Jinsi sera ya kigeni ya utawala wa Trump inavyoikanganya Ulaya

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atakuwa mwenyeji wa viongozi wa Ulaya mjini Paris kwa mazungumzo ya dharura kuhusu mustakabali wa Ukraine.
Muda wa kusoma: Dakika 6

Viongozi wa Ulaya wanataharuki. Mkutano wao wa usalama ulioitishwa ghafla huko Paris Jumatatu ni uthibitisho wa hilo.

Bado wanakutana kutokana na shinikizo linaloshuhudiwa baada ya mataifa hayo kutoalikwa na Marekani kwenye majadiliano na Urusi kuhusu mustakabali wa Ukraine.

Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema Jumapili kuwa anaweza kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, "hivi karibuni."

Je, Ulaya inaweza, ikikabiliwa na shinikizo, kuweka kando tofauti za kisiasa na masuala ya kiuchumi, na kuja na msimamo mmoja kuhusu matumizi ya fedha za usalama na mustakabali wa Ukraine, ikiwa ni pamoja na kutuma vikosi huko - ili kujipatia nafasi ya kujadili?

Watajaribu kufanya hivyo.

Jumatatu asubuhi, waziri mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer alisema Uingereza "iko tayari na ina shauku ya kutuma jeshi la ardhini." Hata Ujerumani, kabla ya uchaguzi wenye mivutano, msemaji wa sera za nje wa chama cha CDU, ambacho kinatarajiwa kushinda viti vingi, alisema nchi hiyo kubwa zaidi ya Ulaya pia itakuwa tayari kutuma vikosi ndani ya mfumo wa kimataifa.

Utawala wa Trump ni wazi hauko na uhakika 100% kuhusu kile kinachopaswa kufanywa kuhusu Ukraine. Kulikuwa na ujumbe mchanganyiko mwishoni mwa juma.

Hii inawaachia Ulaya dirisha dogo la fursa ya kujaribu kumshawishi rais wa Marekani kwamba ni mshirika muhimu. Inatarajiwa kufanya hivyo kupitia mkutano huu wa Paris, ikianza kujadili masuala mawili muhimu yanayotakiwa na Donald Trump: kwamba Ulaya itumie na kufanya zaidi kwa ajili ya ulinzi wake, na kwamba Ulaya itume vikosi Ukraine baada ya mapatano ya kusitisha vita.

Viongozi wa Ulaya wanasisitiza kwamba Kyiv iwe sehemu ya majadiliano ya kusitisha vita pia.

Wamekuwa wakishikilia msimamo kwamba "hakuna maamuzi kuhusu Ukraine, bila Ukraine."

Lakini ni zaidi ya hayo kwa Ulaya.

Ni hali ya kuwanyong'onyeza - iliyohofiwa, lakini haikutarajiwa - kwamba utawala wa Trump usingetoa kipaumbele kwa uhusiano na washirika wa Ulaya, wala usalama wao.

Ulaya imekuwa ikitegemea kivuli cha usalama kilichotolewa na Marekani tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Kulingana na vigezo vya majadiliano ya Urusi na Marekani kuhusu Ukraine, na jinsi Putin atajihisi kuwa na nguvu kutokana nayo, kuna hofu ya Ulaya kwamba hili linaweza kubadilisha ufanisi wa usalama wa bara lao.

Putin kihistoria anachukia upanuzi wa Nato kuelekea mashariki.

Nchi ndogo jirani na Urusi - za Baltiki, pamoja na Poland - sasa zinahisi hasa kuwa hatarini.

Unaweza pia kusoma
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Si nchi zote za Ulaya zitakuwepo katika mkutano wa Jumatatu. Ni zile zenye uwezo wa kijeshi: Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Uhispania na Denmark - ambayo inatarajiwa kuwakilisha nchi za Baltic na Nordic, pamoja na rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya na katibu mkuu wa muungano wa kijeshi, Nato.

Nchi nyingine zitakuwa na mikutano ya baadaye, kwa mujibu wa taarifa.

Hata katika mkutano mdogo wa Paris, itakuwa vigumu,kufikia makubaliano kuhusu nyongeza ya matumizi katika ulinzi.

Poland inapanga kutumia 4.47% ya Pato lake la Taifa kwa ajili ya ulinzi mwaka 2025. Uingereza inajitahidi kufikia, na bado haijafikia, 2.5% ya Pato la Taifa.

Lakini viongozi hao wanaweza kuahidiana ushirikiano bora, kuweka matumizi zaidi ndani ya Nato na kusaidia ujenzi wa Ukraine baada ya vita.

Umoja wa Ulaya pia unatarajiwa kuimarisha jitihada zake za ulinzi.

Sehemu kubwa ya mkutano wa Paris pia itajikita kwenye swala la kupelekwa vikosi Ukraine baada ya kusitisha vita.

Wazo linalojadiliwa si la vikosi vya kulinda amani bali "vikosi vya tahadhari'', kuhakikisha usitishwaji wa vita.

Lengo la uwepo wa vikosi vya Ulaya litakuwa tatu: Kutuma ujumbe kwa Waukraine: kwamba hawajawaacha peke yao. Ujumbe mwingine kwa Marekani, kuonyesha kwamba Ulaya "inajitahidi" kulinda bara lake, na ujumbe wa mwisho kwa Moscow, kuonya kwamba ikiwa itakiuka masharti ya mapatano ya kusitisha vita, haitakuwa ikipambana na Kyiv pekee.

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake kamili mnamo Februari 2022, miji na majiji ya Ukraine yamekumbwa na mashambulizi makubwa ya mabomu.

Lakini ni dhana inayozua mtafaruku na inaweza isiwe maarufu kwa wapiga kura. Kwa mfano, nchini Italia, asilimia 50 ya watu waliohojiwa hawataki kupelekwa silaha zaidi kwa Ukraine, achilia mbali kupeleka ndugu na jamaa zao.

Kuna maswali mengi ambayo bado hayajapata majibu:

Ni wanajeshi wangapi kila nchi ya Ulaya itahitaji kutuma, kwa muda gani, na chini ya amri ya nani?

Je, dhamira yao itakuwa nini - kwa mfano ikiwa Urusi itakiuka masharti ya kusitisha vita yaliyofikiwa, hiyo itamaanisha kwamba wanajeshi wa Ulaya watajiunga katika vita moja kwa moja na Urusi? Je, Marekani itawasaidia ikiwa itatokea?

Ulaya ingependa dhamana ya usalama kutoka kwa Marekani kabla ya kutuma wanajeshi Ukraine. Huenda haitapata.

Ni mengi sana yatakayoamuliwa Jumatatu hii.

Na viongozi, wakiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, wanakuja Paris wakiwa na masuala yao - je, wanaweza kumudu nyongeza ya matumizi ya kiulinzi, wana vikosi vya kutuma Ukraine?

Richard – sasa Lord – Dannatt aliwahi kuwa mkuu wa Jeshi la Uingereza.

Aliiambia BBC kuwa jeshi la Uingereza limepungukiwa sana kiasi kwamba haliwezi kutoa sehemu kubwa ya vikosi kwa ajili ya Ukraine.

Alisema kwamba takriban wanajeshi 100,000 watahitajika kwa jumla na Uingereza itatarajiwa kutoa idadi kubwa ya hao.

Jeshi la Uingereza linasisitiza kuwa limejijengea sifa ya ubora duniani.

Lakini mkutano huu ni maandalizi zaidi kuliko hatua za kina.

Mazungumzo yanaweza kuanza hadharani.

Je, Donald Trump atakuwa akifuatilia?

Ni vigumu kujua.

Kuna mazungumzo ya kutuma mjumbe kwenda Washington baada ya mkutano wa Paris ili kuwasilisha hoja za Ulaya.

Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, ana uhusiano wa karibu na utawala wa Trump.

Sir Keir Starmer ana mipango ya kwenda Washington katika siku chache zijazo. Hii inaweza kuwa nafasi yake ya kuwa daraja kati ya Ulaya na Marekani.

Mkutano wa Paris pia unatoa fursa kwa Uingereza na viongozi wengine wa Ulaya kutengeneza tena uhusiano baada ya maumivu ya kujitoa kwake katika Umoja wa Ulaya.

Mark Leonard, mkuu wa Baraza la Ulaya la Mambo ya kigeni, anasema kwamba Starmer anaweza "kuonyesha kwamba Uingereza ni mshirika mwenye kuwajibika kwa usalama wa Ulaya ... Kitu kitakachozingatiwa na kuleta hisia nzuri wakati wa majadiliano kuhusu masuala mengine."

Masuala kama vile uhusiano wa kibiashara na ushirikiano wa utekelezaji wa sheria ambao Uingereza inatumai kuboresha na Umoja wa Ulaya kwa siku zijazo.

Nchi mwenyeji Ufaransa inajivunia. Rais Macron amekuwa akitetea kwa muda mrefu kwamba Ulaya isiwe tegemezi kwa nchi za nje kwa minyororo ya usambazaji, uwezo wa kiteknolojia na zaidi linapokuja kwa suala la ulinzi. Aligonga vichwa vya habari mwaka jana kutangaza wazo la kutuma vikosi vya ardhini.

Ufaransa ni "inajivuna sana" kwamba huduma zake za upelelezi na usalama hazijaunganishwa na Marekani, tofauti na Uingereza, anasema Georgina Wright, naibu mkurugenzi wa chuo cha kimataifa cha Montaigne. Hii inafanya kuwa rahisi kujiondoa, sasa kwamba Trump yupo Ikulu ya White House, akitaka Ulaya ijifadhili yenyewe.

...

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mkutano huo wa kilele mjini Paris unafuatia Mkutano wa Usalama wa Munich, ambapo maazimio ya Marekani yalisababisha taharuki kati ya viongozi wa Ulaya

Marekani imetuma nyaraka kwa washirika wa Ulaya ikijumuisha hoja sita na maswali, kama vile ni nchi gani zitakuwa tayari kutuma vikosi Ukraine kama sehemu ya makubaliano ya amani, na ni serikali zipi zitakuwa tayari kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi, ikiwa ni pamoja na kutekeleza vikwazo vilivyopo kwa umakini.

Lakini Julianne Smith, ambaye alikuwa balozi wa Marekani katika muungano wa Nato, anasema kazi hii tata ya kidiplomasia kawaida huchukua wiki kadhaa za mikutano na haiwezi kuandaliwa kwa nyaraka zilizojazwa.

Anaongeza kwamba chochote ambacho viongozi wa Ulaya watafanikiwa kufikia huko Paris, ikiwa watajipatia nafasi ya kukaa katika meza ya majadiliano kuhusu Ukraine, mkono wao ni dhaifu.

" Ikiwa Trump atainama na kusema hapana, je, Ulaya itakataa kusaidia kabisa? Hawawezi kujikata tumbo kwa ajili ya uso wao."

Kwa kifupi, ikiwa Marekani ina mpango wa kujiepusha na Ukraine na kujiondoa Ulaya kwa jumla linapokuja suala la usalama, lazima wajitahidi kuimarisha ulinzi wao hata hivyo.

Ikiwa Donald Trump hatazingatia, Vladimir Putin hakika atafanya hivyo.