Orodha ya mazungumzo kuhusu vita vya Gaza tangu Oktoba 7 hadi sasa

Chanzo cha picha, Reuters
Qatar inahodhi mazungumzo ya kusitisha mapigano huko Gaza siku ya Alhamisi, ikitarajia kufikia makubaliano ambayo yatazuia Iran kufanya mashambulizi dhidi ya Israel ambayo yatapanua mzozo huo.
Marekani, Misri na Qatar zimetoa wito kwa Israel na Hamas kufanya mazungumzo ya kusitisha vita vilivyodumu kwa zaidi ya miezi kumi.
Mapema Oktoba 7, vita hivi vilizuka wakati wanamgambo wa Hamas waliposhambulia maeneo ya Israel huko Gaza, na kuua takribani Waisraeli 1,200 na kuwateka nyara wengine 240. Israel ilijibu katika kampeni inayoendelea hadi leo, ikigharimu maisha ya Wapalestina wapatao 40,000 na kujeruhi makumi ya maelfu.
Tangu siku za kwanza za kuzuka kwa vita hivyo, kumekuwa na wito mwingi wa kuzima moto wake. Ifuatayo ni mfululizo wa matukio muhimu zaidi kati ya majaribio hayo:
- Oktoba 16, 2023 : Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kutaka kusitishwa kwa mapigano mara moja , lakini Marekani, Uingereza, Ufaransa na Japan zilipiga kura kupinga azimio hilo.
- Oktoba 18, 2023 : Marekani ilizuia azimio jingine la Baraza la Usalama la kutaka "suluhisho la kibinadamu" ili kuruhusu misaada kuingia Gaza, ikisema kuwa azimio hilo halikutaja haki ya Israel ya kujilinda.
- Oktoba 25, 2023 : Marekani inapendekeza azimio la Baraza la Usalama la kutaka "kusitishwa kwa uhasama" na wakati huu ikitambua haki ya Israel ya kujitetea, lakini Urusi na China zilipinga pendekezo la Marekani, zikisema kwamba "haisaidii kutatua tatizo. .”
- Novemba 15, 2023 : Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linalotaka "kusitishwa kwa dharura na kwa muda mrefu kwa sababu za kibinadamu na kufunguliwa kwa njia na barabara," na kuachiliwa bila masharti kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas. Marekani, Urusi na Uingereza zimejizuia kupiga kura kuhusu azimio hilo. Azimio hilo halitaji usitishaji mapigano.
- Novemba 24, 2023 : Makubaliano yaliafikiwa kuhusu mapatano ya wiki moja yaliyosimamiwa na Misri na Qatar. Maandishi ya makubaliano hayo hayakuwekwa hadharani, bali yalijumuisha kuachiliwa kwa Waisraeli 80 na mataifa mengine 25 yanayoshikiliwa na Hamas, kwa kubadilishana na Israel kuwaachia huru wafungwa 240 wa Kipalestina, pamoja na kuruhusu misaada zaidi katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa.
- Desemba 8, 2023 : Marekani ilipinga pendekezo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka "kusitishwa mara moja kwa mapigano.
- Desemba 13, 2023 : Australia, New Zealand na Canada zinaungana na nchi 150 kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kudai kusitishwa kwa mapigano na kuachiliwa kwa mateka waliosalia wa Israeli. Hata hivyo, maazimio ya Baraza Kuu sio ya lazima.
- Desemba 22, 2023 : Urusi na Marekani zilijizuia kupigia kura azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka "hatua za haraka" kuruhusu misaada kuingia Gaza na "kuweka mazingira ya kukomesha uhasama endelevu." Azimio hilo linapita, lakini bila ya athari yoyote inayoonekana kwa wale walionaswa huko Gaza.
- Januari 26, 2024 : Mahakama ya Kimataifa ya Haki yapata sababu "za msingi" za madai ya "mauaji ya halaiki" ya Israel huko Gaza, na kutoa uamuzi usio wa mwisho unaoamuru Israel kuchukua hatua za haraka na madhubuti za kuruhusu huduma muhimu na misaada ya kibinadamu kuingia Gaza. Mahakama haiamuru kusitisha mapigano, hata hivyo.
- Februari 20, 2024 : Marekani ilizuia tena azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa mara moja kwa usuluhishi wa kibinadamu, lakini badala yake inasukuma mpango tofauti unaotaka "mapatano ya muda mfupi."
- Machi 25, 2024: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la "kusitisha mapigano mara moja" huko Gaza, lakini Marekani ilikataa, ikisema "haifai." Kwa msingi, azimio la Umoja wa Mataifa lina athari ndogo.
- Mei 6, 2024 : Hamas inakubali pendekezo la mara moja la kusitisha mapigano lililotolewa na Misri na Qatar. Pendekezo hilo lilitoa wito wa kubadilishana mateka na wafungwa kati ya pande hizo mbili katika hatua ya kwanza, kufuatiwa na "utulivu endelevu," kisha "kuondoka kwa wanajeshi wa Israel kutoka Gaza" na "mwisho wa kuzingirwa" kwenye Ukanda huo. Lakini Israel inakataa pendekezo hilo na inajiandaa kuivamia Rafah, ambako Wapalestina wapatao milioni 1.4 wanapata hifadhi.
- Mei 14, 2024 : Qatar inasema uvamizi wa Israel mjini Rafah tarehe 7 Mei umesababisha mazungumzo kukwama.
- Mei 24, 2024 : Mahakama ya Kimataifa ya Haki yaiamuru Israel kusitisha operesheni zake za kijeshi mjini Rafah, kufuatia ombi lililowasilishwa na Afrika Kusini, lakini mahakama hiyo haiamuru kusitishwa kwa mapigano.
- Mei 31, 2024 : Rais wa Marekani Joe Biden atangaza pendekezo la Israel la kusitisha mapigano. Pendekezo hilo linajumuisha hatua tatu: ya kwanza inaanza na usitishaji vita wa wiki sita, kuondolewa kwa majeshi ya Israel kutoka maeneo yenye watu wengi huko Gaza, na kubadilishana mateka na wafungwa kati ya pande hizo mbili. Hatua ya pili ni pamoja na kuondolewa kabisa kwa wanajeshi wa Israel kutoka Ukanda wa Gaza, huku Hamas ikiwaachilia mateka wote waliosalia, kabla ya kuhamia kusitisha mapigano ya kudumu. Hatua ya tatu ya mpango huo ni pamoja na kuzindua mchakato wa ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza.
- Juni 6, 2024 : Marekani, Argentina, Australia, Brazil, Bulgaria, Canada, Colombia, Denmark, Ufaransa, Ujerumani, Poland, Ureno, Romania, Serbia, Uhispania, Thailand na Uingereza zilitia saini taarifa ya kutaka kusitishwa kwa mapigano na kuachiliwa kwa raia wao waliokuwa wameshikwa mateka na Hamas.
- Juni 10, 2024 : Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa laidhinisha pendekezo la kusitisha mapigano linaloungwa mkono na Marekani.
- Juni 11, 2024 : Hamas na Islamic Jihad zakubaliana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kusitisha mapigano.
- Juni 23, 2024 : Katika mahojiano yake ya kwanza kwa lugha ya Kiebrania tangu vita vilipoanza, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anakataa uwezekano wa kusitisha mapigano ya kudumu, akisema, "Tumejitolea kuendeleza vita baada ya mapatano yoyote ili kufikia lengo letu la kuangamiza Hamas. "
- Julai 5, 2024 : Serikali ya Israel inatuma timu inayoongozwa na mkurugenzi wa Mossad kwenda Qatar ili kujadili pendekezo la Biden.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi








