Moja kwa moja, Pakistan yaishambulia Afghanistan huku Waziri Mkuu akisema vikosi vyake viko tayari 'kuangamiza' Taliban

Wakati wa uhasama huu, pande zote mbili zimedai kusababisha hasara kubwa kwa upande mwingine huku zikipata uharibifu mdogo kwa upande wao.

Muhtasari

Moja kwa moja

Rashid Abdallah

  1. Epstein alijaribu kununua jumba la kifahari huko Morocco siku chache kabla ya kukamatwa kwake 2019

    .

    Chanzo cha picha, US Department of Justice

    Maelezo ya picha, Jumba la Bin Ennakhil, iliyoko katika kitongoji cha kifahari cha Palmeraie cha Marrakech, imeelezewa kama kazi bora ya usanifu.

    Jeffrey Epstein alijaribu kununua jumba la mamilioni ya dola huko Morocco siku moja kabla ya kukamatwa kwake mnamo 2019, kulingana na hati zilizotolewa na Idara ya Sheria ya Marekani mwezi uliopita.

    Epstein alitaka kumiliki Bin Ennakhil tangu 2011, lakini mizozo na muuzaji kuhusu bei na mpangilio wa ununuzi iliendelea kwa miaka kadhaa.

    Jumba la kifahari katika kitongoji cha kifahari cha Palmeraie cha Marrakech limefafanuliwa kuwa kazi bora ya usanifu, iliyojengwa na mafundi 1,300 na kuangazia nakshi na vinyago vya kupendeza.

    Epstein alitia saini uhamisho wa kielektroniki wa $14.95m (£11m) tarehe 5 Julai 2019, siku moja kabla ya kukamatwa kwake, kufuatia makubaliano ya kununua kampuni ya kigeni iliyomiliki mali hiyo kwa €18m (£13.3m).

    Kulingana na hati zilizotolewa, uhamisho huo ulikuwa shughuli kuu ya mwisho ya kifedha ya Epstein katika kipindi hicho kabla ya kukamatwa kwake na mamlaka ya Marekani kwa mashtaka ya biashara ya ngono aliporejea New York.

    Siku tatu baada ya kukamatwa, mhasibu wa Epstein Richard Kahn alighairi uhamisho wa kielektroniki na ununuzi wa jumba hilo la kifahari haukukamilika .

    Pia unaweza kusoma:

  2. Ukraine: Zaidi ya waafrika 1,700 wanapigana kwa niaba ya Urusi

    Baadhi ya wahamiaji wamezuiliwa Urusi upande wa mpaka wa Finland baada ya muda wa visa yao kumalizika na wamepelekwa katika mpaka wa Ukraine.

    Chanzo cha picha, GOVERNOR OF MURMANSK/TELEGRAM

    Maelezo ya picha, Baadhi ya wahamiaji wamezuiliwa Urusi upande wa mpaka wa Finland baada ya muda wa visa yao kumalizika na wamepelekwa katika mpaka wa Ukraine.

    Zaidi ya Waafrika 1,700 wanapigana upande wa Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, alisema Jumatano, akiongeza kuwa Moscow inatumia udanganyifu kuwashawishi kujiunga na mapigano hayo.

    Akizungumza pamoja na mwenzake wa Ghana, Sybiha alisema mazungumzo yanaendelea na serikali mbalimbali barani Afrika ili kuzuia raia wao kuhadaiwa katika mipango hiyo. Ghana itakuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika mwaka ujao.

    “Tunaona wazi kuwa Urusi inajaribu kuwahadaa raia wa Afrika kuingia katika vita vya maangamizi,” Sybiha aliambia mkutano na wanahabari. “Kwa mujibu wa takwimu zetu, kwa sasa kuna zaidi ya raia 1,780 kutoka bara la Afrika wanaopigana katika jeshi la Urusi.”

    Aliongeza kuwa wapiganaji hao wanatoka katika nchi 36 tofauti za Afrika.

    Mamlaka za Urusi zimekanusha madai ya kuwaajiri kinyume cha sheria raia wa Afrika kujiunga na majeshi yake.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, alisema wengi wa Waafrika wanaopigana kwa niaba ya Urusi ni waathiriwa waliotapeliwa, wakihadaiwa kupitia mtandao wa siri (dark web) kwa ahadi za ajira za kawaida.

    “Hawana historia ya kiusalama. Hawana uzoefu wa kijeshi. Hawajapata mafunzo,” alisema Ablakwa. “Walishawishiwa na kudanganywa, kisha wakawekwa mstari wa mbele vitani.”

    Ablakwa alionesha mshikamano wake na Ukraine na akatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano ili kumaliza vita hivyo, ambavyo vilitimiza miaka minne tangu kuanza kwake Jumanne. Alisema atamwomba Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, kuwaachilia huru raia wawili wa Ghana waliotekwa wakiwa wanapigana upande wa Urusi.

    Aidha, Ablakwa alisema Ghana itahamasisha kampeni za uelimishaji wa umma kuhusu mitandao ya usafirishaji haramu wa watu inayowadanganya Waafrika kujiunga na majeshi ya Urusi, wakati wa uongozi wake katika Umoja wa Afrika.

    Soma Pia:

  3. China yawaondoa maafisa tisa wa kijeshi kabla ya mkutano muhimu wa kisiasa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Tangu kuingia madarakani, Xi amezindua mawimbi ya harakati za kupambana na ufisadi

    China imewaondoa maafisa 19, wakiwemo tisa kutoka jeshini, kwenye orodha ya wabunge wake kabla ya mkutano wake mkubwa zaidi wa kila mwaka wa kisiasa wiki ijayo.

    Uondoaji huo ulitangazwa na chombo kikuu cha kutunga sheria nchini humo, Kamati ya Kudumu ya Bunge la Wananchi (NPC).

    Hakuna sababu rasmi ya kuondolewa kwao imetolewa, lakini inakuja wiki chache tu baada ya Rais Xi Jinping kumuondoa Zhang Youxia, jenerali wake wa ngazi ya juu na pia mmoja wa washirika wake wa karibu wa kijeshi, kutoka kwa jukumu lake.

    Tangu aingie madarakani, Xi amezindua mawimbi ya misukumo ya kupinga ufisadi, akiita ufisadi "tishio kubwa" kwa Chama cha Kikomunisti.

    Hatahivyo, wakosoaji wengine wanasema imekuwa ikitumika kama zana ya kuwasafisha wapinzani wa kisiasa Kwa mujibu wa ripoti ya vyombo vya habari vya serikali, walioondolewa ni pamoja na Li Qiaoming, kamanda wa Jeshi la Ukombozi la Wananchi (PLA) Ground Force na Shen Jinlong, kamanda wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la PLA.

    Pia katika orodha hiyo walikuwemo maafisa wengine kadhaa wa kijeshi na maafisa kadhaa wa mkoa akiwemo Sun Shaochong, mkuu wa zamani wa chama katika eneo la Inner Mongolia.

    Hatua hiyo inakuja wiki chache tu baada ya Zhang kuondolewa kwenye wadhifa wake, baada ya kushutumiwa kwa "ukiukaji mkubwa wa nidhamu na sheria"

    Soma Zaidi:

  4. Habari za hivi punde, 'Tulidhani ni tetemeko la ardhi, kisha tukasikia mlipuko mkubwa' - mkazi wa Kabul

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mkazi wa Dashti Barchi katika Wilaya ya 6 ya Kabul, ambayo iko karibu na eneo lililoripotiwa kulengwa na shambulio la anga la Pakistani la jana usiku, alisema kuwa nyumba yake ilitikisika sana kutokana na mlipuko uliosababishwa na mojawapo ya mashambulizi.

    "Kwanza, tulifikiri kuwa ni tetemeko la ardhi, kwa sababu kulikuwa na tetemeko la ardhi huko Kabul siku chache zilizopita," alisema.

    "Kisha tukasikia mlipuko mkubwa." Mkazi huyo, ambaye jina lake halijatajwa kwa sababu za usalama, aliongeza kuwa watu wa Dashti Barchi walikimbilia nje na kukesha usiku kucha.

    "Hakuna mtu aliyelala baada ya hapo. Kila mtu aliogopa." Alisema kuwa ndege zilionekana zikiruka juu ya Kabul muda mfupi baada ya mlipuko huo.

    "Tulipoona ndege zikiwa juu, tuligundua kuwa ni ndege za Pakistani." Eneo lililolengwa lilikuwa takriban kilomita 4 hadi 5 kutoka nyumbani kwake, alisema.

    “Mke wangu na wazazi wangu waliogopa sana, sote tulikuwa macho usiku kucha.

  5. Wizara ya sheria Marekani yashutumiwa kuficha faili za Epstein zinazohusiana na Trump

    o

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Trump amesema alikosana na Epstein miaka kadhaa kabla ya Epstein kukamatwa kwa mara ya kwanza kwa makosa yake

    Afisa wa ngazi ya juu wa chama cha Democratic katika kamati ya bunge inayomchunguza Jeffrey Epstein ameishutumu wizara ya sheria ya Marekani kwa kuficha faili zenye madai ya unyanyasaji wa kingono kwa mtoto mdogo yaliyotolewa dhidi ya Rais Donald Trump.

    Robert Garcia, ambaye ni mwanachama wa Kamati ya Uangalizi ya Baraza la Wawakilishi, amesema yeye binafsi aliziona hati zenye madai hayo ambazo hazijawekwa wazi.

    Kujibu, wizara ya sheria imesema "HAKUNA kilichofutwa", ikiongeza kuwa hati zilizuiliwa ikiwa "zilikuwa nakala rudufu au sehemu ya uchunguzi unaoendelea."

    Trump amekataa kufanya makosa yoyote kuhusiana na kesi ya Epstein

    Wizara ya sheria pia imesema hapo awali kwamba baadhi ya faili hizo zina "madai yasiyo ya kweli na ya kutia chunvi dhidi ya Rais Trump".

    Epstein, mhalifu wa ngono alikuwa rafiki wa Trump kwa miaka kadhaa. Baadaye walitofautiana - jambo ambalo lilitokea mwanzoni mwa miaka ya 2000, kulingana na Trump, miaka miwili kabla ya Epstein kukamatwa kwa mara ya kwanza.

    Idara ya sheria imetoa mamilioni ya faili zinazoonyesha uchunguzi dhidi ya Epstein.

    Baadhi ya faili zilitiwa wino, na maafisa wamekiri kwamba faili zingine hazikutolewa kabisa.

    Garcia amesema faili alizoziona "zinaweka wazi" kwamba mwanamke mmoja "alitoa madai " dhidi ya Trump ambayo "hayajaonyeshwa" katika rekodi ambazo zimetolewa hadharani na wizara hiyo.

    Siku ya Alhamisi, Garcia alisema yeye na wanachama wa chama chake watafanya kazi katika siku chache zijazo kudai faili zilizobaki ambazo hazijatolewa ili zitolewe, ikiwa ni pamoja na zile zinazohusiana na madai ya mwanamke huyo dhidi ya Trump.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye X, wizara hiyo imesema itapitia upya kujua kama kuna faili zozote zimefichwa isivyofaa.

    Mwakilishi wa Republican wa Kentucky, James Comer, mwenyekiti wa Kamati ya Uangalizi ya Baraza la Wawakilishi, alisema Alhamisi wabunge bado wanachunguza shutuma kwamba idara ya sheria imeficha faili zinazomhusu Trump.

  6. Maafisa 10 wa FBI walioshiriki katika uchunguza dhidi ya Trump wafutwa kazi

    l

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mkurugenzi wa FBI, Kash Patel

    FBI imewafukuza kazi takriban maafisa 10, ambao wote walishiriki katika uchunguzi kuhusu jinsi Donald Trump alivyoshughulikia nyaraka za siri baada ya muhula wake wa kwanza.

    Kusitishwa kwao kazi Jumatano, kumethibitishwa na CBS, na kulitangazwa muda mfupi baada ya mkurugenzi wa FBI, Kash Patel, kuiambia Reuters kwamba maafisa hao wa shirikisho walimchunguza alipokuwa raia wakati wa uchunguzi wa hati hizo.

    Patel hakutoa ushahidi wowote wa makosa yaliyofanywa na wafanyakazi wa FBI waliofukuzwa kazi.

    Baada ya Trump kuondoka Ikulu ya White House mwaka 2021, Wakili Maalum Jack Smith aliongoza uchunguzi dhidi ya Trump ambaye sasa ni Rais. Kesi moja ililenga kujua ikiwa Trump alijaribu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020.

    Nyingine ilihusisha hati za siri ambazo Trump alizipeleka katika makazi yake ya Mar-a-Lago huko Florida na juhudi zake za kuzuia Wizara ya Sheria ya Marekani kuzipata.

    Wafanyakazi wa FBI waliofutwa kazi Jumatano wote walishiriki katika kesi juu ya hati za siri.

    Trump na washirika wake wawili walishtakiwa mwaka 2023, kufuatia uchunguzi wa Smith kuhusu hati hizo.

    2024, jaji wa shirikisho huko Florida alifuta kesi dhidi ya Trump, baada ya kugundua kuwa Smith aliteuliwa kinyume cha sheria.

    Mwaka huu, mahakama ya rufaa ya shirikisho huko Georgia ilifuta kesi dhidi ya washtakiwa wawili wa mwisho kwa ombi la wizara ya sheria ya Trump.

    Tangu Trump aliporejea Ikulu ya White House mwezi Januari, wizara ya sheria na FBI wamewafukuza kazi wafanyakazi walioshiriki katika uchunguzi dhidi yake.

    Wizara ya sheria pia imefungua mashtaka dhidi ya mkurugenzi wa zamani wa FBI James Comey, ambaye Trump alimfukuza kazi wakati wa muhula wake wa kwanza mwaka 2017, na Mwanasheria Mkuu wa New York Letitia James, ambaye aliongoza kesi dhidi ya Trump.

  7. Raia wa Marekani ni miongoni mwa waliopigwa risasi na kuuawa katika boti Cuba

    reuters

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema Washington inachunguza tukio hilo "lisilo la kawaida."

    Raia mmoja wa Marekani alipigwa risasi na kufa na mwingine kujeruhiwa na maafisa wa Cuba waliokuwa wakizuia boti ya mwendo kasi nje ya pwani ya nchi hiyo siku ya Jumatano, amesema afisa mmoja wa Marekani.

    Walinzi wa mpaka waliwapiga risasi watu wanne na kuwajeruhi wengine sita waliokuwa ndani ya boti ya mwendo kasi iliyosajiliwa Florida. Cuba inawashutumu watu 10 waliokuwa kwenye boti hiyo kwa kupanga kufanya "uvamizi wenye malengo ya kigaidi" na imesema watu hao walifyatua risasi kwanza.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema Washington inachunguza tukio hilo "lisilo la kawaida."

    Cuba imesema wote 10 walikuwa raia wa Cuba wanaoishi Marekani.

    Pia mtu wa 11 amekamatwa na kukiri kuwa sehemu ya njama hiyo.

    Wizara ya mambo ya ndani imesema kwamba boti hiyo ya mwendo kasi iliingia katika maji yake na ilikuwa "maili moja kutoka Cayo Falcones" kwenye pwani ya kaskazini mwa nchi hiyo.

    Cuba imesema Kamanda wa boti ya Cuba alijeruhiwa katika mapigano ya risasi.

    Cuba imesema abiria wengi kwenye boti hiyo iliyosajiliwa Marekani wana "rekodi za awali zinazohusisha shughuli za uhalifu na vurugu."

    Bunduki na vifaa vya kulipuka vilivyotengenezwa kwa mikono vilipatikana kwenye boti, kulingana na taarifa hiyo.

    Ufyatuaji risasi huo unakuja wakati ambapo mvutano kati ya nchi hizo mbili umeongezeka.

    Chini ya miezi miwili iliyopita, vikosi vya Marekani vilimkamata kiongozi wa Venezuela Nicolás Maduro, mshirika wa karibu wa Cuba, na kumzuia mrithi wake kuiuzia Cuba mafuta.

    Rubio amesema tukio hilo halikuwa operesheni ya Marekani na hakuna wafanyakazi wa serikali ya Marekani waliohusika.

    Rais wa Cuba Miguel Díaz-Canel siku ya Alhamisi aliapa kuilinda nchi ya Karibi dhidi ya uchokozi.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Hillary Clinton asema hakujua kuhusu uhalifu wa Epstein

    pp

    Chanzo cha picha, REUTERS/Shannon Stapleton TPX IMAGES OF THE DAY

    Hillary Clinton ameliambia jopo la Bunge kwamba "hakujua" kuhusu uhalifu wa Jeffrey Epstein, huku akiwataka wabunge kumuuliza Rais Donald Trump kuhusu uhusiano wake wa zamani na mhalifu huyo wa ngono.

    "Nataka kuona ukweli ukifichuka," waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani alisema baada ya kutoa ushahidi faraghani kwa saa kadhaa kwa kamati ya bunge inayomchunguza Epstein.

    Mumewe, Rais wa zamani Bill Clinton, atatoa ushahidi Ijumaa.

    Awali wanandoa hao walikataa wito wa jopo hilo, wakisema umechochewa kisiasa, kabla ya kukubali kutoa ushahidi kwa hofu ya kufunguliwa kesi ya kudharau Bunge.

    Clinton na Trump wanakana makosa yanayohusiana na Epstein.

    Baada ya kutumia saa sita Alhamisi akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Uangalizi ya Bunge, Clinton aliwaambia waandishi wa habari kwamba "amesikitishwa" kwamba ushahidi huo haukutolewa hadharani, "kwani nisingelazimika kuwa hapa kuzungumza nanyi."

    Pia alimpongeza Mwenyekiti James Comer kwa kuuliza maswali muhimu kuhusu uchunguzi na kwa kumsikiliza kuhusu maeneo ambayo anadhani yanahitaji kuchunguzwa.

    Clinton pia alisema aliwakosoa wanachama wa kamati ya Republican kwa kutomuuliza mtu mwingine yeyote kuhusu Epstein au mshirika wake aliyehukumiwa, Ghislaine Maxwell.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Pakistan yaishambulia Afghanistan

    p

    Chanzo cha picha, Reuters

    Pakistan imethibitisha kufanya mashambulizi katika miji ya Afghanistan ya Kabul na Kandahar, kulingana na afisa wa serikali, katika kile alichosema ni kulipiza kisasi.

    Ni saa chache baada ya Pakistan kusema wanajeshi wake wawili wameuawa baada ya operesheni ya Taliban wa Afghanistan kando ya mpaka.

    Kulingana na Mosharraf Zaidi, msemaji wa waziri mkuu wa Pakistan, jumla ya Taliban 133 wa Afghanistan wameuawa na zaidi ya 200 wamejeruhiwa hadi sasa na vikosi vya Pakistan.

    Lakini Zabihullah Mujahid, msemaji wa Taliban ya Afghanistan, aliandika kwenye X kwamba "hakuna mtu aliyejeruhiwa" katika mashambulizi hayo ya hivi karibuni ya Pakistan.

    Wakati wa uhasama huu, pande zote mbili zimedai kusababisha hasara kubwa kwa upande mwingine huku zikipata uharibifu mdogo kwa upande wao.

    Wizara ya ulinzi ya Taliban imesema iliteka vituo 19 vya kijeshi vya Pakistan na kambi mbili Alhamisi usiku na jumla ya wanajeshi 55 wa Pakistani waliuawa

    Ni vigumu kuthibitisha takwimu hizi.

    Mashambulizi dhidi ya Kabul na Kandahar ni ya hivi karibuni katika mfululizo wa mapigano kati ya Pakistan na Afghanistan, licha ya mataifa yote mawili kukubaliana kusitisha mapigano kwa muda mfupi Oktoba 2025.

    Wiki iliyopita, Pakistan ilifanya mashambulizi mengi ya anga usiku dhidi ya Afghanistan, ambayo Taliban ilisema yaliwaua watu wasiopungua 18, wakiwemo wanawake na watoto.

    Islamabad ilithibitisha mashambulizi hayo yalilenga kambi saba zinazodaiwa kuwa za wanamgambo karibu na mpaka wa Pakistan na Afghanistan, na ikasema yalizinduliwa kufuatia mashambulizi ya mabomu ya kujitoa mhanga nchini Pakistan.

    Taliban ya Afghanistan ilisema imeanzisha operesheni "kubwa" kujibu na siku ya Alhamisi ilidai mashambulizi yao yaliwaua wanajeshi "wengi" wa Pakistan.

    Hili lilikataliwa na msemaji wa waziri mkuu wa Pakistan, ambaye pia alipinga madai ya msemaji wa Taliban kwamba vituo 15 vya kijeshi vilitekwa.

    Baadaye siku hiyo, Pakistan ilithibitisha kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa na wengine watatu kujeruhiwa, baada ya wanajeshi kujibu "mashambulizi ya risasi " kando ya mpaka.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Mazungumzo kati ya Marekani na Iran yamalizika kwa maendeleo makubwa

    o

    Chanzo cha picha, Foreign Ministry of Oman

    Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Badr Albusaidi amesema Marekani na Iran zimeonyesha "uwazi" baada ya kukutana na Jared Kushner na Steve Witkoff

    Waziri wa mambo ya nje wa Oman amesema maafisa wa Marekani na Iran wamepata "maendeleo makubwa" katika mazungumzo ya nyuklia huko Geneva, lakini uwezekano wa kuwepo kwa makubaliano ambayo yanaweza kuzuia vita bado hauko wazi.

    Badr Albusaidi, ambaye alikuwa mpatanishi, amesema pande hizo mbili zimepanga kuanza tena mazungumzo "hivi karibuni,” na majadiliano ya ngazi ya kiufundi yatafanyika wiki ijayo huko Vienna.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, ambaye aliongoza ujumbe wa nchi yake, amesema "maendeleo mazuri" yamepatikana, ingawa kuna makubaliano kuhusu baadhi ya masuala, bado kuna tofauti kuhusu masuala mengine.

    Amesema duru inayofuata ya mazungumzo itafanyika katika kipindi cha chini ya wiki moja.

    Matarajio ya kuwepo kwa mazungumzo zaidi yanaweza kupunguza uwezekano wa Rais Donald Trump kuishambulia Iran.

    Trump ameamuru kupelekwa wanajeshi wengi wa Marekani katika Mashariki ya Kati, ikiwa ni idadi kubwa tangu uvamizi wa Marekani nchini Iraq mwaka 2003, huku Iran ikiapa kujibu shambulio lolote.

    Kwa miongo kadhaa, Marekani na Israeli zimeishutumu Iran kwa kujaribu kutengeneza silaha ya nyuklia kwa siri. Iran imekana mara kwa mara kwamba inaunda bomu hilo na inasema mpango wake ni wa amani tu, ingawa nchi hiyo ndiyo taifa pekee lisilo na silaha za nyuklia ambalo limeongeza urani katika kiwango cha karibu cha silaha.

    Kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Iran, wapatanishi walisisitiza kwamba Iran ina haki ya kuwa na nishati ya nyuklia ya amani na walikataa madai ya Marekani ya kusimamisha kabisa urutubishaji wa urani na kuhamisha akiba yake ya kilo 400 (880lb) ya urani iliyorutubishwa kutoka nchini humo.

    Ingawa mapendekezo hayo hayajawekwa wazi lakini mojawapo ya chaguzi zilizoripotiwa ni Iran kuruhusiwa kurutubisha urani kwa kiwango kidogo chini ya ufuatiliaji wa kimataifa.

    Na kwa upande wa Iran, Araghchi ameiambia televisheni ya Iran kwamba wapatanishi wao wanataka kuondolewa kwa vikwazo ambavyo vimedhoofisha uchumi wa Iran.

    Mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja yalifanyika katika vikao viwili. Kipindi kimoja asubuhi, ambacho kilidumu kwa saa tatu, na kingine, kifupi jioni. Hakuna kauli ya Marekani kuhusu matokeo ya mkutano huo.

    Kama ilivyokuwa katika raundi zilizopita, Marekani iliwakilishwa na mjumbe maalum Steve Witkoff na mkwe wa Trump, Jared Kushner. Rafael Grossi, mkuu wa shirika la kimataifa la ulinzi wa nyuklia, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), pia alijiunga na mazungumzo hayo.

    Iran tayari imekataa kujadili mipaka ya mpango wa makombora ya balestiki na kukomesha uungaji mkono wake kwa washirika wake katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na Hamas huko Gaza, Hezbollah huko Lebanon, wanamgambo nchini Iraq, na Houthi huko Yemen.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Hujambo na karibu

    Nakukaribisha katika taarifa zetu za moja kwa moja, leo Ijumaa ya tarehe 27/2/2026