'Mungu ndiye aliyetuma majeshi yake ya mbinguni ili kutuokoa na kifo' - Mke wa Vital Kamerhe

Chanzo cha picha, HAMIDA CHATUR KAMERHE/FACEBOOK
Mke wa Vital Kamerhe aliripoti kuwa nyumba yao ilikuwa eneo la mapigano ya bunduki kwa takriban saa moja kati ya washambuliaji na walinzi wa nyumba yao.
Hamida Chatur Kamerhe alieleza jinsi ilivyotokea, akisema kwamba aliamshwa na mumewe Vital, aliposikia milio ya risasi nje ya nyumba mwendo wa saa 10 asubuhi siku ya Jumapili wakati wa tukio linaloripotiwa na wanajeshi wa DRC kuwa jaribio la mapinduzi .
Hamida alisema: “Washambuliaji walifanikiwa kuingia nyumbani kwetu, wakipiga risasi bila kusogeza chochote. Waliua walinzi wetu wawili. Mmoja wa askari wetu pia alifanikiwa kumuua mmoja wao, lakini hilo halikuzuia vurugu zao."
Mke huyo wa Vital Kamerhe alisema kuwa kabla ya kuvamiwa, wavamizi hao walikuwa wametumia kwanza 'droni' kujua jinsi ulinzi ulivyo katika nyumba hii.
Katika taarifa yake, Billy Kambale, katibu mkuu wa chama cha Vital Kamerhe cha Union Pour La Nation Congolaise (UNC), alisema shambulio hilo lililenga "kumuua kiongozi wa chama, ambaye aliokolewa tu kwa neema ya Mungu na ujasiri wa walinzi wake”
Hamida alisema katika fujo hizo, mumewe alifanikiwa kuzungumza na mlinzi wake mmoja kwa simu na kumwambia kwa sauti ya hofu;
"Bwana, ni wewe wanakutafuta, wanauliza uko wapi, wapo zaidi ya 40 wakiwa na silaha nyingi".

Chanzo cha picha, UNC
Anaongeza: “Hapo ndipo nilipohisi kwamba mwisho wetu ulikuwa karibu. Milio ya risasi iliongezeka nje, na kuifanya nyumba yetu kuwa uwanja wa vita.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
“Mnamo saa moja hivi, mimi na mume wangu tulikuwa peke yetu ndani, tukiwa tumezungukwa na woga mwingi.”
Hamida anasema kwamba msaada ulikuja karibu saa kumi na moja asubuhi, "kukomesha mahangaiko yetu". Anasema kwamba waligundua baadaye kwamba watu hao walienda mara moja katika ofisi ya rais wa jamhuri.
Wengi kwenye mitandao ya kijamii wanasema kuwa shambulizi hilo kimsingi lililenga kumuua Vital Kamerhe, mgombea pekee wa muungano unaotawala kwa nafasi ya spika wa bunge.
Msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alisema kuwa shambulio hilo lilifanywa na Christian Malanga, ambaye alikuwa katika jeshi la Kongo kabla ya kwenda nje ya nchi, na kwamba ni 'mapinduzi' ambayo yalizuiwa, huku wizara ya habari ikisema kuwa ilikuwa "jaribio la kutoroka taasisi za kitaifa".
Hakuna chombo huru kinachochunguza tukio hili, huku wengine wakihusisha na uhasama ambao umekuwa ukiripotiwa siku nyingi katika muungano wa vyama tawala ambapo wazee wanashikilia nyadhifa za uongozi.
Chama cha Vitali Kamerhe (UNC) kinataka uchunguzi wa kina kuhusu tukio hili.
Christian Malanga, ambaye alikuwa msimamizi wa shambulio hili, aliuawa baadaye, wakati mtoto wake Marcel Malanga na wengine, ikiwa ni pamoja na wageni wawili, walikamatwa wakati wakijaribu kutoroka.
Hamida Chatur Kamerhe alisema kuwa “Mungu alizuia shambulio la mauaji ambapo mume wangu alikuwa mlengwa wa kwanza'
' Ninamshukuru Mungu kwamba alimnusuru mume wangu kutoka gerezani kwa wakati ufaao, na usiku huu pia, kwamba alituma majeshi ya mbinguni ili kutuokoa na kifo.”
End of Unaweza pia kusoma
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












