'Ngozi yangu ilichubuka': Jinsi wanawake wa Kiafrika walivyolaghaiwa kutengeneza ndege za kivita za Urusi

A composite image of the Russian flag, South Sudanese flag, drones in silhouette and an anonymous woman in silhouette.

Chanzo cha picha, Getty Images / BBC

    • Author, Mayeni Jones
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Siku ya kwanza kazini, Adau aligundua kuwa alikuwa amefanya kosa kubwa.

"Tulipewa sare zetu bila hata kujua tutafanya kazi gani hasa. Kuanzia siku ya kwanza tulipelekwa kwenye kiwanda cha kutengeneza ndege zisizo na rubani.

Tulipoingia, tuliona ndege zisizo na rubani kila mahali na watu wakifanya kazi. Kisha tukagawanywa kwenye vituo vyetu vya kazi."

Adau mwenye asili ya Sudan Kusini anasema akiwa na umri wa miaka 23 mwaka jana alivutiwa kwenda katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Alabuga, katika Jamhuri ya Tatarstan, Urusi, baada ya kuahidiwa ajira ya kudumu.

Aliomba nafasi hiyo kupitia mpango wa Alabuga Start, mpango wa uajiri unaolenga wanawake wenye umri wa miaka 18 hadi 22, wengi wao kutoka Afrika, lakini pia kutoka Amerika ya Kusini na Asia ya Kusini-Mashariki.

Mpango huo ulikuwa umetoa ahadi ya mafunzo ya kitaalamu katika nyanja kama vile usafirishaji, mapishi na huduma za hoteli.

Hata hivyo, mpango huo umeshutumiwa kwa kutumia hila katika uajiri wake na kwa kufanya wafanyakazi wake vijana wafanye kazi katika mazingira hatari kwa mshahara mdogo kuliko walivyoahidiwa.

Wasimamizi wa mradi huo wamekanusha tuhuma hizo zote, ingawa hawajakataa kwamba baadhi ya wafanyakazi wao husaidia kutengeneza ndege za kivita.

Mpango wa Alabuga Start (AS) uligonga vichwa vya habari duniani hivi karibuni baada ya wanamitandao wa Afrika Kusini waliokuwa wakiutangaza kushutumiwa kwa kuhusika na usafirishaji haramu wa binadamu.

BBC iliwasiliana na wahusika hao na mshirika aliyewaunganisha na mpango huo, lakini hakuna aliyejibu.

Kwa makadirio, zaidi ya wanawake 1,000 wameajiriwa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kufanya kazi katika viwanda vya silaha vya Alabuga.

Mwezi Agosti, serikali ya Afrika Kusini ilianzisha uchunguzi na kuwaonya raia wake kutojiunga na mpango huo.

Adau ameomba BBC isitumie jina lake kamili wala picha yake, kwani hataki kuhusishwa na mpango huo. Anasema alisikia kuhusu mpango huo kwa mara ya kwanza mwaka 2023.

"Rafiki yangu alichapisha tangazo kuhusu udhamini wa mafunzo nchini Urusi kupitia kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Tangazo hilo lilionekana kutoka Wizara ya Elimu ya Juu ya Sudan Kusini," anasema.

A typed memo from the Republic of South Sudan advertising jobs in Russia

Chanzo cha picha, Supplied to the BBC

Maelezo ya picha, Adau alituma maombi baada ya kuona tangazo rasmi lililodhaminiwa na Urusi

Aliwasiliana na waandaaji kupitia mtandao wa WhatsApp.

"Waliniambia nijaze fomu yenye jina langu, umri wangu, na sababu za kutaka kujiunga na Alabuga.

Kisha wakaniambia nichague nyanja tatu ambazo ningependa kufanya kazi."

Adau anasema alichagua kuwa mwendeshaji wa mashine ya kubeba vitu vizito kama chaguo lake la kwanza.

Mara zote alipenda teknolojia, na hata aliwahi kusafiri nje ya nchi kushiriki mashindano ya kuendesha vifaa vvya kiroboti.

"Nilitaka kufanya kazi ambazo si za kawaida kufanywa na wanawake. Ni nadra sana kwa mwanamke kupata nafasi ya kuendesha mashine hiyo kubwa, hasa katika nchi yangu."

Mchakato wa maombi ulichukua mwaka mzima kutokana na taratibu ndefu za kupata viza.

 Screenshot of an online air ticket, showing a flight from Juba to Istanbul on 16 March

Chanzo cha picha, Supplied to the BBC

Maelezo ya picha, Tikiti ya Adau kwenda Tartastan

Safari ya kwenda Urusi

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Machi mwaka jana, hatimaye aliwasili Urusi.

"Nilipofika mara ya kwanza kulikuwa na baridi kali mno, nilichukia. Tulisafiri mwishoni mwa majira ya baridi. Tulipotoka uwanjani, kulikuwa na upepo na kibaridi."

Lakini alipofika Eneo Maalum la Alabuga, alifurahishwa na mandhari aliyoona.

"Nilivutiwa sana. Ilikuwa kama vile nilivyotarajia viwanda vingi, magari, na zana za kilimo."

Adau alipata mafunzo ya lugha kwa miezi mitatu kabla ya kuanza kazi Julai, ambapo mambo yalianza kwenda vibaya.

Anasema yeye na washiriki wengine hawakupewa nafasi ya kuchagua kama wanataka kufanya kazi katika kiwanda cha ndege zisizo na rubani au la. Walikuwa wamesaini makubaliano ya kutofichua siri (NDA), hivyo hawakuweza hata kueleza familia zao walichokuwa wanafanya.

"Tulikuwa na maswali mengi. Sote tulijiandikisha kufanya kazi za kiufundi kama uendeshaji, usafirishaji, au kuendesha mashine lakini wote tukajikuta tukifanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza ndege zisizo na rubani."

Alabuga ilikanusha kutumia hadaa katika uajiri. "Nyanja zote tunazowaajiri zimetajwa wazi kwenye tovuti yetu," waliieleza BBC.

Wafanyakazi hawaruhusiwi kupiga picha ndani ya kiwanda, lakini BBC ilimuonyesha Adau video kutoka kituo cha televisheni cha serikali ya Urusi, RT, ikionyesha kiwanda cha Alabuga kinachotengeneza ndege za kivita za Shahed 136 kutoka Iran. Alithibitisha kuwa hapo ndipo alipofanyia kazi.

"Mazingira halisi ya Eneo Maalum la Alabuga ni ya utengenezaji wa vifaa vya kivita," anasema Spencer Faragasso kutoka Taasisi ya Sayansi na Usalama wa Kimataifa.

"Urusi yenyewe imethibitisha hadharani kwamba wanatengeneza ndege za Shahed 136 huko. Wanajivunia mafanikio hayo."

Spencer anasema, kama Adau, wanawake wengi waliowahoji walisema hawakujua kabisa kwamba wangejikuta wakitengeneza silaha.

"Kwa juu juu, mpango huu unaonekana kama fursa nzuri kwa wanawake hawa kuiona dunia, kupata uzoefu wa kazi na kipato. Lakini walipofika Alabuga, wanakutana na ukweli mchungu ahadi zote hubadilika."

Adau anasema alifahamu kuwa hawezi kuendelea kufanya kazi kiwandani humo.

"Nilianza kuelewa uongo wote tulioambiwa tangu mwanzo. Nilihisi siwezi kufanya kazi na watu wanaoniongopea. Nilihisi nataka kufanya jambo lenye maana zaidi maishani kuliko kutengeneza ndege za kivita."

Alijaribu kuacha kazi, lakini aliambiwa anatakiwa kufanya kazi kwa wiki mbili kabla ya kuacha. Wakati huo, alipewa kazi ya kupaka rangi ya nje ya ndege hizo kwa kutumia kemikali zilizobabua ngozi yake.

"Nilipofika nyumbani niliona ngozi yangu inavimba na kuchubuka. Tulivaa mavazi ya kujikinga, yale makoti meupe ya kazi, lakini kemikali zilipenya ndani. Zilifanya nguo ziwe ngumu."

Kampuni ya Alabuga imesema wafanyakazi wote wanapewa mavazi ya kujikinga ipasavyo.

A man holds out his arm. There is a large area of discolouration.

Chanzo cha picha, Supplied to the BBC

Maelezo ya picha, Mabaki ya alama za kubabuka kwa ngozi kutokana na Kemikali zinavyoonekana katika mikono ya mwenzake Adau

Shambulizi la ndege isiyokuwa na rubani

Hiyo si hatari pekee. Tarehe 2 Aprili 2024, wiki mbili tu baada ya Adau kuwasili Urusi, Eneo Maalum la Alabuga lilishambuliwa na ndege isiyokuwa na rubani ya Ukraine.

"Siku hiyo nilishtuliwa na kengele, lakini hii ilikuwa tofauti. Madirisha ya ghorofa ya juu kwenye bweni letu yalivunjika, na baadhi ya wasichana waliamka baada ya mlipuko. Tukatoka nje."

Walipoanza kutembea mbali na bweni lao katika baridi ya asubuhi, Adau aliona watu wakianza kukimbia.

"Niliona watu wakionyesha kidole juu, nikatazama angani, nikaona ndege ikija. Ndipo nilianza kukimbia pia hadi nikawapita waliokuwa wameanza kukimbia kabla yangu."

BBC ilihakiki video ambayo Adau alituma siku hiyo, na kuthibitisha kuwa ilirekodiwa siku na mahali ambapo Ukraine ilifanya shambulio lake la ndani zaidi katika ardhi ya Urusi wakati huo.

People stand in the snow and appear panicked. A large smoke cloud rises behind them.

Chanzo cha picha, Supplied to the BBC

Maelezo ya picha, Picha alizopiga Adau siku ya shambulizi la ndege isiyokuwa na rubani kutoka Ukraine

"Kuna taarifa nyingi za kupotosha kuhusu Urusi.

Hapo awali Alabuga walikuwa na wafanyakazi kutoka Ulaya na Marekani, lakini waliondoka baada ya vita vya Ukraine na Urusi kutokana na vikwazo.

Hata hivyo Urusi ilipoanza kutafuta Waafrika, niliona kama walikuwa wanajaza nafasi walizoacha Wazungu."

Baada ya kuacha kazi, familia yake ilimtumia tiketi ya kurudi nyumbani. Lakini anasema wanawake wengi hawawezi kumudu gharama ya kurejea makwao, kwani mishahara yao ni duni.

Aliahidiwa dola 600 kwa mwezi, lakini alipokea asilimia sita tu ya kiasi hicho.

"Walikatwa pesa za kodi, kodi ya nyumba, mafunzo ya lugha ya Kirusi, intaneti, usafiri wa kwenda kazini, na nyinginezo.

Walisema ukikosa siku moja ya kazi, wanakata dola 50; ukipiga kengele ya moto kwa bahati mbaya, wanakata dola 60; usipofanya majukumu mengine wanapunguza mshahara."

Alabuga Start iliiambia BBC kwamba mishahara inategemea utendaji na nidhamu kazini.

BBC pia ilizungumza na mwanamke mwingine katika mpango huo ambaye hakutaka kutajwa jina kwa hofu ya usalama wake. Yeye alieleza uzoefu tofauti:

"Kwa kweli kila kampuni ina sheria. Unawezaje kulipwa mshahara kamili kama hukufanya kazi vizuri? Hakuna anayelazimishwa kufanya jambo asilotaka. Wengi wanaoondoka ni wale waliokosa kazi au kuvunja sheria.

Alabuga hawamshiki mtu kwa nguvu; unaweza kuondoka wakati wowote," alisema.

Lakini kwa Adau, kufanya kazi katika viwanda vya sialaha za kivita vya Urusi lilikuwa jambo la kuumiza moyo.

"Ilinisikitisha sana. Kulikuwa na wakati nilirudi bwenini nikalia. Nikajiuliza: 'Siamini kwamba hiki ndicho ninachokifanya sasa.' Nilihisi uchungu kujua nimehusika kwa njia yoyote katika kutengeneza kitu kinachoua watu wengi."