Bab el Mandeb: Fahamu mkondo wa Bahari ya Shamu unaotumiwa na Houthi kushambulia meli

Chanzo cha picha, Getty Images
Jina la mlango wa Bahari ya Sham, ni Bab el Mandeb, likimaanisha kwa Kiarabu "mlango wa machozi" au "mlango wa huzuni."
Ni kutoka na mikondo na upepo, uharamia na migogoro - iliyodumu kwa milenia wanayokabiliana nayo mabaharia wanaopitia lango hilo la Bahari ya Shamu kati ya Yemen, Djibouti na Eritrea kutokea Bahari ya Hindi.
Mlango wa bahari wa Mandeb uko kwenye vichwa vya habari kutokana na mashambulizi ya wanamgambo wa Houthi wa Yemen dhidi ya meli zinazopitia katika njia hiyo yenye shughuli nyingi za biashara ya kimataifa.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Marekani na Uingereza zimeshambulia kwa mabomu maeneo kadhaa yanayodhibitiwa na Wahouthi.
Kundi hilo linaundwa na wanachama wengi wa Kiislamu wenye itikadi kali za Kishia wanaopigania madaraka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea Yemen.
Kwa hivyo, Mlangow a Bahari wa Mandeb umekuwa uwanja wa mzozo wa kimataifa. Lakini umuhimu wake wa kibiashara na kijiografia ni upi?
Ukanda wa kihistoria

Ukanda huu una urefu wa kilomita 115, Mlango Bahari wa Bab el Mandeb unaunganisha Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden.
Una upana wa kilomita 36 kwenye sehemu yake nyembamba zaidi, ambapo kuna kisiwa cha Perim, kinachougawa mlango huo katika njia mbili.
Eneo hili lina umuhimu mkubwa katika biashara, utamaduni na migogoro kwa sehemu kubwa ya historia ya ustaarabu wa binadamu.
Limetumika kwa shughuli za kibiashara tangu Misri ya kale, na safari za kutafuta bidhaa za thamani kama vile viungo, dhahabu na wanyama, wakati Warumi waliitumia njia hiyo kufanya biashara na India na Mashariki.
Kuanzia Enzi za Kati, Mlango wa Bab el Mandeb ulikuwa njia muhimu ya biashara ya viungo, nguo na bidhaa nyinginezo, na kutajirisha madola ya wakati huo.
Na baadaye, madola ya Ulaya kama vile Ureno, Hispania na, baadaye, Uingereza walitumia njia hiyo kuelekea India na Kusini na Mashariki-Kusini mwa Asia.
Hata hivyo, ufunguzi wa Mfereji wa Suez mwaka 1869 uliufanya mlango wa Bab el Mandeb kuwa njia muhimuzaidi ya njia fupi ya baharini kati ya Ulaya na Asia.
Ahari za Mgogoro wa sasa

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Migogoro katika eneo hilo pamoja na shughuli za maharamia, ndio chanzo cha uwepo majeshi ya kimataifa yenye nguvu duniani, hasa Marekani.
Ukanda wa Bahari ya Shamu una shughuli nyingi za kibiashara, ukibeba karibu robo ya biashara ya baharini duniani.
Kati ya mabilioni ya tani za bidhaa zinazopitia njia hii, mapipa milioni 4.5 ya mafuta hupita kutoka nchi za Mashariki ya Kati na Asia hadi Magharibi kila siku, kwa mujibu wa Marekani.
Zaidi ya hayo, 8% ya shehena ya gesi asilia duniani (LNG) ilipita katika mkondo huo mwaka jana, na kuifanya kuwa mshipa muhimu wa usambazaji wa nishati duniani.
Kwa hakika, matukio yanayotokea Bab el Mandeb yana athari za haraka kwa bei za duniani za rasilimali hizi muhimu.
Kati ya Jumatano na Ijumaa, bei ya mafuta ghafi ya Brent ilipanda kwa 5%, jambo ambalo wataalamu walilihusisha na mvutano katika Bahari ya Shamu.
Mgogoro huo umelazimisha meli nyingi za mafuta kutumia njia nyingine, na kusababisha kuchelewesha usafirishaji na kuongezeka kwa gharama.
Mbali na mafuta na gesi, Mlango huo ni njia kuu kati ya Mashariki na Magharibi, na meli kadhaa za mizigo hupitia kila siku.
Meli nyingi kwa sasa zinapita magharibi mwa Bahari ya Hindi kwa - njia ndefu zaidi kuelekea Rasi ya Afrika Kusini
Katika wiki kadhaa sasa bei ya kusafirisha kontena kutoka Asia Mashariki hadi Ulaya Kaskazini imepanda kwa mara tatu.
Ajali, maharamia hadi makombora

Chanzo cha picha, Getty Images
Hii sio mara ya kwanza kwa matukio kama haya katika eneo hili kuathiri safari za baharini na kuleta athari kubwa kwa biashara ya kimataifa.
Mwaka 2021, meli yenye bendera ya Panama, Ever Given ilikwama katika Mfereji wa Suez, na kusababisha mkwamo katika mnyororo ya kimataifa ya usambazaji, na kuongezeka kwa gharama na ucheleweshaji wa utoaji wa mafuta na bidhaa za kila aina.
Kati ya 2008 na 2012, Mlango wa Bab el Mandeb na eneo lote la bahari lilikumbwa na mashambulizi mengi ya maharamia, hasa kutoka Somalia, ambao waliwateka nyara wafanyakazi wa meli ili kudai pesa na waachiliwe.
Hilo lilichoche jumuiya ya kimataifa pamoja na makampuni ya meli kuimarisha usalama.
Zaidi ya muongo mmoja baadaye, tishio katika mkondo huo linatoka upande wa pili, ni mashambulizi kutoka kwa waasi wa Houthi.
Waasi wa Houthi wamehalalisha mashambulizi yao katika Mlango-Bahari wa Mandeb na Bahari kama jibu la vita vya Israel dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Wanasema mashambulizi yao ya ndege zisizo na rubani na makombora yanalenga meli zinazoingia au kuelekea Israel.
Katika mashambulizi hayo, hata hivyo, huathiri aina zote za meli ambazo mara nyingi, hazina uhusiano na Israel na zinaelekea nchi nyingine.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












