Uchaguzi wa Marekani 2024: Kwa nini Kamala Harris ameshindwa?

l

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Mwezi mmoja uliopita, Kamala Harris alionekana kwenye kipindi cha The View cha ABC kwa mahojiano. Alipoulizwa, atafanya kipi cha tofauti na rais aliyeko madarakani, Joe Biden: Akajibu, "hakuna jambo linalokuja akilini."

Jibu la Harris – likawa tangazo la shambulio la Republican – na kampeni zake za kisiasa hatimaye zimeshindwa kumshinda Donald Trump siku ya Jumanne.

Alikubali kushindwa mbio hizo, hadharani Jumatano alasiri, akiwaambia wafuasi wake "musife moyo."

Maafisa wa timu ya kampeni ya Harris walikuwa kimya siku ya Jumatano - wakati wafuasi wakionyesha mshtuko juu ya kile walichokiona.

"Kupoteza inauma sana. Ni ngumu," meneja wa kampeni wa Harris, Jen O'Malley Dillon alisema katika barua pepe kwa wafanyakazi siku ya Jumatano. "Hii itachukua muda mrefu kuikubali."

Kama makamu wa rais aliye madarakani, Harris hakuweza kujitenganisha na rais aliyepoteza ushawishi na alishindwa kuwashawishi wapiga kura kwamba ataweza kuleta mabadiliko waliyokuwa wakiyatafuta – katikati ya wasiwasi mkubwa wa kiuchumi.

Pia unaweza kusoma

Mizigo ya Biden

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Baada ya Biden kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho kufuatia matokeo mabaya baada ya mdahalo, Harris aliteuliwa kuwania kiti hicho, na akapita bila kura hata moja kupigwa.

Alianza kampeni yake ya siku 100, akiahidi wanawake kuhusu haki za uavyaji mimba na kuahidi kuwarejesha wapiga kura wa tabaka la wafanyakazi kwa kushughulikia masuala ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kupanda kwa gharama za maisha na uwezo wa kumiliki makazi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati huo ilikuwa ni miezi mitatu tu kabla ya siku ya uchaguzi, aliungwa mkono na nyota maarufu akiwemo Taylor Swift. Lakini Harris hakuweza kuzibadilisha hisia za kumpinga Biden ambazo zilienea kwa wapiga kura wengi.

Ushawishi wa Biden uko chini katika miaka yake minne ya uongozi, huku theluthi mbili ya wapiga kura wanaamini Marekani iko kwenye njia mbaya.

Washirika wengine wamehoji faraghani ikiwa Harris alikuwa mtiifu sana kwa Biden katika azma ya kuchukua nafasi yake.

Lakini Jamal Simmons, mkurugenzi wa zamani wa mawasiliano wa makamu wa rais, anasema huo ni "mtego," kuwa mbali sana na Biden kungewapa Warepublican nafasi ya kufanya mashambulizi kwa kukosoa utiifu wake.

“Hakika huwezi kumkimbia rais aliyekuteuwa,” anasema.

Harris alijaribu kufuata mstari mzuri wa utawala bila kwenda kinyume na bosi wake, akionyesha kusita kwenda kinyume na sera zozote za Biden, pia hakuonekana kuzipigia kampeni sera zake kwenye kampeni.

Lakini alishindwa kutoa hoja za kuridhisha kuhusu kwa nini anapaswa kuongoza nchi, na jinsi atakavyo shughulikia matatizo ya kiuchumi pamoja na wasiwasi ulioenea juu ya uhamiaji.

Matatizo ya Kiuchumi

Watu 3 kati ya wapiga kura 10 wanasema hali ya kifedha ya familia zao ni mbaya, kutoka watu 2 katika miaka 10 iliyopita, kulingana na data kutoka AP VoteCast, uchunguzi uliofanywa kwa wapiga kura zaidi ya 120,000 wa Marekani.

Wapiga kura tisa kati ya 10 walikuwa na wasiwasi sana au kwa kiasi fulani kuhusu bei ya bidhaa za nyumbani.

Utafiti huo huo uligundua wapiga kura 4 kati ya 10 walisema wahamiaji wanaoishi Marekani kinyume cha sheria wanapaswa kuhamishwa na kupelekwa nchi zao za asili, kutoka watu 3 kati ya 10 ambao walisema vivyo hivyo mwaka 2020.

Ingawa Harris alijaribu kutumia kampeni yake kusisitiza utawala wake hautokuwa ni mwendelezo wa Biden, lakini alishindwa kuelezea waziwazi sera zake mwenyewe, mara nyingi akizunguka maswala badala ya kushughulikia mapungufu yanayoonekana.

Timu ya kampeni ya Harris ilikuwa na matumaini ya kuyauganisha tena maeneo msingi ya wapiga kura ambayo yalimpa ushindi Biden 2020, ambayo ni wapiga kura weusi, Walatino na vijana na pia wapiga kura wa vyuo vikuu.

Lakini hakufanya vyema katika kambi hizo kuu. Amepoteza pointi 13 za wapiga kura wa Latino, pointi mbili za wapiga kura weusi, na pointi sita za wapiga kura chini ya miaka 30.

Seneta wa kujitegemea Bernie Sanders wa Vermont, ambaye alishindwa uchaguzi wa mchujo wa urais wa Democratic mwaka 2016 kwa Hillary Clinton na mchujo wa 2020 kwa Biden, anasema katika taarifa yake "sio mshangao kwamba wapiga kura wa tabaka la wafanyakazi wamekiacha chama.

"Kwanza, lilianza tabaka la wafanyakazi wazungu, na sasa ni wafanyakazi wa Kilatino na weusi. Wakati uongozi wa Democratic unaitetea hali iliyopo, Wamarekani wana hasira na wanataka mabadiliko," alisema. "Na wako sahihi."

Wanawake kwa kiasi kikubwa walimuunga mkono Harris dhidi ya Trump, lakini hakufanikiwa. Na hakuweza kutimiza matarajio yake ya kupata kura za wanawake wa Republican, amepoteza kwa 53% ya wanawake wazungu.

Katika uchaguzi wa kwanza wa urais tangu Mahakama ya Juu ilipobatilisha haki ya kikatiba ya uavyaji mimba, Democratic walikuwa na matumaini kwamba mtazamo wake katika kupigania haki za uzazi ungeleta ushindi.

54% ya wapiga kura wanawake walipiga kura zao kwa Harris, lakini ilikuwa chini ya 57% ambao walimuunga mkono Biden 2020, kulingana na taarifa za tume ya uchaguzi.

Kumshambulia Trump

k

Chanzo cha picha, Reuters

Hata kabla ya kuteuliwa kuwa mgombea, Harris alikuwa na mtazamo kwamba kinyang'anyiro hicho ni kama kura ya maoni juu ya Trump, na sio Biden.

Mwendesha mashtaka wa zamani wa California aliegemea rekodi yake ya utekelezaji wa sheria, ili kuendeleza kesi dhidi ya rais huyo wa zamani.

Lakini kampeni zake ziliamua kuachana na hoja ya msingi ya Biden kwamba Trump ni tishio kwa demokrasia, na kutanguliza mbele ujumbe wa furaha kuhusu kulinda uhuru wa binafsi na kusaidia kiuchumi tabaka la kati.

Katika nyakati za mwisho, hata hivyo, Harris alifanya uamuzi wa kimbinu na kuangazia hatari ya muhula wa pili wa Trump, akimwita ni rais "fashisti" na kufanya kampeni na Warepublican waliochukizwa na kuchoshwa na maneno yake.

Baada ya Mnadhimu Mkuu wa zamani wa Trump, John Kelly, kuliambia gazeti la New York Times kwamba Trump alizungumza kwa kumuunga mkono Adolf Hitler, Harris alitoa matamshi nje ya makazi yake rasmi akimtaja Trumo kama "mtu asiye na msimamo na asiye imara.”

"Kamala Harris amepoteza uchaguzi huu alipoweka nguvu zaidi kumshambulia Donald Trump," mchambuzi wa chama cha Republican Frank Luntz alisema siku ya Jumanne usiku.

"Wapiga kura tayari wanajua kila kitu kuhusu Trump - lakini walitaka kujua zaidi kuhusu mipango ya Harris - ya saa ya kwanza, siku ya kwanza, mwezi wa kwanza na mwaka wa kwanza wa utawala wake."

Hatimaye Harris ameshindwa na Trump, na kukataa kwa wapiga kura kukipigia kura chama cha Democrats kunaonyesha kuwa chama hicho kina tatizo kubwa kuliko rais asiye na ushawishi.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah