Karim Khan: Mwendesha mashtaka wa ICC ni nani?

Chanzo cha picha, REUTERS
- Author, Paula Rosas
- Nafasi, BBC
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ambaye ameomba vibali vya kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na viongozi wa Hamas, aliwahi kuwa wakili wa watu wenye utata wanaotuhumiwa kwa uhalifu sawa na wale anaowafuatilia hivi sasa.
"Sioni tofauti yoyote kati ya kufungua kesi na kumtetea mtuhumiwa," alisema muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwa muhula wa miaka 9 ulioanza 2021.
“Kuwa na uzoefu wa sheria kwa pande zote mbili hukufanya uaminike zaidi na pia inakusaidia kuepuka mawazo mabaya kama vile kufikiri wakili wa utetezi ni mwili wa shetani au mwendesha mashtaka, anafanya kazi ya Mungu.”
Vitisho dhidi ya Khan

Chanzo cha picha, REUTERS
Wiki hii Khan ameonyesha kwamba haogopi kuanzisha kesi zenye uzito duniani.
Karim Khan amekumbana na ukosoaji kutoka Israel na washirika wake, ikiwemo Marekani na Uingereza, kwa kumweka Waziri Mkuu wa Israel kwa mara ya kwanza katika kundi moja na Omar al-Bashir, Vladimir Putin na Joseph Kony; watuhumiwa wa uhalifu wa kivita.
Sasa kundi la majaji wa ICC wanasubiriwa watoe uamuzi - iwapo kuna ushahidi kuunga mkono kutolewa hati za kukamatwa watu hao.
Katika mahojiano na CNN alisema alipokuwa akifanya uchunguzi wa kuanzisha kesi dhidi ya Netanyahu, kuna kiongozi alimwendea na kumwambia waziwazi; "mahakama hii imeundwa kwa ajili ya Afrika na majambazi kama Putin," Khan alidai rais, ambaye hakufichua utambulisho wake, ndiye alisema hayo.
Kundi la maseneta wa chama cha Republican nchini Marekani walimtumia barua ya wazi - walimtishia yeye na familia yake kumuwekea vikwazo vya kuingia nchini humo iwapo ataendeelea na uchunguzi dhidi ya Israel. "Umeonywa," barua ilihitimisha.
Lakini hakurudi nyuma. Na siku ya Jumatatu alipokuwa akitangaza uamuzi wake, hakusita kujibu, akisema "jaribio la kuwazuia, kuwatisha au kuwashawishi maafisa wa mahakama, ofisi yake haitasita kuchukua hatua ikiwa tabia hiyo itaendelea.”
Kesi za kimataifa

Chanzo cha picha, REUTERS
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Karim Khan alizaliwa Machi 30, 1970 huko Edinburgh, Scotland. Alizaliwa na baba Mpakistani na mama Mwingereza. Ni Mwislamu wa madhehebu ya Ahmadiyya.
Alisomea Sheria katika Chuo cha King's College huko London na baadaye kufanya kazi katika ofisi ya mwanasheria mkuu na kutoka hapo akafanikiwa kufika majukwaa ya haki ya kimataifa.
Alihudumu kama wakili wa utetezi na mwendesha mashtaka katika mahakama mbalimbali za kimataifa, ikiwemo mahakama ya jinai kwa ajili ya Yugoslavia ya Zamani, Rwanda, Lebanon na Sierra Leone.
Amekuwa na wateja wengi wenye utata – akiwemo Seif al Islam, mtoto wa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar al Gaddafi, na Charles Taylor, rais wa zamani wa Liberia aliyetuhumiwa kwa uhalifu wa kivita.
Pia alimtetea aliyekuwa makamu wa rais wa wakati huo wa Kenya William Ruto, ambaye alishtakiwa kwa kuanzisha ghasia za baada ya uchaguzi na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200 mwaka 2007, na kuitaka mahakama kutupilia mbali kesi hiyo.
Khan aliteuliwa mwaka 2018 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kama mshauri maalumu na mkuu wa timu inayohusika na uchunguzi wa uhalifu uliofanywa na kundi la Islamic State nchini Iraq.
Mnamo Februari 12, 2021, Khan alichaguliwa kuwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC kwa muda wa miaka 9 na aliapishwa Juni 16, 2021.
Yeye ni mwendesha mashtaka wa tatu katika historia ya ICC, iliyoundwa Julai 2002.
Wakili huyo wa Uingereza alichukua nafasi ya jaji wa Gambia Fatou Bensouda, ambaye serikali ya Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump ilimwekea vikwazo kwa uamuzi wake wa kuchunguza uhalifu wa kivita wa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan.
Uchunguzi huo ulipaswa kuanza mwaka 2020 na alitaka kuchunguza sio tu uhalifu wa kivita wa wanajeshi wa Marekani katika nchi hiyo ya Asia ya Kati, lakini pia uhalifu wa Taliban na wanajeshi wa Afghanistan.
Jibu la aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wakati huo Mike Pompeo lilikuwa kwamba, “ICC taasisi imepoteza maana na fisadi."
Washington, hata hivyo, iliondoa vikwazo hivi Aprili 2021, wakati ikijuulikana kuwa Khan angechukua nafasi ya Bensouda, ingawa alikuwa bado hajachukua madaraka.
Miezi kadhaa baadaye, Karim Khan alitangaza kuindoa Marekani katika uchunguzi wa Afghanistan ili kuichunguza Taliban na Dola ya Kiislamu, uamuzi huo ulipata ukosoaji mkubwa kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu.
Kukwama kesi za Palestina

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Mtangulizi wa Khan aliamua 2019, kwamba kulikuwa na msingi wa kuanzisha uchunguzi juu ya uhalifu wa kivita katika ardhi za Palestina na wanajeshi wa Israel, Hamas na vikundi vingine vyenye silaha vya Palestina.
Mahakama ya ICC ilitoa ruhusa mwaka 2021, kwani mahakama hiyo inaweza kutumia mamlaka yake juu ya maeneo ya Palestina.
Miongoni mwa mambo mengine, mwendesha mashtaka alitaka kuchunguza juu ya makazi haramu katika Ukingo wa Magharibi na ukiukaji wa Mkataba wa Geneva wakati wa vita vya 2014 vya Gaza.
Israel ilishutumiwa kushambulia, vituo vya Msalaba Mwekundu huku Hamas na wanamgambo wengine walituhumiwa kutumia raia kama ngao.
Hata hivyo, mara Karim Khan alipoingia madarakani, uchunguzi huo ulionekana kukwama, na hivyo kuyakatisha tamaa makundi mengi ya haki za binadamu ambayo yamekuwa yakijaribu kwa miaka mingi kutaka kesi kufika katika mahakama hiyo.
Ziara yake nchini Israel baada ya mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba, ambayo yalizua vita vya sasa vya Gaza, ilimletea ukosoaji kutoka kwa wale walioona kuna upendeleo kwa upande wa Israel, huku uchunguzi wa matukio katika maeneo ya Palestina ukionekana kuachwa nyuma.
Muda mfupi baadaye, alitembelea kivuko cha mpakani cha Rafah kati ya Gaza na Misri, ambapo misaada ya kibinadamu ilikuwa imekwama kutokana na Israel kuizuia kwenda Ukanda huo.
Khan alionya kwamba kuzuia kupitishwa kwa msaada kwa watu wa Gaza kunaweza kuwa uhalifu.
Miezi saba baadaye, Khan anamtuhumu Netayahu na Waziri wake wa Ulinzi, Yoav Gallant - kutumia njaa kama silaha ya vita na kusababisha mateso makubwa kwa watu wa Gaza kwa makusudi.
Pia ameomba vibali vya kukamatwa viongozi watatu wa Hamas: Yahya Sinwar, ambaye ni mkuu wa kundi hilo huko Gaza, pamoja na viongozi Ismail Haniya na Mohammed al Masri.
Anawashutumu wote kwa kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, kwa vitendo vya Oktoba 7 na baada yake, kama vile mauaji, kuchukua mateka au ubakaji.
Putin na Netanyahu

Chanzo cha picha, EPA
Hati ya kutaka Netanyahu akamatwe ni hati ya pili dhidi ya kiongozi wa nchi kutolewa na mwendesha mashtaka mkuu wa ICC katika muda wa mwaka mmoja tu, ingawa ile ya waziri mkuu wa Israel bado haijathibitishwa na majaji wa Mahakama hiyo.
Machi 2023, mahakama ya jinai huko The Hague iliamuru kukamatwa Rais wa Urusi Vladimir Putin, akituhumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita kwa uhamishaji haramu wa watoto kutoka Ukraine hadi Urusi.
ICC pia ilitoa hati ya kukamatwa kwa kamishna wa Urusi wa haki za watoto, Maria Alekseevna Lvova-Belova.
Urusi, kama Marekani, Israel na China, sio watia saini wa Mkataba wa Roma, ambao ulianzisha rasmi Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, hivyo mahakama hiyo haiwezi kuwa na mamlaka katika eneo lake na inaweza tu kumkamata Putin au Netanyahu ikiwa watasafiri kwenda nchi iliyotia saini.
Hata hivyo, kesi ya Urusi, Israel na maeneo ya Palestina sio kesi pekee zinazochunguzwa hivi sasa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.
'Kazi yangu ni kutekeleza sheria'

Chanzo cha picha, EPA
Karim Khan alitangaza Novemba 2021 kufunguliwa kwa uchunguzi wa awali kuhusu uhalifu dhidi ya ubinadamu dhidi ya maafisa wa serikali ya Nicolas Maduro kwa ukandamizaji wa maandamano ya upinzani ya Venezuela 2017.
Venezuela ndio nchi pekee huko Amerika Kusini ambayo inachunguzwa na ICC. Kulingana na Khan, kuna sababu za kuamini maafisa wa serikali na jeshi waliwapoteza watu kwa nguvu, mauaji ya kiholela, kuwekwa kizuizini na kuteswa wapinzani wakati wa maandamano ya 2017, ambapo watu 125 walikufa.
Serikali ya Maduro iliwasilisha rufaa kwa ICC ikitaka uchunguzi usitishwe. Majaji wa rufaa hiyo kwa kauli moja walikataa madai yote ya rufaa hiyo Machi mwaka jana na kutoa ruhusa kwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa ICC kuanza tena uchunguzi.
Kwa vyovyote vile, maneno ya hivi karibuni ya Khan mbele ya bunge la Venezuela, alilolitembelea Aprili iliyopita, yanafupisha kazi yake, iwe kwa Urusi, Venezuela, Israel au maeneo ya Palestina; "kazi yangu si kuwa maarufu na nina hakika sitokuwa maarufu, bali kazi yangu ni kutekeleza sheria."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












