Vita vya Ukraine: Je, India inaweza kukata uhusiano wake wa ulinzi na Urusi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Uhusiano wa muda mrefu wa India na Urusi umeangaziwa - haswa katika sekta ya ulinzi - kufuatia uvamizi wa Ukraine.
Waziri wa Fedha Nirmala Sitharaman alisema wakati wa ziara yake nchini Marekani mnamo Aprili kwamba India ingependa kuwa ''rafiki mzuri'' kwa nchi za Magharibi.
Lakini aliongeza kuwa India haitaki kudhoofishwa, na ilihitaji kuhakikisha usalama wake - ukichukuliwa kumaanisha utegemezi wake wa muda mrefu wa zana za kijeshi za Urusi - utaendelea.
Je, India inategemea kwa kiasi gani silaha za Urusi?
India ni mojawapo ya wanunuzi wakubwa wa silaha duniani, na ilikuwa na uhusiano wa karibu wa ulinzi na uliokuwa Muungano wa Sovieti kwa miaka mingi.
Ushindani wa India na Pakistan, na kuongezeka na Uchina, inamaanisha Urusi imesalia mshirika mkuu wa Delhi, hata baada ya kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti katika miaka ya 1990.

Chanzo cha picha, Getty Images
Tangu mwaka 1992, karibu theluthi mbili ya vifaa vya kijeshi vya India vimetoka Urusi, kulingana na Sipri (Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm), ambayo hufuatilia uhamishaji wa silaha duniani na matumizi ya kijeshi.
Kituo cha Stimson, kikundi cha utafiti chenye makao yake nchini Marekani, kinakadiria kuwa silaha za Urusi zinaweza kuchangia asilimia 85 ya mifumo kuu ya silaha za India.
Hii ni pamoja na ndege za kivita, manowari zinazotumia nyuklia, zile za kubeba ndege, vifaru na makombora.
Je, India inajaribu kubadilisha silaha zake?
Katika miaka kumi iliyopita, utegemezi wake kwa silaha za Kirusi umepungua na imenunua vifaa zaidi kutoka nchi nyingine - hasa kutoka Ufaransa, lakini pia kutoka kwa Israeli na Marekani na, kwa kiasi kidogo, Uingereza.

Takwimu kutoka Sipri zinaonyesha kwamba thamani ya mauzo ya silaha na Ufaransa, Marekani na Israel kwa India mwaka 2021 ilikuwa mara mbili ya ilivyokuwa mwaka 2017, ingawa Urusi inasalia kuwa msambazaji mkuu.
India imenunua ndege aina ya Rafale, ndege za kivita za Mirage na manowari za Scorpene kutoka Ufaransa.
Wakati wa ziara ya hivi majuzi huko na Waziri Mkuu Narendra Modi, nchi zote mbili zilisema zimekubali kuongeza ushirikiano wao katika teknolojia ya hali ya juu ya ulinzi.
Vile vile, wakati wa safari ya Delhi mwezi Aprili na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, Uingereza na India ziliahidi kuimarisha uhusiano wa ulinzi na usalama, zikiangazia ushirikiano wa pamoja katika teknolojia ya hali ya juu ya ndege ya kivita.
India pia imegeukia Israeli kwa baadhi ya mahitaji yake ya teknolojia ya juu ya ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na:
- vifaa vya ndege zisizo na rubani
- mifumo ya kutoa onyo angani
- ulinzi dhidi ya makombora
- silaha zinazoongozwa kwa usahihi
Na uhusiano wa kijeshi wa India na Marekani umekuwa ukiongezeka sana, na biashara ya ulinzi kati yao kuongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka 2018 hadi 2019.
Ununuzi mkubwa ni pamoja na ndege za doria za baharini za masafa marefu za Marekani na ndege za usafiri za C-130, pamoja na makombora na ndege zisizo na rubani, na taarifa ya hivi karibuni ya Pentagon ilizungumzia ''ushirikiano wa kina.'' katika ulinzi wa anga na kimtandao.
Je, India inafikiria upya utegemezi wake kwa silaha za Urusi?
Kubadilika kwa siasa za kimataifa katika miaka ya hivi karibuni kunamaanisha kuwa uhusiano wa India na nchi kama vile Ufaransa, Marekani na Israel umekuwa karibu zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya hayo, India haijajiunga na kulaani kimataifa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, ikiweka wazi kuwa haitaki kuunga mkono upande wowote.
Baadhi ya wataalam wa masuala ya ulinzi wanaamini kwamba India inaweza kupata kwamba haina chaguo ila kupunguza utegemezi wake kwa Moscow, kutokana na athari za vikwazo kwa Urusi.
Sameer Lalwani, mchambuzi wa masuala ya ulinzi na usalama katika Kituo cha Stimson, anasema sasa kunaweza kuwa na matatizo na masuala muhimu ya mfumo wa makombora wa kutoka ardhini hadi angani wa S-400, ambao India ilinunua mwaka wa 2018, ambayo ni sehemu tu ya mfumo huo imewasilishwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
''Kuna sababu kubwa ya kuamini kwamba... Urusi haitaweza kutimiza ahadi zake za kimkataba kwa India kwa kuwasilisha mfumo wote wa S-400,'' asema Bw Lalwani.
Pia anaamini kuwa hasara ambayo Urusi imepata nchini Ukraine inaweza kumaanisha kuwa haiwezi kukidhi mahitaji ya India ''kwa sababu itakuwa na hamu ya kutumia vipuri vyote kujaza nguvu zake''.
Na anasema watunga sera wa India wanaweza kuwa wanazingatia baadhi ya masuala ambayo yamekabili vifaa vya vitani na silaha za Urusi nchini Ukraine.
Je, India inaweza kujisimamia bila silaha za Kirusi?
Hilo linaonekana kutowezekana kwa sasa.
Ripoti ya Congress ya Marekani mwezi Oktoba mwaka jana ilisema kuwa ''jeshi la India haliwezi kufanya kazi kwa ufanisi bila vifaa vinavyotolewa na Urusi na litaendelea kutegemea mifumo ya silaha za Kirusi katika muda wa karibu na wa kati''.
Ripoti hiyo ilibainisha kuwa Urusi inatoa silaha zake kwa bei ya kuvutia.
Sangeeta Saxena, mhariri wa kampuni ya Aviation and Defence Universe, yenye makao yake mjini Delhi, anasema jeshi la India hasa litaendelea kununua silaha zake kutoka Urusi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Anasema sio tu ukweli kwamba wafanyikazi wake wanafahamu vifaa vyao, lakini pia kwamba uhusiano na Urusi umehimili majaribio ya waka
Lakini anaongeza kuwa India inataka kukuza tasnia yake ya ulinzi ya nyumbani, wakati mwingine kwa ushirikiano wa pamoja na nchi zingine.
Hii inahusisha kutumia teknolojia ya hali ya juu kutoka nje ya nchi ili kutoa msukumo mkubwa kwa utengenezaji wa silaha chini ya programu kama vile ''Make in India'', anaelezea Bi Saxena.
India itanunua kutoka kwa yeyote inayefikiria kutoa ofa inayofaa zaidi au ya bei bora - iwe Urusi au nchi zingine, anaelezea.












