa mauaji ya jaji wa Mahakama Kuu. Mfululizo mpya wa mashambulizi dhidi ya vituo vya serikali na vikosi vya usalama katika maeneo tofauti ya Balochistan ulianza mwaka 2000, ghasia ambazo zimeongezeka na kuenea katika maeneo tofauti ya Balochistan.

Mashambulizi haya mengi yaliendelea kudaiwa na kutekelezwa na BLA, na serikali ya Pakistan ililiongeza kundi la BLA kwenye orodha ya mashirika yaliyopigwa marufuku mwaka 2006.

Shirika hilo pia limekuwa likipinga mradi wa China-Pakistan wa Ushoroba wa kiuchumi (Economic Corridor) na limeshambulia maeneo ya China nchini Pakistan kwa mashambulizi ya kujitoa muhanga katika operesheni za hivi karibuni.

Shambulio la kwanza la aina hiyo lililodaiwa kufanywa na BLA mwezi Agosti 2018 lilitekelezwa karibu na mji wa Dalbandin, na lililenga basi lililowabeba wafanyakazi wa China katika mgodi wa dhahabu na shaba wa Saindak. Ni mshambuliaji pekee aliyeuawa katika shambulio hilo.

Kundi la BLA lililopigwa marufuku lilidai kuhusika na shambulio hilo katika ubalozi mdogo wa China mjini Karachi mwezi Novemba 2018, ambalo lilitekelezwa na watu watatu wenye silaha na walipuaji wa kujitoa muhanga na kuwaua watu wengine wanne.

f

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Iran ilirusha makombora yanayofanana na haya (hapa yanaonekana katika mazoezi) katika kambi za wanamgambo nchini Pakistan

Jaish al-Adl (au "Haki kwa ajili ya Usawa") ni kundi la wanamgambo wenye silaha ambalo linaipinga serikali ya Iran.

Kundi hilo, ambalo linajielezea kama "mtetezi wa haki za Wasunni" katika jimbo la Sistan-Baluchestan nchini Iran, lilikuwa lengo la mashambulizi ya Iran dhidi ya Pakistan.

Jaish al-Adl limedai kuhusika na mashambulizi kadhaa dhidi ya vikosi vya usalama vya Iran katika siku za nyuma (hasa katika jimbo la Sistan-Baluchestan), na Iran inadai kuwa linaungwa mkono na Marekani na Israel.

Idara ya ujasusi ya Marekani imelihusisha kundi hilo na shambulio dhidi ya rais wa zamani wa Iran Mahmoud Ahmadinejad mwaka 2005.

Mwaka 2009, Iran ilimkamata Abdolmalek Rigi, mkuu wa kundi la wanamgambo, kwa tuhuma za kuvishambulia vikosi vya usalama vya Iran na kuwa kibaraka wa Uingereza na Marekani. Aliuawa kwa kunyongwa mwaka 2010.

Mohammad Abbasi, mwanadiplomasia wa zamani wa Pakistan aliyetumwa nchini Iran wakati huo, alisema kuwa Pakistan ilihusika sana katika kukamatwa kwa Rigi.

Kwa nini haya yanatokea sasa?

Mchambuzi Syed Mohammad Ali ameiambia BBC kwamba kwa sasa Iran iko chini ya shinikizo - ndani na kutoka kwa washirika wake Hamas, Hezbollah na Wahouthi - kufanya operesheni.

Kwa maoni yake, Iran imeshambulia nchini Iraq, Syria na kisha Pakistan ili kuondoa umakini wa masuala ya ndani na hali katika Mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, usiku ambao mashambulizi hayo yalitekelezwa, kulikuwa na mikutano kati ya maafisa wa Pakistan na Iran, lakini Pakistan ilishambuliwa na Iran bila ya uchokozi, hali iliyoifanya Iran ilipize kisasi.

Dr Kamran Bukhari wa taasisi ya New Lines Institute for Strategy and Policy mjini Washington anasema kuwa "Pakistan inaweza kuwa imeamua kulipiza kisasi kwa sababu hawataki kuiruhusu Iran kuwa na tabia na Pakistan kama Iran inavyofanya mara nyingi na Iraq."

Profesa Qandeel Abbas wa Idara ya Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Quaid-e-Azam ameiambia BBC kuwa kuna maeneo katika pande zote mbili za mpaka wa Iran na Pakistan ambapo waasi na wanamgambo wanaleta changamoto ya pamoja kwa nchi zote mbili.

Kwa mujibu wa Prof Abbas, Iran na Pakistan zimechukua hatua dhidi ya wanamgambo katika mpaka huo baada ya kuafikiana juu ya mashambulizi hayo, ingawa mamlaka za nchi zote mbili hazithibitishi wala kukanusha taarifa za hatua hiyo.

Anabainisha kuwa hakuna wanajeshi waliopelekwa katika mpaka wa kilomita 1,000 kati ya Iran na Pakistan hadi mwaka 2013, licha ya ghasia za wanamgambo, biashara ya watu na biashara ya madawa ya kulevya.

Kwa mujibu wa Prof Abbas, Pakistan na Iran zinalichukulia kundi hilo la wanamgambo ambalo Iran inalilenga, Jaish al-Adl, kama tisho, na kwa sasa wanafikiria kutumia hali ya sasa kwa faida yao.

Nini kitatokea baada ya hapo?

g
Maelezo ya picha, Wapakistan wamekuwa wakifuatilia kwa karibu matukio

Waangalizi wanaofuatilia kwa karibu masuala ya Iran na Pakistan wanaamini kuwa mvutano wa hivi karibuni kati ya nchi hizo mbili utakuwa na athari mbaya kwa eneo lote.

Mchambuzi wa masuala ya siasa za Marekani Dkt Bukhari ameiambia BBC kwamba "rawamu ya kwanza kati ya nchi hizo mbili imekwisha na sasa jumukumu limebaki tena kwa mahakama ya Iran: jinsi wanavyoitikia hatua ya Pakistan bado inaonekana," lakini anatarajia kusitishwa kwa mashambulizi hayo.

Alisema uamuzi wa Pakistan wa kuyalenga makundi ya wanamgambo wanaoipinga Pakistan katika ardhi ya Iran badala ya Wairan unaweza kuiruhusu Pakistan kuonekana ikijibu bila kuzidisha mapigano zaidi, lakini anasema uwezekano wa mapigano zaidi pia unawezekana.

Hata hivyo, Baqir Sajjad, mwandishi wa habari na mchambuzi kutoka Pakistan, anaamini kwamba mvutano kati ya nchi hizo mbili unaweza kuongezeka zaidi katika siku zijazo.

Ameiambia BBC kwamba "inaonekana kuwa kuna uwezekano kwamba mvutano kati ya nchi hizo mbili utapungua ghafla baada ya shambulio la Pakistan la kuwalenga wanamgambo wa Iran."

"Wapiganaji wa Iran wanasisitiza kulipiza kisasi dhidi ya Pakistan. Kuongezeka kwa kutoaminiana kati ya nchi hizo mbili kunaweza kuchochea wimbi jipya la harakati za kijeshi kati ya Iran na Pakistan katika eneo la Balochistan, na hivyo kuathiri zaidi hali ngumu ya usalama katika eneo hilo."

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi