Ziara ya Modi Ukraine: India mshirika wa Urusi, itatafuta nini Ulaya?

wd

Chanzo cha picha, PIB India

Maelezo ya picha, Modi (kulia) alikutana na Zelensky kando ya mkutano wa kilele wa G7 mwezi Juni
    • Author, Vikas Pandey
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amezuru Ukraine (Ijumaa) wiki chache tu baada ya kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin mjini Moscow.

Ziara hiyo ni muhimu kwa sababu Kyiv na baadhi ya miji mikuu ya nchi za Magharibi, ilikosoa ziara ya Modi katika mji mkuu wa Urusi mwezi Julai.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema, "nimesikitishwa kuona kiongozi wa nchi kubwa ya kidemokrasia duniani, akimkumbatia mhalifu aliyemwaga damu nyingi zaidi duniani huko Moscow."

Kutofungamana na upande wowote

sx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwezi Julai, Modi alitembelea Moscow kukutana na Vladimir Putin, na kukosolewa na mataifa ya Magharibi

Haishangazi kuona India ikisawazisha uhusiano wake kati ya mataifa au kambi mbili zinazoshindana. Mbinu maarufu ya nchi hiyo ya kutofungamana na siasa za jiografia, imetumika vyema kwa miongo kadhaa.

Ziara ya wiki hii – ni ya kwanza ya waziri mkuu wa India nchini Ukraine – ni kama kutoa tamko kuwa, India itaendelea kuwa na uhusiano mzuri na Urusi, na bado itafanya kazi kwa karibu na Magharibi.

Michael Kugelman, mkurugenzi wa South Asia Institute katika kituo cha Wilson Center huko Washington, anasema, “ni safari inayokusudiwa kuendeleza maslahi ya India, kwa kurejesha urafiki na Kyiv.”

Lakini muda wa ziara hiyo unaonyesha, wanadiplomasia wa India wamezingatia ukosoaji kutoka Marekani wa ziara ya Modi huko Moscow.

India imejiepusha kuikosoa Urusi moja kwa moja juu ya vita, kiasi cha kuyaudhi mataifa ya Magharibi. Hata hivyo, Delhi mara nyingi imezungumzia juu ya umuhimu wa kuheshimu mipaka na uhuru wa mataifa mengine. Imeendelea kusukuma diplomasia na mazungumzo ili kumaliza vita.

Ziara ya Modi mjini Moscow mwezi Julai ilikuja saa chache baada ya shambulio la bomu la Urusi, lililowauwa takribani watu 41 nchini Ukraine, wakiwemo watu katika hospitali ya watoto mjini Kyiv, na kulaaniwa duniani kote.

Waziri Mkuu wa India alisema vifo vya watoto ni vya uchungu na vya kutisha, lakini hakuilaumu Urusi.

Hakuna uwezekano kwa Modi kukengeuka msimamo huu wakati wa ziara yake huko Kyiv, kwani India ina uhusiano imara na wa muda mrefu na Moscow na inategemea zana za kijeshi za Urusi.

Utegemezi wa India kwa Urusi

fc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Modi akiwa na Waziri Mkuu wa Poland ,Donald Tusk mjini Warsaw siku ya Alhamisi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

India ni muagizaji mkuu wa silaha duniani, na pia imekuza utengenezaji wake wa ndani wa silaha katika miaka ya hivi karibuni, lakini bado inanunua zaidi ya 50% ya vifaa vyake vya ulinzi kutoka Urusi.

India pia imeongeza uagizaji wake wa mafuta kutoka Urusi, ikitumia fursa ya bei nafuu inayotolewa na Moscow. Urusi ilikuwa muuzaji mkuu wa mafuta nchini India mwaka jana.

Marekani na washirika wake mara nyingi wameisihi India kuchukua msimamo wa wazi zaidi kuhusu vita hivyo, lakini bado wamejiepusha kuiwekea vikwazo vikali au shinikizo.

Nchi za Magharibi zinaiona India kuwa ni mshindani wa China na hawataki kuharibu hali hiyo. India, ambayo sasa ni ya tano kwa uchumi mkubwa duniani, pia ni soko kubwa la kibiashara linalokuwa.

Kugelman anasema nchi za Magharibi zitakaribisha ziara hiyo na kuiona kama nia ya Delhi kushirikiana na pande zote.

India pia inaihitaji Magharibi kwani China, hasimu wake wa Asia, na Urusi zimeunda uhusiano wa karibu katika miaka ya hivi karibuni.

Wachambuzi wengi wanaamini Modi anataka kujiweka kama mpenda amani, kutokana na uhusiano wa karibu wa India na Moscow na Magharibi.

Lakini hakuna uwezekano wa kuleta mpango wa amani kati ya Ukraine na Urusi.

Ulaya na ziara ya India

efd

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Modi alikutana na Zelensky mwaka 2023 katika mkutano wa G7 nchini Japan

Ukraine imeikaribisha ziara ya Modi na kuiona kama fursa ya kuwasiliana na mshirika wa karibu wa Moscow, jambo ambalo haijafanya tangu vita kuanza.

Zelensky, hata hivyo, hatoacha kuibua ukosoaji wake kwa Putin mbele ya Waziri Mkuu wa India. Na Modi anaweza kuvumilia hilo kwani amekumbana na hali kama hiyo mara nyingi katika miji mikuu mingine ya Magharibi.

Moscow haitoudhika na ziara hiyo, kwani imekuwa ikikubali mbinu ya Delhi katika kuziendea siasa za kikanda.

Lakini zaidi ya kusisitiza sera yake ya kutofungamana na upande wowote, Delhi pia ina malengo makubwa katika ziara hii. Inataka kuendelea kuimarisha uhusiano wake na mataifa manne makubwa - Uingereza, Italia, Ujerumani na Ufaransa - lakini pia inataka kuongeza ushirikiano na mataifa mengine barani Ulaya.

Modi pia ataruzu Poland katika safari hii – akiwa Waziri Mkuu wa kwanza wa India kuzuru nchi hiyo katika kipindi cha miaka 45. Pia alikua waziri mkuu wa kwanza wa India kuzuru Austria katika kipindi cha miaka 41 mwezi Julai.

Wachambuzi wanasema hii inaashiria uelewa wa India kwamba mataifa ya Ulaya ya Kati, yatachukua jukumu kubwa katika siasa za kikanda siku zijazo na uhusiano nzuri nao utainufaisha vyema Delhi.

Serikali ya India pia imefufua mazungumzo ya kibiashara na Ulaya. Imetia saini mkataba wa biashara na uwekezaji na Jumuiya ya Biashara Huria ya Ulaya.

Kwa hivyo, ingawa mazungumzo makubwa yatakuwa ni kuhusu vita katika ziara yake, wanadiplomasia wa India watazingatia zaidi lengo lao katika ziara hiyo.

“Ziara ya Modi huko Warsaw na Kyiv inahusu kuimarisha uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama baina ya nchi hizo mbili na mataifa ya Ulaya ya Kati,” ameandika mchambuzi wa sera za kigeni C Raja Mohan katika gazeti la Indian Express.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah