Hezbollah yathibitisha 'ushindi' dhidi ya Israel baada ya usitishwaji mapigano

Chanzo cha picha, Reuters
Hezbollah ilithibitisha "kupata ushindi" dhidi ya Israel, ambayo iliitaja kuwa "adui wa kufikirika", kwa zaidi ya miezi 13, baada ya usitishaji mapigano kuanza kutekelezwa na maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kurejea katika miji na vijiji vyao, hasa kusini mwa Lebanon.
Hayo yamejiri katika taarifa iliyotolewa na chama hicho Jumatano jioni, ambapo kilihutubia, kikijivunia kile kinachoita ni ushindi na kuwataka raia wake kurejea katika maeneo yao kwa fahari na ujasiri."
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mashambulizi ya kijeshi ya Hezbollah yalifikia 4,637, tangu kuanzishwa kwa kile kinachojulikana kama "Mafuriko ya Al-Aqsa" Oktoba 7, 2023, kwa kasi ya operesheni 11 kwa siku.
Hezbollah ilisema kuwa upande wa Israel ulipoteza wanajeshi 130 wakati wa uvamizi wa ardhini nchini Lebanon, pamoja na vifaru 59 vya Merkava na ndege nane zisizo na rubani, ikibainisha kuwa hasara hiyo haijajumuisha yale yaliyofanyika huko upande wa Israel katika ngome, kambi za kijeshi, makazi na miji iliyokaliwa kimabavu.”
Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa "ujumbe huo ni kwa ajili ya jeshi ambalo liliweza 'kuangusha' malengo ya Israel na 'kulishinda jeshi lake'," na kuongeza kuwa wapiganaji wake "watasalia tayari kikamilifu kukabiliana na nia ya mashambulizi ya adui, Israel, na kwamba macho yao yataendelea kufuatilia mienendo na uondoaji wa majeshi ya adui nje ya mipaka yake."
Kwa upande mwingine shirika la habari la Lebanon limeripoti kwamba waandishi wa habari wawili walijeruhiwa katika mashambulizi ya Israel siku ya ijumaa walipokuwa wakiripoti kuhusu kurejea kwa watu walioyahama makazi yao kutoka mji wa mpakani baada ya makubaliano ya usitishwaji wa mapigano kati ya Hezbollah na Israel kuanza kutekelezwa.
Shirika hilo lilisema: "Vikosi vya adui Israel katika mji wa Khiyam viliwafyatulia risasi kundi la waandishi wa habari walipokuwa wakiandika habari za kurejea kwa wakaazi na kujiondoa kwa Israel katika mji huo, jambo ambalo lilipelekea wawili kati yao kujeruhiwa."
Mpiga picha Abdelkader El-Bay alieleza kwamba alikuwa akiripoti matukio katika mji wa “Al-Khayam” na wanahabari wengine wakati milio ya risasi ilipofyatuliwa na yeye na mwenzake kujeruhiwa.
Tuliona watu wakikagua nyumba zao, na wakati huo huo tukasikia sauti ya vifaru vikiondoka,” Al-Bay alisema, akiongeza kuwa mwandishi mwingine aliyejeruhiwa alipelekwa hospitalini.
"Wakati tunapiga picha, tuligundua kuwa kulikuwa na wanajeshi wa Israeli kwenye jengo na ghafla walitufyatulia risasi. Ilionekana wazi kuwa sisi ni waandishi wa habari," aliongeza.
Mpiga picha wa Lebanon Ali Hashisho alikuwa na Al-Bay huko Khiam wakati tukio hilo lilipotokea, lakini hakujeruhiwa. Wote wawili walithibitisha kuwa waliona ndege isiyo na rubani kwenye mji huo kabla ya ufyatuaji risasi huo.
"Tuliona nguo za kijeshi chini," Hashisho aliambia AFP, kabla ya kuwaona wanajeshi wa Israel karibu.
Jeshi la Israel latoa taarifa ya onyo kwa wakazi wa kusini mwa Lebanon
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jeshi la Israel lilitoa taarifa ya onyo kwa wakaazi wa kusini mwa Lebanon, likisisitiza haja ya kutohama au kuvuka Mto Litani, na kuthibitisha kwamba harakati zozote kuelekea maeneo haya ni kujihatarsiha.
Kauli hii ilikuja katika taarifa ya video ya msemaji wa jeshi la Israeli, Avichay Adraee, ambapo alielezea umuhimu wa kutohama, kuanzia saa 17:00 kwa saa za huko (saa 3:00 GMT) hadi 7 asubuhi siku ya Alhamisi (5 pm GMT).
Adraee alionya dhidi ya kuelekea kusini vijiji ambavyo jeshi la Israeli lilidai hapo awali kuhamishwa, akisema kwamba wale wa kaskazini mwa Mto Litani walikatazwa kuhamia kusini, na wale wa kusini "lazima wabaki hapo walipo.
Jeshi la Israel lilitoa taarifa ya onyo kwa wakaazi wa kusini mwa Lebanon, likisisitiza haja ya kutohama au kuvuka Mto Litani, na kuthibitisha kwamba harakati zozote kuelekea maeneo haya ni kujihatarsiha.
Kauli hii ilikuja katika taarifa ya video ya msemaji wa jeshi la Israeli, Avichay Adraee, ambapo alielezea umuhimu wa kutohama, kuanzia saa 17:00 kwa saa za huko (saa 3:00 GMT) hadi 7 asubuhi siku ya Alhamisi (5 pm GMT).
Adraee alionya dhidi ya kuelekea kusini vijiji ambavyo jeshi la Israeli lilidai hapo awali kuhamishwa, akisema kwamba wale wa kaskazini mwa Mto Litani walikatazwa kuhamia kusini, na wale wa kusini "lazima wabaki hapo walipo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika taarifa iliyofuatia baadae, jeshi lilitoa wito kwa raia wanaorejea katika vijiji na miji ya mpakani kusini, "hasa katika wilaya za Tiro, Bint Jbeil na Marjeyoun," kutokaribia maeneo ambayo majeshi ya Israeli yapo, likionya kwamba wanaweza kushambuliwa kwa risasi kutoka kwa "majeshi ya uadui."
Jeshi la Lebanon limewaonya wakaazi wanaorejea katika maeneo yao kuripoti haraka mara wanapoona silaha za mlipuko na vitu vya kutiliwa shaka vilivyotokana na vita.
Jeshi la Lebanon na vikosi vya UNIFIL vinatazamiwa kuchukua nafasi ya Hezbollah katika eneo hilo.
UNIFIL ilipongeza tangazo la kusitisha mapigano na kuthibitisha kujitolea kwake kusimamia azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama "njia ya amani," ikieleza kuwa tayari imeanza kurekebisha shughuli zake "ili kukidhi hali mpya."
Amesisitiza katika taarifa yake kwamba wanajeshi wake "wako tayari kuunga mkono Lebanon na Israel katika awamu hii mpya na katika utekelezaji wao wa azimio hilo."
Usitishaji vita uliotangazwa na Marekani na Ufaransa ulianza kutekelezwa saa 04:00 a.m. saa za huko (02:00 GMT) siku ya Jumatano.
Iwapo mapatano hayo yatafanyika, majeshi ya Israel yataondoka Lebanon na Hezbollah itasonga kaskazini mwa Mto Litani, takriban kilomita 30 kaskazini mwa mpaka na Israel.
Rais wa Marekani Joe Biden amedokeza kuwa usitishaji mapigano unafaa kuwa wa kudumu, lakini Israel inasema ina haki ya kuishambulia Hezbollah iwapo itakiuka makubaliano hayo.
Iran ilikaribisha kile ilichokiita mwisho wa "uchokozi" wa Israel.
Juhudi za kidiplomasia kufikia makubaliano kuhusu Gaza
Rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kuzindua juhudi mpya siku ya Jumatano kufikia usitishaji vita huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka,kufuatia makubaliano kati ya Israel na Hezbollah, kwa mujibu wa mshauri wake wa masuala ya usalama, Jake Sullivan.
Makubaliano hayo yaliyoanza mapema Jumatano kusini mwa Lebanon yanamaanisha kuwa Hezbollah haipigani tena kuiunga mkono Hamas huko Gaza, jambo ambalo litaongeza shinikizo kwa vuguvugu la Palestina kukubali kusitishwa kwa mapigano na kuwaachilia mateka hao, Sullivan aliiambia MSNBC.
Vyanzo viwili vya habari vya Misri viliiambia BBC kwamba ujumbe wa usalama kutoka Misri unakaribia kuelekea Israel ili kufanya upya juhudi za kurejesha mazungumzo yaliyokwama kuhusu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza na kubadilishana mateka na wafungwa kati ya Hamas na Israel, hasa baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Lebanon kuanza kutekelezwa alfajiri siku ya Jumatano.
Vyanzo hivyo viwili vilithibitisha kuwa majadiliano ambayo wajumbe hao watafanya nchini Israel yatazingatia mapendekezo yanayohusiana na usitishaji mapigano kwa muda huko Gaza, na kufikia makubaliano ya kubadilishana huko, pamoja na mapendekezo yanayohusiana nah atua za baada" ya kusitishwa kwa vita.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo Uturuki inaweza kuwa na jukumu katika hatua inayofuata katika juhudi za upatanishi kati ya Israel na Hamas, pamoja na Misri, Qatar na Marekani.
Vyanzo hivyo viwili vilisema kuwa ujumbe wa Israel utaelekea Cairo katika siku zijazo ili kujadili maendeleo katika kufufua mazungumzo ya kusitisha vita ambavyo vimekuwa vikiendelea huko Gaza kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Pia walitarajia kwamba wajumbe wa Palestina wataelekea Cairo hivi karibuni kujadili maendeleo katika pendekezo la "Kamati ya Kusaidia Jamii", ambayo Misri ilitoa ili kuunda usimamizi wa sekta hiyo baada ya vita huko Gaza kusitishwa.
Changamoto ya hofu ya kusini na kaskazini

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kusini mwa Lebanon wamekaidi onyo kutoka kwa jeshi la Israel na mamlaka ya Lebanon kutorejea makwao bado magari yalionekana yakiwa yamejaa kwenye barabara kuu inayounganisha Beirut na kusini mwa Lebanon, yakiwa na watu waliofurushwa kutoka kusini mwa Lebanon kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel katika miezi ya hivi karibuni, wakielekea kusini baada ya utekelezwaji wa kusitisha kwa mapigano.
Baadhi ya madereva walipeperusha bendera na mabango ya Hezbollah yakionyesha kiongozi wa kundi hilo marehemu Hassan Nasrallah, ambaye aliuawa na Israel mwishoni mwa Septemba.
Maoni yalitofautiana miongoni mwa Walebanon kwa ujumla na wale wanaorejea kusini mwa Lebanon hasa, kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hezbollah na Israel.
Wengine wanatilia shaka ufanisi na uendelevu wa makubaliano hayo kwa sababu ya “kama wanavyoyaelezea” vifungu vya makubaliano, ambavyo vinatoa au kuruhusu pande zote mbili kujibu au kujitetea.
“Hatuwezi kuiamini Israeli kwa sababu tunaijua,” asema mwanamke mmoja Mlebanon, na kuongeza, “Hatuwezi kutumaini kwamba kutakuwa na usitishaji vita, kwa hiyo hatuwezi kurudi kwenye vijiji na vitongoji vyetu.”
Lakini kijana wa Lebanon alikataa, akisema kwamba alikuwa akiunga mkono kusitishwa kwa mapigano. Alisisitiza kuwa makubaliano hayo yatasonga mbele kwa sababu pande zote mbili zilikubaliana juu ya hatua zitakazofuatia usitishaji huo wa mapigano.
Mlebanon mwingine aliunga mkono, akisema kuwa watu wote walitaka usitishaji wa mapigano, ingawa alihofia kuwa baadhi ya masharti ya makubaliano hayo yalionekana kutoeleweka.
Kaskazini mwa Israel, kuna wasiwasi kuhusu usalama, kwani takriban Waisraeli 60,000 pia wanafikiria kurejea makwao karibu na mpaka.
Msemaji wa serikali ya Israel David Mancer alisema Israel itatii makubaliano hayo, huku ikiwa na "uhuru kamili wa kuchukua hatua za kijeshi" iwapo makubaliano hayo yatakiukwa.
Uri, mkazi wa Kibbutz Yiron karibu na mpaka wa Lebanon, alisema amefurahishwa na usitishwaji wa mapigano na uwezekano wa watoto kurejea shuleni.
Hata hivyo, Yuri, ambaye kwa sasa anaishi Haifa, alielezea hofu yake kuhusu uwepo wa Hezbollah nchini Lebanon.
Yaron, muuza duka huko Haifa, ambayo imekuwa shabaha ya roketi za Hezbollah, alishiriki wasiwasi wake, akisema usitishaji wa mapigano "unapaswa kuwa na maana halisi," sio kwamba kila mtu aende nyumbani kaskazini, "na siku mbili baadaye tunalengwa tena."
Mikati: Tunatumai usitishaji wa mapigano utakuwa "ukurasa mpya" kwa Lebanon

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati alithibitisha kuwa Lebanon leo inaanza ngwe ya kuimarisha uwepo wa jeshi kusini, na kwamba nchi yake itaanza mchakato huo upya.
Aliongeza kuwa serikali ya Lebanon imejitolea kufikia uthabiti kwenye kutekeleza Azimio nambari 1701, akisisitiza kuwa kila upande una jukumu kubwa.
Aliamini kuwa pande zote zinapaswa kuunganisha nguvu ili kuleta mageuzi, kuimarisha serikali, na kurejesha imani ya ulimwengu.
Mikati pia aliitaka Israel kujiondoa katika maeneo yote iliyoingia na kutii masharti yote ya usitishaji mapigano.
Mikati alisisitiza kwamba "matumaini yote yamewekwa kwa jeshi kuruhusu mamlaka ya serikali," akitumai "itafungua ukurasa mpya" na kumchagua rais wa jamhuri.
Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri alisema katika hotuba yake: "Tunafunga wakati wa kihistoria ambao ulikuwa hatari zaidi kwa Lebanon na kutishia watu na historia yao." Ameongeza kuwa, Lebanon na watu wake wanahitaji sana umoja wa kitaifa miongoni mwao.
Pia alitoa wito wa rais kuchaguliwa haraka.
Hamas: "Tunapongeza Hezbollah kwa kubeba jukumu muhimu la kusaidia Gaza
Hamas ilisifu "jukumu muhimu lililofanywa na vuguvugu la Kiislamu nchini Lebanon katika kuunga mkono Ukanda wa Gaza na la Palestina, na kujitolea kwa ajili ya Hezbollah na uongozi wake."
Kundi hilo lilisema katika taarifa yake kuhusu usitishaji vita kati ya Lebanon na Israel, "Makubaliano haya yasingewezekana bila ya kuwepo uthabiti wa upinzani na uungwaji mkono wa wananchi husika.
Tuna imani kwamba vuguvugu hili litaendelea kuwaunga mkono watu wetu na kukabiliana nao kwa namna zote zinazowezekana."
Hamas imeongeza kuwa,hatua ya Israel kufikia makubaliano hayo na Lebanon "bila kutimiza masharti iliyoweka" kunaashiria "hatua muhimu katika kusambaratisha dhana potofu za Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu za kubadilisha ramani ya Mashariki ya Kati kwa nguvu, na hadaa ya kuvishinda vikosi pinzani au kuwanyang'anya silaha."
Alionyesha dhamira yake ya kushirikiana na juhudi zozote za kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza, ambazo zitajumuisha uondoaji wa vikosi vya Israeli, kurejea kwa waliokimbia makazi yao, na kukamilika kwa makubaliano ya kweli na kamili ya kubadilishana mateka.
Katika taarifa yake, kundi hilo limezitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu na madola yenye nguvu duniani "kuchukua hatua kali na kuishinikiza Washington na utawala Israel kusimamisha hujuma yake ya kikatili dhidi ya watu wa Palestina na kukomesha vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza."
Kwa upande wa misimamo ya kimataifa, nchi nyingi zilipongeza makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hezbollah na Israel, zikiwemo Marekani, Ufaransa, Iran, Ujerumani, Uingereza, Umoja wa Ulaya, Uturuki, Iraq, Misri, Jordan, Qatar, na Mamlaka ya Palestina.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Seif Abdalla












