Vita vya Ukraine: China inaisaidia Urusi kwa msaada gani?

Chanzo cha picha, Reuters
China imekuwa mshirika muhimu zaidi wa kibiashara wa Urusi huku ikijaribu kupunguza athari za vikwazo vya kiuchumi ilivyowekwa na baadhi ya nchi ili kukabiliana na uvamizi wake nchini Ukraine.
Marekani sasa inasema Beijing inafikiria kusambaza silaha na risasi kwa Urusi, madai ambayo China inakanusha vikali.
Je, China inaipatia Urusi silaha?
China imekuwa ikipanua uwezo wake wa uzalishaji wa kijeshi na sasa ni nchi ya nne kwa mauzo ya silaha duniani.
"Silaha za China zinazidi kupiga hatua kiteknolojia," anasema Siemon Wezeman kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm.
"Drones zake, kwa mfano, ni eneo moja ambalo Urusi ingependezwa sana nayo."
Marekani inasema makampuni ya China tayari yametoa "msaada usio wa kuua" kwa Urusi, na kwamba ina habari mpya zinazopendekeza Beijing inaweza kutoa "msaada hatari" hivi karibuni.
Maria Shagina, mtaalam wa vikwazo vya kiuchumi katika Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati, anasema China haijaipatia Urusi silaha kwa njia ya wazi lakini inaweza kuwa inaiuzia kwa siri bidhaa za hali ya juu ambazo zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kijeshi.
"Kuna ushahidi kwamba China ndiyo muuzaji mkubwa zaidi wa semicondukta - mara nyingi kupitia makampuni ya Shell huko Hong Kong na UAE - kwenda Urusi," anasema.
"Baadhi ya makampuni ya Kichina pia yanatoa ndege zisizo na rubani za kiraia, zikitumia nafasi iliopo kati ya madhumuni ya kijeshi na ya kiraia."
Kituo cha Mafunzo ya Juu ya Ulinzi chenye makao yake makuu nchini Marekani kinasema kuwa makampuni ya China huenda yanaitumia Urusi sehemu za kielektroniki kwa ajili ya rada za kukinga makombora ya ndege.
Marekani pia imeiwekea vikwazo kampuni ya China ambayo Washington inasema imetoa picha za satelaiti kuunga mkono vikosi vya mamluki vya Urusi vinavyopigana nchini Ukraine.
Mshirika muhimu zaidi wa biashara wa Urusi
Baada ya Urusi kuivamia Ukraine mwaka mmoja uliopita, mataifa ya Magharibi yaliiwekea Urusi vikwazo vikali - kupiga marufuku uagizaji wa mafuta na usafirishaji wa bidhaa za hali ya juu.
Makampuni mengi ya Magharibi yalikata uhusiano wao na Urusi kabisa, na biashara yake na Marekani, Uingereza, na nchi za Umoja wa Ulaya ilidorora katika kipindi cha 2022.
Hathivyo, biashara ya jumla ya Uchina na Urusi ilifikia kiwango cha juu cha $190bn mnamo 2022 - ongezeko la 30% la mwaka uliopita.
Grafu inayoonyesha biashara ya Urusi/Uchina kuanzia 2015 hadi 2022

Uagizaji wa bidhaa za Urusi kutoka Uchina uliongezeka kwa 13% hadi $ 76bn na usafirishaji wake kwenda Uchina uliongezeka kwa 43% hadi $ 114bn.
Biashara ya Urusi na nchi za Magharibi iliposhuka mwaka 2022, China ikawa, mshirika wake muhimu zaidi wa kibiashara.
Chati inayoonyesha washirika wakubwa wa biashara wa Urusi

Uchina inanunua mafuta na gesi kiasi gani kutoka Urusi?
Takriban nusu ya mapato yote ya kila mwaka ya serikali ya Urusi yanatokana na mafuta na gesi, na mauzo yake kwa nchi za Umoja wa Ulaya yameshuka katika mwaka uliopita huku vikwazo vikiendelea.
Kiasi kikubwa cha upungufu huu kimeundwa na kuongezeka kwa mauzo kwa Asia.
Urusi ilisafirisha gesi ya mafuta ya petroli (LPG) mara mbili zaidi kwa Uchina mnamo 2022 kuliko mwaka uliopita. Pia ilitoa gesi asilia kwa 50% zaidi kupitia bomba la Power of Siberia, na 10% zaidi ya mafuta ghafi.
Kundi la G7 la nchi zilizoendelea kiuchumi, pamoja na Umoja wa Ulaya na Australia, limejaribu kuweka kikomo duniani kote kwa bei ya mafuta ya Urusi yanayosafirishwa kwa njia ya bahari, lakini China imekataa kufuata sheria hiyo na kununua mafuta ghafi ya Urusi kwa bei ya soko.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pia kuna mipango ya muda mrefu ya kupanua uhusiano wa nishati.
Nchi hizo mbili zimekubaliana kujenga bomba jipya la gesi (The Power of Siberia 2). Iliyopo ilianza kufanya kazi mnamo 2019, chini ya kandarasi ya miaka 30 yenye thamani ya zaidi ya $400bn.












