Kombora la masafa marefu linaloweza kurushwa kutoka bara moja hadi jingine ni la aina gani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Urusi inatumia ardhi ya Ukraine kama uwanja wa majaribio ya silaha zake.
"Maelezo yote, ikiwa ni pamoja na kasi na urefu, yanalingana na sifa za kombora la masafa marefu la ICBM," Zelenskiy alisema baada ya shambulio la Alhamisi asubuhi kwenye jiji la mashariki mwa Ukraine la Dnipro.
Maafisa kadhaa wa nchi za Magharibi wameelezea mashaka yao kuhusu matumizi ya kombora la masafa marefu .
Hii ni mara ya kwanza kwa kombora hilo kutumika katika vita vya kijeshi duniani baada ya Marekani kuthibitisha .
Sasa swali ni je, makombora ya masafa marefu yanayoweza kurushwa kutoka bara moja hadi jingine ni ya aina gani na kwa nini matumizi yake ni muhimu sana?
Kombora la masafa marefu linaloweza kurushwa kutoka bara moja hadi jingine ni la aina gani?
Kama jina la ICBM linavyopendekeza, silaha hizi zimeundwa kurusha makombora kwa umbali mrefu sana.
Kila kombora linaweza kubeba makombora kadhaa, ambayo yanaweza kujitegemea na kulenga shabaha tofauti.
Umoja wa Kisovyeti ilikuwa nchi ya kwanza kufanya majaribio ya ICBM mnamo Agosti 1957. Lakini leo, Urusi, Marekani na Uchina pia zina silaha kubwa za ardhini za makombora haya. Nchi kama vile Uingereza, Ufaransa, India, Israel na Korea Kaskazini pia zina idadi ndogo ya makombora haya yanayoweza kurushwa kupitia nyambizi.
Makombora ya masafa marefu yanaweza kusafiri masafa marefu na kuwa na kasi zaidi ikilinganishwa na makombora mengine yenye uwezo kama huo.
Je, makombora haya yanaweza kuruka kwa umbali gani?
Kulingana na ufafanuzi wa kawaida, kombora la masafa marefu lazima liwe na kiwango cha chini cha kilomita 5500. Bila shaka, baadhi ya makombora haya yanaweza kusafiri umbali mkubwa zaidi.
Inaaminika kuwa kombora lililorushwa na Urusi lilirushwa kutoka mkoa wa Astrakhan kusini mwa nhi hiyo.
Makombora ya balestiki ya Urusi yanaweza kusafiri zaidi ya kilomita 10,000. Hii ina maana kwamba makombora yanayorushwa kutoka eneo hili yanaweza kinadharia kufika Pwani ya Mashariki ya Marekani.
Je, makombora haya yana kasi ya kiwango gani?
Inaaminika kuwa Urusi ilitumia kombora la RS-26 Rubzh katika shambulio la Dnipro. Makombora haya yana kasi ya kilomita 24,500 kwa saa, ambayo ni takriban kilomita 7 kwa sekunde.
Yanaitwa makombora ya balestiki kwa sababu yanarushwa kwa nguvu ya roketi hadi kwenye njia ya juu ya angahewa na kisha kushuka kuelekea kwenye shabaha.
Ni kutokana na hatua hiyo inalolipa kombora hilo kasi ya juu sana. Teknolojia hiyo pia huyafanya kuwa vigumu kudunguliwa ikilinganishwa na makombora ya cruise, ambayo hayana kasi kubwa na husafiri kwa njia ya tambarare.
Je, makombora ya masafa marefu ni makombora ya nyuklia?
Mkombora ya ICBM yanaweza kubeba vichwa vya nyuklia au vichwa vya makombora ya kawaida.
Bila shaka, hakuna dalili kwamba kombora lililorushwa na Urusi lilikuwa limebeba kichwa cha nyuklia.
Jeshi la anga la Ukraine lilitangaza kuwa silaha hiyo ililenga shabaha "bila matokeo". lakini, hawakutoa habari yoyote juu ya kiwango cha uharibifu au uwezekano wa majeruhi
Je, unahitaji gharama ya pesa ngapi kumiliki kombora moja la masafa marefu?
Haijulikani ni kiasi gani Urusi inatumia katika mpango wake wa makombora ya balestiki , lakini habari kuhusu matumizi ya Marekani inapatikana.
Mwezi Julai, Pentagon iliidhinisha mpango mpya wa kuunda makombora ya balestiki kwa bajeti ya $140 bilioni.
Ripoti zinaonyesha kuwa gharama ya kuunda kombora moja la masafa marefu imefikia dola milioni 162.
Silaha hizi zinachukuliwa kuwa ghali sana kwa viwango vyovyote na katika nchi zote.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwanini Urusi ililitumia kombora hilo wakati huu?
Zaidi ya siku 1,000 zimepita tangu uvamizi mkubwa wa Urusi nchini Ukraine
Kutumwa kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini katika eneo la Kursk nchini Urusi, ambako Waukraine walikuwa wameteka zaidi ya kilomita za mraba 1,000 katika shambulio la mwaka 2024, kuliashiria ongezeko kubwa la vita.
Labda kwa sababu hii, kwa mara ya kwanza, Rais Biden aliidhinisha matumizi ya mfumo wa makombora wa Atcoms kushambulia shabaha ndani ya Urusi.
Makombora ya Scallop ya Uingereza na Ufaransa pia yamerushwa kwenye shabaha ndani ya Urusi.
Hapo awali Urusi ilionya kwamba ikiwa Ukraine itatumia makombora ya masafa marefu kushambulia eneo lake, itatoa jibu "linalofaa".
Jibu hilo linajiri huku rais mteule Donald Trump akijiandaa kurejea Ikulu ya White House.
Trump ameahidi kumaliza vita nchini Ukraine ndani ya saa 24, ingawa haijabainika wazi jinsi anavyopanga kufanya hivyo.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Yusuf Jumah












