“Ninamchukia Trump, ila yeye anampenda – lakini sote tunaamini majaribio ya kumuua yalipangwa”

Chanzo cha picha, Getty Images/BBC
- Author, Marianna Spring
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Wild Mother – jina maarufu la mtandaoni la mwanamke anayeitwa Desirée - anaishi katika milima ya Colorado, huchapisha video kwa wafuasi wake 80,000 kuhusu maisha yake na binti yake. Anataka Donald Trump ashinde uchaguzi wa urais.
Takribani maili 70 kaskazini katika vitongoji vya Denver, yuko Camille, mfuasi mkubwa wa usawa wa kijinsia na mpinzani wa ubaguzi wa rangi, ambaye anaishi na kundi la mbwa na amekipigia kura chama cha Democratic kwa miaka 15 iliyopita.
Wanawake hao wawili wanatofautiana sana kisiasa - lakini wote wanaamini majaribio ya kumuua Trump yalipangwa. Lile shambulio la risasi mwezi Julai na njama iliyoshindwa ya mauaji ya mapema mwezi huu.
Nilisafiri hadi Colorado - kitovu cha nadharia za njama kuhusu uchaguzi wa 2020 kwamba uliibiwa. Nilitaka kuelewa ni kwa nini nadharia za mauaji hupangwa, zimeenea katika siasa na kwa watu kama Camille na Wild Mother.
Machapisho yanayopendekeza kwamba matukio yote mawili yamepangwa, yametazamwa zaidi ya mara milioni 30 kwenye X. Baadhi ya machapisho haya yalitoka katika akaunti zinazompinga Trump, huku sehemu ndogo yakitumwa na baadhi ya wafuasi wa rais huyo wa zamani.
Kwa mfuasi wa Democratic, Camille, timu ya Trump ilipanga hili ili kuongeza nafasi yake ya kushinda uchaguzi. Wild Mother - anaamini timu ya Trump ilifanya shambulio hilo ili kuunda maadui.
Hakuna ushahidi wa kuunga mkono nadharia yoyote za wanawake hawa.
Camille, mfuasi wa Democratic

Camille, anasema hii ni mara yake ya kwanza kutumia neno "kupangwa” kuelezea tukio kama hii. Siku zote aliamini Covid-19 ni kweli na alikuwa akipinga sana madai ya uwongo kuwa uchaguzi wa 2020 uliibiwa.
Lakini tarehe 13 Julai mwaka huu, alipokuwa amekaa mbele ya TV yake nyumbani akitazama moja kwa moja, wakati Donald Trump alipopigwa risasi kwenye mkutano wa kampeni huko Pennsylvania, anasema mara moja alifikiria: "Oh, hili limeandaliwa."
Namna Donald Trump alivyoweza kuinua ngumi hewani na akapigwa picha, ndilo lililomtia shaka Camille. Alikuwa na maswali kuhusu Secret Service kuruhusu shambulio hilo kutokea. Mkurugenzi wa kikosi hicho amejiuzulu kwa makosa ya siku hiyo.
Mshambuliaji alikuwa kijana wa miaka 20, Thomas Matthew Crooks, ambaye aliuawa na wadunguaji wa Secret Service. Sababu ya kufanya shambulio bado haijajulikana – na hilo limeacha maswali mengi. Na kwa hivyo mawazo ya Camille yanaendelea kuongezeka.
Akiwa tayari ana mashaka kwamba kuna kitu hakiko sawa, Camille aligeukia X kupata majibu zaidi.
"Nakubali siku hizi ninatumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii, na hilo, naamini ni aina ya tatizo," ananiambia.
Wild Mother, mfuasi wa Trump

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wild Mother pia aligeukia mitandao ya kijamii kutafuta majibu. Tunaposimama kuzungumza kwenye maporomoko ya maji katika mji mdogo anaouita nyumbani, anaeleza jinsi alivyoanza kuchapisha maoni yake mwaka 2021 kuhusu dawa za mitishamba na kuwa mama.
Kisha akaanza kuchapisha nadharia ambazo hazijathibitishwa kuhusu kile kilichokuwa kikitendeka nyuma ya vichwa vya habari - kama vile afya ya Binti wa Mfalme wa Wales au kuporomoka kwa daraja la Baltimore mapema mwaka huu - na wafuasi wakazidi kuongezeka.
Anasema amezama katika kile anachokiita "wazo mbadala kuhusu ukweli" tangu akiwa na umri mdogo na anaamini tumedanganywa kuhusu kilichotokea wakati John F Kennedy alipouawa katika miaka ya 1960, tukio la Septemba 11 mwaka 2001 na janga la Covid-19.
Alianza kumpenda Trump alipoanza kutumia muda mwingi mtandaoni wakati wa janga hilo.
Wafuasi wa QAnon walikuwa miongoni mwa umati wa watu waliovamia jengo la Bunge la Marekani tarehe 6 Januari, 2021, katika maandamano ya kupinga ushindi wa Joe Biden baada ya uchaguzi.
Sasa Wild Mother anataka kuamini madai aliyoyasoma kwenye mitandao ya kijamii kwamba watu hao wanaweza kuwa walihusika kwa njia fulani katika kuandaa shambulio dhidi ya Trump mwezi Julai. Lengo lao ni kuvilaumu vikosi vya usalama.
Lakini Wild Mother anasema, kulingana na machapisho mengine ambayo ameyaona mtandaoni, "watu wema katika jeshi," wanaojulikana kama White Hats, walikuwa wakifanya operesheni za siri ili kukabiliana na vikosi viovu vya usalama.
Na nadharia iliyoibuka inadai, jaribio la mauaji ya Julai lilifanywa na White Hats ili kuonyesha umma tishio ambalo Trump linamkabili.
Wild Mother anasema hana uhakika ikiwa nadharia ya QAnon ni ya kweli.
"Nadhani nchi yetu inahitaji kuokolewa kutoka serikali ya hivi sasa. Hali ni mbaya. Mbaya," anasema.
"Ni sawa na kwenda kwenye maonyesho ya uchawi ukiwa mtoto halafu unagundua kwa mara ya kwanza kuwa mchawi sio kitu cha kweli. Sasa kila ukienda kwenye maonyesho ya uchawi unajua wanachofanya." ananiambia.
Mitandao ya Kijamii

Chanzo cha picha, Getty Images
Kadiri Camille na Wild Mother walivyoanza kutegemea zaidi mitandao ya kijamii, imani walizozibeba zilichangia kuwaondoa katika ulimwengu wa uhalisia.
Camille hupata tabu kufanya mazungumzo na baadhi ya watu katika familia yake ambao wanamuunga mkono Trump, huku Wild Mother, anasema imani zake zilichangia katika kutengana na mume wake wa zamani, ambaye anasema alipinga vikali nadharia hizo.
Mazingira haya ya mashaka na migogoro hayaleti matokeo mabaya kwa maisha binafsi tu ya wanawake hawa - lakini kwa jamii pia.
Maafisa, wafanyakazi wa uchaguzi - na wanasiasa kote Marekani wamejikuta chini ya chuki na vitisho kama matokeo ya imani hii pana kwamba karibu kila kitu - ikiwa ni pamoja na uchaguzi - huibiwa na matokeo hupangwa.
Kwa Wild Mother: "Sio kuwaandika maseneta wako na kuwaita majina ya kibaguzi. Lakini kama ukiwa mtu ambaye kweli ulifanya utafiti na kugundua kulikuwa na suala fulani, naamini unapaswa kutumia sauti yako kusema?" anasema.

Chanzo cha picha, Reuters / Martin County Sheriff's Office
"Nadhani sote tuna njia za kufanya hivyo."
Ingawa Wild Mother na Camille wanasema hawajawahi kumtishia mtu yeyote - na wanaonekana ni watu wenye huruma, wema - lakini kutoamini kwao ambako kunachochewa kwa sehemu na mitandao ya kijamii kumeondoa imani yao katika jamii na taasisi zake.
Camille, ambaye alipinga nadharia za njama, sasa anajikuta akitumia lugha hiyo hiyo.
Anaonekana kuwa mmoja wa watu wengi walioingizwa katika njia hii ya kufikiri kuhusu jaribio la mauaji la Julai na mitandao ya kijamii inayowavuta watu zaidi katika ulimwengu wa mtandaoni ambao hauendani na ukweli.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Seif Abdalla












