Homa ya Nyani: Mlipuko wa Mpox Afrika watangazwa kuwa dharura ya kiafya - nini kitakachofuata?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, David Wafula and Gem O'Reilly
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka, Nairobi and London
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Vituo vya Umoja wa Afrika vya Kudhibiti Magonjwa (CDC), vimetangaza rasmi aina mpya ya virusi vya mpox kuwa dharura ya kiafya kwa umma siku ya Jumanne.
Onyo hili juu ya mpox, ambayo zamani iliitwa Monkeypox, inaashiria awamu mpya na muhimu katika kushughulikia ugonjwa huu. Kamati ya wataalamu iliunga mkono kwa kauli moja uamuzi huo.
Virusi hivyo vinaenea kwa kasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku wataalamu wakisema ni aina hatari zaidi ya virusi.
Katika sehemu za magharibi na kati mwa Afrika, kesi zimekuwa zikiongezeka kwa miongo kadhaa. Lakini mwaka huu, kesi zimeongezeka kwa kiasi kikubwa huku mpox ikiripotiwa katika nchi 16 za Afrika.
Mwishoni mwa Julai, CDC iliripoti jumla ya kesi 37,583 tangu mwanzoni mwa 2022 na vifo 1,451 viliripotiwa kutoka nchi 15 Wanachama wa Umoja wa Afrika. Barani Afrika, CDC inaonya hali inaweza kuwa mbaya na imeomba chanjo ya haraka.
"Mpox si tishio tu Afrika, ni tishio la kimataifa, tishio ambalo halijui mipaka, halijui rangi wala imani," anasema mkurugenzi mkuu wa Afrika CDC, Jean Kaseya.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kipi cha kufanywa?
Michael Marks, profesa wa afya ya binadamu kutoka Taasisi ya London School of Hygiene & Tropical Medicine (LSHTM), aliiambia BBC "inawezekana mlipuko huo utasababisha maambukizi ya kimataifa."
Amesisitiza kuwa ni muhimu mwitikio wa kimataifa uende kusaidia nchi kama vile DR Congo. Tuweke nguvu zetu katika kusaidia watu ambao wako hatarini na kuwapa chanjo na huduma ya afya.
Aliongeza: "Changamoto moja kuu kwa sasa ni kwamba hatujui ukubwa wa kweli tatizo hili na ni kesi ngapi zisizo rikodiwa, kwa hivyo hatujui kiwango cha kweli cha vifo."
Mpox ni nini?
Ugonjwa wa Mpox husababishwa na virusi vya monkeypox, virusi kutoka familia ya virusi vya smallpox. Awali maambukizi yalianza kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu, hasa katika nchi zilizo karibu na misitu ya mvua ya kitropiki.
Katika maeneo haya, kuna maelfu ya maambukizi na vifo kutokana na ugonjwa huo kila mwaka - na watoto chini ya umri wa miaka 15 wameathirika zaidi.
Hali mbaya zaidi ya mlipuko wa kimataifa ilikuwa mwaka 2022, ambao ulienea katika karibu nchi 100 ambazo hazina historia ya virusi hivyo.
Virusi vya aina ya pili na hatari zaidi, vipo zaidi katika eneo la Afrika ya kati. Na ndio virusi vilivyogunduliwa nchini DR Congo na kuenea hadi Kenya, Rwanda, na Uganda.
Dalili ni zipi?
Huenezwa kwa mgusano wa moja kwa moja na watu walioambukizwa. Dalili ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa, uvimbe, maumivu ya mgongo na misuli kuuma.
Mara baada ya kupata homa, upele unaweza kutokea, mara nyingi huanza kwenye uso kisha kuenea kwenye sehemu nyingine za mwili, viganja vya mikono na nyayo za miguu.
Upele ambao unaweza kuwasha au kuuma, hubadilika hatua tofauti kabla kutengeneza kipele ambacho hupasuka baadaye. Vidonda vinaweza kusababisha makovu.
Maambukizi kwa kawaida huisha yenyewe na hudumu kati ya siku 14 na 21. Kesi mbaya zinaweza kusababisha vidonda kushambulia mwili mzima, na haswa mdomo, macho na sehemu za siri.
Shirika la Afya Ulimwenguni linashauri ikiwa umeambukizwa Mpox, unapaswa kujitenga kwa kipindi chote cha maambukizi hadi upele utakapo pasuka. Pia kufunika vidonda na kuvaa barakoa kunaweza kusaidia kuzuia kuenea.

Chanzo cha picha, Reuters
Dharura ya Afya ni nini?
Tangazo la dharura ya afya kwa umma litasaidia serikali kuratibu mapambano na kuongeza usambazaji wa vifaa vya matibabu na misaada katika maeneo yaliyoathirika.
Profesa Marks kutoka LSHTM anasema, aina hii ya tangazo linaweza kusaidia mataifa ya Afrika kupata usaidizi wa kifedha. Linaweza kupelekea kutolewa kwa aina maalumu ya ufadhili. Kwa mfano, Umoja wa Ulaya umetoa tafiti hivi karibuni ili kusaidia.
"Pia tangazo hili huzalisha hatua katika ngazi ya kitaifa kwa kuongeza vipaumbele vya wizara za afya."

Chanzo cha picha, Getty Images
Vipi kuhusu aina mpya?
Profesa Marks anasema kumekuwa na tofauti kubwa ya idadi ya vifo kati ya Afrika Magharibi na vile vya Afrika ya kati.
"Virusi vya Clade 2- ambavyo vinapatikana Afrika Magharibi kwa kawaida husababisha kiwango cha chini cha vifo yaani 1%. Lakini Clade 1 ambayo ipo DRC ina kiwango cha juu cha vifo, kati ya 1-10%."
Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya CDC, kiwango cha vifo nchini DR Congo kwa sasa ni 4%. Lakini profesa huyo anasema, asilimia hiyo inaweza kuwa juu zaidi, ikiwa kesi zote zinazotokea zitarikodiwa.
Unasambaa vipi na nani aliye hatarini?
Njia kuu ya kuenea kwa maambukizi ni kugusana moja kwa moja kimwili na vidonda kwenye ngozi ya aliyeambukizwa, hii inaweza kutokea kwa njia ya ngono, lakini pia inaweza kutokea kwa kugusana kawaida, kwa mfano kugusana na mtoto wako.
Profesa Marks anasema "kufanya ngono kunachukua sehemu kubwa ya maambukizi ya janga hili".

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwezi Juni, mtu wa pili alikufa kutokana na Homa ya nyani nchini Afrika Kusini, chini ya saa 24 baada ya kifo cha kwanza kutokana na virusi hivyo kuripotiwa.
Wote waliogunduliwa walikuwa wanaume wenye umri wa kati ya miaka 30 na 39 ambao hawakuwa wametembelea nchi zingine zilizokumbwa na mlipuko, na kuashiria kuwa ugonjwa huo unasambazwa ndani.
Vipi kuhusu chanjo?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Profesa Marks anasema suala kubwa katika kukabiliana na mlipuko huo ni usambazaji wa chanjo, lakini kuna shida ya kutolingana kabisa kati ya idadi ya dozi za chanjo zinazopatikana katika nchi za Afrika na idadi ya watu ambao watahitaji kuchanjwa.
Dk Adeola Fowotade, Daktari Bingwa wa elimuvirusi katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Ibadan nchini Nigeria, anasema, wiki kadhaa zilizopita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Nigeria ziliashiria kuwa ziko tayari kutoa leseni ya chanjo muhimu.
"Hii ni hatua ya kupongezwa katika kusaidia kupunguza kuenea kwa virusi katika nchi za Afrika na ninatumai nchi zingine zitapokea chanjo."
Lakini Dk Fowotade pia alieleza kuhusu umuhimu wa kutoa chanjo sawa na kampeni ya kutoa taarifa sahihi. "Taarifa potofu husababisha kukwama kwa chanjo," anasema.
"Moja ya changamoto ambayo tutakuwa nayo, ni hii ambayo tumekuwa nayo kila wakati wa utoaji wa chanjo barani Afrika - taarifa na habari za uongo na watu kukosa imani, haswa kwa kuwa huu ni mpango unaoungwa mkono na serikali."
DR Congo ina uzoefu wa utoaji wa chanjo kwa kiasi kikubwa kutokana na milipuko wa Ebola - virusi hatari ambavyo vinaweza kusababisha homa ya ghafla, kuchoka, maumivu ya misuli na koo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












