Kukamatwa, shutuma, madai dhidi ya familia ya Mugabe baada ya kupoteza madaraka

Bellarmine Mugabe, pamoja na mshtakiwa mwenzake Tobias Tamirepi Matonhodze, walifika mahakamani kwa mara ya kwanza mwezi uliopita.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Bellarmine Mugabe, pamoja na mshtakiwa mwenzake Tobias Tamirepi Matonhodze, walifika mahakamani kwa mara ya kwanza mwezi uliopita.
Muda wa kusoma: Dakika 8

Kukamatwa nchini Afrika Kusini kwa mtoto wa mwisho wa rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe, kumeleta tena mjadala kuhusu familia hiyo ya zamani ya rais na migogoro mbalimbali iliyowahi kuwazunguka kwa miaka mingi.

Bellarmine Mugabe, anashtakiwa kwa jaribio la mauaji, pamoja na makosa mengine, baada ya kijana wa miaka 23 kupigwa risasi na kujeruhiwa katika nyumba iliyoko katika kitongoji cha kifahari cha Johannesburg.

Bado hajasema chochote kuhusu tuhuma hizo.

Baba yake, Robert Mugabe, aliiongoza Zimbabwe kwa miaka 37 kabla ya kuondolewa madarakani mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 93. Alifariki miaka miwili baadaye.

Rais huyo wa muda mrefu pamoja na mke wake wa pili Grace Mugabe walipata watoto watatu pamoja:

Bona Mugabe – sasa ana miaka 37

Robert Mugabe Jr – sasa ana miaka 33

Bellarmine Mugabe – sasa ana miaka 28

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Grace pia alikuwa na mtoto mmoja kutoka ndoa yake ya awali:

Russell Goreraza – sasa ana zaidi ya miaka 40.

Mhariri mkuu wa tovuti binafsi ya habari ya Zimbabwe NewsHawks, Dumisani Muleya, aliiambia BBC kwamba familia ya Mugabe iliishi maisha ya kifahari, na kwamba watoto hao walikulia katika mazingira yaliyowalinda dhidi ya hali halisi ya kisiasa na kiuchumi ya Zimbabwe.

Familia hiyo pia ilikusanya utajiri mkubwa binafsi, ikiwemo:

dola milioni 10 taslimu, nyumba nne magari 10, shamba na bustani ya matunda, pamoja na mali nyingine.

Maelezo haya yalijitokeza miezi mitatu baada ya kifo cha Robert Mugabe, kupitia barua ya kisheria iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Zimbabwe na binti yake Bona Mugabe.

Wakati huo, wakili wa familia Terrence Hussein aliiambia BBC kwamba mali hizo hazikuwa zimesajiliwa kwa jina la kiongozi huyo wa zamani.

Mwaka 2013, Grace Mugabe alikanusha madai kwamba mume wake alikuwa akikusanya utajiri akiwa madarakani, akisema kuwa kama mtumishi wa umma hakupata mshahara mkubwa kama watu walivyodhani.

"Posho ninayopata ni ndogo sana. Mimi ni mtu wa biashara, na ninamsaidia mume wangu kwa kuendesha biashara zetu binafsi," alisema.

Hapa chini ni muhtasari wa kile kilichotokea kwa wanafamilia hiyo:

Bellarmine Mugabe

Kama ilivyo kwa ndugu zake, Bellarmine Mugabe alikulia mbele ya macho ya umma, na tangu akiwa mdogo alikuwa akifuatiliwa na kukosolewa na watu wengi.

Lakini alipokuwa kijana, mtazamo wake kuhusu masomo ulionekana kuwa jambo lililowatia wasiwasi wazazi wake.

Katika mahojiano marefu mwaka 2013 kwenye televisheni ya Afrika Kusini, wazazi wake walizungumzia tabia yake ya ucheshi na kutokuwa makini sana na masomo.

Mama yake, Grace Mugabe, alisema alitaka abadili tabia zake na azingatie zaidi masomo yake.

"Anapaswa kuwa makini zaidi kuliko alivyo sasa," baba yake, Robert Mugabe, aliongeza.

Kwa aibu kidogo, Bellarmine alikiri kwamba alitumia muda mwingi kucheza michezo ya video kuliko kufanya kazi zake za shule.

Robert, Grace na Bellarmine Mugabe

Chanzo cha picha, Gallo Images/Getty Images

Maelezo ya picha, Robert, Grace na Bellarmine Mugabe .

Bellarmine Mugabe na kaka yake mkubwa Robert Mugabe Jr wamekuwa wakitajwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari kwa maisha yao ya kifahari, wakati huo huo umaskini ukiendelea kuongezeka nchini Zimbabwe.

Mwaka 2017, wiki chache kabla ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa madarakani baba yao Robert Mugabe, Bellarmine alichapisha picha kwenye Instagram akionesha saa ya dola 60,000 aliyokuwa amevaa.

Miezi michache kabla ya hapo, yeye na kaka yake waliripotiwa kufukuzwa katika jengo la ghorofa la kifahari katika kitongoji tajiri cha Sandton baada ya majirani kulalamika kuhusu kelele walizokuwa wakifanya.

Katika miaka ya karibuni pia amekutana na matatizo kadhaa ya kisheria.

Mwaka 2024, alikamatwa kwa madai ya kumpiga afisa wa polisi katika mji wa mpakani wa Beitbridge. Aliachiliwa kwa dhamana, lakini baadaye hati ya kukamatwa kwake ilitolewa baada ya kushindwa kufika mahakamani, kulingana na gazeti la serikali la The Herald.

Mwaka uliofuata, mwezi Juni, alikamatwa tena kwa madai ya kumpiga mlinzi wa usalama katika eneo la mgodi huko Mazowe, takribani saa moja kwa mwendo wa gari kaskazini mwa mji mkuu Harare.

Aliachiwa tena kwa dhamana, na kesi hiyo bado haijamalizika.

Kesi ya sasa dhidi ya Bellarmine nchini Afrika Kusini imeahirishwa mara kadhaa tangu alipokamatwa katikati ya mwezi Februari, na kusikilizwa kwa ombi lake la dhamana kumeahirishwa tayari mara mbili.

Robert Mugabe Jr

Robert Mugabe Jr pia si mgeni katika kukutana na matatizo na polisi. Mwaka 2023 alikamatwa kutokana na madai kwamba alihusika kuharibu mali wakati wa sherehe iliyofanyika katika mji wa Harare.

Kwa mujibu wa wakili wake, alikabiliwa na:

mashtaka matatu ya kuharibu mali kwa makusudi,

na mashtaka mawili ya kumshambulia afisa wa polisi.

Alituhumiwa kuvunja vioo vya mbele vya magari na hata kumtemea mate askari wa polisi.

Hata hivyo, Robert Mugabe Jr alisisitiza kuwa hana hatia. Baadaye aliachiliwa huru baada ya kukubaliana kusuluhisha kesi nje ya mahakama na mlalamikaji, ambaye alikuwa rafiki yake.

Robert Jr (kushoto) na Bellarmine Mugabe wakimuomboleza baba yao.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Robert Jr (kushoto) na Bellarmine Mugabe wakimuomboleza baba yao.

Mwaka 2025, baada ya kukiri kosa, Robert Mugabe Jr alipatikana na hatia na kutozwa faini nchini Zimbabwe kwa kumiliki bangi.

Kulingana na nyaraka za mahakama, alikamatwa baada ya kuendesha gari kinyume cha mwelekeo katika barabara ya njia moja. Polisi walimpekua na kukagua mfuko mweusi aliokuwa amevaa begani, na kudai walipata vifuko viwili vidogo vya bangi.

Maafisa wa polisi walisema walipata gramu 2 za bangi, zenye thamani ya takribani dola 30 kwa bei ya mtaani. Hata hivyo, wakili wake alisema kuwa kiasi hicho kilikuwa gramu 0.02 tu.

Grace Mugabe

Grace Mugabe, aliyekuwa mke wa rais wa zamani na sasa ana umri wa miaka 60, alipata sifa pamoja na ukosoaji mkubwa kwa miaka mingi kutokana na madai ya kupenda sana ununuzi wa bidhaa za kifahari na maisha ya anasa. Hali hiyo ilimfanya apewe jina la utani "Gucci Grace."

Hata hivyo, alikanusha madai hayo ya kumdharau. Katika mahojiano ya mwaka 2013, alisema wakosoaji wake walimwona kama "mlengwa rahisi" wa lawama.

"Kwa kweli mimi si kama wanavyosema, na ninashangazwa na baadhi ya mambo wanayosema. Nafanya kazi kwa bidii sana na sina muda wa kujipamba au kujifurahisha. Ninashona nguo zangu mwenyewe na kufunga kitambaa changu mwenyewe kichwani," alisema.

Katika miaka ya mwisho ya utawala wa mume wake, Robert Mugabe, alianza kujiweka katika nafasi ya kuwa mrithi wake kisiasa.

Alikuwa kiongozi wa jumuiya ya wanawake ya chama tawala cha ZANU-PF nchini Zimbabwe, na alichangia kwa kiasi kikubwa kuwaondoa au kuwanyima nguvu baadhi ya wagombea waliokuwa wapinzani wake ndani ya chama.

 Grace alipigwa picha akimsaidia Robert Mugabe, mwenye umri wa miaka 93, siku chache kabla ya kuondolewa madarakani mwaka 2017.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Grace alipigwa picha akimsaidia Robert Mugabe, mwenye umri wa miaka 93, siku chache kabla ya kuondolewa madarakani mwaka 2017.

Mipango ya Grace Mugabe ya kurithi madaraka ilivunjika baada ya Robert Mugabe kuondolewa madarakani mwaka 2017, kufuatia hatua yake ya kumfukuza aliyekuwa makamu wa rais Emmerson Mnangagwa mwezi Novemba mwaka huo.

Baada ya kuondolewa kwa Mugabe madarakani, himaya ya biashara ya Grace Mugabe ilianza kudhoofika. Kampuni yake kubwa ya maziwa yenye thamani ya mamilioni ya dola, Gushungo Dairy Estates, ilifungwa mwaka 2022, ikiripotiwa kuwa na madeni makubwa.

Baadhi ya wachambuzi walisema kampuni hiyo iliendelea kufanya kazi kwa muda mrefu kwa sababu ya msaada na upendeleo wa serikali, ambao ulipotea baada ya Mugabe kuondolewa madarakani.

Hata hivyo, Grace Mugabe bado anaishi katika jumba kubwa la kifahari la Blue Roof mansion lililoko Harare. Nyumba hiyo ilinunuliwa na chama tawala cha ZANU-PF kwa ajili ya Robert Mugabe alipokuwa bado madarakani.

Baada ya kifo chake, chama hicho kilihamisha umiliki wa nyumba hiyo kwa familia ya Mugabe.

Grace Mugabe hawezi kusafiri kwenda Afrika Kusini kwa sababu anakabiliwa na hati ya kukamatwa inayohusiana na tukio lililotokea muda mfupi kabla ya familia ya Mugabe kuondolewa madarakani.

Mwaka 2017, alituhumiwa kumshambulia msichana aitwaye Gabriella Engels kwa kutumia waya wa umeme ndani ya chumba cha hoteli jijini Johannesburg.

Grace alisema wakati huo kwamba alijitetea baada ya kushambuliwa katika chumba ambacho wanawe Bellarmine Mugabe na Robert Mugabe Jr waliishi. Kwa upande wa Engels, alisema yeye na rafiki yake walikuwa wameenda kuwatembelea ndugu hao.

Uchunguzi ulianzishwa, lakini Grace alipewa kinga ya kidiplomasia iliyomruhusu kuondoka Afrika Kusini bila kuhojiwa. Kinga hiyo ilifutwa mwezi Julai 2018, miezi minane baada ya mapinduzi ya kijeshi, na ndipo hati ya kukamatwa ikatolewa.

Tukio hilo lilifanana na jingine lililotokea mwaka 2009, wakati aliyekuwa mke wa rais alituhumiwa kumshambulia mpiga picha wa gazeti la Uingereza aitwaye Richard Jones huko Hong Kong, ambako binti yake Bona Mugabe alikuwa akisoma.

Richard Jones alisema kuwa Grace alimpiga ngumi akiwa amevaa pete yenye almasi. Hata hivyo, hakushtakiwa kwa sababu alipewa kinga ya kidiplomasia na serikali ya China.

Baadaye Grace alisema alifikishwa mpaka mwisho wa uvumilivu wake, na kwamba alikuwa anamkinga binti yake.

"Nililazimika kumpiga, lakini kwa kweli sijui nini kilitokea, nilikuwa na nguvu nyingi sana," alisema katika mahojiano ya mwaka 2013.

Bona Mugabe

Wakati matukio na tabia za wanafamilia wengine zilikuwa zikivutia vichwa vya habari kwa miaka mingi, Bona Mugabe kwa kiasi kikubwa aliendelea kuwa mbali na vyombo vya habari, hadi pale talaka yenye mgogoro mkali ilipomrudisha kwenye macho ya umma.

Binti mkubwa na mtoto wa pekee wa kike wa Robert Mugabe aliwasilisha ombi la talaka mwaka 2023 dhidi ya aliyekuwa rubani Simbarashe Chikore, jambo lililosababisha mapambano makubwa ya kisheria yaliyotangazwa sana kwenye vyombo vya habari kati yao.

Chikore alitaka sehemu ya mali alizodai kuwa na thamani ya takribani dola milioni 80, ikiwemo:

jumba la kifahari huko Dubai na mashamba 21.

Madai hayo yalionekana kupingana na sera ya zamani ya baba yake, iliyojulikana kama "kaya moja, shamba moja", ambayo ilihusishwa na sera za ardhi wakati wa utawala wa Mugabe nchini Zimbabwe.

Maelezo ya utajiri wa familia yalijitokeza wakati wa kesi ya talaka ya Bona

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Maelezo ya utajiri wa familia yalijitokeza wakati wa kesi ya talaka ya Bona

Simbarashe Chikore pia alitoa orodha ya mali nyingine alizodai kuwa zinamilikiwa na Bona Mugabe, akisema kwamba mali alizotaja hapo awali zilikuwa tu "tone katika bahari", akimaanisha kwamba kulikuwa na mali nyingi zaidi.

Bona hakujibu hadharani madai ya mume wake aliyekuwa ametengana naye, lakini msemaji wa zamani wa baba yake Robert Mugabe alikanusha madai kwamba wanandoa hao walikuwa na mashamba 21.

Hatimaye, baada ya uchunguzi mkali wa umma na hasira ya watu kuhusu madai hayo, waliamua kumaliza talaka yao kwa makubaliano ya faragha.

Bona Mugabe na Simbarashe Chikore walifunga ndoa kwa harusi kubwa na ya kifahari mwaka 2014, iliyohudhuriwa na viongozi kadhaa wa nchi za Afrika na hata kurushwa moja kwa moja kwenye televisheni ya taifa. Wana watoto watatu pamoja.

Russell Goreraza

Mnamo mwaka wa 2015, mtoto wa kwanza wa Grace, Russell Goreraza, alihukumiwa kwa mauaji bila kukusudia na kutozwa faini ya dola 800.

Hii ilitokea baada ya kugonga na kumuua mtu asiyejulikana kwa gari lake jijini Harare mapema mwaka huo.

Goreraza alikuwa akiendesha gari kwa kasi wakati wa ajali hiyo. Hukumu ya mauaji yasiyotarajiwa inatofautiana kulingana na hakimu na tafsiri yao ya hali hiyo, lakini vifungo vya miaka miwili jela vimetolewa katika kesi kama hizo.

Hakimu aliyesimamia kesi hii alisema alikuwa ameamua kutofungwa jela kwa sababu ya majuto ya Goreraza na ukweli kwamba alikuwa mkosaji mara ya kwanza.

Familia ya Mugabe iko wapi sasa?

Familia hiyo kwa kiasi kikubwa imepunguza kuonekana hadharani tangu mwaka 2017.

Rais aliyefukuzwa madarakani alikuwa amechukizwa na jinsi alivyotendewa na chama chake cha ZANU-PF na aliendesha kampeni kwa ajili ya upinzani katika uchaguzi wa mwaka 2018.

Lakini tangu kifo chake, mke wake, binti yao Bona Mugabe na Robert Mugabe Jr wanaonekana kurekebisha uhusiano na chama, huku wakiwahi kuhudhuria uapisho a wa rais Emmerson Mnangagwa mwaka 2023.

Inaaminika kwamba wanakaa Zimbabwe, isipokuwa Bellarmine Mugabe.

BBC iliwasiliana na msemaji wa familia kwa maoni, lakini walikataa kuthibitisha mahali familia hiyo inapoishi.