Maandamano Kenya: Afisa wa polisi ashtakiwa kwa mauaji ya mchuuzi
Mshukiwa, Klinzy Barasa Masinde mwenye umri wa miaka 32, anadaiwa kumpiga risasi Boniface Kariuki katika maandamano ya Juni 17, 2025.
Muhtasari
- Brazil yaapa kuilipiza Marekani baada ya Trump kutishia kutoza ushuru wa 50%
- Maandamano Kenya: Afisa wa polisi ashtakiwa kwa mauaji ya mchuuzi
- Tamasha la muziki lililomshirikisha Kanye West lasitishwa Slovakia
- Uingereza yakabiliwa na tishio kutoka Iran, ripoti yaonya
- Muasi wa Korea Kaskazini kumshtaki Kim Jong Un kwa unyanyasaji
- Watoto wauawa Gaza kwa shambulizi la Israel
- China yakanusha madai ya Ujerumani kuwa ililenga ndege ya kijeshi ya leza
- DCI yathibitisha kukamatwa kwa mshawishi wa TikTok Kenya
- Kadhi Mkuu Kenya Abdulhalim Hussein afariki dunia
- Shambulio jipya la ndege zisizo na rubani la Urusi laripotiwa Kyiv
- UNAIDS kutoa ripoti ya kwanza ya VVU duniani tangu Marekani kusitisha ufadhili wa USAID
- Ugiriki yasitisha maombi ya kufatufa hifadhi kwa wahamiaji kutoka Afrika Kaskazini
- Marekani yamuwekea vikwazo Albanese, mjumbe maalum wa UN na mkosoaji wa mashambulizi ya Israel Gaza
- Trump atishia Brazil kwa ushuru wa 50% na kutaka kesi ya Bolsonaro itupiliwe mbali
- Wahouthi wazamisha meli ya pili ya mizigo Bahari ya Shamu ndani ya wiki moja
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Brazil yaapa kuilipiza Marekani baada ya Trump kutishia kutoza ushuru wa 50%

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amesema yuko tayari kulipiza ushuru wowote utakaotozwa Brazil na Marekani.
Lula alikuwa akijibu tishio la Jumatano la mwenzake wa Marekani, Donald Trump, la kutoza ushuru wa 50% kwa bidhaa za Brazil kuanzia tarehe 1 Agosti.
Katika barua, Trump alitaja jinsi Brazili inavyomtendea Rais wa zamani Jair Bolsonaro kama kichocheo cha kupandisha ushuru.
Bolsonaro kwa sasa anashtakiwa kwa madai ya kujaribu kufanya mapinduzi dhidi ya Lula baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 2022.
Trump alimtaja Bolsonaro kama "kiongozi anayeheshimika sana duniani kote". "Kesi hii haipaswi kufanyika," aliandika.
Uungwaji mkono wa Trump kwa Bolsonaro haushangazi kwani watu hao wawili wamefahamika kuwa washirika kwa muda mrefu.
Soma zaidi:
Maandamano Kenya: Afisa wa polisi ashtakiwa kwa mauaji ya mchuuzi

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Kenya (DPP) ameidhinisha shtaka la mauaji dhidi ya afisa wa polisi anayedaiwa kumpiga risasi mchuuzi wa barabarani Boniface Kariuki wakati wa maandamano ya hivi karibuni dhidi ya serikali jijini Nairobi.
Mshukiwa, Konstebo Klinzy Barasa Masinde mwenye umri wa miaka 32, anadaiwa kumpiga risasi Kariuki tarehe 17 Juni 2025 wakati wa maandamano yaliyochochewa na ghadhabu ya umma kuhusu kifo cha mwalimu na mwanablogu akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Boniface Kariuki, mchuuzi wa barakoa mwenye umri wa miaka 22, alipata majeraha mabaya kichwani na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa wiki mbili kabla ya madaktari kuwafahamisha jamaa zake kwamba ubongo wake umekufa.
Baadaye alithibitishwa kuwa amefariki dunia. Madaktari wa upasuaji walikuwa wamefanya upasuaji kadhaa, lakini vipande vingine vya risasi vilibakia kwenye ubongo wake.
Konstebo Masinde atafanyiwa tathmini ya kiakili kabla ya kufikishwa mahakamani rasmi.
Anatarajiwa kurejea mahakamani tarehe 28 Julai 2025 kwa ajili ya kujibu maombi yake. DPP pia ametupilia mbali mashtaka dhidi ya afisa wa pili, Duncan Kiprono, akitaja ukosefu wa ushahidi.
Tamasha la muziki lililomshirikisha Kanye West lasitishwa Slovakia

Chanzo cha picha, Getty Images
Tamasha la muziki wa rap ambalo waandaaji walidai kuwa lingekuwa tamasha pekee barani Ulaya mwaka huu na rapa mtata wa Marekani Kanye West limesitishwa.
Waandaaji wa tamasha la Rubicon nchini Slovakia walitangaza kwamba hafla hiyo, iliyopangwa kufanyika wikendi ijayo ilikuwa imeahirishwa "kutokana na shinikizo kutoka nje na changamoto za ugavi".
Makundi ya waandamanaji yalikuwa yameweka pingamizi kuhusu kuonekana kwa West kwa sababu ya matamshi ya chuki dhidi ya Wayahudi na yanayounga mkono Wanazi ambayo ameyatoa katika miaka ya hivi karibuni.
Wasanii wa rap wa Kislovakia walianza kujiondoa, wakifuatiwa na mmoja wa waandaaji.
Hatimaye, West mwenyewe, ambaye sasa anajulikana rasmi kama Ye alifuta chapisho la Instagram linalotangaza tamasha hilo.
Akaunti ya Instagram ya tamasha hilo ilisema: "Ni kwa masikitiko kwamba tunatangaza: Tamasha la Rubicon halitafanyika mwaka huu.
"Huu haukuwa uamuzi rahisi. Kutokana na shinikizo la vyombo vya habari na kujiondoa kwa wasanii kadhaa na washirika, hatukuweza kutoa tamasha katika kiwango cha ubora unaostahili."
West alichapisha msururu wa maneno ya chuki, akijitangaza kuwa Mnazi, na kutoa wimbo uitwao Heil Hitler uliomtukuza kiongozi wa Nazi.
Uingereza yakabiliwa na tishio kutoka Iran, ripoti yaonya

Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images
Uingereza inakabiliwa na ongezeko la tishio na lisilotabirika kutoka kwa Iran na serikali lazima ifanye jitihada zaidi kukabiliana nayo, kamati ya kijasusi na usalama ya Bunge imeonya.
Wito huo unakuja wakati inachapisha matokeo ya uchunguzi mkubwa ambao unahusu mauaji na utekaji nyara wa taifa la Iran, ujasusi, mashambulizi ya mtandaoni na mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.
Kamati hiyo ambayo ina jukumu la kusimamia mashirika ya kijasusi ya Uingereza, imeibua wasiwasi hasa juu ya "ongezeko kubwa" la vitisho vya kimwili dhidi ya wapinzani wa utawala wa Iran nchini Uingereza.
"Iran inaleta tishio kubwa, endelevu na lisilotabirika kwa Uingereza, raia wa Uingereza na maslahi ya Uingereza," alisema Lord Beamish, mwenyekiti wa kamati.
Kamati hiyo inaishutumu serikali kwa kuzingatia "usimamizi wa migogoro" na "kuidhibiti Iran", pamoja na mpango wake wa nyuklia, bila kujali vitisho vingine.
Inasema tishio la usalama wa taifa kutoka Iran linahitaji rasilimali zaidi na mbinu ya muda mrefu. "Wakati shughuli za Iran zinaonekana kutokuwa za kimkakati na kwa kiwango kidogo kuliko Urusi na China, Iran inaleta tishio kubwa kwa usalama wa taifa la Uingereza, ambalo halipaswi kupuuzwa: ni endelevu na muhimu, haitabiriki."
Kuhusu tishio la kimwili kwa watu wanaoishi Uingereza, kamati hiyo ilisema imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kasi na kwa idadi tangu kuanza kwa 2022.
Inalenga wapinzani na wapinzani wengine wa utawala wa Iran, ilisema, na kuongeza pia kuna tishio lililoongezeka "dhidi ya masilahi ya Wayahudi na Israel nchini Uingereza".
Kumekuwa na takribani majaribio 15 ya mauaji au utekaji nyara dhidi ya raia wa Uingereza au watu wa Uingereza tangu mwanzo wa 2022, ripoti ilibainisha.
Unaweza kusoma;
Muasi wa Korea Kaskazini kumshtaki Kim Jong Un kwa unyanyasaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Utawala wa Korea Kaskazini chini ya Kim Jong Un kwa kawaida haujibu madai ya unyanyasaji yanayotolewa na waasi wa Korea Kaskazini. Raia wa Korea Kaskazini anapanga kuwasilisha kesi mahakamani dhidi ya rais wa nchi hiyo Kim Jong Un kwa unyanyasaji aliokumbana nao akiwa kizuizini nchini humo.
Choi Min-kyung alitoroka Korea Kaskazini kwenda China mwaka 1997 lakini alirejeshwa nyumbani kwa lazima mwaka 2008.
Anasema alinyanyaswa kingono na kuteswa baada ya kurejea. Atakapowasilisha kesi mjini Seoul siku ya Ijumaa, itakuwa mara ya kwanza kwa mzaliwa wa Korea Kaskazini aliyeasi kuchukua hatua za kisheria dhidi ya utawala huo, lilisema kundi la kutetea haki za watu wa Kusini linalomsaidia Bi Choi.
Mahakama za Korea Kusini katika siku za nyuma zilitoa hukumu dhidi ya Korea Kaskazini kwa madai kama hayo ya Wakorea Kusini lakini hukumu hizo kwa kiasi kikubwa zimepuuzwa na Pyongyang.
Soma pia:
Watoto wauawa Gaza kwa shambulizi la Israel

Chanzo cha picha, Reuters
Takribani Wapalestina 15, wakiwemo watoto wanane na wanawake wawili, wameuawa katika shambulizi la Israel karibu na kituo cha tiba katikati mwa Gaza, hospitali inasema.
Hospitali ya Martyrs ya Al-Aqsa ilisema shambulio hilo liliwakumba watu waliokuwa wakipanga foleni kutafuta virutubisho vya lishe katika mji wa Deir al-Balah.
Video ya picha kutoka hospitali ilionesha miili ya watoto kadhaa na wengine wakitibiwa majeraha yao.
Jeshi la Israel limesema linachunguza ripoti hizo.
Watu wengine 26 waliripotiwa kuuawa katika mashambulizi kwingineko huko Gaza siku ya Alhamisi, wakati wajumbe wa Israel na Hamas wakiendelea na mazungumzo ya makubaliano mapya ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja huko Doha.
Licha ya matumaini yaliyooneshwa na Marekani, ambayo inafanya kazi kama mpatanishi pamoja na Qatar na Misri, hadi sasa wanaonekana hawajakaribia mafanikio.
Siku ya Jumatano usiku, afisa mkuu wa Israel aliwaambia waandishi wa habari mjini Washington kwamba inaweza kuchukua wiki moja au mbili kufikia makubaliano.
Afisa huyo ambaye alikuwa akizungumza katika ziara nchini Marekani na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, pia alisema iwapo makubaliano yatafikiwa kuhusu kusitisha mapigano kwa siku 60, Israel itatumia muda huo kuvimaliza kabisa vita hivyo ambavyo vitawalazimu Hamas kupokonywa silaha.
Ikiwa Hamas itakataa kushusha silaha, Israel "itaendelea" na operesheni za kijeshi, waliongeza. Hapo awali, Hamas ilitoa taarifa ikisema kuwa mazungumzo hayo yamekuwa magumu, ikilaumu Israel "kutokuwa na msimamo".
Kundi hilo limesema limeonyesha kubadilika kwa kukubali kuwaachilia mateka 10, lakini limekariri kuwa linatafuta makubaliano "ya kina" ambayo yatamaliza mashambulizi ya Israel.
Unaweza kusoma;
China yakanusha madai ya Ujerumani kuwa ililenga ndege ya kijeshi ya leza

Chanzo cha picha, Reuters/Taiwan Coast Guard
China imepinga madai ya Ujerumani kwamba ililenga ndege ya kijeshi ya leza iliyoshambuliwa kutoka kwenye meli ya kivita, huku mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili ukizidi kuzorota.
Ujerumani iliishutumu China kwa kujaribu kuvuruga moja ya ndege zake mapema mwezi huu ilipokuwa ikishiriki katika operesheni zinazoongozwa na Umoja wa Ulaya zinazolenga kulinda meli katika Bahari ya Shamu dhidi ya makombora yanayorushwa na kundi la Wahouthi la Yemen.
Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imemwita balozi wa China na kuelezea tukio hilo kuwa "halikubaliki kabisa". Mjumbe wa China katika Umoja wa Ulaya pia ameitwa na jumuiya hiyo.
Hata hivyo, Beijing imekanusha madai hayo, ikisema madai ya Ujerumani "ni kinyume kabisa na ukweli unaojulikana na China".
Siku ya Jumanne, Ujerumani ilisema ndege yake ya upelelezi ililengwa ilipokuwa ikipaa juu ya Bahari ya Shamu, ambapo nchi kadhaa za Ulaya zimekuwa zikichangia juhudi za ufuatiliaji na ulinzi tangu mapema mwaka 2024 kulinda meli dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa kutoka Yemen.
Soma zaidi:
DCI yathibitisha kukamatwa kwa mshawishi wa TikTok Kenya

Chanzo cha picha, DCI/ KENYA
Mshawishi wa mtandao wa Tiktok nchini Kenya anayeshtumiwa kwa kuchochea vurugu dhidi ya maafisa wa polisi amekamatwa jijini Nairobi.
Mtuhumiwa huyo, aliyetambuliwa kama Godfrey Mwasiaga Kakan Maiyo, alichukuliwa na maafisa wa DCI siku ya Jumatano baada ya video iliyowekwa kwenye akaunti yake ya Tiktok kusambaa mitandaoni iliyodaiwa kutoa wito wa mashambulizi dhidi ya maafisa wa usalama.
Kulingana na polisi wa DCI, Maiyo alifuatiliwa hadi jengo la Kimathi House, ambako ambako ana ofisi yake binafsi.
"Wapelelezi walimfuata mshukiwa hadi Kimathi House, ambako ana ofisi kwa jina LetaPeleka Logistics. Kwa sasa yuko rumande akisubiri kufikishwa mahakamani," DCI ilisema.
Mamlaka zilisema kukamatwa huko ni sehemu ya msako mkali dhidi ya watu wanaotuhumiwa kueneza chuki na kuchochea machafuko katika maandamano ya hivi majuzi yaliyopinga serikali.
Sio mara ya kwanza kwa visa kama hivyo kutokea cha karibuni zaidi kikiwa kile cha mwanablogu Albert Ojwang ambaye alichukuliwa na watu waliodaiwa kuwa maafisa wa polisi, akakamatwa na kuzuiliwa kwa madai ya kile alichoandika mtandaoni.
Baadaye Albert Ojwang alifariki dunia katika hali ya kutatanisha akiwa kuzuizini. Hali iliyochochea hasira miongoni mwa vijana na kusababisha maandamano.
Pia unaweza kusoma:
Kadhi Mkuu Kenya Abdulhalim Hussein afariki dunia

Chanzo cha picha, NMG
Kadhi Mkuu nchini Kenya Abdulhalim Hussein amefariki dunia.
Kifo chake kilitangazwa Jumatano, Julai 10, na Sheikh Jamaludin Osman, Imamu wa Msikiti wa Jamia.
“Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na hakika kwake tutarejea, ninasikitika kuwatangazia kifo cha Kadhi wetu Mkuu Sheikh Abdulhalim Hussein kilichotokea muda mfupi uliopita huko Mombasa.
"Atazikwa Mombasa," Sheikh Osman alisema.
Sheikh Abdulhalim aliteuliwa kuwa Kadhi Mkuu wa Kenya mnamo Julai 2023 baada ya mchakato wa usajili ulioongozwa na Tume ya Huduma za Idara ya Mahakama (JSC).
Alichaguliwa kutoka miongoni mwa wagombea watano waliokuwa wameorodheshwa kumrithi Sheikh Ahmed Muhdhar, ambaye alistaafu baada ya kuhudumu kwa miaka 12 na kufikisha umri wa miaka 60.
Jukumu la Kadhi Mkuu ni nafasi ya kikatiba ndani ya Mahakama na imetengwa kwa ajili ya Waislamu wanaokidhi sifa mahususi, ikiwa ni pamoja na kuwa na shahada ya Sharia, kuwa na maadili mema kwa mujibu wa kanuni za Kiislamu, na kuwa wanachama wa jumuiya za Kiislamu zinazotambulika.
Kushikilia nafasi ya Kadhi Mkuu pia inahitaji uzingatiaji wa Sura ya Sita ya Katiba.
Sheikh Abdulhalim alikuwa na jukumu la kushughulikia maswala ya familia kati ya Waislamu, haswa wale wanaohusiana na urithi, talaka, na ndoa.
Shambulio jipya la ndege zisizo na rubani la Urusi laripotiwa Kyiv

Chanzo cha picha, Reuters
Mji mkuu nchini Ukraine, Kyiv umeshambuliwa tena kwa ndege zisizo na rubani za Urusi usiku kucha, maafisa wa eneo hilo wanasema, takriban watu wawili wameripotiwa kuuawa na 13 kujeruhiwa huku moto ukiwaka katika mji huo.
Mamlaka ya Kyiv inasema mabaki ya ndege isiyo na rubani yalianguka kwenye paa la jengo la makazi katikati mwa wilaya ya Shevchenkivskyi.
Video kwenye mitandao ya kijamii, ambayo bado haijathibitishwa na BBC, inaonyesha milipuko angani usiku, huku vitengo vya ulinzi wa anga vikianza kukabiliana na shambulio hilo.
Jeshi la Ukraine pia limeonya kuhusu tishio la shambulizi la kombora la balestiki.
Ukraine iliripoti shambulio kubwa zaidi la anga kuwahi kutokea la Urusi Jumanne usiku, baada ya ndege zisizo na rubani 728 na makombora 13 ya balestiki kushambulia miji kote nchini humo mara kadhaa.
Jeshi la Urusi halijazungumza lolote kuhusu shambulio la hivi punde lililoripotiwa.
Huduma ya dharura ya Ukraine DSNS ilisema Jumatano jioni kwamba watu watatu waliuawa katika shambulio la anga la Urusi katika mji wa Kostiantynivka - karibu na eneo la vita mashariki mwa Ukraine.
Marekani ilianza tena kutuma baadhi ya silaha kwa Ukraine, Reuters iliripoti Jumatano jioni, siku chache baada ya kusitisha usafirishaji wa baadhi ya silaha muhimu.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alianzisha uvamizi wa Ukraine mnamo Februari 2022.
Soma zaidi:
UNAIDS kutoa ripoti ya kwanza ya VVU duniani tangu Marekani kusitisha ufadhili wa USAID

Chanzo cha picha, Getty Images
UNAIDS itatoa ripoti yake ya kwanza juu ya maambukizo ya VVU duniani tangu Marekani kupunguza mgao wake baadaye hii leo huko Johannesburg.
UNAIDS, Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI linakadiria kwamba huenda kukawa na maambukizi mapya ya VVU milioni sita, na vifo milioni nne vinavyohusiana na UKIMWI, kufikia mwaka 2029, kufuatia kupunguzwa kwa fedha za misaada ya kibinadamu na Marekani.
Afrika Kusini ina idadi kubwa zaidi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ulimwenguni.
Pia ilikuwa ni mpokeaji mkubwa wa fedha za UKIMWI kutoka Marekani hadi Machi mwaka huu, wakati utawala wa Rais Trump ulitangaza kufungwa kwa shirika la USAID.
Pesa hii ilisaidia nchi kupunguza kiwango chake cha maambukizo mapya ya VVU kwa zaidi ya 60% tangu kilele chake mnamo 2000.
Pia ilifanya nchi hiyo kuwa moja ya waongozaji katika utafiti wa VVU ulimwenguni.
Mwezi uliopita vyuo vikuu vya juu vya Afrika Kusini viliomba serikali madola ya mamilioni, ili kuendelea na utafiti huu, ambao baadhi umesitishwa kwa sababu ya kupunguzwa kwa fedha na Marekani.
Siku ya Jumatano tarehe 9/07/2025, serikali ya Afrika Kusini na wafadhili wa kimataifa waliahidi karibu dola milioni 54 ili kukabili palipo na mapungufu.
Lakini ikizingatiwa kuwa mwaka jana Marekani ilitumia mara nane ya kiwango hicho kwa ufadhili wa VVU Afrika Kusini, kiwango hiki hakitatosha kutimiza hitaji lililopo.
Soma zaidi:
Ugiriki yasitisha maombi ya kufatufa hifadhi kwa wahamiaji kutoka Afrika Kaskazini

Chanzo cha picha, Getty Images
Ugiriki imesitisha ushughulikiaji wa maombi ya kutafuta hifadhi kutoka Afrika Kaskazini kwa miezi mitatu baada ya kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji.
Wanaowasili kwa boti kutoka eneo hilo watakamatwa na kuwekwa kizuizini, Waziri Mkuu wa kihafidhina Kyriakos Mitsotakis alisema.
Aliongeza kuwa Ugiriki ilikuwa "inatuma ujumbe uliodhamiriwa... kwa wafanyabiashara na wateja wao wote kwamba pesa wanazotumia zinaweza kupotea kabisa, kwa sababu itakuwa vigumu kufika Ugiriki kwa njia ya bahari."
"Hali hii ya dharura inahitaji hatua za dharura vile vile kukabiliana nayo."
Mitsotakis aliongeza kuwa masharti hayo yatatokana na hoja sawa za kisheria Ugiriki ilitumia mwaka 2020 kuwazuia maelfu ya watu kuvuka mpaka wa ardhi yao na Uturuki.
Rasimu ya sheria itawasilishwa bungeni siku ya Alhamisi.
"Ujumbe wa wazi: salia ulipo, kwa sababu hatutakukubali," alisema waziri wa uhamiaji Thanos Plevris kwenye X.
Tangazo la Mitsotakis linafuatia ongezeko kubwa la wahamiaji wanaofika katika visiwa vya kusini vya Crete and Gavdos.
Zaidi ya wahamiaji 2,000 waliwasili Crete katika siku za hivi karibuni na wengine 520 waliokolewa nje ya pwani yake mapema Jumatano, na kufanya idadi ya jumla tangu kuanza kwa 2025 kufikia 9,000.
Soma zaidi:
Marekani yamuwekea vikwazo Albanese mjumbe maalum wa UN na mkosoaji wa mashambulizi ya Israel, Gaza

Chanzo cha picha, Reuters
Utawala wa Trump unamwekea vikwazo mjumbe maalum wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa Francesca Albanese, mkosoaji mkubwa wa mashambulizi ya kijeshi ya Israel huko Gaza.
Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alihusisha hatua hiyo na uungaji mkono wake kwa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), ambayo baadhi ya majaji wake tayari wamewekewa vikwazo na Marekani.
Rubio alisema Marekani inamuwekea vikwazo Albanese kwa kushirikiana moja kwa moja na ICC katika juhudi zake za kuwafungulia mashitaka raia wa Marekani au Israel, ikimtuhumu kuwa hafai kuhudumu kama mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa.
Vikwazo hivyo huenda vikamzuia Albanese kusafiri kwenda Marekani na vitazuia mali yoyote aliyo nayo nchini humo.
Hii ni hatua ya hivi karibuni zaidi ya utawala wa Trump unapoendesha kampeni dhidi ya ICC, ikiwa tayari imewawekea vikwazo majaji wake wanne.
Marekani ilichukua hatua hiyo baada ya mahakama ya ICC mwaka jana kutoa kibali cha kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wake wa Ulinzi wakati huo Yoav Gallant kwa tuhuma za uhalifu wa kivita huko Gaza, tuhuma wanazokanusha.
Hatua hiyo huenda ikazua msukosuko kutoka kwa wale wanaotaka uwajibikaji kuhusu idadi ya vifo vya raia kutokana na mashambulizi ya kijeshi ya Israel huko Gaza.
Jeshi la Israel lilianzisha kampeni huko Gaza kujibu shambulio lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Takriban watu 57,575 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
Soma zaidi:
Trump atishia Brazil kwa ushuru wa 50% na kutaka kesi ya Bolsonaro itupiliwe mbali

Chanzo cha picha, Bloomberg/Getty
Rais wa Marekani Donald Trump amesema anapanga kutoza ushuru wa 50% kwa bidhaa zinazotengenezwa nchini Brazil, na hivyo kuzidisha vita vyake na nchi hiyo ya Amerika Kusini.
Alitangaza mpango huo katika taarifa yake ya hivi karibuni juu ya ushuru, ambayo ilishirikishwa kwenye mitandao ya kijamii.
Trump anaishutumu Brazil kwa "kuhangaisha" kampuni za teknolojia za Marekani na kufanya "hila" dhidi ya rais wa zamani wa mrengo wa kulia Jair Bolsonaro, ambaye anakabiliwa na mashtaka juu ya jukumu lake katika njama ya kubadilisha matokeo ya uchaguzi mwaka 2022.
Akijibu katika chapisho la mtandao wa kijamii, rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva alisema ongezeko la ushuru kwa Brazil litajibiwa vivyo hivyo, na akaonya dhidi ya kuingiliwa kwa aina yoyote katika mfumo wa mahakama wa taifa hilo.
Trump alizungumza na Lula kuhusu kesi ya Bolsonaro mapema wiki hii.
Wakati huo, Lula alisema Brazil haitakubali "kuingiliwa" na mtu yeyote na kuongeza: "Hakuna aliye juu ya sheria."
Trump amechapisha barua kwa nchi 22 kote ulimwenguni wiki hii, zikiwemo washirika wa kibiashara kama vile Japan, Korea Kusini na Sri Lanka, akielezea ushuru mpya kwa bidhaa zao ambao anasema utaanza kutekelezwa tarehe 1 Agosti.
Tofauti na nchi nyingine nyingi, Marekani ilifurahia ziada ya kibiashara na Brazil mwaka jana, ikiuza bidhaa nyingi zaidi nchini humo kuliko ilivyonunua kutoka kwao.
Katika barua hiyo, Trump alitaja kiwango cha 50% "ni muhimu ... kurekebisha dhuluma kubwa za serikali ya sasa".
Alisema ataagiza Mwakilishi wa Biashara wa Marekani kuanzisha uchunguzi unaoitwa 301 kuhusu tabia za kibiashara za kidijitali za Brazil.
Kampuni ya mitandao ya kijamii ya Trump, Trump Media, ni miongoni mwa makampuni ya kiteknolojia ya Marekani yanayopinga maamuzi ya mahakama ya Brazil kuhusu amri ya kusimamisha akaunti za mitandao ya kijamii.
Nchi hiyo pia ilikuwa imepiga marufuku kwa muda mtandao wa X wa Elon Musk, ambayo zamani ilijulikana kama Twitter, baada ya jukwaa hilo kukataa kupiga marufuku akaunti ambazo zilichukuliwa na Brazil kueneza habari potofu kuhusu uchaguzi wa rais wa 2022 wa Brazil.
Mwezi uliopita, Mahakama Kuu ya Brazil iliamua kwamba kampuni za mitandao ya kijamii zinaweza kuwajibika kwa maudhui yaliyochapishwa kwenye majukwaa yao.
Soma zaidi:
Wahouthi wazamisha meli ya pili ya mizigo Bahari ya Shamu ndani ya wiki moja

Chanzo cha picha, EPA
Wafanyakazi sita wameokolewa na takriban wengine watatu kufariki dunia baada ya meli ya mizigo kushambuliwa na Wahouthi wa Yemen na kuzama kwenye Bahari ya Shamu, ujumbe wa wanamaji wa Ulaya unasema.
Meli kubwa ya kubeba mizigo ya Eternity C iliyokuwa na bendera ya Liberia, inayoendeshwa na Ugiriki ilikuwa na wafanyakazi 25 ilipoharibiwa vibaya na kupoteza mwelekeo baada ya kushambuliwa na maguruneti ya kurushwa kwa roketi Jumatatu kutoka kwa boti ndogo, kulingana na shirika la Uingereza la Uendeshaji Biashara Baharini (UKMTO).
Shambulizi hilo liliendelea Jumanne na shughuli za uokoaji zilianza usiku kucha.
Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran walisema walishambulia meli ya Eternity C kwa sababu ilikuwa ikielekea Israel, na kwamba walichukua idadi isiyojulikana ya wafanyakazi hadi "mahali salama".
Ubalozi wa Marekani nchini Yemen ulisema Wahouthi "wamewateka nyara wafanyakazi wengi walionusurika" na kutoa wito waachiliwe mara moja.
Mamlaka nchini Ufilipino ilisema 21 kati ya wafanyakazi hao walikuwa raia wake.
Mwingine kati yao ni raia wa Urusi ambaye alijeruhiwa vibaya katika shambulizi hilo na kupoteza mguu.
Ni meli ya pili ya Wahouthi kuzama ndani ya wiki moja, baada ya kundi hilo Jumapili kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kwenye meli nyingine ya mizigo yenye bendera ya Liberia, Magic Seas, ambayo walidai "ni ya kampuni iliyokiuka marufuku ya kuingia kwenye bandari za Palestina inayokaliwa".
Picha za video zilizotolewa na Wahouthi siku ya Jumanne zilionyesha watu wenye silaha wakiingia kwenye chombo hicho na kuilipua maraa kadhaa kabla ya kuzama.
Mnamo mwezi Mei, Wahouthi walikubali makubaliano ya kusitisha mapigano na Marekani kufuatia wiki saba za mashambulizi makali ya Marekani dhidi ya Yemen kujibu mashambulizi dhidi ya meli za kimataifa.
Hata hivyo, walisema makubaliano hayo hayajumuishi kukomesha mashambulizi dhidi za Israel, ambayo imefanya mashambulizi mengi ya kulipiza kisasi nchini Yemen.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 10/07/2025
