Walionusurika waelezea shambulio la Israel huko Beirut ambalo liliua watu 18

df

Chanzo cha picha, BBC/Goktay Koraltan

Maelezo ya picha, "Hakuna Hezbollah hapa," mwanamke huyu aliyefadhaika kichwa alisema. "Sisi sote ni raia"
    • Author, Orla Guerin
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Mohammed Sukayneh alipitia kwenye vifusi, akiwa ameshika mifuko michache ya plastiki – imebeba vitu alivyovipata kutoka katika nyumba yake ya miaka 45.

Ilishambuliwa yeye akiwemo na familia yake jana usiku katika shambulio la anga la Israel, ambalo liliua watu 18, wanne kati yao wakiwa watoto, kulingana na Wizara ya Afya ya Lebanon.

Shambulio hilo lilitokea bila ya onyo - mita 150 kutoka lango la hospitali kubwa ya umma ya Lebanon, ya Rafik Hariri kusini mwa Beirut.

Muhammad na familia yake walikuwa wamelala vitandani.

"Tulisikia sauti kama 'boom. Na kila kitu kikatuangukia juu yetu. Mawe, chuma, damu, nyama za watu. Huweza kuongea, huweza kupumua.”

Anasema majirani watano bado wako chini ya kifusi cha nyumba yao. Na kulikuwa na wengine, waliouawa papo hapo, katika mtaa wao - ikiwa ni pamoja na wasichana wawili wenye umri wa miaka 19 ambao walikuwa wameketi nje ya mlango wake.

Mohammed, 54, alinusurika kwa kupata michubuko ya mkono, lakini mpwa wake mwenye umri wa miaka 20 sasa yuko katika chumba cha wagonjwa mahututi. "Nusu ya ubongo wake umepondwa," anasema.

Mlinzi wa raia katika eneo la tukio alituambia majengo sita ya makazi yameharibiwa, mengi yao yakiwa na ghorofa tatu au nne kwenda juu.

Mwanamke aliyejifunika utaji aliketi chini, mikono yake ikiwa juu ya kichwa, akitetemeka kwa huzuni. "Hakuna Hezbollah hapa," alisema, "sisi sote ni raia."

Dakika chache baadaye mabaki mengine ya miili yalitolewa kwenye kifusi na kubebwa kwenye mfuko mweusi.

Nilimuuliza Mohammed, anafikiri kwanini Israel imeshambulia eneo hili, lenye watu wengi.

"Wanashambulia kila kitu bila mpangilio," alijibu, kwa sauti ya hasira.

“Bila kujali kuna watoto. Bunduki ziko wapi hapa? Roketi ziko wapi hapa? Vipofu, maadui Israel. Vipofu.”

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema lilishambulia "eneo la Hezbollah karibu na hospitali" bila kutoa taarifa zaidi kuhusu sahaba hiyo. Linasema hospitali yenyewe haikulengwa au kupigwa.

Mkurugenzi wa hospitali ya Rafik Hariri, Jihad Saadeh alisema ilipigwa na vipande vya mawe lakini inafanya kazi kama kawaida na wagonjwa hawatahamishwa.

Pia unaweza kusoma

Ziara ya BBC

tr

Chanzo cha picha, BBC/Goktay Koraltan

Maelezo ya picha, Jumatatu asubuhi, shambulio la anga liliharibu majengo ya makaazi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini hospitali binafsi ya Al Sahel, iliyo umbali wa kilomita 2, watu walihama jana usiku. Uhamisho wa haraka wa wagonjwa 10 na wafanyikazi 50 ulikuja baada ya madai ya jeshi la Israel kwamba hospitali hiyo ina handaki la Hezbollah, lililojaa pesa.

IDF haikutoa uthibitisho lakini ilitoa picha za 3D, ikidai kuonyesha handaki chini ya jengo hilo. "Kuna mamilioni ya dola taslimu na dhahabu ndani ya handaki," alisema msemaji wa IDF, Rear Adm Daniel Hagari.

Madaktari na wasimamizi wa hospitali walikusanyika kukanusha madai waliyoyaita ya "uwongo ya Israel" na kuipa BBC ruhusa ya kuzuru, ikiwa ni pamoja na ghorofa mbili chini ya ardhi.

Hospitali hiyo iko katika vitongoji vya kusini, ngome ya Hezbollah, lakini wafanyakazi wanasisitiza haihusiani na kundi lolote.

"Inashangaza sana kusema Hospitali ya Sahel ina uhusiano na chama chochote nchini Lebanon," anasema Dk Alameh. “Ni hospitali binafsi. Ni hospitali ya kufundishia madaktari na wanafunzi wengine wa matibabu."

Alitupilia mbali madai ya Israel. "Hospitali ilianzishwa miaka 40 iliyopita kwenye nyumba ya zamani," alisema.

"Haiwezekani kuwa na handaki au miundombinu yoyote chini. Mtu yeyote duniani anaweza kuja hapa na kuona kila kitu anachotaka.”

Tulihimizwa kuangalia kila kona. Hakuna mahali ambapo tulizuiwa kuangalia, hata chumba cha kuhifadhi maiti. Mafurushi na vyombo vya upasuaji yalifunguliwa ili kuonyesha hakuna kitu kilichofichwa.

Baada ya ziara, tuliruhusiwa kuzunguka kwa uhuru. Tuliona wodi tupu na wafanyakazi wenye wasiwasi, lakini hakuna kiashiria cha handaki.

Israel ilidai mlango wa handaki uko katika jengo jirani. Tulikwenda kwenye jengo hilo pia na tukaruhusiwa kuingia katika maegesho iliyo chini. Ikiwa kulikuwa na mlango wa handaki la siri, sisi hatukuuona.

Mlango pekee tuliouona ulituongoza kwenye lifti ambayo hatukuweza kuiufungua. Lakini mlango huo haukuwa umefichwa, na haukuonekana kuwa ni mlango wa kukupeleka kwenye handaki lenye chumba kilichojaa dhahabu.

Wakati tunaondoka hospitalini ndege isiyo na rubani ya Israeli ilikuwa ikizunguka. Israel inasema jeshi lake la anga "linafuatilia eneo hilo lakini halitaishambulia hospitali yenyewe."

Kwa sasa, Al Sahel bado imefungwa, lakini madaktari wanataka kurejea kuwatibu wagonjwa.

Mchana wa leo Israel imeshambulia Beirut tena, mwendo mfupi wa gari kutoka hospitalini, kwenye eneo la Hezbollah.

IDF ilitoa onyo, ikiwaambia wakazi wa majengo mawili ya karibu kuondoka kwani "yako karibu na majengo ya Hezbollah."

Nusu saa baadaye majengo mawili ya ghorofa yalitoweka kwenye anga, na mawingu meusi ya moshi na majivu yalitanga.

Katika nyumba, na hospitali, watu wengi wanakabiliwa na hofu.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla