'Mpox iliifanya koo yangu kuniuma sana hadi nikashindwa kulala'

Chanzo cha picha, Mercy Juma / BBC
- Author, Mercy Juma
- Nafasi, BBC News, Bujumbura
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Egide Irambona, 40, anakaa kifua wazi kwenye kitanda chake cha hospitali, karibu na dirisha, kwenye chumba cha matibabu ambacho anaishi na wanaume wengine wawili.
Miale ya jua la jioni inayoangaza juu ya jiji kuu la Burundi, Bujumbura, inachuja ndani. Uso wake, ukiwa na mwanga mwepesi, umefunikwa na malengelenge. Kifua chake pia, na mikono yake.
"Nilikuwa na uvimbe kwenye koo langu. Ilikuwa chungu sana sikuweza kulala. Baadaye maumivu yalipungua hapo na kuhamia kwenye miguu yangu,” anaiambia BBC.
Bw Irambona ana mpox.
Yeye ni mmoja wa zaidi ya watu 170 waliothibitishwa kuwa na maambukizi tangu mwezi uliopita nchini Burundi. Ni moja ya nchi maskini zaidi duniani, inapakana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kitovu cha milipuko kadhaa ya hivi karibuni ya mpox, ambayo imesababisha vifo vya watu 450 na kesi 14,000 zinazoshukiwa kufikia sasa mwaka huu.
Nchini Burundi, hakuna mtu aliyefariki kutokana na ugonjwa huo na bado haijabainika ikiwa mlipuko wa sasa - ni wa aina mpya uitwao Clade 1b - kwa sababu hakuna uwezo wa kutosha wa kufanya upimaji katika maeneo yaliyoathirika.
Lakini, imetangazwa kuwa dharura ya kiafya duniani kwa sababu ya hofu inaweza kuenea haraka kwa nchi na maeneo ambayo hayakuathiriwa hapo awali.
Hii ni siku ya tisa ya Bw Irambona ya matibabu katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha King Khaled. Njia moja ambayo virusi huenezwa ni kwa kuwasiliana kwa karibu na mtu aliyeambukizwa na inaonekana kwamba alimuambukiza mke wake.
Pia anatunzwa katika kituo hicho hicho.
“Nilikuwa na rafiki yangu aliyekuwa na malengelenge. Nadhani nimepata kutoka kwake. Sikujua ni mpox. Tunashukuru watoto wetu saba hawajaonyesha dalili zozote za kuwa nayo,” Bw Irambona asema, huku sauti yake ikififia.
Hospitali hii ya Bujumbura ni mojawapo ya vituo vitatu vya matibabu ya mpox jijini.
Vitanda 59 kati ya 61 vinavyopatikana vinatumiwa na wagonjwa walioambukizwa - theluthi moja ni chini ya umri wa miaka 15 na, kulingana na Shirika la Afya Duniani, watoto ndio waliothiriwa zaidi hapa.

Chanzo cha picha, Mercy Juma / BBC
Odette Nsavyimana ni daktari anayesimamia hospitali hiyo na anasema idadi ya wagonjwa inaongezeka.
"Sasa tunaweka mahema nje." Kuna hema tatu kwa sasa - moja ina watu watatu walioambukizwa, moja ya kushikilia watu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi na moja kuwatenga watu waliothibitishwa kuwa na mpox kabla ya kuhamishiwa wodi.
"Hali ni ngumu, hasa watoto wachanga. Hawawezi kukaa peke yao, kwa hivyo inabidi niwaweke mama zao hapa pia. Hata kama hawana dalili zozote ... ni hali ngumu sana," Dk Nsavyimana anasema.
Burundi sasa inashuhudia ongezeko la maambukizi ya mpox.
"Nina wasiwasi kuhusu idadi hiyo. Ikiwa itaendelea kuongezeka, hatutakuwa na uwezo wa kushughulikia hali hiyo."
Jitihada nyingi hufanywa kuwatenga walioambukizwa kutoka kwa watu wengine wa hospitali. Kuna mkana mwekundu kila mahali, na wageni, ambao wanatakiwa kuvaa vifaa vya kujikinga, wako mbali na wale walioambukizwa.

Chanzo cha picha, Mercy Juma / BBC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Maafisa wa matibabu wana wasiwasi kuhusu rasilimali chache. Kuna maabara moja tu nchini ambapo sampuli za damu zinaweza kupimwa virusi, hakuna vifaa vya kutosha vya kupima na hakuna chanjo.
Kudumisha hali ya usafi kote Bujumbura pia ni vigumu kwani ufikiaji wa rasilimali za kimsingi kama vile maji ni mdogo katika jiji hilo. Kuna uhaba wa maji ya bomba na watu wanaweza kuonekana wakipanga foleni kwenye bomba za umma.
Dk Liliane Nkengurutse, mkurugenzi wa kitaifa wa Kituo cha Operesheni za Dharura za Afya ya Umma, anasema ana wasiwasi sana kuhusu hali ya siku zijazo.
“Hii ni changamoto ya kweli. Ukweli kwamba uchunguzi unafanywa tu katika sehemu moja huchelewesha kugundua wagonjwa wapya.
"Vituo vya afya vinapiga simu kwa maabara vikisema vina watu ambao wanashukiwa kuwa na dalili ya maambukizi, lakini inachukua muda kuwapeleka maafisa wa maabara katika sehemu walipo wale wanaoshukiwa kuwa na maambukizi kuchukua sampuli.
"Na inachukua muda zaidi kutoa matokeo ya vipimo. Tunahitaji takriban dola milioni 14 ili kuweza kupeleka majibu yetu katika ngazi nyingine,” anasema.
Licha ya mazungumzo ya chanjo kufikia DR Congo mapema wiki ijayo, hakuna ripoti za hatua kama hiyo kwa Burundi.

Chanzo cha picha, Mercy Juma / BBC
Uelewa wa umma kuhusu ungonjwa wa mpox ni mdogo.
Mji wa Bujumbura uko umbali wa kama dakika 20 tu kutoka mpaka wa DR Congo na ni kitovu cha usafiri na biashara ya kuvuka mpaka. Lakini hakuna mtu
Jiji hili lina shughuli nyingi. Watu bado wananunua na kuuza bidhaa kama kawaida. Kushikana mikono, kukumbatiana na mawasiliano ya karibu sana ni jambo la kawaida. Kuna foleni ndefu kwenye vituo vya mabasi, huku watu wakihangaika kuingia kwenye magari ambayo tayari yamesongamana.
“Watu wengi hawaelewi uzito wa suala hili. Hata pale ambapo kumekuwa na kesi, watu bado wanachanganyika,” Dk Nkengurutse anasema.
BBC ilizungumza na watu kadhaa mjini Bujumbura na wengi hawakujua mpox ni nini. Na wale waliofanya hawakujua kwamba ilikuwa inaenea katika nchi yao.
“Nimesikia kuhusu ugonjwa huu, lakini sijawahi kuona mtu anayeugua. Nimeiona tu kwenye mitandao ya kijamii,” mtu mmoja alisema.
"Najua inaathiri watoto wachanga na vijana. Ninaogopa, lakini hiyo haimaanishi kuwa nitabaki tu nyumbani. Lazima nifanye kazi. Familia yangu inapaswa kula,” mwingine alisema.
Wahudumu wa afya wanajua kuwa kushawishi watu kuchukua huduma zaidi kunaweza kuwa jambo gumu miongoni mwa watu wenye mashaka ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi.
Lakini wataendelea kuwatibu wagonjwa, kuhakikisha wanapata nafuu na kujaribu kufuatilia wale ambao wamekuwa wakiwasiliana nao katika juhudi za kudhibiti kuenea kwa virusi.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












