DR Congo: Vikosi vya SADC vyatishia 'kuwaangamiza' waasi wa M23

Chanzo cha picha, SADC
Jumuiya ya Maendeleo ya nchini za Kusini mwa Afrika (SADC), imetangaza kuwa vikosi vyake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vitafanya mashambulizi, kwa ushirikiano na vikosi vya serikali, ili "kuwamaliza waasi wa M23 na kurejesha amani na usalama."
SADC ilitangaza hayo katika taarifa yake ikilaani shambulio la bomu dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Mugunga nje kidogo ya mji wa Goma, ambalo inasema lilitekelezwa na M23, kusababisha vifo vya watu takriban watu 16 na kujeruhi wengine takriban 30.
M23 walikanusha vikali madai hayo. Gavana wa Jimbo la Kivu, Ruguru, alisema kuwa watu 14 walifariki na wengine zaidi ya 35 kujeruhiwa katika shambulio la kambi ya Mugunga.
Vikosi vya SADC vimekuwa Kivu Kaskazini tangu mwishoni mwa mwaka jana, tangu Januari (1) vimeshiriki katika makabiliano ya "moja kw amoja" dhidi ya M23 kwa kutumia "mizinga nzito, ndege za kivita, ndege zisizo na rubani, na vifaru" katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa M23, kama mkuu wa M23 alivyotangaza wakati huo.
Maswali yamekuwa yakiulizwa ikiwa onyo hili jipya kutoka kwa vikosi vya SADC linamaanisha kwamba vikosi hivi, hasa kutoka Afrika Kusini, vitatumia nguvu za kijeshi za ajabu katika mzozo huo.
Mwezi uliopita, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akiwa nchini Rwanda, aliwaambia waandishi wa habari kwamba ana "nguvu mpya na azma" ya kutafuta "suluhisho la kisiasa" la mzozo wa DR Congo.
Taarifa ya SADC iliyotolewa siku ya Jumapili ilisema kwamba vikosi vyake lazima vifanye mashambulizi haya ili "kuwalinda raia na mali zao, wanaokabiliwa na tishio la kushambuliwa", "kufungua barabara ili kukidhi mahitaji", "na kulinda raia wanaokimbia kuua."
Ni nani aliyeshambulia kambi ya wakimbizi Mugunga?
Serikali za Marekani na DR Congo zilithibitisha kwamba shambulio hilo lilifanywa na waasi wa M23 kwa msaada wa Rwanda. SADC pia ilithibitisha kwamba ilifanywa na M23.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
M23 inakanusha kmadai hayo, ikilaumu vikosi vya serikali na waasi wa watiifu kwa serikali ya Kinshasa, ikisema kuwa walitumia silaha nzito karibu na kambi za wakimbizi.
Kujibu madai hayo, serikali ya Rwanda iliikosoa Marekani kwa "kufikia uamuzi mara moja wa kuilaumu Rwanda bila uchunguzi wowote", ikisema kwamba uchunguzi wa kuaminika lazima kwanza ukamilike ili kufichua kilichotokea.
Watu wengine 30 walijeruhiwa wakati makombora yalipopiga kambi za wakimbizi karibu na mji wa Goma mashariki mwa Congo siku ya Ijumaa iliyopita.
Katika taarifa yake, serikali ya Rwanda iliikosoa Marekani kwa "kufikia uamuzi mara moja wa kuilaumu Rwanda bila uchunguzi wowote" ikisisitiza kwamba uchunguzi wa kuaminika lazima kwanza ukamilike ili kufichua ni nini hasa kilitokea.
Kwa mjibu wa tangazo lilitolewa na msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo ,Rwanda haitabeba jukumu la shambulio hilo la makombora katika kambi za Mugunga na Lac Vert karibu na mji wa Goma, au kushindwa kwa utawala wa Congo kurejesha usalama mashariki mwa Congo.

Kwa upande mwingine ,tume ya umoja wa nchi za ulaya nchini DRC Katika taarifa yake haulaumu waasi wa M23 kwa mashambulizi haya dhidi ya wakimbizi, ingawa tume hiyo inashutumu kundi hilo kuendelea kusonga mbele_umeomba tu wahusika wafikishwe mbele ya sheria. Ujumbe wa EU pia unalaani "kuongezeka kwa matumizi ya silaha nzito karibu na kambi za wakimbizi", ukisema kuwa "yana athari mbaya sana kwa idadi ya watu".
Katika taarifa yake, MONUSCO hailaumu upande wowote kwa mashambulizi haya kwa wakimbizi wa kambi ya Mugunga, lakini inazitaka pande zinazohusika na mzozo "kutunza maisha ya raia", na inaziomba mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo "kuwafikisha mbele ya sheria" wahusika wa mashambulizi haya kwa sababu. "inaweza kuwa uhalifu wa kivita".
Rais wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, alilaani mashambulizi hayo dhidi ya wakimbizi , na kuzihimiza pande zinazozozana kufikia suluhu la amani. Moussa Faki pia hakulaumu upande wowote kwa mashambulizi hayo.
Jeshi la Congo na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda walilaumiana kwa mashambulizi hayo. Rwanda imekuwa ikikanusha kuunga mkono waasi wa M23 na kuishtumu serikali ya Congo kushirikiana na waasi wa Rwanda wa FDLR shutuma ambazo pia Congo inakanusha.

Chanzo cha picha, SADC
Kambi ya Mugunga iko kati ya jiji la Goma na 'kituo' cha Sake lakini ni karibu na Goma kuliko Sake, maeneo yote mawili yanadhibitiwa na vikosi vya serikali ya Kongo na washirika wao.
Waasi wa M23 wanadhibiti baadhi ya maeneo ya juu ya 'kituo' cha Sake.
Sio mara ya kwanza kwa kwa kambi ya Mugunga kushambuliwa, lakini hii ni mara ya kwanza kwa watu waliokimbia kuuawa kwa njia hii.
Wakimbizi katika kambi ya Mugunga wamekuwa wakilalamikia mauaji na ukosefu wa usalama unaosababishwa na kundi la FDLR linaloshirikiana na jeshi la serikali linalofanya kazi ndani na nje ya kambi hiyo.
Wakimbizi hao pia wamesikika wakilalamikia mashambulizi ya mabomu ambayo wanasema yanarushwa na M23 kutoka eneo linalodhibitiwa na waasi hao.
Mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakionya kwamba wakimbizi hao walioacha makazi yao katika maeneo ya Rutshuru na Masisi wako katika kambi zinazozunguka mji wa Goma, ambao wako katika hatari ya kushambuliwa, kwa sababu wanaonekana kuwa kati ya pande zinazozozana.
Kutokana na ukosefu wa uchunguzi huru kuhusu mzozo huo, ni vigumu kuthibitisha iwapo mabomu hayo yalirushwa moja kwa moja kutoka maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa M23 au kutoka kwa maeneo yanayodhibitiwa na vokosi vya serikali.
Hofu ya hali kuwa mbaya zaidi
Siku ya Ijumaa usiku, ofisi ya Rais Félix Tshisekedi ilitangaza kwamba alisitisha ziara yake ya kikazi huko Ulaya na kurejea Kinshasa kutokana na mashambulizi dhidi ya wakimbizi katika kambi ya Mugunga.
Utawala wa DR Congo unakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa raia wake wanaosema kuwa serikali inapaswa kuongeza juhudi za kukabiliana mashambulizi ya waasi ikiwa ni pamoja na shambulio la hivi punde dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Mugunga.
Kinshasa inaichukulia Kigali kama "adui wake halisi" na imekuwa ikirudia mara kwa mara madai kwamba M23 ni chombo cha Kigali. Kuna hofu kwamba kilichotokea Mugunga siku ya Ijumaa kinaweza kusababisha mzozo huu kuchukua mkondo mwingine.
Serikali ya Rwanda inasema Rais Tshisekedi na serikali ya Congo "wanaendelea kutishia kuivamia Rwanda na kuiondoa serikali kwa nguvu", hivyo Rwanda "itaendelea kuchukua hatua zote za kisheria kulinda nchi yetu".
Bintou Keita, Mkuu wa MONUSCO, alitoa wito kwa pande zote katika mzozo huo " kutafuta njia ya kufikia suluhu la amani na la kudumu la mzozo katika eneo hilo."
Imetafsiriwa wa Ambia Hirsi
Maelezo ya ziada na Yves Bucyana












