Nyota wa soka wanaocheza soka Ulaya huku wakiwa wamefunga Ramadhan

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika maeneo mengi duniani, mwezi mtukufu wa Ramadhani huadhimishwa kwa Waislamu kufunga kuanzia alfajiri hadi machweo ya jua, wakijizuia kula na kunywa na kukithirisha ibada.
Moja ya mambo yaliyovutia wengi ni mabadiliko yaliyojitokeza katika ulimwengu wa soka, ambapo mechi husimamishwa kwa muda mfupi wakati wa magharibi ili kuwapa wachezaji Waislamu fursa ya kunywa maji na kufungua saumu yao.
Hii imetuchochea kuangazia baadhi ya wachezaji Waislamu wanaofunga Ramadhani huku wakicheza soka barani Ulaya.
Mohamed Salah – Liverpool

Chanzo cha picha, Getty Images
Mohamed Salah, aliyezaliwa Juni 15, 1992, ni mchezaji wa kulipwa kutoka Misri anayecheza kama winga wa kulia au kiungo wa pembeni katika klabu ya Liverpool ya Ligi Kuu England (Premier League). Pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Misri.
Anachukuliwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa kizazi chake na mmoja wa mawinga bora katika historia ya soka.
Akiitwa "Mfalme wa Misri", ndiye mchezaji wa kigeni aliyefunga mabao mengi zaidi katika historia ya Ligi kuu ya Uingereza na pia Mwafrika aliyefunga mabao mengi zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League).
William Saliba – Arsenal

Chanzo cha picha, Getty Images
Mfaransa huyu mwenye umri wa miaka 24 ni miongoni mwa mabeki bora na thabiti zaidi duniani kwa sasa, na ni mhimili muhimu katika safu ya ulinzi ya Arsenal.Wakati huu wa ramadhan anafunga licha ya kuwa anashiriki mechi ambazo timu yake bado iko kidedea katika jedwali la ligi kuu ya Uingereza.
Hugo Ekitike – Liverpool

Chanzo cha picha, Getty Images
Mchezaji huyu chipukizi kutoka Ufaransa, aliyezaliwa mwaka 2002, alijiunga na Liverpool mwaka 2025 akitokea Eintracht Frankfurt. Licha ya kuwa amefunga msimu wa ramadhan kama inavyotakikana katika dini ya kiislamu hakujamzuia yeye kucheza soka.
Amad Diallo – Manchester United

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni mchezaji kutoka Ivory Coast ambaye ameichezea Manchester United tangu msimu wa 2024/2025. Akiwa na umri wa miaka 23, amekuwa mmoja wa wachezaji wanaojivunia sana klabu hiyo kwa sasa.
Ousmane Dembélé – PSG

Chanzo cha picha, Getty Images
Ousmane Dembélé, aliyezaliwa Ufaransa Mei 15, 1997, ni miongoni mwa wanasoka maarufu zaidi duniani kwa sasa. Anashikilia tuzo ya kifahari zaidi ya mwanasoka duniani, Ballon d'Or.
Paul Pogba – Monaco

Chanzo cha picha, Getty Images
Paul Pogba, aliyezaliwa Machi 15, 1993, ni mchezaji wa Ufaransa anayekipiga kwa sasa katika klabu ya Monaco kwenye Ligue 1.
Lamine Yamal – Barcelona

Chanzo cha picha, Getty Images
Lamine Yamal, aliyezaliwa Hispania Julai 13, 2007, anaichezea Barcelona katika La Liga na anatajwa kuwa miongoni mwa vipaji vinavyochipukia kwa kasi duniani.
Antonio Rüdiger – Real Madrid

Chanzo cha picha, Getty Images
Antonio Rüdiger, aliyezaliwa Ujerumani Machi 3, 1993, kwa sasa anaichezea Real Madrid katika La Liga.
Hakan Çalhanoğlu – Inter Milan

Chanzo cha picha, Getty Images
Hakan Çalhanoğlu, aliyezaliwa Uturuki Februari 8, 1994, anaichezea Inter Milan katika Serie A.
Yunus Musah – Atalanta

Chanzo cha picha, Getty Images
Yunus Musah, aliyezaliwa Marekani Novemba 29, 2002, kwa sasa anaichezea Atalanta katika Serie A kwa mkopo kutoka AC Milan.
Mapumziko mafupi ili wachezaji waislamu kufungua saumu uwanjani

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mnamo mwaka 2021, makubaliano yaliwekwa ili kuwaruhusu wachezaji Waislamu kufungua saumu yao wakati wa mechi za Ligi Kuu England (Premier League).
Mapumziko ya kwanza ya aina hiyo yalifanyika Aprili 2021 katika mchezo kati ya Leicester City na Crystal Palace. Mechi ilisimamishwa kwa muda mfupi wakati wa mpira wa kipa (goal-kick) takribani dakika ya 30, ili kuwapa nafasi wachezaji wa Leicester, Wesley Fofana, na wa Palace, Cheikhou Kouyate, kunywa maji na kutumia virutubisho vya kuongeza nguvu.
"Katika Ligi Kuu Uingereza uko huru kufanya kile kinachokufaa. Kamwe hawatafanya jambo lolote linalokwenda kinyume na imani yako, na hili ni jambo zuri sana," alisema mchezaji wa zamani wa Everton, Abdoulaye Doucoure, katika mahojiano na BBC Sport mwaka 2023.
"Nafunga kila siku, sikosi hata siku moja. Sasa imekuwa jambo la kawaida na rahisi kwangu. Mazoezi huwa yaleyale wakati wa Ramadhani, lakini tunaposafiri kwa mechi za ugenini, huenda tukahitaji kula baadaye kuliko wachezaji wengine. Hivyo mpishi hututayarishia chakula maalum, akihakikisha kila kitu kiko sawa kama nyumbani. Tunapatiwa chakula cha halali, kwa hiyo hakuna tatizo lolote," aliongeza Doucoure.
Aidha, mwaka 2022, mchezaji wa zamani wa Liverpool, Sadio Mane, alifichua kuwa klabu hiyo ilibadilisha ratiba za mazoezi ili kuwasaidia wachezaji wake Waislamu katika mwezi wa Ramadhani.
'Sio kila mtu anapaswa kufunga...'

Chanzo cha picha, MCS
Wazee, wagonjwa na wanawake wajawazito, wanaonyonyesha au wanaopata hedhi hawalazimiki kufunga.
Yeyote anayesafiri umbali wa zaidi ya maili 48 (kilomita 80) pia ameruhusiwa kula, lakini lazima alipe saumu baadaye, kwa hivyo hii inajumuisha wachezaji wanaoenda kwenye michezo ya ugenini.
Muslim Chaplains in Sport (MCS) ilianzishwa mwaka wa 2014 na ndilo shirika pekee la aina yake kuidhinishwa na kufadhiliwa na Premier League na EFL, likifanya kazi katika vilabu vyote 92 vya taaluma ya kandanda kutoa mihadhara na semina za elimu.
Vilabu vya Ligi Kuu ya Uingereza mara kwa mara hutafuta mwongozo wa Kiislamu kutoka kwa MCS kwa niaba ya wachezaji wao Waislamu, ikiwa ni pamoja na masuala kama vile kuahirisha mifungo ili uchezaji wao wa mazoezi na wakati wa mechi usiathiriwe.
"Ingawa hakuna uamuzi wa Kiislamu kwa wanariadha, tunatoa ushauri kuhusu jinsi wanavyoweza kudumisha imani zao na kujadili kama wanafuzu kusamehewa, kama vile wanapokuwa safarini au wagonjwa," mkurugenzi mkuu wa MCS Ismail Bhamji aliambia BBC Sport.
"Wacheza kandanda wa Kiislamu wanatoka katika asili tofauti na inabidi tutafute suluhu ambazo zitafanya kazi kwa wote kutekeleza imani yao.
"Klabu moja ya Ligi Kuu iliniomba nizungumze na mchezaji Mwislamu ili kuahirisha mfungo wake wa Ramadhani. Kiislam hana sifa kwa sababu masharti fulani yaliyotajwa lazima yatimizwe na lazima niwe muwazi na mkweli kwao juu ya ukweli mbaya."
MCS inafanya kazi kwa karibu na klabu mbili kuu nchini, Manchester City na Liverpool, na Bhamji alitoa hotuba ya Ramadhani katika Kampasi ya Etihad siku ya Jumatano, huku pia akisifu mbinu zao za utofauti na kupanua ujuzi wao kuhusu masuala haya.
"City na Liverpool zinafanya vizuri zaidi na ninaona misingi iliyowekwa kwenye klabu hiz mbili," alisema. "Kuanzia chuo cha mafunzo na kuendelea, wana watu sahihi na wenye fikra sahihi na maono ya kusaidia klabu hadi kwenye kikosi cha kwanza.
"[Makocha] Pep Guardiola na Jurgen Klopp wanasifika kwa sababu wana maendeleo na wanafikiria mbele kwa hivyo nimeona maboresho yakifanywa katika kllabu kwa misimu kadhaa."
Kwa wachezaji hawa, kufunga Ramadhani huku wakishiriki mashindano ya kiwango cha juu barani Ulaya ni mfano wa nidhamu, imani na kujituma kwa hali ya juu katika taaluma yao ya soka.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












