Uchaguzi wa urais Uganda: Ni rasmi Kizza Besigye hatagombea urais nchini humo

Chanzo cha picha, Reuters
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Dr. Kizza Besigye amewaambia wafuasi wake kwamba hatagombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2021.
Alikuwa akizungumza katika ofisi za chama cha Forum for Democratic Change katika siku za mwisho za uteuzi wa wale wanaogombea urais katika chama hicho .
Besigye ambaye aliwahi kuwa daktari wa maungo wa rais Museveni alimpinga Museveni mara nne katika uchaguzi tangu 2001 lakini akapoteza mara zote hizo.
Hatahivyo amedai kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu. Alienda mahakamani kupinga matokeo hayo mwaka 2006 na 2011 katika mahakama ya juu lakini jaji akaidhinisha matokeo hayo.
Basigye awali alikataa kuzumgumza hadharani iwapo atawania uchaguzi lakini katika siku za hivi karibuni alisema kwamba taifa linafaa kumuunga mkono kiongozi wa mpito ambaye atamuunga mkono.
Uamuzi wa Dkt. Besigye wa kutogombea urais mwaka 2021 umekiacha chama cha FDC kikimtafuta atakayekiwakilisha katika uchaguzi huo.
Tayari chama hicho kimeahirisha mara mbili uteuzi wa wagombea wake wa urais kwa matumaini kuwa Dkt. Besigye angebadili msimamo wake na kuchukua fomu za uteuzi.
2019 mbunge wa upinzani Uganda Robert Kyagulanyi na mwanaharakati wa kisiasa pamoja na Dkt Kizza Besigye waliahidi kushirikiana kukiondosha madarakani chama tawala National Resistance Movement (NRM) kinachoongozwa na rais Yoweri Museveni.
Chama tawala cha NRM kimekuwa madarakani tangu 1986.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha NTV, Bwana Besigye alikataa kujibu swali juu ya iwapo atagombea urais 2021 au la.
Mara nyingi alisisitiza kuwa swali hilo ni kosa. Alisema hakuna uchaguzi utakaomng'oa madarakani Rais Museveni.
"Hatuhitaji uchaguzi ili tupate uhuru. Mkakati unaopaswa kutuandaa kupigana kwa ajili ya nchi yetu uchaguzi uwepo au la," alisema Dkt Besigye ni mpiganaji wa zamani na daktari binafsi wa Museveni wakati wa vita vyao vya msituni vya kati ya mwaka 1981 hadi 1986 vilivyoweka madarakani vuguvugu la National Resistance Movement (NRM).
Safari ya Besigye kuwania urais
Safari ya kutaka kuwania kiti cha urais nchini Uganda ya Dkt Kizza Besigye haikuwa rahisi. Mara kwa mara alikataa kufungwa na hata kupigwa na maafisa wa usalama hususan alipojaribu kutafuta haki yake kuhusu ukweli kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais.

Chanzo cha picha, BBC WORLD SERVICE
Watu walioshuhudia kukamatwa kwake walisema alikamatwa alipokuwa akijaribu kuondoka nyumbani kwake.
Alikamatwa baada ya kuwa kwenye kizuizi cha nyumbani wakati polisi walipomtuhumu kuwa alipanga kujitangazia matokeo.
Besigye alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Kira Road, Kampala baada ya kukamatwa.
Kulikuwa na habari kwamba angefika makao makuu ya Tume ya Uchaguzi kuitisha matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais, kabla ya kukamatwa kwake.
Bwana Besigye alikuwa msatari wa mbele kupinga muswada wa Januari mwaka 2019 wa kufuta kikomo cha umri wa miaka 75 ambao ulikuwa sheria mwezi Disemba 2017 uliohojiwa kwenye mahakama ya juu kabisa nchini Uganda.
Hata hivyo sheria hiyo ilipitishwa na Bunge na hivyo kumpatia fursa hasimu wake kugombea tena Urais na kumnyima fursa ya kupata kiti hicho cha ngazi ya juu zaidi nchini Uganda.
Kizza Besigye ni nani?

Kanali (Mstaafu) Dkt Kizza Besigye Kifeefe alizaliwa mwaka 1956 katika wilaya ya Rukungiri, magharibi mwa Uganda.
Besigye alifuzu kama daktari baada ya kusomea Chuo Kikuu cha Makerere, mjini Kampala.
Alijiunga na chama cha Museveni cha Uganda Patriotic Movement muda mfupi baada ya kuondolewa madarakani kwa Idi Amin 1978.
Mwaka 1982, alijiunga na Museveni vitani baada ya kuzuiliwa miezi miwili katika hoteli moja mjini Kampala akituhumiwa kushirikiana na waasi.
Baada ya Museveni kuingia uongozini, alimteua Dkt Besigye, wakati huo akiwa na umri wa miaka 29, kuwa waziri wa nchi aliyesimamia masuala ya ndani na masuala ya siasa za taifa.
Dkt Besigye alipanda cheo jeshini na kufikia cheo cha kanali.
Alistaafu muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2001, miezi michache kabla ya kujitokeza na kutangaza kwamba angewania urais.
Alipata asilimia 28 ya kura zilizopigwa akilinganishwa na mshindi, Museveni, aliyepata asilimia 69.
Baada ya kushindwa, Besigye aliwasilisha kesi Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya uchaguzi. Alishindwa kesi hiyo na akakimbilia uhamishoni Afrika Kusini akilalamikia kudhulumiwa kisiasa.
Alirejea Novemba 2005 na kuongoza chama cha FDC kwenye uchaguzi wa februari.

Chanzo cha picha, HISANI
Hata hivyo alikamatwa wiki chache baadaye na kufunguliwa mashtaka kadhaa yakiwemo yale ya uhaini na ubakaji.
Aliachiliwa huru wiki mbili baada ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi.
Besigye husifiwa sana kutokana na moyo anaoonyesha anapotoa hotuba zake na wengi wamemsifu kwa kusimama na kupinga utawala wa Museveni.
Hata hivyo, wakosoaji wake humshutumu wakisema hana uchu wa madaraka na baadhi husema hawezi kufanikisha mabadiliko yoyote kutokana na uhusiano wake wa muda mrefu na Museveni.













