Narendra Modi: Waziri Mkuu wa India ambaye siasa zake zimemfanya kuwa mtata

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwaka huu zaidi ya nchi 60 zinafanya uchaguzi - kura tayari zimepigwa nchini Bangladesh, Taiwan na Pakistan huku Uingereza na Marekani zikijiandaa kwa uchaguzi baadaye mwakani.

Lakini uchaguzi wa kitaifa wa India katika majira ya machipuo utaonekana kama zoezi kubwa zaidi la kidemokrasia kuliko zote, na watu bilioni moja wanastahili kupiga kura.

Baada ya takriban miaka 10 madarakani, Waziri Mkuu Narendra Modi anatawala nyanja ya kisiasa ya India. Yuko kila mahali - kwenye tovuti za serikali, redio, televisheni, mabango, na hata vioski vya picha kwenye vituo vya reli - akitoa nafasi ndogo kwa wanasiasa wengine.

Kiongozo huyo mwenye umri wa miaka 73 ndiye nyota wa chama tawala cha Bharatiya Janata Party (BJP) na ndiye mtaji wao wa kutisha zaidi katika uchaguzi.

Yeye ni mmoja wa viongozi wa dunia wanaofuatiliwa zaidi kwenye YouTube, Facebook, Instagram na X, zamani ulijulikana kama Twitter.

Uwepo wake mkubwa kwenye mitandao ya kijamii katika nchi yenye watu bilioni 1.4 unamfanya kuonewa wivu na wapinzani wake.

Ingawa India ina aina ya serikali ya bunge, mtindo maalum wa Modi wa kufanya kampeni una hisia za kupendeza na shamrashamra za kampeni za urais kama wa Marekani.

Kazi ya kisiasa ya Modi: "Mzungumzaji mkuu"

Wafuasi wa Modi wanamuona kama mzungumzaji mzuri.

Ana njia ya kutangamana vizuri na watu, kwa kutumia hotuba kama chombo chenye nguvu cha mawasiliano.

Hata wapinzani wake wa kisiasa wanakiri ustadi wake.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya umahiri wa Modi ni umahiri wake na ustadi wa kujua ni matukio gani makubwa atakayotumia kujitangaza, kulingana na Santosh Desai, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kujitangaza.

.

Lakini anasema serikali ya Modi ilikadiria G20 kama mafanikio ya kibinafsi ya waziri mkuu, licha ya ukweli kwamba India ingekuwa mwenyeji bila kujali ni nani alikuwa kiongozi wa nchi.

"Modi aliigeuza kuwa tukio kubwa. Kwa njia nyingi, ana uelewa wa tukio linahusu nini na jinsi linapaswa kutumiwa."

Waangalizi wanaona kwamba ujuzi wa mawasiliano wa Modi unaenea zaidi ya mazungumzo tu. Uwezo wake wa kuwasilisha hisia, ikiwa ni pamoja na kumwaga machozi hadharani, unamfanya awe na ubinadamu machoni pa wafuasi wake bila kuhatarisha taswira yake kama mwanamume.

Kwa nini Narendra Modi ana utata?

Ujuzi huu wa upangaji na mawasiliano umefanya Modi kujikuta kwenye utata.

Mojawapo ni machafuko ya Gujarat ya 2002 alipokuwa waziri mkuu wa jimbo hilo.

Kufuatia kuchomwa moto kwa treni iliyokuwa imebeba mahujaji wa Kihindu huko Godhra, ghasia dhidi ya Waislamu zilizuka kote Gujarat, na kusababisha hasara kubwa ya maisha, haswa miongoni mwa jamii ya Waislamu.

Wakosoaji walishutumu serikali ya jimbo la Modi kwa kushindwa kuzima ghasia hizo.

Wakati Modi alikanusha kosa lolote na kutetea jinsi anavyoshughulikia hali hiyo, tukio hilo lilizua uchunguzi mkali wa kitaifa na kimataifa, na kumharibia sifa.

Baadaye aliondolewa hatia na mahakama ya juu zaidi ya India.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakosoaji wa Modi wanasema kwamba sera zake na matamshi yake, ambayo mara nyingi yanaleta migawanyiko, yanaakisi ajenda inayounga mkono Uhindu, inayolenga Wahindu walio wengi nchini India.

Wengi wa wafuasi wake humtaja kama "maliki wa mioyo ya Kihindu" ili kuonyesha upendo wao wa kina na kuvutiwa na kujitolea kwake kwa maadili ya Kihindu.

Lakini Modi pia amewakumbusha watu kuwa yeye ndiye kiongozi wa Wahindi wote bilioni 1.4.

Katika hatua ya kutatanisha mnamo 2016, wakati wa muhula wake wa kwanza kama waziri mkuu, ghafla alitangaza kwamba noti za benki za madhehebu ya juu hazitakuwa halali tena.

Lengo lilikuwa ni kupambana na rushwa, soko nyeusi na fedha ghushi.

Lakini hatua hiyo ilisababisha mtafaruku mkubwa na foleni ndefu kwenye benki na uhaba wa pesa ulioathiri biashara na uchumi usio rasmi.

Wakosoaji walidai kuwa alishindwa kufikia malengo yake na kusababisha matatizo makubwa kwa wananchi wa kawaida, hasa wale wa vijijini na maeneo yanayotegemea fedha.

Je, Modi amebadilishaje taswira ya India?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Baada ya ghasia za Gujarat Modi alinyimwa visa ya Marekani, lakini miongo miwili baadaye, mwezi Juni mwaka jana, aliadhimishwa katika Ikulu ya White House wakati wa ziara ya kiserikali.

Modi alifurahi baada ya kukumbatiana na kupeana mikono kwenye Ofisi ya Oval, pamoja na vifijo vya shangwe kubwa wakati wa hotuba yake katika kikao cha pamoja cha Congress.

Wafuasi wake walichukulia taswira ya kuibuka kwake kama kiongozi mashuhuri wa kimataifa, anayeweza kushawishi mambo ya ulimwengu.

Mapokezi nchini Marekani lazima yalihisi kwake kama ushindi wa kibinafsi na akautumia kutoa ujumbe kwamba mbali na kuwa pariah, sasa alikuwa anaheshimiwa sana katika nchi za Magharibi.

Jinsi Modi alivyojitengenezea jina

Lakini nyumbani India, uungwaji mkono unaonekana kuwa wa kibinafsi. Wengi wanaamini Modi amejitengenezea jina kweli kweli kiasi kwamba yeye ni mkubwa kuliko chama chake.

"Ukimwondoa Modi kwenye eneo la tukio, chama cha BJP sio kitu," anasema mwandishi wa habari Darshan Desai. "Sera ya BJP ni sera yake. BJP inamhitaji zaidi kuliko anavyohitaji chama."

Mtaalamu wa chapa Santosh Desai anaamini Modi amejiweka kama mtu mkuu kuliko mtu anayeonekana kuwa juu ya kila mtu.

“Hata akikaa kwenye vikao vya baraza la mawaziri huwa anakaa sehemu kando kidogo peke yake, anaonekana wazi kuwa yeye ndiye kiongozi na wengine ni wafuasi,” aeleza.

Modi na vyombo vya habari

Ukosoaji ambao Modi amekabiliana nao mara kwa mara tangu enzi zake kama waziri mkuu huko Gujarat ni jinsi anavyoshughulikia vyombo vya habari na kwamba mara chache huwa na mikutano na waandishi wa habari kujibu maswali yao.

"Huko Gujarat kulikuwa na mikutano michache ya waandishi wa habari, labda mara moja au mbili kwa mwaka," anaelezea ripota Darshan Desai.

“Alikuwa akitumia vyombo vya habari na wakati mwingine hata vibaya.

"Hata leo anasimamia vyombo vya habari kwa ustadi. Sisemi hivi kwa maana yoyote mbaya. Vyombo vya habari vinafuata yaani wanafanya anavyotaka. Vyombo vya habari vinageuka kuwa vimetengwa. Hivi ndivyo tunavyohisi."

Wakosoaji wanasema Modi kuwa madarakani, uhuru wa vyombo vya habari nchini India umekuwa chini ya tishio kubwa, na waandishi wa habari kukanyagwa, kunyanyaswa, na hata kukamatwa kwa kufanya kazi zao.

Hivi majuzi, serikali ya Modi imependekeza kitengo cha kuangalia ukweli kufuatilia mitandao ya kijamii na kukomesha habari za uwongo, lakini wanahabari wengi wanahofia hii itapanua wigo wa udhibiti.

Shutuma za unyanyasaji wa vyombo vya habari si jambo geni - kumekuwa na ukosoaji katika majimbo ambayo yanaendeshwa na vyama vya siasa tofauti na BJP na huko nyuma kulikuwa na wasiwasi kama huo, haswa chini ya Waziri Mkuu wa zamani Indira Gandhi.

Asili ya familia ya Modi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Modi mara nyingi amezungumza juu ya kusaidia baba yake kuuza chai katika kituo cha gari la moshi cha Vadnagar wakati wa utoto wake.

Alikua na kaka zake wanne, ambao hawajulikani sana, na ndoa yake na Jashodaben Modi, ambaye anaishi peke yake huko Gujarat, ilipangwa akiwa na umri wa miaka 18 hivi.

Alikiri hadharani hali yake ya ndoa baadaye sana maishani, kwani alihitajika kufichua habari hii alipoingia kwenye siasa. Hawana watoto.

Kwa kifupi, Narendra Modi anamaanisha vitu tofauti kwa watu tofauti. Kwa wengine yeye ndiye mtu mwenye nguvu zaidi nchini India na wafuasi wake wengi wanaamini kwamba India imefika kwenye jukwaa la kimataifa kutokana na uongozi wake.

Wakosoaji wake wanamwona kama mbabe na wanadai kuwa ameongoza kurudi nyuma kwa demokrasia ya India kwa kukandamiza sauti za upinzani na kukandamiza kwa kiasi kikubwa uhuru wa wanahabari.

Kwa wapinzani, msisitizo wake juu ya itikadi ya Hindutva na utaifa mkubwa ni kinyume na wingi wa India na maadili ya kidemokrasia ya kilimwengu.

Imetafsiriwa na Asha Juma