Alitoroka mabomu ya Israel mara 4, lakini akapatikana mwishowe

- Author, Joel Gunter
- Nafasi, mwandishi,Beirut
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Rihab Faour alitoroka nyumbani kwao.Na akatoroka mara nyingine hadi mara ya tatu.Mara yake ya nne kutoroka nyumbani ,mwaka mmoja baada yakutoroka kwa mara ya kwanza alikuwa akihepa mabomu ya Israel yasimpate asijue ni wapi pakukimbilia na salama kwake.
Safari yake ilianzia mwezi Oktoba 2023, wakati Hamas iliposhambulia Israel. Hilo lilisababisha Hezbollah, kundi la kisiasa na la kijeshi la Lebanon, kutuma makombora kuelekea Israel na Israel kujibu kwa kulipua maeneo ya kusini mwa Lebanon.
Mabomu ya Israeli yalilipukia karibu na kijiji alichoishi Rihab ambaye ana umri wa miaka 33 akiwa na mumewe Saeed,mfanyikazi katika kampuni ya maji ya manispaa,walikusanya mabinti zao Tia na Naya wenye umri wa miaka minane na sita mtawalia,na kutorokea nyumbani kwa Rihab eneo la Dahieh,kitongoji kilichozunguka Beirut.
Katika eneo la Dahieh,maisha yalikuwa ya kawaida ,ingawa mabinti zao walitamani marafiki zao ,vitanda walivyovizoea na nguo walizoziacha nyumbani kwao.
Na kikubwa zaidi walitamani kwenda shuleni,ambapo walikuwa wakisoma kupitia mitandao ya kijamii.
Walifurahia kuendelea na masomo yao shuleni mwezi Agosti baada ya mama yao kuwasajili katika shule mpya huko Beirut na kuwanunulia sare mpya ya shule.

Lakini kabla ya siku yao ya kwanza ya kuingia shuleni , Israel ilipanua mashambulizi yake ya anga katika maeneo ya Beirut, hasa kitongoji cha Dahieh ambacho familia hiyo ilikuwemo.
Israel ilikuwa ikiuwa viongozi wakuu wa Hezbollah katika kitongoji hicho, lakini walikuwa wakitumia mabomu makubwa yanayoweza kubomoa mahandaki, kila moja likiwa na uwezo wa kuharibu jengo la makazi.
Katika baadhi ya mashambulizi, Israel iliangusha mamilioni ya mabomu kwa wakati mmoja na kuporomoa vizuizi vya miji.
Kwa hiyo familia ya Faour ilikusanya tena na kukimbilia kwenye nyumba ya kukodi katika kitongoji kingine cha Beirut, Jnah.
Baada ya shambulio kubwa la angani huko Jnah, walihamia kwa wazazi wa Saeed katika kitongoji cha Barbour.
Huko waliishi na watu 17 katika nyumba moja - kukawa na msongamano wa watu.
Kwa Tia na Naya,ambao kwa sasa walikuwa na umri wa miaka saba na tisa mtawalia ilikuwa ni raha isiyo kifani kukutana na binamu zao usiku na mchana.
Hata babake Rihab ,ambaye ni mwajeshi wa Lebanese aliyestaafu alipoamua kuwakodishia nyumba katika eneo la Basta ili waishi ,wasichana hao walisita kuhamia eneo hilo.

“Naya alituomba tusikose kubaki hapo na familia nzima,” alikumbuka Rihab. “Tulimwambia tutakwenda kulala kwenye nyumba mpya tu, kisha turudi kwa familia na watoto wote.”
Na aliwaahidi mabinti zake - “Njoo tukae kwenye nyumba mpya, kisha mtaweza kuchagua chakula cha jioni.” Hivyo, walipokuwa wanarudi nyumbani walifanya mapumziko na kununua kuku wa kuchoma na vitafunwa kutoka dukani, na majira ya saa moja jioni, familia ilifika kwenye jengo la zamani huko Basta, katikati ya Beirut.
Katika vita ya 2006, wakati wa vita ya awali kati ya Israel na Hezbollah, mashambulizi yalikuwa yamejikita katika maeneo fulani ya Lebanon - kusini, Dahieh, na baadhi ya miundombinu.
Kwa kuwa viongozi wa Hezbollah walikuwa wameenea katika maeneo mbalimbali ya nchi, Israel ilishambulia pale walipoenda.
Na hali hii ilifanya kila mahali katika nchi hiyo kulikoaminika ni salama kukilipuliwa ikiwemo katika mwa Beirut.

Lakini Tia na Naya hawakuwa na mawazo kuhusu hayo wakati familia yao ilikuwa ikihamishia vitu kwenye nyumba mpya.
Kwa sasa, wasichana walikuwa wanajali zaidi kuhusu kurudi kwa binamu zao haraka.
Tofauti na nyumba ya wazazi wa Saeed, nyumba mpya ya Basta ilikuwa na maji ya mvua na jenereta ya umeme.
Wasichana walifurahi walipoona kwamba familia yao hatimaye ilikuwa na nafasi yao wenyewe.
Rihab na Saeed walijitahidi kupumzika kidogo.
Labda kulikuwa na ndege zisizo na rubani za Israeli zikiruka angani, lakini sauti yake ilikuwa imekuwa ya kawaida juu ya Beirut kiasi kwamba ilikuwa rahisi kuiepuka.
Rihab aliweka chakula na vitafunwa mezani. “Tulikaa kula na tulikuwa tunacheka,” alisema. “Na hiyo ilikuwa ni kumbukumbu yangu ya mwisho kuhusu watoto wangu.”

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bomu lilikuwa la aina ya Jdam, lililotengenezwa na Marekani.
Lililipuka kwenye jengo mnamo Oktoba 10 saa mbili usiku, nusu saa baada ya familia kuhamia hapo.
Lilisababisha uharibifu mkubwa kwenye ghorofa tatu na kuharibu sehemu za majengo jirani na magari, na kuua watu 22, akiwemo Saeed, Tia, Naya na watoto wengine, na kufanya shambulio hilo kuwa la kifo kikubwa zaidi katikati ya Beirut tangu mwanzo wa vita mwaka mmoja kabla.
Jeshi la Israeli halikutoa tahadhari kwa wakaazi kabla ya shambulio, kwa hivyo jengo lilikuwa limejaa watu.
Ikiripotiwa kuwa Israel ilikuwa ikimlenga Wafiq Safa, mkuu wa kitengo cha uratibu na uhusiano wa Hezbollah, lakini Safa hakuripotiwa kuwa miongoni mwa waliofariki. Alikuwa amepona, au hakuwa pale tangu mwanzo.
Hata hivyo, Jeshi la Ulinzi la Israeli lilikataa kutoa maoni kuhusu shambulio au ukosefu wa onyo kabla ya shambulizi hilo dhidi ya wenyeji.
Rihab aligutuka akiwa katika hospitali ya Zahraa mjini Beirut ,akishindwa kuinuka.
Mkono wake na mgongo ulikuwa na majeraha mabaya na alihitajiwa kufanyiwa upasuaji mara mbili.
Kumbukumbu za akicheka na mabinti zake zilikuwa zikimjia na kisha kutofahamu alijipataje hospitalini.

Alipojipumzisha usiku huo, familia yake ilikuwa ikimtafuta katika hospitali za Beirut.
Kufikia usiku wa manane, walijua kwamba Saeed na Tia walikuwa wamefariki.
Vipimo vya DNA vilihitajika kuthibitisha kuwa Naya alikuwa amekufa, pamoja na msichana mwingine wa umri wake aliyeletwa hospitalini hiyo, kwa sababu majeraha yao yalikuwa yamezuia utambuzi rahisi.
Madaktari waliokuwa wakimhudumia Rihab walishauri familia yake kutomuambia chochote kuhusu vifo vyao wanawe.
Walikuwa na wasiwasi kwamba, kwa kuwa alikua anatayarishwa kufanyiwa upasuaji, habari hiyo ingeweza kuwa nzito kwake.
Kwa hiyo kwa wiki mbili, alikua akifanya operesheni na kurejea kutoka kwa operesheni zake, mama yake Basima alimhakikishia kwamba Saeed na wasichana walikuwa wanatibiwa katika hospitali tofauti.
Lakini Rihab alihisi kuwa kuna jambo lisilo la kawaida, na alianza kuonyesha dalili za kutaka kuona picha na video za wasichana wake. “Alihisi moyoni,” alisema Basima.
Siku kumi na moja baada ya shambulio, vipimo vya DNA vilithibitisha kuwa Tia alikuwa amekufa, na siku ya kumi na tano daktari wa hospitali alimwambia Rihab kwamba Saeed na wasichana walikuwa wamefariki.

Miezi sita baadaye, Rihab alikua amekalia kiti cha plastiki katika nyumba ya kukodi huko Beirut, macho yake yakiwa meusi na uso wake ukiwa umejaa huzuni.
Alikuwa bado akiuguza majeraha kutoka kwa upasuaji wake mgongoni na kiunoni.
Alikuwa amelala kwa muda mrefu, na sasa alikuwa akijaribu kuketi na kutembea kidogo, ingawa kila alifanyalo ilimletea maumivu makali.
Siku ya kusherehekea miaka nane ya Naya ilikuwa siku nne kabla ya tukio hilo. Rihab alikuwa akitumia wakati wake “ima kulia au kulala,” alivyosema. Lakini alitaka kuzungumza kuhusu familia yake.
“Naya alikuwa kipenzi changu sana, alinifuata popote nendapo. Tia alizipenda sana familia za mababu na alifurahia nikienda kumwacha na mababu zake.Wasichana wote wawili walipenda kuchora, walipenda kucheza na midoli, walikosa kwenda shuleni. Walikuwa wakicheza wakiigiza kuwa mwalimu na mwanafunzi kila wakati.”

Kikubwa zaidi walipendelea kutazama video pamoja hasa Tiktok.
Rihab na Saeed waliamua kuwa walikuwa wadogo sana kuanza kuchapisha picha zao mtandaoni ,Rihab alikuwa akiwanasa kwa video wakidensi na kuwahadaa kuwa amezichapisha mitandaoni na walifurahia kusikia hivyo.
Saeed alikutana na Rihab mwaka 2013.
Rihab alilelewa Beirut lakini familia yake ilikuwa na mazoea ya kutembelea kijiji cha Mays El Jabal msimu wa joto ,kwasababu kulikuwa na upepo baridi kutokana madhari yakijiji na msimu huo wa joto walikutana na Saeed kupitia marafiki wa karibu.
Rihab alihitimu shahada yake ya uanasheria na kuanza masomo ya uzamili ,lakini wawili hao walifunga ndoa na Tia akazaliwa na Rihab akaamua kusitisha ndoto yake ya kuwa wakili ili alee mtoto wake.
Sasa ,akiwa katika hali ya majonzi ,ameanza kufikiria kuendeleza masomo yake.
“Nitahitaji kitu cha kujaza siku zangu,” alisema.

Saeed na Tia walizikwa siku moja baada ya kufariki, na baba wa Rihab na wajomba zake waliwazika kwenye jeneza la muda la mbao kwenye kaburi lisilokuwa na alama huko Dahieh.
Wiki mbili baadaye, wanaume wa familia walichimba tena kwenye sehemu ile ile na kumzika Naya.
Mjomba wa Rihab aliweka shada mbili za maua ya cheri ya bandia juu ya kaburi, kwa ajili ya wasichana wawili, na baadaye mtu mwingine akaweka shada la maua kwa mgeni aliyezikwa kando yao.
Isitoshe, shambulio la anga la Israeli lilipiga jengo lilio karibu na kaburi, na mtikisiko wa mlipuko pamoja na vifusi vilivunja mawe ya makaburi na kuchimbua ardhi karibu nayo.
Siku chache baadaye, shambulio lingine la anga la Israeli lililenga nyumba ya familia yao huko Dahieh, likiharibu vitu kadhaa ambavyo Rihab alitaka kuvihifadhi, ikiwemo sare mbili mpya za shule za mabinti zake ambazo hawakuzivaa.
Haijachukua muda tangu mkasa huo ,hali ya utulivu ikarejea.
Kusitishwa kwa mapigano yaliyotangazwa wiki iliyopita kuliwaruhusu maelfu ya watu waliokimbia kurudi vijijini mwao kusini mwa Lebanon.
Kijiji cha Rihab na Saeed kilikuwa kimepigwa mabomu sana na Waisraeli na nyumba yao huko imeharibiwa, alisema mjomba wake, lakini Rihab hawezi kurudi nyumbani kwa sasa, kwa sababu ana mkanda wa mgongo kwa miezi kadhaa na hawezi kusafiri.
Wakati furaha ikienea Lebanon kwa habari za kusitishwa kwa mapigano, picha mpya zilionyesha Wafiq Safa, ambaye alikuwa amelengwa na bomu lililoua Saeed, Tia, Naya na wengine 19.
Safa alikuwa hajaonekana hadharani tangu shambulio hilo, lakini ameonekana kuwa mzima na mwenye afya njema.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












