Watu 18 wameuawa katika shambulio la Israel kaskazini mwa Lebanon

Ripoti zinaonyesha majeruhi wengi ni katika eneo lenye Wakristo wengi kaskazini mwa nchi hiyo.

Muhtasari

  • Uingereza yatangaza vikwazo dhidi ya maafisa wa kijeshi wa Iran
  • Timu ya taifa ya Nigeria yaagizwa kurejea nyumbani
  • Watu tisa wameuawa katika shambulizi la kaskazini mwa Lebanon, maafisa wanasema
  • Israel inasema ilidungua ndege mbili zisizo na rubani kutoka Syria
  • Mtu aliyekuwa na bunduki akamatwa karibu na mkutano wa Trump na kuachiliwa
  • Zimbabwe yarekodi maambukizi ya kwanza ya Mpox
  • Timu ya Nigeria kutocheza mechi ya kufuzu ya Afcon 2025 na Libya
  • DR Congo, Rwanda zakubaliana juu ya mpango wa usalama wa mashariki mwa DRC
  • Wakenya waonywa dhidi ya kwenda Myanmar huku visa vya utekaji nyara, utumwa vikiongezeka
  • Mwanariadha wa Kenya Chepngetich avunja rekodi ya dunia ya mbio za Chicago Marathon
  • Bloomberg yaripoti kuhusu uharibifu wa shambulio la Iran dhidi ya majengo ya makazi nchini Israeli
  • Tazama: Ndege za kivita za Taiwan zapaa kujibu mazoezi ya China
  • Mashambulizi ya makombora ya Israel dhidi ya shule ya Gaza yawaua takriban watu 15
  • Tazama: Video ya China ikionyesha uwezo wake wa kijeshi
  • China yaizunguka Taiwan kwa mazoezi ya jeshikama 'adhabu' kwa hotuba ya rais
  • Shambulio la ndege zisizo na rubani lawaua wanajeshi wanne wa Israel na kuwajeruhi zaidi ya 60

Moja kwa moja

Na Dinah Gahamanyi & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo.Kwaheri.

  2. Uingereza yatangaza vikwazo dhidi ya maafisa wa kijeshi wa Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Uingereza imetangaza vikwazo dhidi ya maafisa wa kijeshi wa Iran na mashirika kufuatia shambulio lake la Oktoba 1 dhidi ya Israel.

    Orodha hiyo inajumuisha Abdolrahim Mousavi, kamanda wa jeshi la Iran na mjumbe wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran na Hamid Vahedi, kamanda wa jeshi la anga la Iran.

    Watu waliowekewa vikwazo watakuwa chini ya marufuku ya kusafiri na mali zao kuzuiliwa, Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilisema.

    Shirika la Anga za Juu la Iran, ambalo linatengeneza teknolojia ambazo zinatumika katika uundaji wa makombora ya balestiki, pia litakuwa chini ya mali zinazozuiliwa.

    Iran ilirusha zaidi ya makombora 180 ya balistiki kuelekea Israel tarehe 1 Oktoba.

    Jeshi la Israel limesema makombora mengi yalinaswa. Mtu pekee aliyeripotiwa kuuawa alikuwa Mpalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

    Soma zaidi:

  3. Timu ya taifa ya Nigeria yaagizwa kurejea nyumbani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa michezo wa Nigeria, Seneta John Enoh ameagiza timu ya Super Eagles iliyokwama nchini Libya tangu Jumapili mchana kurejea nyumbani, akisisitiza kuwa 'wasiwasi wa Serikali na watu wa Nigeria ni usalama wa timu na kurejea kwao salama.'

    Katika taarifa yake kwenye akaunti ya mtandao wa X iliothibitishwa, Enoh alisema amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais na Katibu Mkuu wa CAF, ambao walielezea wasiwasi wao lakini akaomba timu iruhusiwe kucheza mechi iliyopangwa.

    Alisema 'Shirikisho la Soka la Nigeria limeagizwa kuwasilisha malalamiko rasmi kwa CAF bila kuathiri hatua zozote ambazo tayari zimechukuliwa,' huku akitaka shirikisho hilo la soka barani kuchukua hatua dhidi ya Shirikisho la Soka la Libya.

    Following the statement by Enoh, the Super Eagles are now set to depart Libya after a 16-hour ordeal that has left the players fatigued and helpless.

    Kufuatia kauli ya Enoh, Super Eagles sasa wanatarajiwa kuondoka Libya baada ya kukaa uwanja wa ndege kwa saa 16, wachezaji wakiachwa na machovu na kukosa la kufanya.

    Wakati huo huo, Shirikisho la kandanda barani Afrika (CAF) limetoa taarifa likisema kwamba limekuwa na mawasiliano na mamlaka ya Libya na Nigeria baada ya kuarifiwa kuwa Timu ya Taifa ya Kandanda ya Nigeria (''Super Eagles'') na timu yao ya ufundi walikuwa wamekwama katika mazingira ya kutatanisha kwa saa kadhaa katika uwanja wa ndege ambao wanadaiwa kuagizwa kutua na mamlaka ya Libya.

    Suala hilo limewasilishwa kwenye Bodi ya Nidhamu ya CAF kwa uchunguzi na hatua stahiki zitachukuliwa kwa waliokiuka Sheria na Kanuni za CAF.

    Soma zaidi:

  4. Watu 18 wameuawa katika shambulio la Israel kaskazini mwa Lebanon

    Shirika la Msalaba Mwekundu la Lebanon pia limetoa taarifa, likisema watu 18 wameuawa na wanne wamejeruhiwa.

    Wakati huo huo, maafisa wa Lebanon wamesema shambulizi la Israel katika mji wa Aitou mkoa wa Zgharta kaskazini mwa Lebanon limesababisha mauaji ya watu tisa na mtu mmoja kujeruhiwa, huku shughuli za uokoaji zikiendelea.

    Hii itakuwa ni mara ya kwanza Israel kulenga eneo lenye Wakristo wengi katika kipindi cha mwaka wa mapigano tangu mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba mwaka jana.

    Israel bado haijatoa maoni yoyote kuhusu shambulizi lililoripotiwa.

  5. Israel inasema ilidungua ndege mbili zisizo na rubani kutoka Syria

    Saa chache zilizopita, jeshi la Israel limesema kuwa lilidungua ndege mbili zisizo na rubani zilizokuwa zikielekea Israel kutoka Syria.

    Ndege hizo zisizo na rubani zilinaswa na IDF kabla ya kuingia katika eneo la Israel, jeshi linasema.

    Vyombo vya habari vya Lebanon vinasema miji ya kusini imeshambuliwa na Israel

    Wakati huo huo, katika mfululizo wa tahadhari, vyombo vya habari vya serikali ya Lebanon vinasema kuwa Israel imefanya mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa kusini mwa nchi hiyo.

    Miji ya Kharayeb, Tire na Nmairrieh yote ilikumbwa na mashambulizi siku ya Jumatatu, Shirika la Habari la Kitaifa (NNA) limeripoti.

    Jeshi la Israel halijatoa maelezo zaidi, lakini awali lilisema "linaendelea na operesheni dhidi ya miundombinu ya kigaidi kusini mwa Lebanon".

    Asubuhi ya leo, IDF iliamuru watu katika vijiji 25 kusini mwa Lebanon kuhama.

  6. Mtu aliyekuwa na bunduki akamatwa karibu na mkutano wa Trump na kuachiliwa

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Mwanamume aliyekuwa na bunduki kinyume cha sheria na nyingine iliyojaa silaha alikamatwa kwenye makutano karibu na mkutano wa hadhara wa Donald Trump huko Coachella, California, Jumamosi, polisi walisema.

    Mshukiwa mwenye umri wa miaka 49, Vem Miller, alikuwa akiendesha gari nyeusi aina ya SUV aliposimamishwa katika kituo cha ukaguzi cha usalama, na kupatikana na bunduki hizo mbili na "kifaa maalum cha kuhifadhi kiasi kikubwa cha silaha".

    Kisha Bw Miller aliwekwa kizuizini, ofisi ya Sheriff ya Kaunti ya Riverside ilisema, na kuandikishiwa taarifa za kumiliki bunduki iliyojaa silaha na kumiliki kifaa cha uwezo mkubwa wa kuhifadhi silaha. Baadaye aliachiliwa.

    Huduma Maalum ya Usalama Marekani ilisema Trump "hakuwa katika hatari yoyote", na kuongeza kuwa tukio hilo halikuathiri shughuli za ulinzi.

    Soma zaidi:

  7. China 'yaadhibu' matamshi ya rais wa Taiwan na mazoezi mapya

    th

    Chanzo cha picha, EPA

    China siku ya Jumatatu ilianzisha mazoezi mapya ya kijeshi katika pwani ya Taiwan katika kile ilichoeleza kama "adhabu" kwa hotuba iliyotolewa na rais wake William Lai, alipoapa "kupinga kunyakuliwa" au "kuingilia uhuru wetu".

    China inadai kisiwa kinachojitawala cha Taiwan kuwa chake na rais wake Xi Jinping ameapa kukitwaa tena kwa nguvu ikiwa itabidi.

    Taiwan ilisema iligundua meli 34 za majini na ndege 125 zikiwa zimepangwa kuzunguka kisiwa hicho siku ya Jumatatu.

    Ramani zilizochapishwa na vyombo vya habari vya serikali ya Uchina zilionyesha vikosi vyake viko karibu na kisiwa kizima. Ilisema baadaye Jumatatu kwamba mazoezi hayo yamekamilika kwa mafanikio.

    Jeshi la China, linalojulikana kama Jeshi la Ukombozi wa Watu (PLA) lilisema mazoezi hayo yalihusisha vitengo vyote vya jeshi na yalipangwa kuiga kushambulia Taiwan kwa nchi kavu, baharini na angani.

    Kapteni Mkuu Li Xi, msemaji wa Kamandi ya Mashariki ya PLA alisema mazoezi "yalijaribu kikamilifu uwezo wa pamoja wa operesheni ya pamoja" ya askari wake.

    Viwanja vya ndege na bandari za Taiwan ziliendelea kufanya kazi kama kawaida.

    Taarifa ya awali ya wizara ya ulinzi ya Taiwan ililaani hatua hiyo ya China na kusema kipaumbele chake ni kuepusha makabiliano ya moja kwa moja ambayo yanaweza kuzidisha mzozo huo. Visiwa vya nje viliwekwa katika hali ya tahadhari, iliongeza.

    Soma pia

  8. Zimbabwe yarekodi maambukizi ya kwanza ya Mpox

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wizara ya afya imethibitisha visa viwili vya maambukizi ya Mpox nchini Zimbabwe.

    Mgonjwa wa kwanza ni mvulana mwenye umri wa miaka 11 huko harare huku wa pili akiwa na umri wa miaka 24 kusini mwa nchi hiyo.

    Wote wawili walikuwa wamesafiri nje ya nchi hivi majuzi.

    Wagonjwa wote wako katika hali thabiti na wanaendelea kupata afueni wakiwa wamejitenga majumbani mwao.

    Kufikia sasa zaidi ya nchi 15 zimethibitisha maambukizi ya virusi vya Mpox.

    Afrika imeripoti maambukizi zaidi ya elfu saba na mia tano na vifo zaidi ya 30 kufikia sasa mwaka huu.

    Shirika la Afya Ulimwenguni lilitangaza mlipuko huo kuwa dharura ya afya ya umma ambayo inatia wasiwasi kimataifa huku ugonjwa huo ukiendelea kuenea.

    Soma zaidi:

  9. Nigeria kususia mechi ya kufuzu Afcon nchini Libya

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Nahodha wa Nigeria, William Troost-Ekong alielezea walivyopokelewa nchini Libya kama "mchezo wa kuwavuruga akili"

    Timu ya Nigeria ambayo imekuwa katika uwanja wa ndege wa Al-Abraq nchini Libya tangu Jumapili imeamua kutocheza mechi ya kufuzu kwa mashindano ya Afcon 2025 dhidi ya Mediterranean Knights baada ya kukabiliwa na mazingira magumu tangu wawasili nchini humo.

    Kulingana na taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) Jumatatu asubuhi, ‘’wachezaji wameamua kutocheza tena mechi hiyo huku maafisa wakipanga mipango ya kuirejesha nyumbani timu hiyo.’’

    NFF pia ilishutumu Shirikisho la Soka la Libya kwa kutotuma timu yoyote ya mapokezi au hata magari ya kuwachukua wajumbe kutoka uwanja wa ndege hadi hoteli yao, ambayo ni saa 3 kutoka Benghazi.

    Kwa sasa Nigeria wanaongoza Kundi D la mchujo wakiwa na pointi 7, huku Libya wakiwa mkiani kwa pointi 1 pekee.

    Kwa mujibu wa Kifungu cha 18 cha kanuni ya mashindano ya CAF, Shirikisho mwenyeji ina jukumu la kuhakikisha usalama wa usafiri wa timu inayokuja ugenini na kuchukuliwa kwa wakati, haswa ikiwa umbali wa kusafiri kutoka mahali pa kuwasili hadi uwanjani unazidi kilomita 200.

    Sheria hiyo pia inasema kwamba ikiwa ucheleweshaji mkubwa utazuia timu kufika kwa wakati au kufanya mazoezi ya kutosha, hii itakuwa chini ya "sababu zisizoweza kutabirika" na CAF inaweza kupanga upya mechi ili kuhakikisha uchezaji wa haki.

    Shirikisho la Soka la Libya (LFF) lilisema "lina wasiwasi mkubwa" na ripoti kuhusu hali ya wasafiri lakini likakanusha mapendekezo ya mchezo mchafu.

    "Tuna heshima kubwa kwa wenzetu wa Nigeria na tunataka kuwahakikishia kwamba kubadilishwa kwa safari yao ya ndege haikuwa kwa makusudi," ilisema.

    LFF iliongeza kuwa usumbufu unaweza kutokea kutokana na itifaki za kawaida za trafiki ya anga, ukaguzi wa usalama au changamoto zingine za vifaa na ikasema inatumai kutokuelewana huko "kunaweza kutatuliwa kwa maelewano na nia njema".

    Mchezai Victor Okoh Boniface ambaye pia anacheza kama mshambuliaji wa klabu ya Bundesliga Bayer Leverkusen kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa X, amesema hali inazidi kuwa ya kutisha na kuomba waruhusiwe kurejea Nigeria, hata kama itamaanisha kupoteza pointi tatu.

    .

    Chanzo cha picha, X/Victor Okoh Boniface

    Waziri wa michezo Seneta John Owan Enoh, amelaani walichofanyiwa wachezaji wa Super Eagles waliowasili Libya na maafisa wengine wa Timu ya Taifa kupitia mtandao wake wa Twitter.

    .

    Chanzo cha picha, Senator John Owan Enoh/ Twitter

    Shirikisho la Soka barani Afrika limetumiwa ombi la kutoa maoni yake.

    Hali hii inafuatia malalamiko ya Libya ya madai ya kutendewa visivyo wakati wa ziara yao nchini Nigeria kwa ajili ya mechi ya marudiano huko Uyo Ijumaa iliyopita.

    Maafisa wa Libya walidai kuwa walisafirishwa hadi Port Harcourt na pia waliwashutumu Wanigeria hao kwa kutowapa basi la kusafiri umbali wa kilomita 130 hadi Uyo, na kuwaacha wamekwama kwa saa nyingi.

    Pia unaweza kusoma:

  10. DR Congo, Rwanda zakubaliana juu ya mpango wa usalama wa mashariki mwa DRC

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    DR Congo na Rwanda wametia saini juu ya mpango wa usalama wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambao hatimaye unaweza kusababisha kuondolewa kwa maelfu ya wanajeshi ambao Kigali inaaminika kuwapeleka katika eneo lenye machafuko, tovuti ya habari ya kibinafsi ya Actualite imeripoti.

    Tangazo kuhusu makubaliano hayo lilitolewa na serikali ya Angola, ambayo ni mpatanishi wa Umoja wa Afrika (AU) wa mzozo wa mashariki mwa DR Congo, lakini uthibitisho rasmi bado haujatolewa na nchi hizo mbili.

    Actualite ilisema mawaziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Rwanda walifikia makubaliano mjini Luanda juu ya "mpango uliooanishwa" wa "kuondoa" kundi la waasi wa Kihutu lililoundwa na wahusika wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, FDLR.

    Ilisema kuwa mpango wa kina utafanyiwa kazi katika mazungumzo yajayo kati ya pande hizo mbili.

    Majaribio ya hapo awali ya kukamilisha makubaliano hayo, ambayo maelezo yake yalitolewa wakati wa mazungumzo ya siri mwezi Agosti kati ya wakuu wa kijasusi wa nchi hizo mbili, yalishindwa kutekelezwa huku kila upande ukitaka upande mwingine utimize wajibu wake kwanza.

    Actualite alibainisha kuwa wajumbe hao wawili pia walisisitiza umuhimu wa kuheshimu usitishaji mapigano ulioyumba kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 wanaotawaliwa na Watutsi.

    Soma zaidi:

  11. Wakenya waonywa dhidi ya kwenda Myanmar huku visa vya utekaji nyara, utumwa vikiongezeka

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Kenya kwa mara nyingine tena imewaonya raia wake kutosafiri kwenda katika nchi ya Myanmar.

    Myanmar imekuwa ikikabiliwa na mzozo wa muda mrefu na hivyo kusababisha kuwepo kwa mazingira mazuri ya utumwa na uhalifu.

    Balozi wa Kenya nchini Thailand Kipness Lindsay Kimwole amewataka Wakenya kutotuma maombi katika nchi hiyo iliyopo kusini mwa bara Asia baada ya kubainika kwa taarifa ghushi za kazi mtandaoni.

    Ubalozi wa Kenya kwa mara ya kumi na moja unawaonya Wakenya dhidi ya kusafiri Kwenda Myanmar. ‘‘Onyo hilo linakuja huku vijana wengi wa Kenya wakiomba usaidizi wa makundi ya walaghai, huku wengine wakiendelea kuwa watumwa wa makundi ya wahalifu nchini China’’, Balozi Kimwole alisema katika taarifa yake ya tarehe 12 Oktoba, 2024.

    Ubalozi huo umesema kuwa Wakenya 10 kwasasa wamekwama katika nchi hiyo, huku watekaji nyara wakiomba mamilioni ya pesa kama kikombozi ili wawaachilie.

    Umeelezea wasiwasi wake kutokana na baadhi ya Wakenya kuendelea kutuma maombi ya kazi mynmar, licha ya tahadhari zake za awali.

  12. Mwanariadha wa Kenya Chepngetich avunja rekodi ya dunia ya mbio za Chicago Marathon

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Rekodi ya dunia ya Chicago Marathon imevunjwa na Ruth Chepngetich

    Mwanariadha wa Kenya Ruth Chepngetich amevunja rekodi ya dunia kwa kushinda mbio za masafa marefu za Chicago Marathon Jumapili.

    Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 30 alitumia muda wa saa mbili, dakika tisa na sekunde 57 na hivyo kupita rekodi ya awali ya Tigst Assefa wa Ethiopia kwa karibu dakika mbili.

    Chepngetich ndiye mwanamke wa kwanza kukimbia marathon chini ya saa mbili na dakika 10.

    Assefa aliweka rekodi ya awali kwa ushindi wa Berlin Marathon 2023 kwa saa mbili, dakika 11 na sekunde 53.

    "Ninajisikia vizuri sana, ninajivunia. Hii ni ndoto yangu ambayo imetimia," alisema Chepngetich, bingwa wa dunia wa marathon 2019.

    "Nimepigana sana nikifikiria rekodi ya dunia na nimeitimiza."

    Ushindi kwa Chepngetich ni wa tatu kwake huko Chicago, ambapo alishindwa kuvunja rekodi ya dunia ya wakati huo ya Brigid Kosgei kwa sekunde 14 mnamo 2022 .

    Mashindano manne ya mbio za Marathon kati ya matano ya kasi zaidi ya wanawake yamekuwa yaikifanyika Chicago katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

    Mshindi wa wanaume Korir ampa heshima Kiptum

    Katika kinyang'anyiro cha wanaume, Mkenya John Korir alikimbia muda wake wa kibinafsi na kujinyakulia ushindi kabla ya kutoa heshima kwa mwanariadha anayeshikilia rekodi ya dunia Kelvin Kiptum, ambaye alishinda rekodio hiyo mwaka jana.

    Korir aliibuka kutoka kwa kundi la wakimbia saba waliokuwa wakiongoza na kumaliza mbio hizo kwa saa mbili, dakika mbili na sekunde 44.

    Mohamed Esa wa Ethiopia alikuwa wa pili, huku Amos Kipruto, aliyemaliza wa tatu, akiwa mmoja wa Wakenya wanne katika tano bora.

    Kiptum aliweka rekodi ya sasa ya dunia ya saa mbili na sekunde 35 mjini Chicago, miezi minne kabla ya kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 24 katika ajali ya gari , na Korir alisema alitumia rekodi ya mwenzake kama motisha siku ya Jumapili.

    "Ilikuwa vizuri sana kukimbia (BP) yangu (mbio binafsi) na kushinda huko Chicago," Korir alisema.

    "Leo nilikuwa nikifikiria kuhusu Kiptum na nikasema 'mwaka jana kama angeweza kukimbia chini ya 2:01, kwa nini isiwe mimi?' Kwa hivyo ilibidi nijiamini na kujaribu kuwa bora mwenyewe."

    Unaweza pia kusoma:

  13. Bloomberg yaripoti kuhusu uharibifu uliofanywa na shambulio la Iran nchini Israeli

    g

    Chanzo cha picha, Getty

    Maelezo ya picha, Uharibifu wa shule kutokana na shambulio la kombora la Iran la tarehe 1 Oktoba dhidi ya Israel

    Kituo cha habari cha Bloomberg kimekadiria uharibifu uliosababishwa wa nyumba na mali binafsi nchini Israel wakati wa shambulio la hivi karibuni la kombora la Iran kuwa ni karibu shekeli milioni 150 hadi 200, sawa na dola milioni 40 hadi 53.

    Ikizungumzia takwimu za shirika la ushuru la Israel, Bloomberg ilitangaza kuwa katika wiki mbili zilizopita, wamiliki wa nyumba za makazi 2,500 na maeneo ya biashara wamechukua hatua ya kuchukua bima.

    Nusu ya ripoti hizi zinahusiana na vitongoji vya kaskazini mwa Tel Aviv.

    Kwa mujibu wa Bloomberg, karibu nyumba 1,000 ziliharibiwa katika mji wa Hod Hasharon katikati mwa Israel.

    Shule moja pia imeharibiwa kusini mwa mji wa Tel Aviv.

    Kwa mujibu wa Bloomberg, haijulikani ni kiasi gani cha uharibifu ulioripotiwa unahusiana na makombora ya Iran na kiasi gani cha makombora hayo husababishwa na kuanguka kwa makombora ya ulinzi.

    Uharibifu unaosababishwa na makombora katika ngome za kijeshi za anga za Novatim na Telenov hauzingatiwi katika ripoti hii pia.

    Shambulio la kombora la Iran la tarehe 1 Oktoba dhidi ya Israel lilifanyika kama ulipizaji kisasi kwa mauaji ya Hassan Nasrallah, kiongozi wa Hezbollah, na Ismail Haniyeh, kiongozi wa Hamas, mjini Tehran.

    Hili ni shambulio la pili la moja kwa moja la Iran dhidi ya Israel, ambapo mfanyakazi mmoja tu wa Kipalestina aliuawa.

    Katika kujibu mashambulizi hayo, Marekani imetangaza kuwa itaipa Israel mfumo wa kupambana na makombora wa THAAD ili kuisaidia Israel kujilinda.

    Unaweza pia kusoma:

  14. Tazama: Ndege za kivita za Taiwan zapaa kujibu mazoezi ya China

    Picha zilizotolewa na shirika la habari la AFP zinaonyesha ndege za kivita za Taiwan zikiruka na kutua katika ngome ya vikosi vya anga ya Hsinchu kaskazini-mashariki mwa kisiwa hicho.

    Pia walirekodi gari la jeshi la nchi kavu linaloongozwa kwa mitambo kwenye eneo la ngome hiyo.

    Hapo awali, wizara ya ulinzi ya Taiwan ilithibitisha kuwa ndege na meli zimetumwa ili kukabiliana na kupelekwa kwa jeshi kubwa la China kwenye pwani yake.

    Maelezo ya video, Tazama : Ndege za kivita za Taiwan zikipaa kutoka kenye ngome yake

    Wakati huo huo kiongozi wa Taiwan amejibu kuhusu mazoezi ya kijeshi ya China.

    Ofisi ya Rais wa Taiwan William Lai imesema China inapaswa "kuheshimu chaguo la watu wa Taiwan la maisha huru na ya kidemokrasia, kujiepusha na chokochoko za kijeshi".

    Ilisema kudumisha amani na utulivu katika pande zote za mlango wa bahari wa Taiwan ni "jukumu la kawaida".

    "Serikali yetu itaendelea kutetea mfumo wetu wa kikatiba wa demokrasia na uhuru. Tuna imani na uwezo wa kulinda usalama wa taifa," ilisema.

    Unaweza pia kusoma:

  15. Mashambulizi ya makombora ya Israel dhidi ya shule ya Gaza yawaua takriban watu 15

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Takriban Wapalestina 50 pia walijeruhiwa katika shambulizi la makombora katika shule ya al-Mufti katikati mwa Gaza

    Shambulizi la Israel dhidi ya shule inayotumika kuwahifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao limewaua takriban watu 15 katikati mwa Gaza, maafisa wanasema.

    Shirika la Ulinzi la Raia la Gaza linaloendeshwa na Hamas lilisema eneo la kambi ya Nuseirat lilipigwa na mizinga siku ya Jumapili, na kuua familia nzima huku makumi ya watu wengine wakijeruhiwa.

    Jeshi la ulinzi la Israel (IDF) limesema linachunguza ripoti hizo.

    Hapo awali, watoto watano waliripotiwa kuuawa kwa shambulio la ndege zisizo na rubani walipokuwa wakicheza kwenye kona ya barabara kaskazini mwa Gaza.

    Unaweza pia kusoma:

  16. Tazama: Video ya China ikionyesha uwezo wake wa kijeshi

    Kamandi ya maonyesho ya kijeshi ya Mashariki ya jeshi la China imetoa video inayoonyesha mazoezi ya kijeshi usiku wa kuamkia leo ya kuizunguka Taiwan.

    Video hiyo inaonyesha uwezo wa kijeshi wa Beijing - meli za kivita, ndege za kivita, askari wenye silaha, vifyatuzi vya makombora na magari ya kivita ya amphibious (yenye uwezo wa kusafiri baharini na nchi kavu)

    Maelezo ya video, Tazama: video ya matangazo ya Jeshi la china (China's People's Liberation Army)

    Chombo cha habari kinachosimamiwa na serikali ya China cha Global Times kimesema video hiyo inaangazia "utayari na uwezo wa amri ya kushiriki katika mapigano".

    Unaweza pia kusoma:

  17. China yaizingira Taiwan kwa mazoezi ya jeshi kama 'adhabu' kwa hotuba ya rais

    g

    Chanzo cha picha, People's liberation Army

    China inafanya mazoezi ya kijeshi kuizunguka Taiwan, katika kile inachoita "onyo kali" dhidi ya wale wanaotaka "uhuru" wa kisiwa hicho kinachojitawala.

    Haya ndiyo tunayojua kufikia sasa kuhusu mazoezi ya hivi punde ya kijeshi ya China:

    • China imezindua michezo mipya ya vita katika pwani ya Taiwan, na hivyo kuzidisha mvutano kati ya serikali hizo mbili
    • Meli na ndege za kivita zinashiriki katika mazoezi hayo, ambayo Beijing imeyapa jina la Joint sword 2024B.
    • Taiwan inasema imegundua ndege 25, meli saba za kikosi cha wanamaji na meli nyingine nne
    • Mazoezi hayo yanafanyika katika maeneo tisa karibu na kisiwa hicho na kuigiza shambulio dhidi ya Taiwan, jeshi la China limesema.
    • Walinzi wa pwani wa China pia wametuma meli kadhaa kufanya "ukaguzi" kuzunguka kisiwa hicho
    • Hii inakuja siku chache baada ya rais wa Taiwan kutoa hotuba kali akisema serikali yake haitakubali udhibiti wa China
    • China imefanya mazoezi makubwa ya vita kuizingira Taiwan hapo awali, na kudai udhibiti wa kisiwa hicho cha kidemokrasia

    Ni ipi sababu ya mvutano kati ya China na Taiwan?

    Madai ya China kuhusu Taiwan inayojitawala ndiyo kiini cha suala hilo.

    Beijing inakiona kisiwa hicho kama jimbo lililojitenga ambalo hatimaye litakuwa sehemu ya Uchina. Haijaondoa uwwezekano wa matumizi ya nguvu kufanikisha hili.

    Lakini watu wengi wa Taiwan wanajiona kuwa sehemu ya taifa tofauti, ingawa wengi wanapendelea kudumisha hali ilivyo sasa, ambapo Taiwan haitangazi uhuru kutoka kwa Uchina wala kuungana nayo.

    Unaweza pia kusoma:

  18. Shambulio la ndege zisizo na rubani lawaua wanajeshi wanne wa Israel na kuwajeruhi zaidi ya 60

    G

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wanajeshi wanne wameuawa na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa katika shambulio la ndege isiyo na rubani lililoilenga kambi ya jeshi kaskazini mwa Israel, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema.

    IDF liliongeza kuwa wanajeshi saba wamejeruhiwa vibaya katika shambulio hilo kwenye kambi "karibu na Binyamina" - mji ulioko umbali wa maili 20 (33km) kusini mwa Haifa.

    Hezbollah imedai kuhusika na shambulio hilo ambalo ilisema liliilenga kambi ya mafunzo ya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) Brigedi ya Golani katika eneo hilo lenye makao yake makuu kati ya Tel Aviv na Haifa.

    Ofisi ya vyombo vya habari vya kundi hilo lenye silaha imesema kuwa shambulio hilo lilikuwa ni kujibu mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon na Beirut siku ya Alhamisi.

    Kundi hilo limesema lililenga kambi hiyo kaskazini mwa Israel kwa kutumia "kundi la ndege zisizo na rubani".

    Unaweza pia kusoma:

  19. Karibu kwa matangazo yetu ya mubashara ikiwa leo ni Jumatatu tarehe 14.10.2024, tukikuletea taarifa za matukio ya kikanda na kimataifa.