Jeshi la Pakistan 'lajiandaa kukabili mashambulizi yoyote kutoka Iran'

Jeshi la Pakistan limesema limesalia "katika hali ya utayari wa hali ya juu" baada ya kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi nchini Iran.

Moja kwa moja

Yusuf Jumah and Dinah Gahamanyi

  1. Iran yamwita balozi wa Pakistan baada ya watu tisa kuuawa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kama tumekuwa tukiripoti, kumekuwa na mwitikio wa kidiplomasia kutoka kwa Iran na Pakistan kwa kushambuliana Jumanne na asubuhi ya leo.

    Wizara ya mambo ya nje ya Iran imeitisha mashitaka dhidi ya maafisa wa Pakistan kuhusu suala hilo, nayo Pakistan ikimrudisha nyumbani balozi wake kutoka Iran na kumzuia mjumbe wa Tehran kurejea Islamabad.

    Lakini kuna umuhimu gani kwa mwanadiplomasia mkuu wa Pakistani nchini Iran kuitwa?

    Jibu fupi ni kwamba ni hatua ya kawaida ya kutoridhika, lugha ya diplomasia inayoeleweka kimataifa ambayo inaweka wazi utashi wa kisiasa wa nchi kutaka maelezo au kufukuzwa kwa afisa mkuu wa kigeni.

  2. Arnold Schwarzenegger akamatwa kutokana na kodi ya saa ya kifahari

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Schwarzzeneger

    Arnold Schwarzenegger alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Ujerumani kwa madai ya kushindwa kutangaza saa ya kifahari aliyokuwa akipanga kuipiga mnada kwa ajili ya kutoa misaada.

    Muigizaji huyo wa Hollywood alizuiliwa kwa saa tatu katika uwanja wa ndege wa Munich siku ya Jumatano.

    Uchunguzi wa madai ya kukwepa kulipa kodi ulianzaiswa baada ya kubainika kwamba saa hiyo ilinuiwa kuuzwa ndani ya Umoja wa Ulaya (EU).

    Kulingana na sheria za Umoja wa Ulaya, mtu yeyote anayefika na "pesa au vitu fulani vya thamani" zaidi ya €10,000 (£8,580) lazima atangaze.

    Hata hivyo, chanzo kiliiambia CBS News, mshirika wa BBC wa Marekani, kwamba Schwarzenegger hakuulizwa kujaza fomu ya kutangaza alichobeba.

    Muigizaji, mwanasiasa na mwanaharakati huyo wa mabadiliko ya hali ya hewa hatimaye aliweza kulipa kodi, lakini tu baada ya kukabiliana na matatizo kadhaa.

    Baada ya mashine ya kadi kutofanya kazi, iligundulika kuwa benki ya karibu ilikuwa imefungwa na ukomo wa kutoa ATM ulikuwa chini sana, ikimaanisha kuwa mzee huyo wa miaka 76 alilazimika kusubiri mashine mpya ya kadi kuletwa na maafisa wa forodha, chanzo kilisema.

    Msemaji wa muigizaji huyo aliliambia gazeti la udaku la Ujerumani Bild kwamba tukio hilo la uwanja wa ndege lilikuwa "mzaa uliojaa makosa, lakini ungweza kutengeneza filamu ya kuchekesha ya polisi ".

    Bild ilisema "alichukua tukio hilo kwa utulivu" na picha iliyochapisha ilionyesha Schwarzenegger akitabasamu akipiga picha na kushikilia kisanduku cha saa na barua inayosema " ni ya Austria".

    Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, saa hiyo ilitengenezwa maalum kwa ajili ya nyota ya Terminator na mtengenezaji wa saa wa kifahari Audemars Piguet, ambaye hutengeneza saa ambazo zinaweza kuuzwa kwa mamia ya maelfu ya dola.

    Saa hiyo ilisemekana kupigwa mnada katika chakula cha jioni cha kuchangisha fedha kwa ajili ya The Schwarzenegger Climate Initiative huko Kitzbuhel, Austria, takriban kilomita 89 (maili 55) kutoka Munich, baadaye siku ya Alhamisi.

    Taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hafla hiyo, inayotarajiwa kufanyika katika hoteli ya nyota tano ya Stanglwirt, ilisema "kazi za sanaa, maonyesho yaliyotiwa saini, na uzoefu kutoka kwa ulimwengu wa michezo na filamu" zitauzwa.

    Orodha ya mnada wa saa hiyo, iliyopatikana na Bild, ilisema ni moja kati ya 20 zilizopo, na itajumuisha "picha ya Arnold katika pozi lake la kitambo lenye maneno 'Arnold Classic'". Bei ya kuanzia ya mnada ilikuwa €50,000.

  3. Bobi Wine, Besigye wazuiliwa kabla ya maandamano Uganda

    .

    Chanzo cha picha, Kizza Bisgye X

    Maelezo ya picha, Polisi wameapa kuzuia maandamano yaliyopangwa kupinga hali mbaya ya barabara nchini humo

    Vikosi vya usalama vya Uganda vimezingira nyumba za wanasiasa mashuhuri wa upinzani, kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanyika katika mji mkuu, Kampala.

    Kiongozi mkongwe wa upinzani Kizza Besigye na Bobi Wine, mwimbaji nyota wa zamani ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, wanasema kuwa vikosi vya usalama vinazingira nyumba zao na kuwazuia kuondoka.

    "Wanajeshi waoga na polisi wamezingira nyumba yetu na kutuweka chini ya kizuizi cha nyumbani, lakini maandamano yanaendelea," Bw Kyagulanyi alisema katika mtandao wa X.

    Bw Besigye pia alishiriki chapisho muda mfupi baadaye, huku picha zikionyesha maafisa kadhaa wa usalama wakizuia lango la kuingia nyumbani kwake.

    "Tumezuiliwa nyumbani na waoga! Hakuna kurudi nyuma; tunastahili bora," alinukuu picha hizo.

    Wakosoaji hao wawili wa serikali wamewataka Waganda kuendelea na maandamano yaliyopangwa siku ya Alhamisi ya kuitaka serikali kurekebisha barabara zilizochakaa.

    Polisi wameapa kuzuia maandamano hayo, wakisema kuwa maandamano yaliyoandaliwa na wanasiasa "hayajawahi kuwa ya amani" na yatavuruga mkutano mkuu unaoendelea katika mji mkuu.

    Baadhi ya wajumbe 4,000 wanahudhuria mkutano wa 19 wa Jumuiya ya nchi zisizofungamana na Siasa mjini Kampala.

  4. Bomu lililotegwa katika mkokoteni wa punda laua afisa wa polisi wa Kenya

    .

    Bomu lililokuwa limefungwa kwenye mkokoteni wa punda limeripuka kwenye mpaka wa Kenya na Somalia na kumuua afisa mmoja wa polisi, vyombo vya habari vya ndani vinaripoti.

    Watu wengine wawili walijeruhiwa, kulingana na chapisho kwenye mtandao wa X kutoka gazeti la Nation.

    Inasemekana kwamba punda hao wawili waliokuwa wakivuta mkokoteni walinusurika.

    Maafisa wa polisi walikuwa wakikagua bidhaa zilizokuwa nyuma ya toroli baada tu ya kuvuka hadi Kenya katika eneo la Mandera, ambalo liko kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, wakati bomu lilipolipuka, ripoti zinasema.

    Video inayosemekana kutoka eneo la tukio inaonyesha moshi mkubwa mweusi ukifuka kutoka mahali ambapo mlipuko huo ulitokea. Picha za matokeo zinaonyesha punda aliyejeruhiwa akiwa amesimama.

    Mandera hapo imekuwa ikilengwa na kundi la wanajihadi la al-Shabab lenye makao yake nchini Somalia.

  5. Habari za hivi punde, Jeshi la Pakistan 'lajiandaa kukabili mashambulizi yoyote kutoka Iran'

    Jeshi la Pakistan limesema limesalia "katika hali ya utayari wa hali ya juu" baada ya kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi nchini Iran.

    Katika taarifa, jeshi lilisema mashambulizi yake dhidi ya "maficho ndani ya Iran yanayotumiwa na magaidi" yalikuwa "yenye ufanisi".

    Taarifa hiyo ilisema wanalenga "mashirika ya kigaidi", ambayo ni Jeshi la Ukombozi la Balochistan na Balochistan Liberation Front.

    Iliongeza kuwa azimio la jeshi la "kuhakikisha kwamba uhuru na uadilifu wa eneo la Pakistan dhidi ya ubaya wowote, unabaki bila kutetereka."

    "Kusonga mbele, mazungumzo na ushirikiano unaonekana kuwa wa busara katika kutatua masuala ya pande mbili kati ya nchi hizo mbili jirani," ilisema taarifa hiyo.

  6. Mzozo kati ya Iran na Pakistan: Tunachojua kufikia sasa

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Pakistan imeanzisha mshambulizi ya kulipiza kisasi nchini Iran mapema siku ya Alhamisi, siku mbili baada ya Iran kushambulia ardhi ya Pakistan.

    Waziri wa masuala ya kigeni nchini Pakistan alisema kwamba baadhi ya watu waliuawa katika eneo la Sistan mkoani Balushistan.

    Watu tisa waliuawa kufuatia shambulio hilo kulinga na vyombo vya Habari vya Iran

    Pakistan ilisema mashambulizi yake yamepiga "maficho ya magaidi" katika mkoa wa Sistan-Baluchestan nchini Iran

    Pakistan ilisema ilichukua hatua kwa kuzingatia "intelijensia ya kuaminika ya shughuli kubwa za kigaidi zinazoendelea" na kusema kwamba "magaidi" kadhaa waliuawa.

    Imeongeza kuwa "inaheshimu kikamilifu" mamlaka na uadilifu wa ardhi ya Iran lakini hatua yake ya Alhamisi ilikuwa "dhihirisho la azimio lisiloyumba la Pakistan la kulinda usalama wa taifa lake dhidi ya vitisho vyovyote."

    Pakistan ililaani vikali shambulio la Iran siku ya Jumanne, ambalo lilipiga eneo la jimbo la Balochistan nchini Pakistan karibu na mpaka wa Iran.

    Iran ilisisitiza kuwa mashambulizi yake yalilenga tu Jaish al-Adl, kundi la Waislamu wa kabila la Baloch Sunni ambalo limefanya mashambulizi ndani ya Iran, na sio raia wa Pakistan.

  7. Umoja wa Mataifa waomba ufadhili wa haraka kukabiliana na ukame nchini Ethiopia

    TH

    Chanzo cha picha, AFP

    Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu linasema lina wasiwasi na ukame unaozidi kuwa mbaya nchini Ethiopia na linahitaji fedha zaidi ili kuongeza juhudi za kukabiliana na hali hiyo.

    Ukame umeathiri watu milioni nne katika mikoa yenye migogoro ya Amhara na Oromia, pamoja na Afar na Tigray, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema Jumatano.

    "Migogoro mingi na mara nyingi inayoingiliana imedhoofisha sana uwezo wa watu wa kukabiliana na majanga ya hali ya hewa kama vile ukame - na kuacha mamilioni ya watu wakiwa katika hatari ya kutumbukia katika uhitaji mkubwa na ufukara," Shirika hilo limesema

    Serikali kuu mjini Addis Ababa hapo awali iliondoa hofu ya kutokea baa la njaa, na imesema kuwa inajitahidi kutoa misaada.

    Wiki hii, mamlaka ya Tigray ilifichua kuwa zaidi ya watu 200 walikufa kwa njaa, baada ya onyo mwezi uliopita kwamba eneo hilo "liko karibu na janga la kibinadamu".

  8. Kenya yawakamata polisi wanaohusishwa na utekaji nyara wa raia wa China

    Maafisa watatu wa polisi nchini Kenya wametiwa mbaroni kwa madai kuwa walihusika katika utekaji nyara wa raia wa Uchina na kuitisha kikombozi.

    Maafisa hao wamehusishwa na kitengo maalum cha polisi (GSU).

    Wanadaiwa kumvizia Mchina huyo alipokuwa akiendesha gari kuelekea kazini tarehe 8 Januari, kumfunga pingu na kwenda naye.

    Maafisa hao kisha walimwibia mgeni huyo kabla ya kumwachilia, polisi wanasema.

    Mamlaka pia inamsaka raia wa China anayeaminika kuwa kiongozi wa kundi la utekaji nyara.

    "Kiongozi wa genge hilo aliipigia simu familia ya mwathiriwa Uchina akidai kiasi ambacho hakijathibitishwa cha pesa ambacho kilitumwa kwa akaunti ya benki nchini Uchina," polisi walisema kwenye X.

    "Baada ya pesa kuwekwa, washirika wa genge hilo nchini Uchina walithibitisha kuwa familia ilitii, na mwathiriwa aliachiliwa".

    Polisi wanasema kuwa tukio hilo "limefichua kuwepo kwa kundi la wahalifu la kimataifa ambalo limekuwa likiwalenga watu baada ya kukaguliwa na uwezo wao wa kifedha kufahamika".

    Mamlaka ya Kenya inashirikiana na Interpol kutafuta washirika hao nchini China.

  9. Pakistan yashambulia Iran siku mbili baada ya shambulio la kombora

    th

    Chanzo cha picha, EPA

    Pakistan imesema kuwa imefanya mashambulizi ya makombora katika nchi jirani ya Iran, siku mbili baada ya shambulio la Iran kuzidisha uhasama kati ya mataifa hayo ya nyuklia.

    Pakistan ilisema mashambulizi hayo yamepiga "maficho ya kigaidi" katika eneo la mpakani la Sistan-o-Balochistan.

    Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kuwa wanawake watatu na watoto wanne wameuawa.

    Wawili hao wamekuwa wakilaumiana kwa muda mrefu kwa kuhifadhi makundi ya wapiganaji wanaofanya mashambulizi katika maeneo ya mpakani mwao.

    Siku ya Jumatano jioni, vyombo vya habari vya Iran viliripoti kwamba milipuko kadhaa ilisikika karibu na mpaka na Pakistan, karibu na mji wa Saravan.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ilithibitisha mashambulizi hayo katika taarifa yake, na kusema kuwa "idadi isiyojulikana ya magaidi waliuawa wakati wa operesheni hiyo ya Kijasusi".

    Hatua hiyo ya kijeshi ya Pakistan inajiri baada ya kulaani vikali shambulio la Iran siku ya Jumanne, ambayo ilisema iliua watoto wawili.

    Iran ilisema mashambulizi yake yalilenga kundi la waasi lenye makao yake Pakistan, lakini Pakistan ilisema raia waliuawa.

    Ilikuwa imeionya Tehran juu ya "madhara makubwa" kwa hatua hiyo "haramu" na ikapiga marufuku balozi wa Iran kurejea nchini na pia ilimuondoa mjumbe wake kutoka Pakistan.

    Iran ilisisitiza kuwa mashambulizi yake yalilenga tu Jaish al-Adl, ambayo inalitaja kuwa kundi la kigaidi, na sio raia wa Pakistan.

    Hata hivyo jirani yake wa mashariki alikasirishwa na hatua hiyo.Pakistan ilisema imetokea "licha ya kuwepo kwa njia kadhaa za mawasiliano".

    Siku ya Alhamisi, Pakistan ilitetea mashambulizi yake yenyewe katika ardhi ya Iran, ikisema hatua zake zililenga tu "magaidi" wanaojulikana kama Sarmachars.

    th

    Unaweza pia kusoma

  10. Mwanamke aachiliwa baada ya kupatikana na hatia ya kutoa mimba El Salvador

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mtoto wa kike wa Lilian alifariki chini ya uangalizi wa madaktari, lakini alifunguliwa mashtaka ya kupuuza na mauaji.

    Mwanamke nchini Salvador ameachiliwa kutoka gerezani zaidi ya miaka saba baada ya kupatikana na hatia ya kutoa mimba.

    Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 28, aliyetambulika kwa jina la Lilian pekee, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela mwaka 2015.

    Alijifungua mtoto wa kike katika hospitali ya umma mwaka wa 2015, lakini mtoto huyo alipata matatizo ya kiafya na kufariki hospitalini siku tatu baadaye.

    Kuna marufuku kamili ya utoaji mimba nchini El Salvador, ambayo ina mojawapo ya sheria kali zaidi za kupinga kutoa mimba.

    Waendesha mashtaka walikuwa wamemshtaki Lilian kwa kutomtunza mtoto mchanga wakati wa ujauzito wake, na alishtakiwa kwa uzembe na mauaji mabaya.

    Lilian, ambaye ana binti mwenye umri wa miaka 10, amekuwa akisisitiza kuwa hana hatia kila wakati, na alisema hakuwahi kukusudia kumaliza ujauzito wake.

    Vikundi vya kampeni ambavyo vilimuunga mkono Lilian vilisema aliachiliwa mnamo Disemba, lakini habari hiyo imetolewa kwa umma sasa.

    Walisema uamuzi wa hakimu kumuachilia huru Lilian ulitokana na kwamba alikuwa katika mazingira magumu hospitalini alipofiwa na mtoto wake.

    Makumi ya wanawake wanaaminika kufungwa kimakosa nchini El Salvador kwa tuhuma za kutoa mimba.

    Wale wanaopatikana na hatia ya kumaliza ujauzito wao wanakabiliwa na kifungo cha kati ya miaka miwili hadi minane gerezani. Lakini mara nyingi shtaka hubadilishwa na kuwa mauaji ya kuchochewa na adhabu yake ni kifungo cha chini cha miaka 30.

  11. Mwanamke wa Marekani ahukumiwa miaka 26 kwa mauaji ya mama yake

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanamke mmoja nchini Marekani ambaye alisaidia kumuua mama yake na kuuweka mwili wake kwenye sanduku wakati wa likizo ya 2014 huko Bali amehukumiwa kifungo cha miaka 26 jela.

    Heather Mack alipatikana na hatia nchini Indonesia mwaka 2015 na kuhukumiwa miaka 10 jela, lakini akaachiliwa huru mwaka wa 2021.

    Kisha alikamatwa alipofika Marekani na kushtakiwa kwa njama ya kumuua raia wa Marekani.

    Mack amekaa miaka miwili iliyopita katika gereza la Chicago alipokuwa akisubiri hukumu.

    Siku ya Jumatano, Jaji Matthew Kennelly aliamua kwamba Mack, 28, atapokea afueni kwa muda ambao amehudumu hadi sasa, na hivyo kupunguza kifungo chake rasmi hadi takriban miaka 23.

    Waendesha mashtaka walikuwa wamependekeza kifungo cha miaka 28 jela kwa Mack, ambaye alipanga njama na mpenzi wake wa wakati huo Tommy Schaefer kumuua mamake, msomi tajiri Sheila von Wiese-Mack.

    Wawili hao inasemekana walifanya hivyo ili kupata $1.5m (£1.17m) mali iliyowekwa katika hazina ambayo bintiye angeipata baadaye.

    Waendesha mashtaka walidai kuwa Bi Mack - ambaye alikuwa na umri wa miaka 18 wakati wa mauaji hayo na mjamzito - aliziba mdomo wa mamake huku Bw Schaefer akimpiga kichwani kwa bakuli la matunda.Mwili huo baadaye uligunduliwa ukiwa umeingizwa ndani ya sanduku.

    Baada ya mauaji ya Wiese-Mack katika hoteli hiyo, Bi Mack na Bw Schaefer waliacha sanduku la mabaki yake kwenye buti ya teksi, waendesha mashtaka walisema.Baadaye dereva alitoa taarifa kwa polisi.

    Wanandoa hao waligunduliwa baadaye wakiwa katika hoteli nyingine huko Bali.

    Wakati wa hukumu yake, kakake Wiese-Mack, Bill Wiese, aliiomba mahakama kutoa adhabu ya juu iwezekanavyo, akisema kuwa Mack hajaonyesha kujutia uhalifu huo.

  12. Uchunguzi wafanyika baada ya mtoto wa miaka miwili na baba yake kupatikana wamekufa Uingereza

    h

    Chanzo cha picha, Facebook

    Maelezo ya picha, Bronson Battersby anaaminika kufariki akiwa peke yake kutokana na njaa baada ya baba yake kuugua mshtuko wa moyo

    Mvulana wa miaka miwili na babake wamepatikana wamekufa katika mali huko Skegness, na kusababisha "uchunguzi wa haraka".

    Bronson Battersby alipatikana peke yake ndani ya nyumba na baba yake mwenye umri wa miaka 60, Kenneth Battersby, mnamo 9 Januari.

    Inafikiriwa kuwa mtoto huyo anayetembea, ambaye ameelezewa kuwa "mwanga wa jicho la baba yake", alikufa kwa njaa baada ya Bw Battersby kupata mshtuko wa moyo.

    Familia hiyo ilitambuliwa na huduma ya watoto katika Baraza la Kaunti ya Lincolnshire ambayo imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

    Mkurugenzi wake mtendaji wa huduma za watoto, Heather Sandy, alielezea vifo hivyo kama "cha kusikitisha".

    "Ni msiba kwamba Kenneth alikufa kwa mshtuko wa moyo," aliambia BBC Radio 4's World at One.

    "Alikuwa nyumbani peke yake na Bronson na hiyo ilimaanisha kwamba hakukuwa na mtu yeyote wa kumtunza Bronson, na cha kusikitisha ni matokeo ya hilo, Bronson pia ameaga dunia."

  13. Mwendesha mashtaka wa Ecuador anayechunguza shambulio la studio ya TV auawa

    th

    Chanzo cha picha, Facebook

    Mwendesha mashtaka anayechunguza shambulio kwenye studio ya TV nchini Ecuador wiki jana ameuawa, maafisa wanasema.

    César Suárez aliuawa kwa kupigwa risasi katika mji wa bandari wa Guayaquil, mkoa wa Guayas siku ya Jumatano, mwanasheria mkuu alisema.

    Haijabainika iwapo kifo cha Bw Suarez kinahusishwa na uchunguzi wake kuhusu shambulio la kituo cha televisheni.

    Wakati wa tukio hilo la kushangaza wiki iliyopita, watu waliojifunika nyuso zao walivamia studio ya kituo cha televisheni cha TC wakati wa matangazo ya moja kwa moja na kuwatishia wafanyikazi kwa kwa kuwaelekezea bunduki.

    Picha ambazo zilipeperushwa moja kwa moja hewani zilionyesha mwanahabari Jose Luis Calderon akiwasihi watu hao wenye silaha kutowadhuru huku wafanyakazi wa kituo hicho wakilazimika kuketi au kulala kwenye sakafu ya studio.

    Mpiga picha mmoja alipigwa risasi mguuni, huku mkono wa mwingine ukivunjwa wakati wa shambulio hilo, naibu mkurugenzi wa habari wa TC alisema.

    Vyombo vya habari vya eneo hilo vinaripoti kwamba Bw Suárez alipigwa risasi alipokuwa akiendesha gari karibu na ofisi yake.Picha ambazo hazijathibitishwa kwenye mitandao ya kijamii pia zinaonyesha gari lililo na matundu ya risasi kwenye dirisha.

  14. Binti Mfalme Kate hospitalini huku Mfalme Charles III akitarajiwa kupata matibabu ya tezi dume

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Binti mfalme wa Wales anaendelea kupata nafuu hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji, wakati Mfalme Charles III atazamiwa kufanyiwa upasuaji wiki ijayo.

    Catherine atajiuzulu kutoka kwa wadhifa wake wa kifalme kwa miezi kadhaabaada ya upasuaji wa hali isiyojulikana lakini sio saratani.

    Hali ya tezi dume ya Mfalme itatibiwa wiki ijayo

    Matangazo haya ya afya ambayo hayakurajiwa yalitolewa ndani ya saa mbili Jumatano alasiri.

    Maelezo juu ya afya ya wanagfamilia ya kifalme kwa kawaida huwa ni siri inayolindwa kwa karibu na hutangazwa tu kwa umma katika kwa maelezo macheche, kwa hivyo uamuzi wa kutoa taarifa hizi mbili muhimu kwa siku moja ulikuwa wa kushangaza.

    Mnamo saa nane za mchana, Jumba la Kensington lilifichua kuwa Binti mfalme Kate alilazwa katika hospitali ya kibinafsi katikati mwa London Jumanne kwa matibabu na anaendelea kupata nafuu.

    Inafahamika kwamba anaendelea vizuri, lakini anatarajiwa kukaa hadi wiki mbili hospitalini hadi baada ya Pasaka huku akiendelea kupata nafuu kwa muda wa miezi kadhaa.

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Hakukuwa na dalili kwamba Mfalme au Binti wa Wales alikuwa na afya mbaya wakati walionekana pamoja huko Sandringham wakati wa Krismasi.

    Chini ya dakika 90 baadaye, taarifa tofauti ilichapishwa na Jumba la Buckingham ikifichua kwamba Mfalme anahitaji "utaratibu upasuaji wa kurekebisha" wiki ijayo kwa tezi ya kibofu iliyopanuliwa.

    Hali hiyo ni ya kawaida kwa wanaume wazee na sio saratani. Mfalme alitimiza miaka 75 mnamo Novemba.

    Haijulikani ni utaratibu gani Mfalme anahitaji, lakini ikulu ilisema "mahusiano yake yataahirishwa kwa muda mfupi wa kupona".

    Katika hali kama hizi, "washauri wa serikali" wanaweza kufanya kazi kama wasimamizi wa mfalme na kutekeleza majukumu kama vile kusaini hati rasmi - lakini Jumba la Buckingham limesema hiyo haitakuwa muhimu.

  15. Ernest Bai Koroma: Rais wa zamani anaweza kuondoka Sierra Leone huku kukiwa na tetesi za uwezekano wa kuhamia Nigeria

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa zamani wa Sierra Leone amepewa ruhusa ya kusafiri nje ya nchi kwa matibabu licha ya kukabiliwa na mashtaka ya uhaini.

    Uamuzi huo wa Mahakama Kuu unakuja huku kukiwa na uvumi kwamba Ernest Bai Koroma amekubali kwenda uhamishoni nchini Nigeria ikiwa mashtaka dhidi yake yatafutwa.

    Alishtakiwa kwa uhaini na makosa mengine juu ya mapinduzi yaliyoshindwa Novemba mwaka jana, ambapo watu 20 walikufa.

    Bw Koroma, ambaye alitawala kati ya 2007 na 2018, anakanusha madai haya.

    Amri ya mahakama ambayo BBC iliona Jumatano inaonyesha Bw Koroma anaruhusiwa kusafiri hadi Nigeria kwa sababu za kimatibabu.

    Amri hiyo inasema kwamba hapaswi kukaa huko kwa zaidi ya miezi mitatu na kwamba lazima afike mbele ya mahakama ya hakimu ya Sierra Leone tarehe 6 Machi.

    Wakati wa shambulio la mwaka jana,watu wenye silaha walivamia ghala la silaha la kijeshi na magereza kadhaa katika mji mkuu wa Freetown, na kuwaachilia karibu wafungwa 2,000.

    Serikali ilieleza kuwa jaribio hilo la mapinduzi na mapema mwezi huu, Bw Koroma alishtakiwa pamoja na washukiwa wengine 12.

    Vyanzo visivyojulikana kutoka Umoja wa Mataifa na Ecowas, muungano wa nchi za Afrika Magharibi, viliambia BBC kwamba Ecowas ilikuwa imepanga mpango wa Bw Koroma kwenda uhamishoni nchini Nigeria ikiwa mashtaka yatafutwa.

    BBC pia iliona barua ikisema Bw Koroma amekubali mpango huo, ambao utamfanya aendelee kufurahia marupurupu ya rais wa zamani hata akiwa Nigeria.

    Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sierra Leone Timothy Kabba hapo awali aliiambia BBC kuwa serikali haikuunga mkono pendekezo hilo, ambalo alilitaja kama "pendekezo la upande mmoja" la rais wa Tume ya Ecowas.

    Ecowas imekuwa na wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mvutano nchini Sierra Leone kufuatia jaribio la mapinduzi.Katika miaka ya 1990 Ecowas ilishuhudia kwa karibu maafa ya vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi na kutuma kikosi cha kulinda amani kusaidia kumaliza mzozo huo.

    Baadhi ya wanadiplomasia wanaamini Bw Koroma hatarejea kutoka Nigeria baada ya kusafiri huko kwa misingi ya matibabu na kwamba amri ya mahakama inamruhusu kwenda uhamishoni kama njia ya kurejesha utulivu nchini humo.

    Bw Koroma alikuwa rais kwa miaka 11 hadi 2018, wakati Rais wa sasa Julius Maada Bio alipochaguliwa.

  16. Shambulio la Ukingo wa Magharibi: Israel yashutumiwa kwa kuwalenga raia katika shambulio baya

    TH

    Israel inashutumiwa kwa kulenga kundi la raia wa Palestina wasio na uhusiano na makundi yenye silaha na ambao hawakuwa tishio kwa vikosi vya Israel, kwa mujibu wa mashahidi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

    Wanaume saba - wanne kati yao ndugu - waliuawa katika shambulio la anga la Israeli mapema Januari 7, walipokuwa wameketi karibu na barabara ya kijiji cha al-Shuhada, kilomita 10 kutoka mji wa Jenin.

    BBC imezungumza na jamaa za watu waliouawa, mashahidi katika eneo hilo wakati huo, na mhudumu wa afya katika eneo la tukio.Wote walitoa ushahidi dhabiti kwamba watu hao hawakuwa wanachama wa makundi ya wapiganaji wenye silaha, na kwamba hakuna mapigano na majeshi ya Israel yaliyokuwa yakifanyika katika eneo hilo wakati huo.

    Khalid al-Ahmad, mhudumu wa dharura wa kwanza kufika asubuhi hiyo, anaamini kwamba watu hao hawakufanya chochote kibaya.

    "Mmoja wao alikuwa amevaa pati pati na pajama," aliambia BBC."Je, hufikirii kwamba mtu ambaye anataka kupinga [uvamizi wa Israel] angevaa angalau viatu vinavyofaa?"

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limehusisha shambulio hilo na operesheni ya kijeshi saa chache mapema katika kambi ya wakimbizi ya Jenin, ambapo mwanajeshi wa kike aliuawa.

    IDF ilituelekeza kwenye taarifa iliyoitoa wakati huo, iliyosema kwamba "wakati wa operesheni hiyo, ndege ilishambulia kikosi cha magaidi ambacho kilirusha vilipuzi kwa vikosi vinavyoendesha eneo hilo".

    Picha kutoka kwa IDF na kamera ya karibu ya CCTV hazionyeshi ushahidi wowote wa wazi wa makabiliano na Wapalestina huko al-Shuhada wakati wa mgomo.

    Ndugu hao wanne - Alaa, Hazza, Ahmad, na Rami Darweesh - walikuwa na umri wa kati ya miaka 22 na 29.Walikuwa wahamiaji wa Kipalestina ambao walikuwa wamerejea kutoka Jordan miaka michache iliyopita wakiwa na mama yao na ndugu zao watano.

    Unaweza pia kusoma

  17. Marekani yaanzisha awamu ya nne ya mashambulizi dhidi ya Wahouthi nchini Yemen

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani imefanya duru ya nne ya mashambulizi dhidi ya Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen, maafisa wa Pentagon walithibitisha Jumatano usiku.

    Baadhi ya makombora 14 ya Houthi, ambayo Marekani inasema huenda yalilengwa kwa ajili ya mashambulizi ya meli katika Bahari ya Shamu, yalilengwa na majeshi ya Marekani.

    Centcom - kamandi ya Amerika Mashariki ya Kati - ilisema maeneo hayo yalipigwa na makombora ya Tomahawk yaliyorushwa kutoka kwa meli za Jeshi la Wanamaji la Marekani

    Mashambulizi hayo yanakuja huku Marekani ikiwataja Wahouthi kama "magaidi wa kimataifa".

    Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Marekani, Jake Sullivan alisema hatua hiyo, ambayo ilibatilisha uamuzi wa kuondoa jina hilo katika siku za mwanzo za utawala wa Biden, ni kujibu mashambulizi yanayoendelea ya wanamgambo hao dhidi ya meli za kibiashara katika eneo hilo.

    Waasi wa Houthi walianza kushambulia meli za wafanyabiashara mwezi Novemba, wakisema walikuwa wakijibu operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza. Tangu wakati huo, kundi hilo limeanzisha mashambulizi kadhaa dhidi ya meli za kibiashara zinazopitia Bahari ya Shamu , mojawapo ya njia za meli zenye shughuli nyingi zaidi duniani.

    Waasi wa Houthi wa Yemen wameilenga meli inayomilikiwa na Marekani katika Ghuba ya Aden baada ya Washington kusema italitaja tena kundi hilo kuwa "magaidi wa kimataifa".

    Kundi hilo lilisema liliipiga "Genco Picardy" kwa makombora ambayo yalisababisha "pigo lamoja kwa moja".

    Jeshi la Marekani linasema kuwa meli hiyo ilipigwa na ndege isiyo na rubani Jumatano jioni.

    Unaweza pia kusoma