Fahamu kwanini ni 'kibarua kigumu' kumlinda Trump

,

Chanzo cha picha, Getty Image

Muda wa kusoma: Dakika 4

Jaribio la pili lililo wazi la kumuua Donald Trump limesababisha masuala kadhaa yanayokabili shirika lililopewa jukumu la kumlinda mmoja wa watu mashuhuri zaidi duniani.

Tovuti yenye kuonyesha taarifa za Trump kwa umma umeweka changamoto za kiusalama na ufadhili kwa Huduma Maalum ya Usalama, ofisa wa zamani aliambia BBC News.

"Imezidi," alisema Paul Eckloff, ofisa wa Huduma Maalum ya Usalama wa miaka 20 ambaye alimlinda Trump wakati wa urais wake.

"Kiasi cha muda anachotumia nje, furaha ya mashabiki wake, idadi na ukubwa wa mikutano, na ukosefu wa msaada wa kijeshi, inafanya iwe vigumu zaidi."

Huduma Maalum ya Usalama, ambayo inawalinda marais na maafisa wengine wakuu wa Marekani, ndio yenye jukumu kuu la ulinzi katika matukio yote mawili yaliyotishia maisha ya Trump.

Shirika hilo hivi majuzi limeibua wasiwasi kuhusu rasilimali zinazohitajika kufadhili taarifa za ulinzi wa rais huyo wa zamani.

Mapema wiki hii, shirika hilo liliona mtu mwenye bunduki akiwa amejificha kwenye vichaka karibu na uwanja wa gofu wa rais wa zamani wa West Palm Beach, Florida.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ofisa aliyemuona alimfyatulia risasi mshukiwa huyo ambaye alitoroka kwa gari kabla ya kukamatwa muda mfupi baadaye.

Hii inafuatia jaribio la mauaji lililotokea mnamo mwezi Julai katika mkutano wa hadhara huko Butler, Pennsylvania, ambapo mtu mwenye silaha alifyatua risasi na kumpiga Trump sikioni. Tukio hilo lilisababisha uchunguzi mkali kwa Huduma Maalum ya Usalama.

Uongozi wa shirika hilo umefikishwa mbele ya Bunge tangu wakati huo, mkurugenzi wake akijiuzulu baada ya shinikizo kubwa, na wabunge wameunda kikosi kazi kuchunguza vitisho dhidi ya mgombea wa Republican vilivyotokea kipindi hichi.

Wakati huo huo, tukio la hivi karibuni zaidi likiwa limesababisha wito wa ufadhili mpya kwa Huduma hiyo Maalum ya Usalama ili kuhakikisha inaweza kuwalinda vya kutosha wagombea urais wakati wa joto la kisiasa ambapo wengi wanahofia inaweza kusababisha ghasia zaidi.

Wakati maelezo ya jaribio la mauaji yanapoibuka, Rais Joe Biden aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu kwamba Huduma Maalum ya Usalama "inahitaji msaada zaidi" na Bunge linapaswa kushughulikia suala hilo.

Shirika hilo limeongeza juhudi zake tangu mwezi Julai, lakini inaweza kuwa changamoto kuharakisha ufadhili mpya kwa shirika hilo.

Kuna chini ya siku 50 kabla ya uchaguzi wa Novemba 5, na mgawanyiko wa kisiasa Bungeni haujafanikiwa kukubaliana juu ya bajeti ijayo, ambayo ina maana kwamba Marekani inaweza kukabiliana na changamoto ya kupata fedha za kusimamia shughuli za serikali tarehe 1 Oktoba.

Pesa zaidi kwa Huduma Maalum ya Usalama inaweza kuwa suala gumu kutekelezeka kutokana na ukweli huo wa kisiasa.

Spika wa Bunge la Wawakilishi Mike Johnson, kiongozi wa chama cha Republican ambaye yuko katikati ya vita hivyo vya bajeti ya bunge, alipuuzilia mbali hitaji la Huduma Maalum ya Usalama kupokea pesa zaidi kwenye bajeti yake.

"Sidhani kama ni suala la ufadhili," alisema kwenye chombo cha Habari cha Fox News. "Rais Trump anahitaji kufuatiliwa na kulindwa zaidi ya mtu mwingine yeyote. Yeye ndiye anayeshambuliwa zaidi; ndiye anayetishiwa zaidi."

Lakini Kaimu Mkurugenzi wa Huduma Maalum ya Usalama Ronald Rowe aliandika katika barua kwa Bunge wiki iliyopita kwamba "kuongezeka kwa mahitaji ya misheni ya Huduma Maalum ya Usalama kunahitaji rasilimali zaidi".

Huduma Maalum ya Usalama kwa muda mrefu imekuwa na wasiwasi juu ya kumlinda Trump kwenye viwanja vyake vya gofu, gazeti la Washington Post liliripoti, na hata shirika hilo lilijaribu kumwonya rais huyo wa zamani kuhusu nafasi inatoa kwa mtu aliye na nia ya kumshambulia.

Mnamo mwaka 2022, Mkurugenzi wa Huduma Maalum ya Usalama nchini Marekani wakati huo James Murray aliwaonya wabunge kwamba shirika hilo lilikuwa na changamoto ya kuendana na kasi na ukubwa wa mikutano ya Trump.

Alibainisha kuwa wanajeshi waliopungua ambao alikuwa nao wakati akiwa rais kumekuwa mzigo mkubwa kwa maofisa wanaopewa jukumu la kumlinda Trump baada ya kuondoka Ikulu ya White House.

Huduma Maalum ya Usalama iliwalinda marais kwenye mikutano hapo awali. Lakini kwa Trump, "mambo ni tofauti, na tunachoshuhudia wakati mwingine kunakuwa na hata mikutano miwili, mitatu, minne, kila mwezi", Bw Murray aliiambia Kamati ya Ukadiriaji ya Bunge wakati huo.

Mchezo wa gofu anaocheza Trump unaongeza changamoto nyingine.

"Mchezo anaopenda kucheza wa gofu ni matatizo mengine: uko nje, sehemu iliyowazi kwa saa kadhaa," alisema Bw Eckloff.

Marais wengine, akiwemo Barack Obama, pia walikuwa na tabia ya kucheza gofu wakiwa madarakani. Lakini rais huyo wa zamani mara kwa mara alicheza kwenye kambi ya kijeshi, ambapo usalama ulikuwa rahisi kudhibitiwa, kulingana na Bw Eckloff, ofisa wa zamani wa Huduma Maalum ya Usalama.

Wiki hii, wabunge walitoa wito kwa wagombea urais kutoka pande zote mbili kupata ulinzi wa kiwango sawa na rais aliyeko madarakani wa Marekani.

Kaimu mkuu wa Huduma Maalum ya Usalama wa Marekani alisema wiki hii kwamba usalama wa Trump sasa uko katika "kiwango cha juu zaidi".

Ulinzi uliopo wa Trump uko "karibu iwezekanavyo na usalama wa ngazi ya urais ambao unaweza kufanywa", alisema Bw Eckloff.

Lakini, alikubali, "hiyo haimaanishi kuwa haingeweza kufanya zaidi".

Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Yusuf Jumah