Elimu ya bure yaidhinishwa DRC kwa mara ya kwanza katika historia yake

Chanzo cha picha, TONY KARUMBA
Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo leo inaidhinisha elimu ya bure katika shule za msingi za umma kwa lego la kutekeleza yaliomo katika katiba ya mwaka 2005, ambao inasisitiza elimu ya bure kwa watoto wa shule za msingi.
Tangu mwaka 1993, wazazi wamekuwa wakilipa walimu ada ya mafunzo na hivi sasa serikali imeamua kuwalipa mishara.
Lakini baadhi ya walimu mpaka sasa wana shaka kuhusu utekelezaji wa hatua hiyo mpya ya serikali.
Ndani ya darasa moja katika shule ya msingi ya KILIMANI, iliopo mjini Kinshasa mwalimu anawafunza watoto vokali sita za alpabeti ya lugha ya kifarnsa.
Mijinga ni mzazi aliyefika katika shule hii kumuandkisha mtoto wake wa umri wa miaka sita, kama wazazi wengi.
'Nimekuja kumwandikisha mtoto wangu hapa, lakini alikuwa anasoma kwenye shule ya serikali. Kipya ni kwamba sitalipa tena pesa, kwa sababu watoto walikuwa hawasomi tena vizuri, walikuwa wakifukuzwa kila wakati ikiwa sijalipa.
'Nashukuru rais Felix Tshisekedi kwa kile anachotenda kwa sisi raia wa kongo' anasema mzazi huyo.

Mwalimu Nsumbu Coneil anafundisha katika shule ya msingi ya Kilimani kwa muda wa miaka kumi na mitano sasa lakini anapokea ada ya $60 kila mwezi kutoka kwa wazazi.
Lakini amejumuishwa katika orodha rasmi ya wanfanyakazi wa serkali, mpaka sasa anasema ana shaka na serikali kutekeleza hatua ya kuwalipa mishahara.
Kwa mujibu wa Godé Moju mkurugenzi wa shule ya Kilimani, Kwa sasa watoto wengi wameeanza kukaa sakafuni kutokama na ukosefu wa viti na madarasa yamekuwa madogo kuweza kupokea idadi inayoongezeka ya wanafunzi .
Hali ambayo anaeleza huenda ikachangia 'watoto kusoma katika mazingira mabovu'.
'Licha ya watoto sasa kuwa wengi, walisema tupokee watoto wote, hivi nimeweka kila darasa wawili wawili, watoto wengi sasa wameanza kukaa chini sababu tu wafundishwe'.
Walimu wanatishia kuanza mgomo ikifika tarehe ishinirini mwezi huu ikiwa serkali haitawalipa mshara wa kutosha.
'Amechukuwa (Felix Tshisekedi) hatua hio ya kusema wazazi wasilete tena pesa, sisi tumemunga mkono, hapa kwani nina walimu ambao hawajawahi kupokea pesa kutoka kwa serkali, nadhani ni muhimu kulipa walimu ,kama walimu hawatalipwa haraka, itakuwa athari sana' amesema Moju.
Gharama ya elimu ya bure kwa watoto wa shule ya msinigi ni kama 40% ya bajeti ya nchi ambayo ni ya dola za Marekani karibu bilioni sita.
Wachambuzi wa uchumi wana shaka iwapo hatua hio ya serikali itafanikiwa lakini rais Felix Tshisekedi ana matumaini mengi.
"Itakuwa hatua ambayo itakamilishwa katika miezi michache ijayo. "Mpango huu tumeukuta lakini hakukuwa na bajeti. Hili ndilo nitakalolipa kipaumbele. Congo ina uwezo wa kuongeza mshahara kugharamia elimu na tutalipa" amesema rais Felix tshisekedi.
Serikali mpya ilihiadi kufuatiliwa kwa karibu pia uamuzi huu wa rais wa kutoa elimu ya bure kwa watoto wa shule za msingi.

Chanzo cha picha, -
Funzo gani kutokana na mifano ya kieneo?
Congo inafuata mifano ya mataifa mengine katika eneo la Afrika mashariki kama Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi katika kutoa elimu ya bure katika shule za msingi.
Katika miongo kadhaa ya nyuma, elimu ya bure katika shule ya msingi iliidhinishwa katika baadhi ya mataifa kusini mwa jangwa la Sahara kama sehemu ya jitihada za kufufua mfumo wa elimu ambao umekuwa ukidorora, na kukabiliana na idadi ndogo ya wanafunzi wanaojiunga shuleni, linaripoti shirika la Umoja wa mataifa la elimu sayansi na utamaduni - UNESCO.
Hatua hiyo hatahivyo imekabiliwa na changamoto katika utekelezaji wake tangu kuanzishwa katika vipindi tofuati kwenye mataifa hayo, ikiwemo kucheleweshwa kutolewa kwa ufadhili kutoka kwa serikali, uhaba wa walimu wa kuwafunza idadi kubwa ya watoto, uhaba wa vifaa vya kufundisha pamoja na usimamizi mbaya wa miradi hiyo.
Katika taifa la Burundi kwa mfano, shule kadhaa zimejengwa chini ya utawala wa rais Nkuruzinzana alitangaza elimu ya bure punde tu alipoingia madarakani lakini viwango vya elimu bado havijaridhisha.
Swali kubwa sasa wakati mpango huu unaidhinishwa leo Congo, Je ni vipi hatua hii inaweza kuendelezwa ipasavyo nchini humo?














