Je, rais wa China Xi Jinping anapoteza udhibiti wa jeshi lake?

Chanzo cha picha, Reuters
Habari za magazeti ya Uingereza zinaangazia wasiwasi unaoongezeka kuhusu machafuko ya ndani nchini China, huku kukiwa na ripoti za mvutano kati ya Rais Xi Jinping na baadhi ya viongozi wa kijeshi.
Makala katika gazeti la The Telegraph la Uingereza inaonya juu ya uzito wa hatua za kijeshi nchini China, na kwamba Rais wa China Xi Jinping "huenda akapoteza" udhibiti wa jeshi la taifa hilo.
Mwandishi Gordon Chang anasema kuwa kiongozi huyo wa China anaweza kuwa hatari zaidi kwa ulimwengu ikiwa anahisi msimamo wake unatishiwa ndani ya nchi yake.
Mwandishi anaashiria ripoti zinazodai kutoweka kwa Jenerali He Weidong, makamu mwenyekiti wa Tume Kuu ya Kijeshi ya Chama cha Kikomunisti na amiri jeshi wa pili wa jeshi la China, ambaye alionekana hadharani mara ya mwisho Machi 11, 2025.
Jenerali Weidong anajulikana kuwa mtiifu kwa Rais Xi Jinping katika jeshi, na maafisa wa sasa na wa zamani wa Marekani wanaamini aliondolewa katika nafasi yake katika Jeshi la Ukombozi la China.
Kuna uvumi ambao haujathibitishwa kwamba jenerali huyo alikufa mnamo Mei 2025, ndani ya Hospitali ya Jeshi la Ukombozi la Watu chumba 301 huko Beijing.
Mwandishi anataja wataalam wa Asia ambao wanaamini kuwa kiongozi wa China alimfukuza kazi Jenerali Weidong, "jambo ambalo linaonyesha umakini wake katika kutokomeza ufisadi jeshini."
Aliongeza kuwa Jinping anataka kulibadilisha Jeshi la Ukombozi la Watu kuwa jeshi lenye uwezo nje ya mipaka ya China, huku pia akitumikia ajenda yake ya ndani.

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwandishi anaamini kuwa rais amekuwa na ushawishi mkubwa kila wakati, kwa hivyo ni kawaida kwamba wachambuzi na waandishi wa habari wanamhusisha na kila hatua muhimu nchini China.
Pia alikuwa karibu na udhibiti kamili wa jeshi, ambalo haliko chini ya serikali ya China bali chini ya Chama cha Kikomunisti.
Pia alifaulu kuweka wafuasi waaminifu baada ya kampeni zake zinazoendelea za kupinga ufisadi na upangaji upya kamili wa Jeshi la Ukombozi la Watu katikati ya muongo uliopita.
Mwandishi aliangazia uchanganuzi unaopendekeza kwamba Xi alikuwa amepatwa na "megalomania," sawa na Stalin, na kwamba sasa aliona maadui kila mahali, na hivyo kuwabadilisha maafisa wakuu wa jeshi.
Mwandishi anatoa ushahidi wa uchambuzi huu, akisema kwamba uchapishaji wa PLA Daily, mkono wa propaganda wa jeshi la China, kuanzia Julai 9, 2024, ulikosoa waziwazi matakwa ya rais ya utiifu kamili, katika mfululizo wa makala zinazosifu "uongozi wa pamoja."
Mwandishi anaamini kwamba makala hizo zinaakisi rais kutokuwa na udhibiti kamili wa jeshi, na kwamba walioziandika ni watiifu kwa Makamu Mwenyekiti wa Tume Kuu ya Kijeshi, Jenerali Zhang Youxia.

Chanzo cha picha, Reuters
Mwandishi huyo pia alizungumzia ushahidi wa Xi Jinping kupoteza ushawishi miongoni mwa raia, ikiwa ni pamoja na kutokuwepo kwake kwa mara ya kwanza kwenye mkutano wa kilele wa BRICS, uliomalizika nchini Brazil, jambo linaloonyesha wazi kuwa huenda amepoteza udhibiti wa hali hiyo na hata "hataruhusiwa tena kusafiri nje ya China."
Wengine wanahoji kuwa "kanuni" mpya za uratibu wa Politburo, zilizotangazwa na rais mwenyewe mnamo Juni 30, 2025, zinaonyesha kizuizi rasmi cha mamlaka yake.
Mwandishi anaeleza kuwa utawala wa Kichina umegubikwa na mafumbo katika muongo mmoja uliopita kiasi kwamba imekuwa vigumu kusoma. Hatahivyo kuna ishara wazi za kutokuwa na utulivu.
Watu wenye nguvu kama Xi mara chache huondoka kimya kimya, na ikiwa anahisi kutishiwa, kuna imani kwamba lazima achukue hatua za haraka dhidi ya wengine.
Moja ya fursa zilizopo sasa ni kuivuruga China kwa vita ambavyo vinaweza kuwazuia viongozi wengine wakuu katika Chama cha Kikomunisti cha China kujaribu kumuondoa katikati ya mapigano, hivyo anaweza kuamini kwamba kuchochea migogoro ni kwa manufaa yake.















