Ni nini kilichochea jaribio la mapinduzi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo?

Chanzo cha picha, CHRISTIAN MALANGA/REUTERS
Jaribio hili la mapinduzi katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo limezua wasiwasi, kwani bara la Afrika limekumbwa na mapinduzi sita tangu 2020: mawili nchini Mali, mawili Burkina Faso na moja nchini Guinea na Niger mtawalia.
Brigedia Jenerali Sylvain Ekenge, msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alisema kuwa mnamo tarehe 19 Mei, watu kadhaa wenye silaha walishambulia ofisi ya rais na shambulio la pili lilifanyika karibu na nyumba ya Vital Kamerhe, mkuu wa zamani wa majeshi na mshirika wa karibu wa jeshi. mkuu wa nchi wa sasa.
Kutokana na mashambulizi hayo, watu 50 wakiwemo raia watatu wa Marekani walikamatwa.
Wengi hapo awali waliamini kuwa jaribio hilo la mapinduzi lilikuwa ni kazi ya kundi la wanajeshi wa Congo waliohusishwa na walinzi wa rais.
Hata hivyo, ilithibitishwa baadaye kwamba hatua hii ilikuwa imechukuliwa na mpinzani Christian Malanga, mkosoaji wa muda mrefu wa Rais Félix Tshisekedi.
Mnamo mwaka 2012, alienda uhamishoni nchini Marekani na kupata uraia wa Marekani.

Chanzo cha picha, CHRISTIAN MALANGA/FACEBOOK
Jeshi lilithibitisha kuwa Bw Malanga aliuawa kwa kupigwa risasi katika ikulu ya rais baada ya kukataa kukamatwa na vikosi vya usalama.
Mara ya mwisho alionekana akiwa hai Jumapili asubuhi matangazo ya moja kwa moja kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, pamoja na watu kadhaa waliokuwa na silaha nzito waliovalia sare za kijeshi.
"Felix, uko huru. Tunakuja kukuchukua," alisema Bw. Malanga, akithibitisha nia yake ya kupindua utawala wa Rais Tshisekedi.
Akiwa amesimama karibu na mwanawe Marcel - ambaye pia alikamatwa na vikosi vya usalama - Malanga alizungumza na watazamaji kwa lugha za Kifaransa, Kiingereza na Lingala, akisema wanajeshi "wamechoka" na "hawakuweza kuandamana pamoja" na Kamerhe na Tshisekedi.

Chanzo cha picha, MARCEL MALANGA/FACEBOOK
End of Unaweza pia kusoma:
Christian Malanga ni nani?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Akiwa na umri wa miaka 41, Christian Malanga alijulikana kama sauti pinzani ya kisiasa kutoka nje ya Congo (diaspora )
Akiwa mzaliwa wa Kinshasa, familia ya Christian Malanga iliondoka nchini alipokuwa mtoto na kukimbilia Swaziland, kabla ya kuhamia Salt Lake City, Utah, nchini Marekani mwaka 1998.
Baada ya kumaliza shule ya msingi nchini Marekani, alianzisha biashara kadhaa ndogo ndogo pamoja na Shirika lisilo la faida la Africa Helpline Society, ambalo linasaidia elimu ya watoto katika bara hilo.
Mnamo mwaka 2006, alirudi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutekeleza utumishi wake wa kijeshi. Baadaye alianzisha kampuni iitwayo Malanga Congo, inayojihusisha na kazi za umma na miradi ya ugavi.
Mnamo mwaka 2011, aliingia katika siasa kwa kugombea kama mgombea katika uchaguzi wa wabunge, lakini alikamatwa kabla ya uchaguzi na kuzuiliwa kwa wiki kadhaa.
Baada ya kuachiliwa huru, Malanga aliripotiwa kukataa ombi la serikali la kuwa rais wa vijana kitaifa na akapendelea kufuata njia yake kwa kuunda chama chake cha kisiasa.
Malanga alirejea Marekani mwaka uliofuata na kuanzisha chama cha Unified Congolese Party (UCP), chama kidogo ambacho kinalenga kuunganisha Wacongo wanaoishi nchi za kigeni duniani kote. Pia alikuwa rais wa vuguvugu la "New Zaire", lenye makao yake mjini Brussels, Ubelgiji.
Mwanasiasa huyo pia alikuwa na ushawishi mkubwa katika nyanja ya kidini. Mnamo 2017, alipewa heshima kubwa ya Mkuu wa Agizo la Ufalme wa Mtakatifu Petro na Paulo huko Vatcan.
Alifanikiwa kujenga msingi mkubwa wa kisiasa miongoni mwa Wacongo wa ughaibuni na alijulikana kwa kueleza mara kwa mara ukosoaji wake wa utawala wa Tshisekedi kwenye mitandao ya kijamii.
Katika chapisho kwenye X (zamani Twitter), Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Lucy Tamlyn alisema "ameshtushwa" na ripoti kwamba raia wa Marekani walihusika katika jaribio la mapinduzi ya serikali.

Chanzo cha picha, PRESIDENCY RD CONGO
Tafadhali muwe na uhakika kwamba tutashirikiana na mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kadiri inavyowezekana wanapochunguza vitendo hivi vya uhalifu na kuwawajibisha raia wowote wa Marekani wanaohusika,” mwanadiplomasia huyo aliongeza.
Rais Tshisekedi bado hajatoa maoni yake kwa umma kuhusu mashambulizi hayo.
Alichaguliwa tena Desemba mwaka jana kwa muhula wa pili katika chaguzi zilizozozaniwa, na karibu watu 20 waliuawa kufuatia ghasia zinazohusiana na uchaguzi.
Mwezi Aprili, mwanauchumi Judith Tuluka aliteuliwa kuwa waziri mkuu, na kuwa mwanamke wa kwanza nchini humo kushika wadhifa huo. Lakini Bi Tuluka bado hajataja serikali yake.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni nchi yenye utajiri wa maliasili na idadi ya watu inakadiriwa kuwa zaidi ya wakaazi milioni 100. Lakini nchi hiyo inakabiliwa na migogoro mirefu ya muda mrefu mashariki, mizozo ya kiuchumi na kijamii, na ukosefu wa uaminifu wa kudumu kati ya serikali na upinzani.
Jaribio la kutaka kuipindua serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika siku za hivi karibuni limeibua hali ya wasiwasi katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika, kutokana na majaribio mengi ya mfulurizo yaliyolikumba bara za Afrika hivi karibuni hususan Magharibi mwa Afrika.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Ambia Hirsi












