Mapigano yazuka baada ya wakuu wa jeshi la SADC na Burundi kukutana DR Congo

Jenerali Jacob John Mkunda, Kamanda wa Jeshi la Tanzania na Jenerali Rudzani Maphwanya wa Jeshi la Afrika Kusini katika mkutano mjini Goma.

Chanzo cha picha, X

Maelezo ya picha, Jenerali Jacob John Mkunda, Kamanda wa Jeshi la Tanzania na Jenerali Rudzani Maphwanya wa Jeshi la Afrika Kusini katika mkutano mjini Goma.

Milio ya risasi imesikika tena katika maeneo tofauti ya Mweso na Mabenga katika eneo la Masisi Jumatatu asubuhi, kulingana na baadhi ya watu walio karibu.

Waasi wa M23 walitangaza kuwa asubuhi ya leo vikosi vya serikali viliungana na vikundi vya waasi wa Wazalendo, vikosi vya baadhi ya nchi za SADC na Burundi vikiwashambulia kwa bunduki na vifaru vya vita.

Mapigano hayo yametokea baada ya makabiliano yaliyofikiwa Jumapili katika eneo la mapigano la Masisi karibu na Sake. Hayo pia yanajiri baada ya mkutano wa makamanda wa majeshi ya baadhi ya nchi za SADC ambao walituma wanajeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wakuu wa majeshi ya Burundi, DR Congo, Malawi, Afrika Kusini na Tanzania walikutana mjini Goma mwishoni mwa juma lililopita na kutembelea eneo la Mubambiro nje kidogo ya kituo cha Sake.

Meja Jenerali Sylvain Ekenge, msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, aliwaambia waandishi wa habari kwamba wakuu wenyewe wa wanajeshi wataenda "kufuatilia hali ya operesheni za kijeshi" katika eneo la vita na "kuimarisha hatua za kuendelea na operesheni".

Ekenge alisema kuwa mkutano wa viongozi wa kijeshi mjini Goma ni "ishara kubwa ya nia ya SADC na Burundi pamoja na DR Congo katika kurejesha amani mashariki mwa nchi hiyo."

Uwepo wa majeshi ya Burundi DRC

Mwaliko na uwepo wa mkuu wa jeshi la Burundi Jenerali Prime Niyongabo katika mkutano wa Goma uliondoa sintofahamu kuhusu ushiriki wa vikosi vya Burundi katika operesheni ingawa haijathibitishwa kuwa jeshi la Burundi linapigana na M23 katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ya Desemba (12) mwaka jana ilisema kuwa jeshi la Burundi linapigana na M23 kw aushirikiano na vikosi vya ya DR Congo. Burundi hata hivyo haukukana wala kuthibitisha hilo.

Ripoti hiyo pia ilishutumu jeshi la Rwanda kwa kupigana pamoja na M23 katika mapigano hayo. Kigali imekuwa ikikanusha malalamiko hayo kwa muda.

Ripoti hiyo ilichapishwa siku chache baada ya wanajeshi wa Burundi waliotumwa katika jimbo la Kivu Kaskazini na nchi za EAC kutangazwa kurejea Burundi.

Kundi la M23 liliendelea kusema kuwa jeshi la Burundi linaendelea kushirikiana na serikali, huku likionyesha baadhi ya wanajeshi ni Warundi waliotekwa katika vita hivyo.

Katika mkutano na waandishi wa habari Desemba 29 (12) 2023, Rais Evariste Ndayishimiye alipoulizwa iwapo jeshi la Burundi linapigana na M23, alijibu: "Hufai kuangalia nyumba ya jirani ikiteketea." Alisema kuwa Burundi ilikwenda kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Alikanusha madai ya M23 kwamba waliwakamata wanajeshi wa Burundi, akisema kwamba kile M23 ilifanya kuwaonyesha wanajeshi hao ni "vita vya kisaikolojia"

Mzozo huu utaisha lini?

Serikali ya Kinshasa inatumai kuwa jeshi na waasi wanaounga mkono watawashinda waasi wa M23 na kuwanyang'anya ardhi waliyoikalia kutoka Bunagana hadi Masisi.

Wanajeshi wa SADC walianza kuwasili DR Congo mwezi Disemba mwaka jana, wakitarajia matokeo. Afrika Kusini pekee inaripotiwa na vyombo vya habari vya ndani kupeleka takriban wanajeshi 2,900 na zana za kijeshi.

Wakati nchi za kimataifa zikiendelea kuimarisha juhudi za kusuluhisha mzozo huu kwa njia ya mazungumzo, inaonekana kwamba mapigano hayawezi kukoma hivi karibuni.

Mwezi uliopita, mchambuzi wa Shirika la Kimataifa la Migogoro DR Congo Onesphore Sembatumba aliiambia BBC kwamba pande zote mbili zilitumia mgogoro wa hivi punde "kujitayarisha kwa vita badala ya kuimaliza".

Akasema: "Dalili zote zinaashiria kwamba hali inaweza kuwa mbaya."

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi