Kwaheri hadi kesho
Na hapa ndio mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, tukutane kesho panapo uhai.
Kuna msongamano wa magari kwenye barabara kuu kati ya Beirut na kusini, na magari yamejaa familia, mifuko, masanduku na magodoro.
Na Lizzy Masinga & Rashid Abdallah
Na hapa ndio mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, tukutane kesho panapo uhai.

Chanzo cha picha, Kamol Das
Kukamatwa kwa mtawa wa Kihindu nchini Bangladesh kumezua vita vipya vya maneno na jirani yake India kuhusu hali ya jamii ya wachache nchini humo.
Chinmoy Krishna Das, msemaji wa shirika la Wahindu lenye makao yake Bangladesh, alikamatwa wiki hii kwa tuhuma za uchochezi, na kusababisha vurugu zilizopelekea kifo cha mtu mmoja.
India ilitoa taarifa ikielezea "wasiwasi mkubwa" juu ya kukamatwa kwake na kuitaka Bangladesh kuhakikisha usalama "wa Wahindu na jamii nyingine za walio wachache."
Bangladesh ilijibu saa chache baadaye, ikielezea "kusikitishwa kwake juu ya kueleweka vibaya na baadhi ya watu kuhusu kukamatwa kwake."
Uhusiano kati ya majirani hao, ambao kwa kawaida wamekuwa na uhusiano wa kindugu, umekuwa wa vita baridi tangu waziri mkuu wa zamani Sheikh Hasina kuondolewa madarakani mwezi Agosti baada ya maandamano ya wanafunzi ya wiki kadhaa.
Tangu wakati huo, amekuwa akikaa India, na kutoa changamoto kwa diplomasia kati ya nchi hizo.
Wakati wa uongozi wa Hasina wa miaka 15, Bangladesh ilikuwa mshirika wa kimkakati na mshirika muhimu kwa usalama wa India, hasa katika majimbo ya kaskazini-mashariki.
Tangu kuondolewa kwake madarakani, India mara kwa mara imeelezea wasiwasi kuhusu usalama wa Wahindu walio wachache nchini Bangladesh, madai ambayo Bangladesh inayakanusha.
Wahindu ndio walio wachache zaidi katika nchi ya Bangladesh yenye Waislamu wengi, ambao ni takribani 8% tu ya wakazi.
Pia unaweza kusoma:

Chanzo cha picha, Reuters
Rais Joe Biden amesema Marekani itaanzisha juhudi nyingine kwa kushirikiana na serikali za kikanda ili kufikia usitishwaji mapigano huko Gaza, ikijumuisha kuachiliwa kwa mateka na kuondolewa kwa Hamas mamlakani.
Matamshi yake huko X yanakuja saa chache baada ya kusitishwa kwa mapigano nchini Lebanon kati ya Israel na Hezbollah, na kumaliza kwa vita vya karibu miezi 14.
"Katika siku zijazo, Marekani itafanya juhudi nyingine kwa kushirikiana na Uturuki, Misri, Qatar, Israeli na nchi nyingine kufikia usitishaji wa mapigano huko Gaza na mateka kuachiliwa na kumalizika kwa vita bila Hamas kuwepo madarakani," aliandika Biden kwenye X. .
Hamas imesema inatumai kupata makubaliano kama hayo huko Gaza lakini inaendelea kukataa matakwa ya Israel, ya kujisalimisha.
Israel ilianzisha mashambulizi ya kuiangamiza Hamas kujibu mashambulizi ya kundi hilo kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takribani watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Zaidi ya watu 44,000 wameuawa na zaidi ya 104,000 wamejeruhiwa huko Gaza tangu mashambulizi hayo yalipoanza, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

Chanzo cha picha, Reuters
Rais mteule wa Marekani Donald Trump anasema Jamieson Greer atakuwa mshauri wa sera kibiashara atakapo chukua madaraka tarehe 20 Januari 2025.
Tangazo hilo linakuja baada ya Trump kutishia kuweka ushuru mpya - kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka China, Canada na Mexico ili kudhibiti mtiririko haramu wa watu na dawa za kulevya kuingia Marekani.
Greer, mwanasheria wa biashara, alikuwepo katika muhula wa kwanza wa urais wa Trump - na alichukua jukumu muhimu katika kuweka ushuru mkubwa kwa bidhaa kutoka China.
Ni sera ya muda mrefu ya Trump ili kuhimiza wateja kununua bidhaa za ndani za Marekani kwa kufanya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kuwa ghali.
Pia unaweza kusoma:

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), anasema ameomba hati ya kukamatwa kwa kiongozi wa kijeshi wa Myanmar, Min Aung Hlaing kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu alioufanya dhidi ya Waislamu wa Rohingya.
Karim Khan amesema kuna sababu za kuridhisha za kuamini kuwa Min Aung Hlaing alihusika na utekelezaji wa jinai kwa kuwatesa na kuwafukuza Warohingya hadi nchi jirani ya Bangladesh.
Maelfu ya Warohingya waliikimbia Myanmar mwaka 2017 ili kuepuka mashambulizi ambayo Umoja wa Mataifa umeyataja kuwa mauaji ya halaiki yaliyoanzishwa na jeshi la Burma.
Lakini serikali ya Myanmar imekanusha hilo, ikisema ilikuwa ikiendesha operesheni dhidi ya wanamgambo wa Rohingya.
Mashambulizi dhidi ya Warohingya yalianza mwaka 2017, baada ya wanamgambo wa Rohingya kushambulia vituo zaidi ya 30 vya polisi nchini Myanmar.
Warohingya wanasema askari walijibu mashambulizi hayo kwa kuchoma vijiji vyao, kuwashambulia na kuua raia.
Takribani Rohingya 6,700, ikiwa ni pamoja na watoto wasiopungua 730 walio na umri wa chini ya miaka mitano, waliuawa katika mwezi mmoja baada ya ghasia kuanza, kulingana na shirika la madaktari wasio na mipaka (MSF).
Amnesty International inasema jeshi la Myanmar pia liliwabaka na kuwadhalilisha wanawake na wasichana wa Rohingya.
Ghasia za kutisha dhidi ya Warohingya zilisababisha malalamiko ya kimataifa, lakini kiongozi wa wakati huo wa Burma, Aung San Suu Kyi alikataa kuwafungulia mashitaka majenerali wake.
Myanmar haijajiunga na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, hivyo kufungua kesi dhidi ya jeshi awali ilionekana kuwa haiwezekani.
Hata hivyo, waendesha mashitaka wa ICC baadaye walisema baadhi ya makosa ya jinai, hasa kufukuzwa nchini, yalitokea Bangladesh - ambayo imejiunga na mahakama – na kulikuwa na sababu za kufunguliwa mashitaka.
Baada ya miaka mitano ya uchunguzi, mwendesha mashtaka mkuu anasema ana ushahidi wa kutosha kuomba hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Min Aung Hlaing.
Jopo la majaji watatu wa ICC litatoa uamuzi kuhusu ombi la mwendesha mashtaka.
Pia unaweza kusoma:

Chanzo cha picha, Supplied
Afisa wa polisi aliyempiga shoti kupitia bastola mwanamke mwenye umri wa miaka 95, aliyekuwa na dalili ya tatizo la akili katika nyumba ya kutunza wazee nchini Australia amepatikana na hatia ya mauaji.
Kristian White, 34, alitumia silaha yake dhidi ya Clare Nowland baada ya ajuza huyo kukutwa akirandaranda na kisu kidogo cha jikoni tarehe 17 Mei 2023.
Kifo chake wiki moja baadaye kilisababisha malalamiko ya umma, lakini White - afisa wa ngazi ya juu wa polisi - alisema mahakamani kwamba matumizi yake ya nguvu yalikuwa halali na sawa kwa tishio lililokuwepo.
Hata hivyo, waendesha mashtaka, walisema Bi Nowland - ambaye alitegemea mkongojo kutembea akiwa na uzito wa chini ya kilo 48 - hakuwa hatari na afisa huyo "asiyekuwa na subira" alipuuza wajibu wake wa kumhudumia ajuza huyo.
Maafisa wa polisi walimwomba mara kadhaa adondoshe kisu chake. Muda mfupi kabla ya kupigwa shoti, kanda za video zilionyesha mwanamke huyo akitembea kusonga mbele polepole - mita 1 kwa muda wa dakika moja - kabla ya kusimama na kuinua kisu chake.
White alimuonya Bi Nowland kabla ya kufyatua bastola ya shoti, akiwa umbali wa mita 1.5 hadi 2. Alianguka na kufikia kichwa chake, na kusababisha ubongo kuvuja damu.
Mwendesha mashtaka alisema White alitumia silaha yake dakika tatu tu baada ya kumfikia mwanamke huyo: "Alikuwa amekasirika, hana subira, hakuwa tayari kusubiri."
Familia ya Bi Nowland, iliyokuwa mahakamani kusikiliza uamuzi wa hakimu, iliwashukuru waendesha mashtaka na hakimu.
White, ambaye atasalia nje kwa dhamana, atahukumiwa baadaye.

Chanzo cha picha, CHADEMA
Jeshi la Polisi nchini Tanzania, linamshikilia Askari Magereza kwa tuhuma za kusababisha Kifo cha George Juma (41), aliyekuwa Mgombea katika Kitongoji cha Stendi, Kata ya Mkwese, Jimbo la Manyoni Mashariki kupitia Chadema katika Uchaguzi unaoendelea wa Serikali za Mitaa.
Taarifa ya Polisi inasema marehemu alijeruhiwa na risasi katika purukushani zilizotokea, baada ya wafuasi wa Chadema kuwavamia wafuasi wa chama tawala CCM waliokuwa katika kikao cha ndani na hivyo Askari Magereza katika kituo cha karibu walipigiwa simu.
Taarifa hiyo inasema, walipofika eneo hilo walishambuliwa kwa mawe ambapo walipiga risasi hewani ili kuwazuia wafuasi wa Chadema, na katika purukushani hizo, risasi moja ilimpata Marehemu George Juma.
Lakini taarifa ya Polisi inakinzana na ile ya Chadema, ambapo chama hicho kikuu cha upinzani kinasema mwanachama wake alivamiwa nyumbani kwake na watu waliofahamika kuwa makada wa CCM, ndipo ukatokea mzozo na Polisi walifika nyumbani kwake na kumpiga risasi ndugu George Juma Mohamed na kufariki dunia .
Katika tukio jingine mwanachama na kiongozi wa Chadema katika Mji wa Tunduma, Steven Chalamila ameripotiwa kushambuliwa kwa mapanga na kuuawa.
Vyombo vya habari vya ndani nchini Tanzania, vikinukuu taarifa ya Chadema, vinasema mauaji hayo yamefanyika nyumbani kwa mwanachama huyo usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024.
Ingawa Jeshi la Polisi bado halijatoa taarifa rasmi juu ya tukio hili.
Matukio haya yanakuja wakati Tanzania ikianza uchaguzi wa serikali za mitaa siku ya leo, kuwachagua viongozi wao wa mashinani.
Pia unaweza kusoma:

Chanzo cha picha, AFP
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah nchini Lebanon yalihusisha pande kadhaa za kimataifa; yalisimamiwa na Marekani, huku Ufaransa ikitarajiwa kusaidia kufuatilia makubaliano hayo.
Asubuhi ya leo, Uturuki imeunga mkono kuanzishwa kwa "amani ya kudumu" nchini Lebanon. Katika chapisho kwenye X, wizara yake ya mambo ya nje inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa "kutoa shinikizo" kwa Israel "kutoa fidia kwa uharibifu uliosababisha nchini Lebanon."
Iran, ambayo inaiunga mkono Hezbollah, inasema inakaribisha habari za kumalizika kwa "mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon."
Wakati usitishaji mapigano ukianza nchini Lebanon, mapigano yanaendelea kusini ya Gaza. Hii imeifanya Jordan - ambayo inapakana Israel upande wa Mashariki - kutoa wito wa juhudi kubwa zaidi za kimataifa ili kumaliza vita huko Gaza.
Pia Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, anasema mpango huo lazima uwe "suluhisho la kudumu" nchini Lebanon, na kuongeza kuwa lazima kuwe na "maendeleo ya haraka" kuelekea makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza.
Pia unaweza kusoma:

Chanzo cha picha, EPA
Timua ya uokoaji kutoka Misri imepata miili minne na manusura watano siku ya Jumanne wakati wa msako katika Bahari ya Shamu baada ya boti ya watalii iliyokuwa imebeba watu 44 kuzama siku ya Jumatatu.
Jumla ya watu 33 wameokolewa kufikia sasa lakini saba bado hawajapatikana kufikia Jumanne jioni.
Boti hiyo ya kisasa ilikuwa imebeba watalii 31 na wafanyakazi 13, kabla ya kupigwa na wimbi kubwa karibu na mji wa Marsa Alam na kusababisha kupinduka.
Boti hiyo ilizama ndani ya dakika tano hadi saba tangu kuondoka, kwa mujibu wa gavana wa Bahari ya Shamu, Maj-Gen Amr Hanafi. Anasema baadhi ya watu walishindwa kutoka kwenye vyumba vyao.
Jumla ya watu 28 waliokolewa na wanajeshi na boti ya watalii iliyokuwa ikipita saa chache baada ya boti hiyo kuzama.
Boti hiyo yenye urefu wa mita 44 (futi 144) iliondoka kwenye bandari karibu na Marsa Alam siku ya Jumapili kwa safari ya siku tano ya kupiga mbizi.

Chanzo cha picha, AFP
Upigaji kura unaendelea nchini Namibia katika uchaguzi ambao unaweza kuwa wenye ushindani mkubwa tangu uhuru wake baada ya kutawaliwa na wazungu miaka 34 iliyopita.
Netumbo Nandi-Ndaitwah anatafuta kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini humo.
Anapeperusha bendera ya Chama tawala cha (Swapo), kuchukua nafasi ya Hage Geingob, ambaye alifariki Februari baada ya kukaa madarakani kwa miaka tisa.
Lakini ukosefu mkubwa wa ajira, umasikini, ukosefu wa usawa na madai ya ufisadi yameondoa uungwaji mkono kwa chama.
Mpinzani mkuu wa Nandi, Ndaitwah ni Panduleni Itula wa chama cha Independent Patriots for Change (IPC), pamoja na wagombea wengine 14.
Vyombo vya habari vya ndani vilionesha misururu mirefu iliyokuwa tayari shuleni na vituo vingine vya kupigia kura huku upigaji kura ukianza Jumatano asubuhi.

Vikosi vya Israel bado viko sehemu za kusini, huku kuondoka kwao kukitarajiwa kuwa kwa taratibu wakati wa usitishaji mapigano wa siku 60.
Jeshi la Lebanon, linalotarajiwa kuongeza uwepo wake kusini na wanajeshi 5,000 wa ziada, lilisema linachukua "hatua zinazohitajika" kukamilisha hilo.

Maelfu ya watu wameanza kurejea makwao, saa chache baada ya kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na Hezbollah kuanza kutekelezwa.
Kuna msongamano wa magari kwenye barabara kuu kati ya Beirut na kusini, na magari yamejaa familia, mifuko, masanduku na magodoro.
Tumeona bendera nyingi za Hezbollah zikipeperushwa kwenye madirisha.
Watu wengine, wanapoona kamera yetu, wanatabasamu na kutoa ishara ya "V" ya ushindi.
Hatua hii inafanyika wakati mamlaka ya Israel na Lebanon zikionya watu wasirejee sasa.

Chanzo cha picha, Reuters
Urusi imesema kuwa mfumo muhimu wa ulinzi wa anga na kambi ya anga katika eneo la Kursk ilipigwa na Ukraine kwa makombora ya Atacms yanayotolewa na Marekani.
Taarifa ya wizara ya ulinzi, ambayo ilitishia kulipiza kisasi, imekuja siku moja baada ya Ukraine kusema ilikuwa imefikia malengo katika eneo hilo.
Wakati huohuo jeshi la anga la Ukraine lilisema Urusi ilirusha droni 188 katika shambulio moja Jumatatu usiku, na kuharibu miundombinu muhimu.
Mvutano umekuwa mkubwa tangu Marekani iliporipotiwa kuruhusu Ukraine kutumia makombora ya Atacms kwenye shabaha ndani ya Urusi wiki iliyopita, ili kujibu hatua ya Urusi kupeleka wanajeshi wa Korea Kaskazini.
Wiki hiyo ilimalizika kwa Urusi kutumia kombora jipya la masafa ya kati la Oreshnik kwenye mji wa Dnipro nchini Ukraine.
Mashambulizi ya kwanza yaliyoripotiwa kufanywa na Atacms katika eneo la Urusi yaliripotiwa Jumanne, wakati Urusi iliposema kuwa vipande vilivyoanguka vilisababisha moto katika kituo cha kijeshi.
Unaweza kusoma;

Chanzo cha picha, Faustine Ndugulile/X
Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika, Dkt Faustine Ndugulile ameaga dunia.
Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson ametangaza taarifa za kifo chake kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 27, nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
''Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile. Kwa niaba ya Wabunge ninatoa pole kwa familia, wakazi wa Kigamboni na Watanzania wote.'' Alisema Spika Tulia.
Naye Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kwa familia, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi wa Kigamboni, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote.
Dkt Ndugulile pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya ya Bunge la Tanzania, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabunge ya Kimataifa (IPU) Advisory Group Health na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mtandao wa Kamati za Afya za Bunge la Afrika (NEAPACOH).
Dk. Ndugulile aliwahi kuwa naibu waziri wa Afya wa Tanzania kati ya 2017-2020, pia aliwahi kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari 2020-2021.
Pia alifanya kazi kama mkurugenzi katika Wizara ya Afya Tanzania anayeshughulikia huduma za uchunguzi na pia meneja wa programu mwanzilishi wa Huduma ya Kitaifa ya Usambazaji Damu mwaka 2006.
Kati ya 2007-2010, aliwahi kuwa Mshauri Mkazi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) nchini Afrika Kusini akitoa msaada wa kiufundi kwa nchi nyingine nyingi kama vile Angola, Msumbiji, Tanzania na Rwanda.
Unaweza kusoma;

Watanzania hii leo wanapiga kura kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
Wapiga kura wanapiga jumla ya kura sita; Wajumbe kundi la wanawake 2, Wajumbe kundi mchanganyiko 3, na Mwenyekiti wa Mtaa 1.








Chanzo cha picha, Reuters
Unaweza kusoma

Chanzo cha picha, EPA
Mpango wa makubaliano ya Israel na Hezbollah kusitisha mapigano uliotangazwa siku ya Jumanne lazima sasa kutekelezwa.
Iwapo makubaliano hayo yatadumu, yatamaliza vita vya zaidi ya mwaka mmoja kati ya Israel na kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran.
Mapigano hayo yaliongezeka sana mwezi Septemba, wakati Israel ilipozidisha mashambulizi ya mabomu na kuanzisha uvamizi mdogo wa ardhini.
Kama ukumbusho, chini ya masharti ya usitishaji vita, vikosi vya Israeli vitaondoka Lebanon ndani ya siku 60, wakati vikosi vya Hezbollah vitachukuliwa na vikosi vya jeshi la Lebanon kusini mwa nchi katika kipindi hicho.
Unaweza kusoma;