Uondoaji wa viza utazinufaisha vipi Tanzania na DR Congo?

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, BBC Swahili
Wiki hii Serikali ya Tanzania imetangaza kuondoa viza kwa raia wote wanaotoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo). Uamuzi huu unawafanya raia wa nchi hizo kuwa na uhuru zaidi wa kuingia na kutoka kwa ajili ya biashara na mambo mengine.
Kwa mujibu wa takwimu za makadirio za Umoja wa Mataifa hadi kufikia 2023, DR Congo ina watu milioni 102. Ni taifa la nne Afrika kwa kuwa na watu wengi nyuma ya Nigeria, Ethiopia na Egypt. Na la 15 ulimwenguni kuwa na idadi kubwa ya watu.
Licha ya Tanzania na DR Congo kupakana, pia raia wa nchi hizo wanaunganishwa na lugha ya Kiswahili. Zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania ni wazungumzaji wa Kiswahili. Upande wa DR Congo kuna wazungumzaji wa lugha hiyo wanaokadiriwa kufika 40% ya watu jumla, wakipatikana zaidi katika mikoa ya Mashariki ya nchi hiyo.
DR Congo ni mwanachama wa karibuni wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuondoa viza kunaenda sambamba na malengo ya jumuiya hiyo ya kukuza biashara kati yao, vilevile kuwa na soko huru litakalo rahisisha shughuli za mauzo na manunuzi.
Katika hesabu za kiuchumi wingi wa watu ni jambo muhimu sana. Idadi kubwa ya watu katika nchi zote mbili, kunaweza kuifanya sekta ya biashara kukuwa maradufu. Ikizingatiwa kuwa tayari nchi hizo zinafanya biashara kwa muda mrefu.
Ushirikiano wa Kiuchumi

Chanzo cha picha, Getty Image
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa nchini Tanzania ya mwaka 2020, nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ndio inayoshika nafasi ya kwanza miongoni mwa nchi jirani kupitisha mizigo katika bandari ya Dar es Salaam, DR Congo hupitisha zaidi ya 30% ya mizigo yote.
Kutoka 2018 upitishaji huo umezidi kuongezeka, 2018 DR Congo ilipitisha tani milioni 1.8, 2019 tani milioni 1.9, 2020 tani milioni 1.8, 2021 tani milioni 2.4 na 2022 tani milioni 3.4.
Katika juhudi za kukuza biashara kati ya nchi hizi mbili, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba alieleza mwezi Agosti mwaka huu kuwa Tanzania inatafuta eneo kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupatiwa bandari kavu ya kuhifadhia mizigo ya nchi hiyo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kauli hiyo ilikuja baada ya mazungumzo na Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ekila Libombo, kuhusu mipango ya kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji kati ya nchi hizo ili kukuza biashara na uchumi.
Mbali na bandari ya Dar es Salaam, mkoa wa Kigoma - uliopo kaskazini magharibi mwa Tanzania karibu na fukwe ya Mashariki ya ziwa Tanganyika - pia ni lango kuu la kibiashara kati ya Tanzania na DR. Congo.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwanga Center, mkoani Kigoma, Julai 2023. Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa, ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alieleza:
"Kigoma ni lango la Tanzania. Ipo mizigo mingi sana inayopita kwenye bandari ya Dar Es Salaam kwenda Congo, Burundi na ili ifike vizuri lazima ipite Kigoma."
Mara baada ya serikali ya Tanzania kutangaza kuondoa viza kwa raia wa DR Congo, mwanasiasa wa upinzani wa chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameandika kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter:
"Kwa Miaka zaidi ya 10 nimekuwa nikipigania suala la wananchi wa Kongo (DRC) kuingia nchini Tanzania bila malipo ya viza na vile vile Watanzania kwenda DRC bila malipo ya viza.
Hiki kilikuwa ni kilio kikubwa cha wafanyabiashara wa Kigoma ambao soko lao kubwa ni DRC. Nimefurahi sana kuwa hatimaye malipo ya viza yamefutwa. Biashara ya ukanda wa Ziwa Tanganyika itashamiri sana."
Faida kwa mtu mmoja mmoja

Biashara huendeshwa na watu, usafiri unapokuwa mwepesi wa kuingia na kutoka na hata shughuli za kibiashara nazo zitazidi kuwa nyepesi. Vilevile, wapo ambao huingia kwenye nchi hizi kwa ajili ya masomo na matembezi. Pia, nao watanufaika kwa kuondolewa viza.
Uombaji wa viza hugubikwa na mchakato mrefu, hata baada ya kukamilisha mchakato huo majibu yake wakati mwingine hayaji papo kwa papo. Hukulazimu kusubiri siku kadhaa au hata wiki kabla nchi husika haijakubali maombi yako. Nchi nyingi siku hizi zina utaratibu wa kuomba viza mtandaoni. Ila pia zipo zile ambazo utalazimika uende ubalozi wa nchi husika.
Kuondolewa kwa viza maanake msafiri hatahitajika tena kujaza fomu yenye mambo mengi ya kuomba viza na kusubiri majibu kwa siku kadhaa. Fomu ambayo huambatanishwa na barua; mfano ya mwajiri wako, mwenyeji wako, picha ndogo au taarifa kutoka benki.
Fauka ya yote, viza inapoondolewa hakutohitajika tena malipo ya kulipia viza kama ilivyo kwa nchi ambazo unatakiwa uilipie viza yako. Tiketi ya ndege au basi na pesa za kujikimu ndio mambo muhimu ya kuyazingatia.
Pia utatakiwa kuwa na hati ya kusafiria (paspoti) na labda Cheti cha Kimataifa cha Chanjo, pia kikijulikana kama "kadi ya njano." Hii ni kusema kuwa kazi ya kusafiri kuingia na kutoka itazidi kuwa nyepesi kwa nchi hizi, na shughuli za kibiashara zitakuwa.












