Mambo matano muhimu kuhusu mzozo wa Mashariki mwa DR Congo

DSX

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mapigano yameongezeka kati ya waasi na wanajeshi wa serikali ya DRC
    • Author, Beryl Munoko
    • Nafasi, BBC

Ikiwa unasoma hii makala katika simu au kompyuta yako, fikiria nyenzo zinazokuruhusu kuendelea kusoma. Unatumia simu yako kwa sababu ya madini yanayoitwa Coltan ambayo hutumiwa katika uundaji wa vifaa vya kielektroniki.

Takribani 60% ya madini ya Coltan yanapatikana katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na sehemu kubwa ya madini hayo hutoka mashariki mwa nchi katika mikoa ya Kivu.

Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inakabiliwa na mapigano makali kati ya kundi la waasi linalojulikana kama vuguvugu la M23 na majeshi ya serikali.

Tangu Oktoba 2023, zaidi ya watu milioni 2.5 wamekimbia makazi yao na mamia wamefariki, huku migogoro inayoendelea ikitishia kudhoofisha zaidi usalama wa eneo hilo.

Tumefikaje hapa?

x

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mamilioni ya watu wamelazimika kuacha nyumba zao na kazi zao

Katika miongo mitatu iliyopita, eneo la mashariki mwa DR - Congo lenye utajiri wa madini limekumbwa na misukosuko kwa sababu ya malalamiko ya kisiasa, migogoro ya rasilimali na mivutano ya kikabila.

Mzozo wa sasa kati ya waasi wa M23 na serikali ulianza mwaka 2012. Kundi hilo liliibuka baada ya makubaliano ya amani ya Machi 23, 2009 ambayo yalimaliza mzozo wa awali wa 2006-2009.

M23 walichukua silaha kwa sababu walisema serikali imeshindwa kutekeleza makubaliano hayo. Waasi walisema wanapigana kwa sababu ya kutengwa kisiasa na ukosefu wa uwakilishi wa kabila la Watutsi walio wachache katika eneo hilo.

Kundi la waasi linaloongozwa na Watutsi lilidhibiti maeneo mengi katika jimbo la Kivu Kaskazini, ukiwemo mji mkuu, Goma. Mwaka 2013, walitawala jiji hilo kwa siku 10 kabla ya kuondoka kutokana na shinikizo la kimataifa.

Walikubali kusitisha mapigano na kuacha silaha lakini mwaka 2021, walichukua silaha tena, wakisema serikali imevunja ahadi zake.

Vita vya hivi punde vimetokea katika mji wa Sake, kilomita 25 kaskazini-magharibi mwa Goma.

Serikali ya DRC mara kwa mara imekuwa ikizishutumu nchi jirani, hasa Rwanda, kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, madai ambayo Rwanda imekuwa ikikanusha.

Wahusika wakuu ni akina nani?

''

Mapigano ya hivi karibuni ni kati ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na makundi yenye silaha yanayoiunga mkono serikali.

Majeshi ya serikali pia yanaungwa mkono na jumuiya ya kikanda yenye wanachama 16 inayoongozwa na Afrika Kusini, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afŕika (SADC), pamoja na Buŕundi.

SADC inachukua hatamu kutoka Jeshi la Kikanda la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) linaloongozwa na Kenya, ambalo limeondoka Mashariki mwa DRC mwezi Desemba, mwaka mmoja baada ya kutumwa.

Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, anayehudumu muhula wake wa pili, ameapa kuangamiza uasi na kudumisha ulinzi wa eneo la nchi yake.

Hata hivyo, juhudi za kijeshi za serikali zimekuwa zikikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa waasi wa M23 wenye silaha na waliojipanga vizuri jambo ambalo limechangia vita kukuwa na kuzidisha mateso kwa raia.

Kwa nini Goma ni muhimu?

asx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mashirika ya kibinadamu yanaonya juu ya janga la kibinadamu linalokuja

Goma, ni mji wa tatu kwa ukubwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na ni mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini.

Pamoja na kuwa na utajiri wa madini ya Coltan, Mashariki mwa DRC pia kuna akiba ya dhahabu na bati. Rasilimali hizi kwa muda mrefu zimekuwa chanzo cha mzozo kati ya makundi mbalimbali yenye silaha yanayopigania udhibiti, licha ya shinikizo la kimataifa na makubaliano ya amani yenye lengo la kutatua migogoro.

Mashariki mwa DRC pia ina umuhimu mkubwa kimataifa na kijiografia. Eneo hilo linatumika kama kituo kikuu cha safari za kibiashara na misaada ya kibinadamu. Ni eneo la kimkakati karibu na mpaka na Rwanda.

Kuna kituo kikubwa cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, ambacho kimevutia biashara nyingi, mashirika ya kimataifa na balozi.

Udhibiti wa Goma ni muhimu. Yeyote anayedhibiti jiji hilo anaweza kuwa na ushawishi wa kisiasa na kiuchumi katika eneo lote la Maziwa Makuu barani Afrika.

Athari ya mgogoro ni ipi?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hali ya kibinadamu Mashariki mwa DRC imezorota kwa kasi kutokana na ghasia zinazoendelea.

Maelfu ya raia wamelazimika kuyahama makazi yao, kutafuta hifadhi katika kambi zilizojaa watu waliokimbia makazi yao au nchi jirani.

Umoja wa Mataifa unasema idadi ya wakimbizi wa ndani nchini DRC inaweza kufikia watu milioni 6.9.

Waasi pia wanafunga barabara kuu mbili za Goma kutoka kaskazini na magharibi, na kuzuia mazao kupita.

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanaonya juu ya janga la kibinadamu linalokuja. Raia kutofikiwa na huduma muhimu kama vile chakula, maji, na huduma ya afya kunazidisha mateso ya watu walio hatarini.

"Maisha ya watu yametatizika na usalama wa chakula unatarajiwa kuwa mbaya zaidi na zaidi katika kiwango cha dharura cha uhaba wa chakula - kumaanisha kuwa tunaweza kushuhudia vifo," anasema mkuu wa misaada ya dharura wa WFP, Mashariki mwa DRC, Cynthia Jones.

"Hali mbaya itazidisha unyanyasaji wa kijinsia unaowakabili wanawake, wasichana na wavulana."

Njia ya Amani?

xs

Chanzo cha picha, Getty Images

Kufikia amani ya kudumu huko Goma ni lazima kushughulikia vyanzo vya mzozo huo. Ikiwemo madai ya kubaguliwa kisiasa, ukabila, na serikali kutoweza kutekeleza kikamilifu mikataba ya kusitisha mapigano.

Makubaliano ya kisiasa ambayo yalimaliza vita vya M23 mjini Goma miaka 10 iliyopita hayakuwahi kutekelezwa kikamilifu na majaribio yaliyofuata ya kusitisha mapigano yamevunjika, huku kila upande ukilaumiana.

Waasi wa M23 wanataka kuunganishwa katika jeshi la taifa la Congo na kuwa chama cha kisiasa kinachotambulika.

Wamesema mara kwa mara wanataka kufanya mazungumzo ya amani na Kinshasa, lakini Rais Tshisekedi amesema serikali haiko tayari kufanya mazungumzo.

Kwa kuongezea, ushirikiano wa kikanda ni muhimu katika kuunda makubaliano yoyote ya kudumu ya amani. Nchi Jirani zinapaswa kuzuia uingiliaji kati kutoka nje na kuunga mkono juhudi za kuleta utulivu katika eneo hilo.

Mzozo wa Goma ni mkusanyiko wa changamoto nyingi - yakiwemo malalamiko ya muda mrefu, migogoro ya rasilimali, mivutano ya kikabila, na maslahi ya kijiografia na kisiasa.

Kuelewa hayo yote ni muhimu unapotafuta njia ya kuelekea kwenye amani na utulivu katika mojawapo ya kanda zenye matatizo zaidi barani Afrika.