Jaribio la kumuua Trump lilivyomsafishia njia kuingia White House

.

Chanzo cha picha, AFP /Getty

Maelezo ya picha, Donald Trump
    • Author, Sammy Awami
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Dar es salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Ni kama vile uchaguzi wa urais nchini Marekani umeamuliwa tayari, ngekewa ikimuangukia Trump

Ile picha ya Trump akiwa amezingirwa na maafisa wa usalama, uso wake ukichomoza ukiwa umetapakaa damu, mkono kaunyanyua juu akiwa amekunja ngumi, itadumu daima.

Pamoja na hiyo picha ni kipande cha video kinachomuonyesha Trump akiwa ndio ameinuka kutoka chini tu baada ya kukwepa risasi, akiwa kama anawaambia wafuasi wake neno ‘fight’, yaani ‘pambaneni’.

Achilia mbali kubaki kuwa picha ya muhimu katika historia ya siasa za hivi karibuni za Marekani, wapiga kura wataikumbuka vizuri sana picha hiyo wanapoenda kuchagua rais mwezi Novemba.

Kuna wafuasi wa Trump wa uhakika kutoka Republican ambao sasa wamepandishwa hamasa ya kwenda kupiga kura. Halafu kuna wale ambao walikuwa hawana uhakika sana; wana wasiwasi na hali ya uzee na ushupavu wa akili kwa Biden lakini hawana uhakika sana kama Trump ni chaguo zuri.

Shambulio hili limewafanya hawa wa kundi la mwisho kuamini kwamba inawezekana Trump ni chaguo zuri kweli na kwamba ‘visa’ ambavyo amekuwa akivisema ni vya kweli, na kwamba anafanyiwa makusudi ili asirudi Whitehouse. Shambulio limewasaidia hawa kufanya maamuzi kwa uhakika zaidi

Kwa wapiga kura wote hawa itakuwa uchaguzi wa kati ya mgombea shupavu, aliyekwepa risasi, akaibuka kutoka chini anaimba neno ‘fight’ - yaani pambaneni – na mgombea ambaye anashindwa hata kukumbuka jina la makamu wake wa rais aliyekuwa naye kwa miaka minne ofisini

Trump ni fundi wa maneno na hodari wa kutumia matukio kutengeneza vijembe vya kampeni. Alipopata Uviko-19 Oktoba 2020 alisema ni ‘baraka kutoka kwa Mungu’ ili aipime dawa kuona ni nzuri kiasi gani ili awagawie watu bure.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwanasiasa mkongwe wa Democrat Nancy Pelosi na mumewe walipovamiwa na kujeruhiwa nyumbani kwao aliwacheka na kuwaambia wafuasi wake kwamba “wataendelea kumshughulikia.” Siku chache zilizopita Rais Joe Biden alipochanganya jina la Makamu wake Kamala Harris na kumuita Trump, Trump alimcheka kwenye mtandao wa kijamii na kusema “Safi sana Joe”.

Zaidi sana, Trump atakwenda kulitumia hili tukio kama uthibitisho wa madai yake ya miaka minne sasa akisema amekuwa muhanga wa mbinu chafu za Democrats wasiotaka awe Rais tena. Amekuwa akikumbushia walivyotaka kumng’oa madarakani kwa kura ya kutokuwa na Imani nae, kesi lukuki za jinai anazokabiliwa nazo hivi sasa, lakini amekuwa akidai pia kwamba Democrats wamewatuma maafisa wa FBI kumuua au kumtafutia mashtaka ya kumnyonga hata kama adhabu ya hayo mashtaka si kunyonga.

Miezi minne ijayo, Trump atakuwa na mengi sana ya kusema katika kampeni zake.

Hadharani, wafuasi na makada wa chama cha Democrat watakuwa wanamtakia kheri bwana Trump, na kukemea vurugu za kisiasa. Lakini kimoyomoyo, na labda hata wakiwa wamejifungia chumbani wenyewe, wanalaani namna tukio hilo linamuweka Trump mbele katika uchaguzi huu. Hasa ukizingatia kwamba nyumba yao ipo shagalabagala hivi sasa.

Biden bado anang’ag’ania kuwa mgombea wa Democrat kuchukua muhula wa pili hata kama mashinikizo ya yeye kuachia nafasi hiyo yanazidi kuongezeka. Na kwa kweli hakuna jipya.

Tangu mwanzo kabisa wa awamu yake ya kwanza, kulikuwa na maswali mengi ikiwa Biden atamaliza muhula wa pili. Lakini mdahalo wake na Trump wa juzi ulijibu swali hilo pasi na tashwishwi

Watu kadhaa wa muhimu katika kampeni yake wamemtaka Biden kukaa pembeni. George Clooney, muigizaji maarufu wa Hollywood na mchangiaji mkubwa wa kampeni yake, Seneta wa jimbo la Vermont Peter Welch ameandika Makala katika gazeti la New York Times kuweka hoja kwa nini Biden aachie ngazi. Mwanasiasa mkongwe mwenye ushawishi mkubwa na rafiki wa karibu wa Biden Bi Nancy Pelosi amesema muda wa Biden kujitafakari unazidi kuyoyoma

Hawa ni wale wachache tu na mashuhuri waliojitokeza hadharani, lakini taarifa zinasema wapo wengi ndani ya chama cha Democrat wanaoamini kwamba Biden anapaswa kuachia ngazi.

Changamoto kubwa ya Democrat sio tu kwamba njia ya Trump kuelekea ikulu imenyooka zaidi hivi sasa, au kwamba Biden anang’ang’ania kupata muhula wa pili, lakini ni swali kwamba ikiwa Biden atajiondoa, nani atafaa kuwa mrithi wake?

Kwa haraka haraka, makamu wa rais Kamala Harris ndio anaonekana kuwa mrithi wa wazi. Lakini wakati ana sifa za kumfanya kustahili kuwa rais, sifa za kumenyana vizuri na Trump katika kampeni, Harris pia ana mizigo inayomfanya kuwa si chaguo zuri kwa Democrat kumpambanisha na Trump

Ukimlinganisha na Biden kiumri na kimwili, ndio ni chagua bora zaidi. Zipo tafiti na ubashiri unaomuweka Harris kuwa mbadala unaofaa zaidi. Tafiti hizi zinasema yupo nyuma ya Trump kwa point mbili tu. Biden kwa upande mwingine yupo nyuma kwa point sita

Walipopambanishwa miongoni mwa vijana, kundi muhimu zaidi la kura kwa chama cha Democrat, Kamala alikuwa mbele ya Biden

Uzoefu wake katika masuala ya sheria unamfanya kuwa mtu sahihi wa kupambana na Trump katika kampeni, hasa kwasababu ya dhoruba ya shutuma za kisheria ambazo Trump anakumbana nazo hivi sasa

Lakini rekodi ya Harris katika baadhi ya sera za masuala nyeti ambayo ni kipaumbele katika uchaguzi huu inamuweka Harris katika nafasi mbaya. Kwa mfano sera ya uhamiaji.

Akiwa Makamu wa Rais, Biden alimpa jukumu la kushughulikia suala la mipaka na uhamiaji. Swala hili limekuwa kubwa sana katika kipindi cha miaka minne hii ya mwanzo ya Biden ambapo video nyingi zilizunguka mtandaoni zikionyesha miminiko la wahamiaji hasa kutoka Amerika ya Kati na Kusini.

Washindani wao Republican wamezitumia sana picha na video hizi kuwajaza hofu wafuasi wao kwamba mipaka ya Marekani imekuwa mibovu zaidi katika kipindi cha urais cha Biden na Harris, na kwamba wahamiaji wengi wameingia Marekani kuchukua nafasi zao za kazi huku wengi wakiwa ni wahalifu.

Wapiga kura weusi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris

Biden alitumaini pia kwamba Harris angemsaidia kuleta kura za Wamarekani weusi. Lakini hapa inaonekana Democrat hawafanyi vizuri sana, hasa kwa Wamarekani Weusi wanaume, ambao inaripotiwa kwamba wengi wanasema watamsapoti Trump

Lakini anatajwa kufanikiwa kwa kiwango kizuri katika mapambano ya swala la kuhalalisha utoaji mimba ambapo Mahakama ya Juu iliamua kwamba kila jimbo liamue lenyewe juu ya sheria hizi. Hata Republican wanasherehekea majimbo 14 kupitisha sheria ya kuzuia utoaji mimba, chama hicho kimelegeza msimamo wake kidogo kuhusiana na swala hili ili kuwavutia wapiga kura wa mrengo wa kati. Hii inachukuliwa kama mafanikio ya Harris.

Kwa kawaida Trump huwapachika majina ya utani watu wanaoonekana kuwa tishio kwake kisiasa. Tayari amempa jina “‘Laffin’ Kamala Harris”. Kwa maneno mengine, hata Trump anaona uwezekano wa kupambana na Harris katika uchaguzi na kumuona tishio lisilopaswa kupuuzwa.

Trump ameponea chupuchupu katika shambulio hili ambalo sio la kwanza kwa Marekani huku watangulizi wake kadhaa hawakuwa na bahati kama yeye. April 1865, Rais Abraham Lincoln alipigwa risasi ya kichwa akiangalia maigizo na kufariki kesho yake. Marais wengine kama James A. Garfield, William McKinley na John F. Kennedy wote waliuwawa kwa kupigwa risasi.

Tofauti ya matukio hayo ya nyuma ni kwamba yalikuwa chanzo cha kuwaunganisha Wamarekani. Wanahistoria na wachambuzi wengi wanaamini kwamba tukio hili la Trump litaongeza mpasuko wa kisiasa ambao unaendelea kulitafuna taifa hilo.

Imehaririwa na Abdalla Dzungu