Droni za Ukraine zinazotumia teknolojia ya Magharibi kushambulia ndani ya Urusi

Chanzo cha picha, Planet Labs
- Author, Jonathan Beale & Thomas Spencer
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Teknolojia na fedha za mataifa ya Magharibi zinaisaidia Ukraine kutekeleza mamia ya mshambulizi ya masafa marefu ndani ya Urusi.
Licha ya wanachama wa Nato kukataa kuipa Ukraine ruhusa ya kutumia silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi kufanya mashambulizi ya aina hiyo - hasa kwa sababu ya hofu ya kuongezeka kwa vita.
Ukraine imeongeza mashambulizi yake ya masafa marefu ndani ya Urusi katika miezi michache iliyopita, ikirusha mfululizo ndege zisizo na rubani kushambulia maeneo ya kimkakati ya Urusi.
Maeneo hayo ni pamoja na vituo vya jeshi la anga vya Urusi, bohari za mafuta na silaha na vituo vya kamandi kuu. Makampuni ya Ukraine sasa yanazalisha mamia ya ndege zisizo na rubani kwa mwezi, za bei nafuu.
Kampuni moja iliiambia BBC, tayari droni hizo zinaleta athari katika uchumi wa vita wa Urusi kwa gharama ndogo ya droni hizo.
Droni za Mbao

Chanzo cha picha, Terminal Autonomy
Francisco Serra-Martins anasema mkakati huo tayari unaleta matatizo makubwa kwa Moscow. Anaamini ikiwa kutakuwa na uwekezaji zaidi, Ukraine itakuwa juu katika vita hivyo.
Miezi kumi na minane iliyopita, kampuni aliyoianzisha ya Terminal Autonomy, haikuwepo. Sasa inazalisha zaidi ya droni mia moja za masafa marefu za AQ400 Scythe kwa mwezi, zenye kufika masafa ya kilomita 750 (maili 465).
Kampuni hiyo pia hutengeneza mamia ya ndege zisizo na rubani za masafa mafupi kwa mwezi, ambazo zinaweza kuruka mamia ya kilomita.
Ndege hizo zimetengenezwa kwa mbao zinazokusanywa katika viwanda vya zamani vya samani nchini Ukraine.
Serra-Martins, aliyekuwa Mhandisi wa Jeshi la Australia, alianzisha kampuni hiyo na mwanzilishi mwenza wa Ukraine, akiungwa mkono na fedha za Marekani. Ni mojawapo ya makampuni matatu ambayo sasa yanazalisha ndege zisizo nchini Ukraine kwa kiwango kikubwa.
Anaelezea ndege zake zisizo na rubani kama "fanicha inayoruka."
Inachukua kama saa moja kujenga umbo la nje na nusu ya muda huo kuweka akili mnemba, vifaa vya elektroniki, mota na vilipuzi.
Droni kama hiyo inagharimu dola elfu chache tu. Kinyume chake, kombora la ulinzi wa anga la Urusi linalotumiwa kuidungua linaweza kugharimu zaidi ya dola za kimarekani milioni 1.
Kutambua ulinzi wa anga

Chanzo cha picha, Terminal Autonomy
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Palantir, kampuni kubwa ya kuchambua data ya Marekani, ni mojawapo ya makampuni ya kwanza ya teknolojia ya Magharibi kusaidia juhudi za vita vya Ukraine.
Ilianza kwa kutoa programu ya kuboresha kasi na usahihi wa mashambulio. Sasa imeipa Ukraine zana mpya za kupanga mashambulizi yake ya masafa marefu ya ndege zisizo na rubani.
Wahandisi wa Palantir kutoka Uingereza, wanafanya kazi na wenzao wa Ukraine, wameunda programu ya kuunda ramani bora za kufikia lengo. Palantir inaweka wazi kuwa haihusiki katika mashambulizi, lakini imesaidia kutoa mafunzo kwa zaidi ya raia 1,000 wa Ukraine ya jinsi ya kutumia programu yake.
Kwa kutumia data, inaweza kuonyesha kwenye ramani ulinzi wa anga wa Urusi, rada na mifumo ya ulinzi ya kielektroniki. Na huonekana kama ramani ya nchi.
Kadiri mistari katika ramani inavyokoza, ndicho kiashiria kuwa ulinzi wa anga ni mkubwa katika eneo hilo. Na maeneo hayo tayari yametambuliwa na Ukraine kwa kutumia setilaiti na taarifa za kijasusi.
Louis Mosley wa Palantir anasema mpango huo unasaidia Ukraine kupambana na vita vya kielektroniki vya Urusi na mifumo ya ulinzi wa anga na kufikia lengo lao.
Utekelezaji wa mashambulizi hayo ya masafa marefu ya droni unaratibiwa na mashirika ya kijasusi ya Ukraine, ambayo yanafanya kazi kwa siri.
Mashambulizi ya droni mara nyingi hufanywa usiku. Changamoto ni kuwa, nyingi hudondoshwa. Ni chache tu kama 10% zinazoweza kufikia lengo ndani ya Urusi. Na baadhi ya ndege hizo hata hupigwa na mifumo ya anga ya ulinzi ya Ukraine.
Je, Urusi iko hatarini?
Prof Justin Bronk wa Taasisi ya Royal United Service, anasema mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Ukraine yanazua taharuki kwa Moscow. Ingawa Urusi ina ulinzi mkubwa wa anga, bado haiwezi kulinda kila kitu.
Anasema mashambulizi ya masafa marefu ya Ukraine, yanaonekana kwa Warusi wa kawaida kwamba "serikali haiwezi kuwatetea kikamilifu na Urusi iko hatarini."
Ndege zisizo na rubani za Ukraine zimeonekana zaidi ya kilomita 1,000 (maili 620) ndani ya Urusi. Zimedunguliwa katika anga ya Moscow. Droni hizo hulenga zaidi maeneo ya kijeshi.
Ukraine imeilazimisha Urusi kuondosha ndege za kivita katika kambi na kuzipeleka mbali zaidi na kupunguza kasi ya mashambulizi yao.
Picha za setilaiti zinaonyesha jinsi ndege zisizo na rubani za Ukraine zilivyofanikiwa kuharibu jengo kubwa kwenye kambi ya anga ya Marynovka.
Mipango ya Ukraine

Chanzo cha picha, EPA
Ukraine inaamini inaweza kufanya zaidi kwa msaada wa silaha za masafa marefu zilizotengenezwa na Magharibi. Lakini hadi sasa, washirika wamekataa maombi ya Kyiv.
Bado kuna hofu inayoendelea, haswa huko Washington na Berlin, kwamba silaha zao kushambulia ndani ya Urusi, kunaweza kuziingiza Magharibi katika mzozo huo. Lakini hilo halijazuia makampuni ya Magharibi na fedha kusaidia Ukraine.
Kwa kiasi kikubwa Ukraine bado inalazimika kutegemea juhudi za watu wa nyumbani, ikiamini kupeleka vita nchini Urusi ni ufunguo wa kushinda vita hivi.
BBC imezungumza na kampuni moja ya Ukraine ambayo tayari inatengeneza kombora jipya, ambalo ni mara 10 kwa bei nafuu kuliko kombora la Storm Shadow lililotengenezwa Uingereza.
Licha ya mashaka ya nchi za Magharibi, Ukraine inapanga kuongeza mashambulizi yake dhidi ya Urusi. Serra-Martins anasema: "Unachokiona sasa si chochote ukilinganisha na kile utakachokiona mwishoni mwa mwaka."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












