'Ilibidi tukimbie': Hofu na taharuki nchini Lebanon wakati wa mashambulizi ya Israel

nm

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Raia wa Lebanon waliokimbia makazi yao huko Beirut baada ya kutoroka kusini
    • Author, Orla Guerin, Nafiseh Kohnavard and Carine Torbey
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kusini mwa Lebanon, familia zinapambana kukimbia kuelekea kaskazini kwa magari, malori na pikipiki, huku jeshi la Israel likishambulia maeneo ambayo inayahusisha na kundi la Lebanon la Hezbollah.

Baadhi ya wakazi waliripoti kupokea maonyo kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu na sauti zilizorekodiwa kutoka kwa wanajeshi wa Israel, kuondoka katika maeneo yaliyo karibu na kundi hilo linaloungwa mkono na Iran.

Zahra Sawli, mwanafunzi katika mji wa kusini wa Nabatieh aliiambia BBC, kwamba mashambulizi yalikuwa makali.

"Niliamka saa kumi na mbili asubuhi na kusikia milio ya mabomu. Kufikia saa sita mchana mashambulizi yalikuwa makali sana."

"Nilisikia vioo vingi vikivunjika."

Tofauti na wengi, yeye na wale aliokuwa nao hawakuondoka. "Tunapaswa kwenda wapi? Watu wengi bado wamekwama mitaani. Marafiki zangu wengi bado wamekwama kwenye msongamano wa magari kwa sababu watu wanajaribu kukimbia," alisema.

Kufikia katikati ya mchana barabara za kaskazini kuelekea Beirut zilikuwa zimejaa msongamano wa magari, magari yakielekea mji mkuu katika pande zote za barabara kuu ya pwani ya njia sita.

Picha nyingine zilionyesha watu wakitembea kando ya ufuo wa bahari katika mji wa kusini wa Tyre huku moshi ukiongezeka kutokana na mashambulizi ya anga katika maeneo ya mashambani.

BBC ilizungumza na familia moja ya watu watano waliokuwa wamefika Beirut kwa pikipiki moja, kutoka kijiji cha kusini, na walikuwa wakielekea katika mji wa kaskazini wa Tripoli.

“Ilibidi tukimbie,” anasema baba wa familia hiyo.

Pia unaweza kusoma

Vifo na Majeruhi

M

Chanzo cha picha, Hassan Harfoush

Maelezo ya picha, "Unataka tuseme nini? Ilibidi tukimbie," mtu huyu aliambia BBC
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kufikia Jumatatu jioni wizara ya afya ya Lebanon iliripoti watu 492 wameuawa na zaidi ya 1,600 wamejeruhiwa. Ilisema takribani watoto 35 ni miongoni mwa waliouawa. Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema limefanya mashambulizi 1,100 katika muda wa saa 24 zilizopita.

Huko Beirut pia kulikuwa na wasiwasi. Watu kutoka kusini walipofika katika mji mkuu wakiwa na magari na mizigo, baadhi ya wakazi wa jiji hilo walikuwa wakiondoka.

Israel imewaonya watu kuhama maeneo ambayo inasema Hezbollah inahifadhi silaha - lakini pia ilituma maonyo yaliyorekodiwa kwa watu katika wilaya za Beirut ambazo sio ngome za Hezbollah ikiwemo Hamra, eneo ambalo ni makazi ya wizara za serikali, benki na vyuo vikuu.

Wazazi walikwenda kuwachukua watoto wao shuleni baada ya kupokea maonyo ya kuondoka eneo hilo.

Baba mmoja, Issa, alimtoa mtoto wake shuleni, na akaliambia shirika la habari la Reuters: "Wanampiga simu kila mtu na kutoa vitisho kwa watu kwa njia ya simu. Kwa hivyo tuko hapa kumchukua kijana wangu kutoka shuleni. Hali halitabiriki," alisema.

Taharuki yatanda

M

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Watu wakibeba mali zao wakiondoka mji wa Tire ulio ufukweni mwa bahari - moja ya miji ya kusini mwa Lebanon iliyopigwa Jumatatu

Mohammed, mwanaume wa Kipalestina akiwa barabarani na mkewe, alizungumza na BBC wakiwa njiani kutoka Beirut.

Alipoulizwa kama angesalia katika mji mkuu alisema: "Nchini Lebanon hakuna mahali palipo salama, Israel inasema watapiga mabomu kila mahali. Sasa wanatishia kushambulia mji huu, basi twende wapi?"

"Inatisha, sijui la kufanya."

Shule zimegeuzwa kuwa makazi ya wahamiaji wanaokuja kutoka kusini. Kwa amri ya serikali, shule za Beirut na Tripoli pamoja na mashariki mwa Lebanon zimefanywa kuwa makazi.

Timu ya BBC ilikuwa katika darasa katika shule ya umma huko Bir Hasan, magharibi mwa Beirut siku ya Jumatatu ambayo ilikuwa ikitayarishwa kwa ajili ya watu wanaotoka Bonde la Bekaa - ngome ya Hezbollah kaskazini-mashariki mwa Lebanon ambapo Israel ilisema inalenga kuishambulia.

Madarasa yalikuwa yamejaa magodoro.

Wakati huo huo hospitali za Lebanon pia ziliamriwa kuahirisha upasuaji usio wa lazima siku ya Jumatatu, huku madaktari wakikabiliana na wimbi la maiti na majeruhi.

Kusimama imara

M

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Kumekuwa na misururu mirefu kwenye vituo vya mafuta mjini Beirut

Licha ya hali ya wasiwasi, baadhi ya watu walikuwa imara.

"Ikiwa vita kamili vitatokea, tunapaswa kusimama pamoja kama watu wa Lebanon bila kujali itikadi zetu za kisiasa kwa sababu mwisho wa siku, nchi yetu inashambuliwa kwa mabomu," mtu mmoja aliiambia BBC.

Mohammed, mwenye umri wa miaka 57 katika kitongoji cha Beirut kusini mwa Dahieyh – ngome kuu ya Hezbollah katika mji mkuu - aliiambia BBC amenusurika vita vyote tangu 1975 “kwa hivyo ni kawaida kwangu. Sitaondoka, nitakuwa nyumbani kwangu," alisema.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla