Walioangamia katika ajali ya ndege Marekani ni akina nani?

Chanzo cha picha, Howard University
Juhudi za uopoaji zinaendelea katika eneo la Washington DC, kufuatia ajali ya ndege aina ya American Airlines iliyokuwa ikitoka Kansas ikiwa na abiria 64 kugongana na helikopta ya kijeshi, iliyokuwa ikiendeshwa na marubani watatu usiku wa Jumatano.
Waathiriwa wa ajali hiyo ni kama vile wachezaji mashuhuri wa mchezo wa kuteleza kutoka Marekani na Urusi, rubani, wahudumu wa ndege na wakili aliyekuwa akielekea nyumbani kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Hawa ndio baadhi ya watu wanaoaminika walikuwa wameabiri ndege hiyo iliyopata ajali baada ya kugongana na helikopta.
Abiria wa ndege ya American Airlines
Asra Hussain Raza
Ni mwanamke wa kihindi anayefahamika kama Asra Hussain Raza, mwenye umri wa miaka 26, alikuwa amehamia Washington DC baada ya kuhitimu shahada yake ya uzamili katika kozi ya usimamizi wa hospitali.
"Alikuwa akirejea nyumbani baada ya kusaidia kuinua hadhi hospitali iliyokuwa inahitaji msaada,'' anasema mumewe kwa jina Hamaad Raza, ambaye aliwaonyesha arafa ya mwisho na mkewe kwa simu wafanyikazi wa ndege nje ya uwanja wa ndege.
Akaongezea kuwa: ''alijitolea sana na alisaidia sana, na iwapo kuna mtu aliotumia umri wake vizuri nitasema ni yeye alifanya alichokipenda akiwa na umri wa miaka 26.''
Profesa Kiah Duggins
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Rais wa chuo kikuu cha Howard amethibitisha kuwa Profesa KiahDuggins alifariki katika ajali hiyo ya ndege.
Wakili huyo wa masuala ya umma alikuwa anatarajiwa kuanza kufunza katika chuo hicho kama mhadhiri wa idara ya sheria katika msimu wa baridi.
''Alikuwa amejitosa kupigania sheria za kikatiba kuhusu sera na kupigana vita dhidi ya dhamana za pesa katika eneo la Tennessee, Texas na Washington DC,'' chuo hicho kikuu kilitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari vya Marekani.
Sarah Lee Best
Mawakili wawili wa DC walikuwa wameabiri ndege hiyo, familia zao zimethibitisha.
Sarah Lee Best, mwenye umri wa miaka 33, anatajwa kama mchapakazi na mpole, mumewe Daniel Solomon aliiambia kituo cha Washington.
Bi Best na Bwana Solomon walikuwa na mipango ya kusafiri Hawaii, alikozaliwa Best, katika sherehe za kuadhimisha miaka 10 ya ndoa yao mwezi Mei.
Elizabeth Keys
Wakili Elizabeth Keys, mwenye umri wa miaka 33, alipata kila sababu ya kuburudika...haikujalisha alichokuwa akifanya,'' mpenziwe David Seidman ameiambia gazeti moja huko Marekani.
Amefariki siku aliyokuwa akisherehekea kuzaliwa kwake, Bwana Seidman amesema.
Katika shirika ambalo wote wawili walikuwa wakifanya kazi, Wilkinson Stekloff, ilituma risala za rambirambi kwa kupoteza mmoja wao.
Walikuwa wanasheria wazuri, wafanyikazi wenza na pia marafiki,'' mwanzilishi wa shirika hilo Beth Wilkinson alieleza hayo katika taarifa yake.
Casey Crafton
Risala za rambirambi zilimiminiwa babake mzazi wa CaseyCrafton wa shirika la Salem, Connecticut.
"Salem amepoteza baba wa watoto wake, mume na mwanachama wa jamii,'' Gavana Ned Lamont aliandika kwa mtandao wa kijamii.
Ligi ya Salem Little, ambapo bwana Crafton alikuwa mkufunzi, alisema mji ulikuwa umevunjika moyo kwa kupoteza mwanachama mwenzao.
''Familia ya Crafton, imepoteza mwanafamilia aliyekuwa anapenda familia yake,'' taarifa yasema.
Michael Stovall
Mama ya Michael Stovall alisema mwanawe alikuwa "mtu mwenye furaha" ambaye aliona mema kwa kila mtu.
Michael, aliyetambulika kama Mikey, alikuwa akirejea nyumbani kutoka ziara ya uwindaji na marafiki, alieleza Christina Stovall kwa chombo cha habari cha Wink.
"Mikey hakuwa na adui yoyote. Ikiwa utaona picha zake, alikuwa roho ya sherehe. Aliwapenda wote."
Jesse Pitcher
Jesse Pitcher, ambaye ni rafiki ya Mr. Stovall, pia alikuwa kwenye ndege hiyo, alithibitisha baba yake.
Jesse, mwenye umri wa miaka 30 kutoka Maryland, alifunga ndoa mwaka jana na hivi karibuni alianza biashara yake mwenyewe, alieleza Jameson Pitcher kwa New York Times.
"Alikuwa anaanza maisha yake," alisema. "Aliniambia atanitembelea akirudi."
Pergentino N. Malabed
Kanali Pergentino N. Malabed, mkurugenzi wa Kitengo cha Usimamizi wa Ugavi wa Polisi wa Kitaifa wa Ufilipino, alikuwa pia kwenye ndege hiyo.
Taarifa za polisi zilisema mwili ulio na pasipoti ya Kanali Malabed ulipatikana kutoka kwenye mto Potomac.
Alikuwa safarini na maafisa wawili wa polisi kwenda Marekani kupima vesti za walinda usalama ambazo walikuwa wanakusudia kununua, na alikuwa akielekea ubalozi wa Ufilipino huko Washington.
Wafanyakazi katika ndege
Jonathan J. Campos
Kapteni wa ndege hiyo, Jonathan J. Campos, alikuwa na ndoto ya kuwa rubani tangu akiwa na umri wa miaka mitatu, alieleza shangazi yake kwa idhaa ya New York Times.
"Alitaka kuwa huru, kuruka na kupaa kama ndege," alisema Beverly Lane. Campos, mwenye umri wa miaka 34, alikulia Brooklyn, New York, na alikuwa akifanya kazi kwa PSA Airlines (sehemu ya kikundi cha American Airlines) kwa miaka nane.
Sam Lilley
Baba wa Sam Lilley, rubani mwenye umri wa miaka 28, alisema mwanawe alikuwa amechumbiana akitarajiwa kuoa na alikuwa "katika kilele cha maisha yake."
Tim Lilley aliiambia NewsNation kuwa mwanawe alijipatia leseni ya urubani kwa miaka michache tu kwa sababu alijitolea kwa bidii.
"Sam yuko na Yesu, na najua anakoenda," alisema. Dada yake Tiffany Gibson alimtaja Sam kama "mtu mpenda watu." "Alikuwa na ndoto kubwa za maisha," alisema.

Chanzo cha picha, Facebook/Debi Epstein
Ian Epstein
Ian Epstein, mzaliwa wa Virginia, alikuwa mfanyikazi katika ndege hiyo, ilieleza familia yake.
Alijulikana kwa uwezo wake wa kuwafanya watu kucheka na alikuwa "amejaa furaha." "Alipenda kufanya kazi kwa ndege kwasababu alifurahi sana kusafiri na kukutana na watu wapya.
Lakini upendo wake wa kweli ulikuwa kwa familia yake," ilisema familia yake.
Danasia Elder
Danasia Elder pia alikuwa mfanyikazi wa ndege, ilieleza familia yake kwa vyombo vya habari nchini Marekani.
Ndugu yake Brandon Payne alimkumbuka kwa kusema alikuwa "amejaa furaha." "Alikuwa mke mzuri, mzazi mzuri, rafiki mzuri," alisema. "Alikuwa na maarifa na ndoto kubwa maishani."
Wafanyakazi wa Helikopta
Ryan O'Hara
Ryan O'Hara, mwenye umri wa miaka 29, alikuwa mkuu wa wafanyakazi wa helikopta ya Black Hawk iliyogongana na ndege ya abiria, ilisema CBS News.
Aliacha mkewe na mtoto wa mwaka mmoja, ilithibitisha programu ya Reserve Officers' Training Corps (ROTC) kwenye chapisho la mitandao ya kijamii.
Atakumbukwa kwa kusuluhisha changamoto zilizojitokeza katika ukumbi wa michezo ya mazoezi na alikuwa mwanachama katika kikosi cha rifle,'' chapisho hilo lasema.

Chanzo cha picha, Facebook/Carrie Eaves
Andrew Eaves
Gavana wa Mississippi, Tate Reeves, alithibitisha kuwa Andrew Eaves, Afisa Mkuu wa kitengo ha kutoa hati, alikufa kwenye ajali hiyo.
Mkewe, Carrie Eaves, alieleza kwenye mitandao ya kijamii kuwa Andrew alikuwa rubani wa helikopta ya Blackhawk.
"Tunaomba muelekeze maombi kwa familia yetu na marafiki na kwa familia nyingine zote zinazohuzunika leo. Tunaomba amani wakati tunapoomboleza na majonzi," alisema.
Wachezaji wa mchezo wa kuteleza kwenye barafu waliokuwa kwa ndege
Spencer Lane na Christine Lane
Mchezaji wa kuteleza kwenye barafu Spencer Lane, mwenye umri wa miaka 16, amefariki akiwa na mamake mzazi Christine Lane, mwenye umri wa miaka 49, na walikuwa miongoni mwa wachezaji 14 na wakufunzi waliofariki walipokuwa wakirejea kutoka kambi ya Wichita.
Baba yake Spencer aliambia vyombo vya habari kuwa mwanawe alikuwa akipenda sana michezo na alikuwa na ari katika tasnia aliyokuwa akifanya.
''Alikuwa akifanya mazoezi katika klabu ya Boston mara tano kwa wiki na alikuwa akisoma sekondari kwa njia ya mtandao'' alisema.
Pia aliongezea kuwa mkewe alijihusisha sana na kile watoto wao walikuwa wakifanya.
Jinna Han na Jin Han
Jinna Han, mwenye umri wa miaka 13,alikuwa ameenda kwa kambi ya mazoezi ya mchezo wa kuteleza kwenye barafu akiwa na mama yake, Jin.
Mahojiano ya 2022, jinna aliiambia vyombo vya habari alipendelea kutazama michezo ya Olimpiki."
Doug Zeghibe mkufunzi wa klabu ya Boston alimtaja Jin kama mtu mpole na mzuri.
''Alikuwa akiwapa motisha watoto wote katika mchezo huo bila ubaguzi na sio rahisi kupata mzazi kama huyo'' anasema Doug.
Evgenia Shishkova na Vadim Naumov
Vifo vya makocha maarufu wa mchezo wa kuteleza kwenye barafu Evgenia Shishkova na Vadim Naumov kutoka Urusi vilithibitishwa na Kremlin.
Kocha maarufu Rafael Arutyunyan alisema aliwaambia wanariadha wake wajiandae kwa mazoezi kwa kimya kama ishara ya heshima kwa makocha hao. "Wote walikuwa wanaheshimika," alisema.
Olivia Ter
Olivia Ter, mwenye umri wa miaka 12 kutoka Maryland, alikuwa miongoni mwa wanariadha wa Marekani waliokuwa kwenye ndege hiyo.
Afisa wa eneo hilo alithibitisha kifo chake, akisema Olivia alionyesha kipaji na moyo wa kujitolea katika mchezo wa kuteleza kwenye barafu na alikuwa mfano mzuri kwa vijana.
Brielle na Justyna Magdalena Beyer
Baba wa Brielle, Andy Beyer, alisema binti yake mwenye umri wa miaka 12 na mkewe Justyna, mwenye umri wa miaka 42, walikuwa wakirudi kutoka kambi ya kufaya mazoezi ya mchezo wa kuteleza kwenye barafu.
Brielle alikuwa "mshindani katika kila kitu alichofanya" na alifurahi sana alipopiga wimbo mzuri.
Andy alieleza jinsi alivyogundua ajali ilipotokea, akiwa njiani kwenda kuchukua familia kutoka uwanja wa ndege.
Mkewe alisema familia ilikuwa na huzuni kubwa.

Chanzo cha picha, Facebook/Matthew Alan LaRaviere
Cory Haynos, Roger Haynos na Stephanie Branton Haynos
Cory Haynos alikuwa akirejea nyumbani kutoka kwa kambi ya kuteleza kwenye barafu ya Marekani akiwa na wazazi wake, Roger Haynos na Stephanie Branton Haynos, mwanafamilia aliandika katika mtandao wa kijamii.
"Roger alikuwa akinipa moyo kwa mapenzi yake kwa familia na kujitolea kwake mkewe na watoto,''Matthew Alan LaRavier, binamu wa Roger aliandika.
"Tulikuwa tunatarajia CORY atuwakilishe kama taifa katika mashindano ya Olimpiki''.
Alexandr Sasha Kirsanov
Aliyekuwa mkufunzi Sasha Kirsanov pia alikuwa ameabiri ndege hiyo, Chuo kikuu cha Delaware kilisema.
Mkewe anasema amepoteza kila kitu katika ajali hiyo iliyomuua mumewe.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid














