Joseph Aoun: Kuanzia kamanda wa jeshi hadi kuwa rais wa Lebanon

Chanzo cha picha, EPA
Baada ya zaidi ya miaka miwili ya kudorora vikosi vingi vya kisiasa vya Lebanon vilikubali kamanda wa sasa wa jeshi, Joseph Aoun, na kumuidhinisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Lebanon, akimrithi Jenerali Michel Aoun, ambaye muhula wake ulimalizika Oktoba 30, 2022.
Aoun alipata kura 99 katika duru ya pili ya chaguzi, mchakato ulioendeshwa na bunge la Lebanon siku ya Alhamisi iliyohudhuriwa na wabunge wote 128.
Joseph Aoun anakuwa rais wa nne wa Lebanon kutokea kwenye wadhifa wa kamanda wa jeshi moja kwa moja kwenda kwenye urais wa jamhuri, wakati ambapo mikutano na mashauriano kati ya vigogo wa kisiasa yalijikita katika masaa ya mwisho ya kikao cha Alhamisi, kwa lengo la kufikia "makubaliano" kuhusu kamanda wa jeshi, huku kukiwa na shinikizo la kimataifa la kujaza nafasi ya urais, katika nchi yenye madhehebu na vyama vingi, ambapo bunge halina wingi chama cha walio wengi na rais kwa ujumla huja kwa makubaliano ya kisiasa.
Aoun alimejipata alipigiwa kushinda uchaguzi na uongozi wake umekubalika na kuungwa mkono na nchi kama vile Marekani, Saudi Arabia, na Ufaransa.
Baada ya uchaguzi wake, Aoun atahitaji mabadiliko ya kikatiba ili kushika wadhifa wake mpya, kwani katiba ya Lebanon hairuhusu uchaguzi wa watumishi wanaoshikilia nafasi za daraja la kwanza, na inahitaji kuwa na miaka miwili tangu kujiuzulu au kustaafu kwao.
Ni Kamanda yupi wa jeshi ambaye atakuwa rais wa Lebanon baada ya muda mrefu bila kiongozi wa nchi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais mpya wa Lebanon ni nani?
Joseph Aoun ni muumini wa dini ya kikristo nchini Lebanon, ambapo desturi katika nchi hiyo inahitaji Rais wa Jamhuri kuwa mkristo wa Maronite.
Rais mpya wa Lebanon alizaliwa mwaka 1964, katika mji wa Aishiyeh, kusini mwa Lebanon.
Alipata Shahada ya Kwanza katika Sayansi ya Siasa na shahada ya Sayansi ya Kijeshi, baada ya kujiunga na Chuo cha Jeshi mwaka 1983 na kuhitimu akiwa na cheo cha Luteni mwaka 1985.
Aoun alifanya kazi katika jeshi la Lebanon na kushika nyadhifa kadhaa hadi alipopandishwa cheo cha jenerali mwaka 2017. Tangu Machi mwaka huo, amekuwa kamanda wa jeshi la Lebanon.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mnamo Agosti 2017, Aoun aliongoza jeshi la Lebanon katika vita dhidi ya makundi ya shirika la Dola la Kiislamu, yaliyokuwa yakijificha katika maeneo ya milimani yanayopakana na Syria.
Wakati wa utawala wake kama kamanda wa jeshi, Lebanon pia ilishuhudia maandamano mwaka 2019 kutokana na mgogoro wa kiuchumi, na mapigano yalitokea kati ya jeshi la Lebanon na waandamanaji katika maeneo kadhaa, hasa mjini Beirut na katika mji wa Tripoli kaskazini mwa Lebanon.
Katika kipindi hiki, jeshi la Lebanon pia lilikumbwa na mgogoro wa kiuchumi, baada ya sarafu ya taifa kupoteza thamani kwa kiwango kisichokuwa cha kawaida, huku Aoun akitegemea misaada ya kigeni kutatua matatizo ya jeshi, hasa kutoka Marekani.
Hali hii ilisababisha Aoun kukosolewa kwa jeshi kukubali msaada wa Marekani kulipia mishahara ya wanajeshi baada ya kupoteza sehemu kubwa ya mishahara yao.
Akijibu, Joseph alisema, "Watu wananjaa…na jeshi pia linateseka na njaa," akisisitiza kwamba "kama usingekuwa msaada huo, hali ingekuwa mbaya zaidi."
Joseph Aoun pia alitegemea msaada kutoka nchi nyingine kuendesha jeshi lake, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, Saudi Arabia na Qatar.
Kiongozi anayoeonyesha ufanisi
Jumuiya ya kimataifa inamtegemea sana Joseph Aoun kuongoza nchi katika "awamu nyeti" inayopitia.
Mjumbe wa Marekani nchini Lebanon, Amos Hochstein, alisema wakati wa ziara yake nchini Lebanon kwamba Aoun ana sifa zinazohitajika kwa awamu inayofuata, ingawa sio yeye pekee aliye na sifa hizo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Waangalizi na wataalamu wanadhani kwamba jukumu linalohitajika kwa jeshi katika awamu inayofuata kutekeleza mapatano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah lilikuwa sababu kuu ya kumpendelea kamanda wa jeshi kuwa rais wa nchi.
Aoun atajiuzulu kutoka katika uongozi wa jeshi la nchi yake, lenye takriban wanajeshi 80,000, na katika wiki za hivi karibuni amekuwa akilenga kuimarisha uwepo wake kusini mwa Lebanon kama sehemu ya makubaliano yaliyotekelezwa tarehe 27 Novemba, kumaliza zaidi ya mwaka mmoja wa vita kati ya Israel na Hezbollah.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












