Tunachofahamu kuhusu kampuni inayodaiwa kutengeneza vifaa vya mawasiliano vilivyolipuka Lebanon

Gari la wagonjwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 3

Serikali ya Lebanon inasema watu 12, wakiwemo watoto wawili, waliuawa baada ya maelfu ya vifaa vya mawasiliano vinavyotumiwa na kundi lenye silaha la Hezbollah kulipuka.

BBC Verify imekuwa ikitafuta kampuni inayoitwa BAC Consulting, ambayo imehusishwa na utengenezaji wa vifaa hivyo, licha ya kuwa na jina tofauti la mtengenezaji.

Muda mfupi baada ya milipuko hiyo kutokea Jumanne, picha ambazo hazijathibitishwa za kurasa mbili zilizoharibika ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii.

Katika picha, neno "Gold" na nambari ya ufuatiliaji inayoanzia "AP" au "AR" ilionekana. Hii ilionesha kuwa kampuni ya Taiwan, Gold Apollo, ingeweza kuhusika katika utengenezaji wa vifaa hivyo.

Hata hivyo, kampuni hiyo ilitoa taarifa yenye maneno makali kukana kuhusika.

Picha za mitandao ya kijamii kifaa kilichoharibika zilipelekea Gold Apollo kutambuliwa. Kampuni inakanusha kuhusika

BAC Consulting ni kampuni yenye makao yake nchini Hungary ambayo Gold Apollo inasema ilikuwa na kibali cha kutumia chapa yake kupitia makubaliano ya leseni.

BBC Verify imefikia rekodi za kampuni za BAC, ambazo zinaonesha kuwa ilijumuishwa kwa mara ya kwanza mnamo 2022 na ina mbia mmoja. Imesajiliwa kwa jengo huko Budapest.

Pamoja na BAC, kampuni nyingine 13 na mtu mmoja wamesajiliwa katika jengo moja.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo, utafutaji wetu wa hifadhidata ya taarifa za fedha hauoneshi kuwa BAC ina muunganisho wowote kwa makampuni au watu wengine.

Hifadhidata hiyohiyo inaonesha hakuna maelezo ya biashara kuhusu BAC. Kwa mfano, hakuna rekodi za usafirishaji wowote kati yake na kampuni nyingine zozote.

Hata hivyo, tovuti ya BAC, ambayo sasa haipatikani, awali ilisema inaongeza biashara yake barani Asia, na ilikuwa na lengo la "kukuza ushirikiano wa teknolojia ya kimataifa kati ya nchi kwa uuzaji wa bidhaa za mawasiliano".

Kulingana na rekodi, BAC ilikuwa na mauzo ya jumla ya Forint ya Hungary 256,996,000 ($725,000; £549,000) mwaka wa 2022, na 210,307,000 Forint ya Hungary ($593,000; £449,000).

Kipeperushi cha kampuni, iliyochapishwa kwenye LinkedIn, inaorodhesha mashirika manane ambayo BAC inadai kufanya kazi nayo, ikiwa ni pamoja na Tume ya Ulaya na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DfID).

BBC Verify imeyafikia mashirika yote yaliyoorodheshwa ili kupata maoni. Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza, ambayo imechukua majukumu ya DfID, ilituambia ilikuwa katika mchakato wa uchunguzi. Lakini kulingana na mazungumzo ya awali, ilisema haikuwa na ushiriki wowote na BAC, licha ya madai ya kampuni hiyo.

Tovuti ya BAC ilimuorodhesha mtu mmoja kama mtendaji mkuu na mwanzilishi wake, Cristiana Bársony , Arcidiacono na haionekani kuwataja wafanyakazi wengine.

Mwanzilishi wa Gold Apollo, Hsu Ching-kuang

Chanzo cha picha, Getty Images

BBC Verify imefahamu kuwa alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Catania na shahada ya fizikia mwaka wa 2001. Kulingana na wasifu wake wa LinkedIn, pia ana Shahada ya Uzamivu kutoka vyuo vikuu viwili vya London.

Tumefanya majaribio kadhaa ya kuwasiliana naye, lakini hatukuweza kumpata.

NBC imeripoti kuwa ilizungumza na Bi Bársony-Arcidiacono, ambaye alithibitisha kuwa kampuni yake ilifanya kazi na Gold Apollo. Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu vifaa na milipuko hiyo, alisema: "Sitengenezi. Mimi ni mtu wa kati. Nadhani ulikosea."

BBC imewapigia simu BAC mara kadhaa, lakini hakuna jibu.

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orbán, amesema vifaa vya mawasiliano vinavyolipuka "havijawahi" kuwa nchini Hungary.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi