Je, Jaish al-Adl, kundi linaolengwa na Iran nchini Pakistan ni akina nani?

g

Chanzo cha picha, JEISH ALADL

Maelezo ya picha, Jaish al-Adl ni kundi la wanamgambo wa Sunni lenye harakati mkubwa na ushawishi katika mji wa Sistan-Baluchestan, kwa mujibu wa ofisi ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa wa Marekani.

Na Shumaila Jaffery

Mwandishi wa BBC, Islamabad

Mashambulizi ya hivi karibuni ya Iran dhidi ya kundi la wanamgambo la Jaish al-Adl nchini Pakistan yamezusha hofu kwamba mzozo wa Mashariki ya Kati utapanuka zaidi ya eneo hilo.

Serikali ya Pakistan imethibitisha kuwa watoto wawili waliuawa na wengine watatu kujeruhiwa.

Ilisema mashambulizi ya hivi karibuni ya makombora "hayakubaliki kabisa" na kuonya juu ya kulipiza kisasi "dhidi ya uvamizi usio na sababu" katika anga yake.

Iran inadai kuwa Jaish al-Adl, kundi la wanamgambo wa Sunni linaloendesha harakati zake katika mpaka wa Pakistan na Iran, linaungwa mkono na Marekani na Israel. Kundi hilo limedai kuhusika na mashambulio kadhaa dhidi ya vikosi vya usalama vya Iran katika siku za nyuma.

Licha ya ukosoaji mkubwa kutoka Islamabad kuhusu shambulio la wiki hii, wachambuzi wanasema kwamba Paksistan inaelewa kwamba vigingi ni vya juu, na itaepuka hatua ya kujibu mashambulio hayo moja kwa moja.

Jaish al-Adl – 'Jeshi la Haki'

Jaish al-Adl au 'Jeshi la Haki na Usawa' ni kundi la wanamgambo wenye silaha ambalo linaipinga serikali ya Iran. Kundi hilo linajielezea kama "mlinzi wa haki za Sunni" katika jimbo la Sistan-Baluchestan nchini Iran.

Mwaka 2009, Iran ilimkamata Abdolmalek Rigi, kiongozi wa kundi la wanamgambo ambalo hapo awali lilijulikana kama Jundullah (Wanajeshi wa Mungu), kwa tuhuma za kuvishambulia vikosi vya usalama vya Iran na kuwa kibaraka wa Uingereza na Marekani. Aliuawa kwa kunyongwa mwaka 2010.

Mwanadiplomasia wa zamani wa Pakistan Mohammad Abbasi aliyetumwa nchini Iran wakati huo, alisema kuwa Pakistan ilihusika sana katika kukamatwa kwa Rigi.

Shirika la ujasusi la Marekani linasema kuwa Jaish al-Adl alihusika katika milipuko kadhaa na mashambulizi nchini Iran, ikiwa ni pamoja na shambulio dhidi ya rais wa zamani Mahmoud Ahmadinejad mwaka 2005.

Operesheni zinazodaiwa kufanywa na Jaish al-Adl zimekuwa zikifanyika katika mkoa wa Sistan-Baluchestan.

Kwa nini Iran imeishambulia Pakistan?

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Makombora ya Iran - yaliyoonekana hapa wakati wa mazoezi ya - yameishambulia Pakistan, Iraq na Syria katika siku za hivi karibuni

Shambulio hilo la anga limekuja siku moja baada ya jeshi la Iran Revolutionary Guards Corp (IRGC) kurusha makombora ya masafa marefu dhidi ya maeneo ya Iraq na Syria.

Hatua hiyo ilikuwa ya kushangaza kwa Pakistan, alisema Mushahid Hussain Sayed, waziri wa zamani na mtaalamu wa sera za kigeni.

"Katika kutathmini kwangu, inaonekana kama - operesheni ya siri ya Jeshi la Mapinduzi la Iran na lazima ionekane kwa mtazamo mpana," alisema waziri huyo wa zamani.

Sayed alieleza kuwa mshambulio hilo ni ukiukaji wa makubaliano ya pande mbili na itifaki za kimataifa na ni sawa na kudhoofisha roho ya umoja wa Kiislamu wakati ambapo anasema "kuna mauaji ya kimbari yanayofanyika Gaza".

Amesema badala ya kuelekeza hasira zake kwa Israel, Tehran imezipiga nchi tatu za Kiislamu ndani ya saa ishirini na nne.

"Unafiki na viwango na upendeleo kama huo unafaa kulaaniwa vikali," aliongeza.

Mvutano kati ya Pakistan na Iran

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kihistoria, uhusiano kati ya Pakistan na Iran umetawaliwa na matukio kadhaa ya kudorora.

Iran ilikuwa nchi ya kwanza kuitambua Pakistan kama taifa huru mwaka 1947 na kuwa na ubalozi wake wa kwanza nje ya nchi. Wote wawili walishirikiana wakati wa Vita Baridi na walikuwa na uhusiano wa kijiografia.

Wakati wa vita vya Indonesia na Pakistan vya mwaka 1965, vita vya silaha kati ya Pakistan na India vilivyotokea kuanzia Agosti 1965 hadi Septemba 1965, Tehran iliiunga mkono Islamabad.

Hata hivyo, Mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979 na kuongezeka kwa ushawishi wa aina ya Uislamu ya Wahabi nchini Pakistan (iliyosababishwa na mgogoro nchini Afghanistan) kutoaminiana kati ya Iran na Pakistan kuliongezeka.

Katika miaka ya 1990, Iran ilishutumiwa kwa kuhamasisha madhehebu ya kidini na washirika wa Kishia nchini Pakistan, wakati Tehran ilikuwa na matatizo na msaada wa Islamabad kwa serikali ya Taliban yenye makao yake Kabul katika muongo mmoja.

Kuongezeka kwa ushirikiano wa Iran na India na ushirikiano wa kimkakati wa Pakistan na Washington kuliwafanya waendelee kusambaratika.

g

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Pakistan na Iran zimekuwa zikilaumiana kwa kuyashambulia makundi ya wanamgambo kwa miaka mingi

Mwaka 2018, wakati Iran ilipotia saini makubaliano na India ya kukabidhi udhibiti wa sehemu ya bandari ya Iran ya Chabahar kwa New Delhi, Islamabad ilikuwa na wasiwasi juu ya hilo.

Hatua hiyo ilitafsiriwa nchini Pakistan kama hatua ya India na Iran ya kupunguza umuhimu wa kimkakati wa bandari ya Gwadar, ambayo ilikuwa kilele cha ushoroba wa kiuchumi wa China na Pakistan.

Kwa mujibu wa Arhama Siddiqa, mtafiti katika Taasisi ya Mafunzo ya Kimkakati Islamabad, uhusiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa katika mwelekeo mzuri tangu 2021.

Hata hivyo, Pakistan inafuatilia hali hiyo kwa tahadhari.

"Haiwezi kuathiri uadilifu wake wa eneo, lakini wakati huo huo haitaki kuanzisha mapigano mengine. Uhusiano kati ya India na Afghanistan unatia wasiwasi. Islamabad haiwezi kumudu kupoteza nia njema ya jirani mwingine," Arhama aliiambia BBC.

Ikram Sehgal, mchambuzi wa masuala ya ulinzi ameiambia BBC kuwa Pakistan imeweza kudumisha uhusiano mzuri na Iran.

Kumekuwa na nyakati ambapo ilikataa kuwa sehemu ya "kambi ya Saudia", hasa mwaka 2015 wakati muungano wa Wasunni unaoongozwa na Saudi Arabia ulipoingilia kati vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen na Pakistan ikakataa kuwa sehemu yake.

Pakistan iliona hatari ya kushiriki katika mgogoro wa kieneo wa kimadhehebu ambao ilihisi unaweza kusababisha makosa mapya katika idadi ya watu wa Kisunni na Kishia ndani ya nchi.

Hata hivyo, mvutano wa hivi karibuni kati ya Iran na Saudi Arabia umepunguza shinikizo kama hilo.

Sehgal anaamini kuwa Iran inatambua kuwa haiwezi kuanza makabiliano mengine na jirani yake wakati inahusika katika migogoro mingine kadhaa ya kikanda. Nchi hiyo pia inakabiliwa na vikwazo vya Marekani.

Anasema Pakistan inapaswa kuchukua hatua dhidi ya makundi ya wanamgambo na haipaswi kuruhusu eneo lake litumike kwa kushambulia nchi nyingine.

"Iran pia inapaswa kuepuka vitendo kama hivyo vya kutisha. Wanapaswa kuwasiliana na kuratibu. Vinginevyo, hatua kama hizo zina uwezo wa kulisababishia vita vingine eneo hilo ambavyo watu wake hawawezi kuvimudu," Sehgal alisema.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi