Yafahamu makombora ya masafa marefu ambayo Marekani imeipa Ukraine

jm

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Makombora hayo mapya yana masafa marefu kuliko yale Ukraine ilikuwa nayo hapo awali.

Ukraine imeanza kutumia makombora ya masafa marefu dhidi ya Urusi ambayo yalitolewa kwa siri na Washington, kwa mujibu wa maafisa nchini Marekani.

Silaha hizo zilitumwa kama sehemu ya msaada wa awali wa Marekani na ziliwasili mwezi huu. Maafisa walibainisha kuwa makabidhiano hayo hayakutangazwa hadharani ili kuhifadhi "usalama wa oparesheni" wa Ukraine.

Makombora hayo tayari yametumika angalau mara moja dhidi ya malengo ya Urusi katika rasi ya Crimea inayokaliwa kwa mabavu.

Silaha zaidi za Marekani zinatarajiwa kuwasili hivi karibuni, baada ya Rais Joe Biden kutia saini kifurushi kipya cha msaada wa kiuchumi na kijeshi cha dola za Marekani bilioni 61 kwa Ukraine siku ya Jumatano.

Makombora hayo ambayo tayari yametolewa kwa siri ni toleo la Mfumo wa masafa marefu (ATACMS), kulingana na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje aliyethibitisha Jumatano.

MGM-140 ATACMS ni kombora la balestiki lililotengenezwa na kampuni ya ulinzi ya Kimarekani ya Lockheed Martin.

Linatumia kichocheo kigumu cha mafuta, likiwa na urefu wa takriban mita 4 na upana wa sentimita 60.96.

LIna kichwa cha WDU-18 kilichogawanyika cha kilo 226.

Toleo la hivi majuzi zaidi lililotumwa na Marekani ndilo linalofikia mbali zaidi ya kilimita 300 km , na mfumo wa uongozaji unaosaidiwa na GPS.

Linaweza kurushwa kutoka kwa mifumo aina nyingi ukiwemo M270 au Mfumo wa Kombora wa Artillery wa Juu wa M142, unaojulikana zaidi kwa kifupi kama HIMARS.

Ni mfumo wa kawaida wa mizinga ya ardhini hadi ardhini yenye uwezo wa kufikia shabaha mbali zaidi kuliko mizinga mingine ya kijeshi, roketi na makombora.

‘Makombora yataleta mabadiliko'

jm

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ukraine imekuwa ikishambulia maeneo ya Urusi kwa makombora hayo mapya.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hapo awali Marekani iliipatia Ukraine toleo la makombora ya masafa ya kati ya ATACMS, lakini ilikataa kutuma yale yenye nguvu zaidi, kwa sababu ilihisi inaweza kuhatarisha utayari wake wa kujilinda.

Mamlaka ya Marekani pia walikuwa na wasiwasi kwamba Ukraine ingeweza kutumia silaha hizi kushambulia ndani ya ardhi ya Urusi, na kusababisha kuongezeka kwa vita, kulingana na NBC.

Ukraine ilikuwa imeomba mfumo wa masafa marefu kwa muda, na Biden aliidhinisha kwa siri usafirishaji huo Februari mwaka jana. Ilikuwa "chini ya agizo la moja kwa moja la rais," msemaji wa Idara ya Jimbo alisema Jumatano.

Marekani "haikutangaza hili wakati amri ilipotolewa kudumisha usalama wa uendeshaji ulioombwa na Ukraine," alieleza msemaji Vedant Patel.

Sasa, kuongezeka kwa aina mbalimbali za ATACMS kumeipa Ukraine uwezo wa kugonga zaidi katika maeneo yaliyotekwa na Urusi, hasa vituo vyake, bohari na vituo vya vifaa.

Mara ya kwanza yalitumiwa dhidi ya uwanja wa ndege wa Urusi katika eneo linalokaliwa la Crimea, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Marekani, na kisha katika shambulio dhidi ya wanajeshi wa Urusi katika mji wa bandari unaokaliwa wa Berdyansk Jumanne usiku.

Haijulikani ni makombora mangapi yametumwa kufikia sasa, lakini Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Marekani Jake Sullivan alisema Washington inapanga kutuma zaidi.

"Yateleta mabadiliko," Sullivan alisema.

Kukabiliana na mashambulizi ya Urusi

jm

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baada ya kutoa kifurushi kipya cha msaada, Rais Biden alisema hii itaufanya ulimwengu kuwa salama zaidi.

Uwasilishaji wa silaha hizo mpya umekuwa jibu kwa maombi ya mara kwa mara ya usaidizi yaliyotolewa na Kyiv kwa nchi za Magharibi, kwani hifadhi yake ya risasi imepungua, wakati Urusi ikisonga mbele.

Baada ya miezi kadhaa ya mjadala na mkwamo katika Bunge la Marekani, kifurushi kipya cha msaada hatimaye kilipitishwa na kutiwa saini na Rais Biden siku ya Jumatano.

Msaada mpya wa dola bilioni 61 kwa kiasi kikubwa unajumuisha silaha zaidi. Idadi hii inazidi jumla ya dola bilioni 44 za usaidizi ambazo Marekani imetuma hadi sasa tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi.

"Itatoa usalama zaidi kwa Marekani, itatoa usalama zaidi kwa ulimwengu," rais alitangaza baada ya kuidhinisha msaada huo mpya.

Kwa upande wake, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema: "Sasa tutafanya kila kitu kurejesha nusu mwaka iliyotumika kwenye mijadala na mashaka."

"Kile ambacho Urusi iliyovamia iliweza kufanya wakati huu, kile ambacho Putin anapanga sasa, itabidi tumrudishie," alisema.

Zelensky hivi karibuni alionya kutarajia mashambulizi ya Urusi katika wiki zijazo baada ya Ukraine kupoteza mji wa Avdiivka wakati majira ya baridi.

Vikosi vya Ukraine vimekumbwa na uhaba wa silaha na mifumo ya ulinzi wa anga katika miezi ya hivi karibuni na maafisa wake wanahusisha upotezaji wa maisha na ucheleweshaji wa msaada wa kijeshi kutoka kwa Marekani na washirika wengine wa Magharibi.

Mshauri wa Usalama wa Kitaifa Jake Sullivan alisema Jumatano kwamba "hakika inawezekana kwamba Urusi inaweza kupata mafanikio zaidi katika wiki zijazo."

Tangu Urusi ilipovamia Ukraine mnamo Februari 24, 2022, makumi ya maelfu ya watu, wengi wao wakiwa wanajeshi, wameuawa au kujeruhiwa, na mamilioni ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao.